TUUKATAE MGAWO WA UMEME!
Baada ya kutangaziwa juzi Bungeni kwamba mgawo wa umeme umekuwa ni wakutengenezwa, nimeshawishika kuirudia makala yangu niliyoiandika mwaka 2008, nikiwashawishi watanzania kuukataa mgawo wa umeme… endelea kusoma..
“Shirika la Umeme Tanzania TANESCO, limetangaza mgawo wa umeme nchi nzima. Ni wazi asilimia kubwa ya watanzania na hasa kule vijijini haijapata umeme majumbani, lakini mgawo wa umeme unawagusa maana uzalishaji viwandani unazorota na huduma nyingine zinazotegemea umeme na zinasambaa hadi vijijni zinayumba yumba. Walio wengi na hasa wale wa mijini tunafahamu maana ya mgawo nini? Ni giza, ni kushindwa kupika, ni kushindwa kunyoosha nguo, ni kushindwa kufanya kazi kwenye kompytua, ni vyakula kuharibika kwenye majokovu, ni kazi za uzalishaji kusimama na adha nyinginezo. Naandika makala hii kuwashawishi watanzania kuukataa mgawo huu wa Umme. Tusimame na kushikamana na kusema kwa sauti moja kwamba hatuukubali mgawo wa umeme ni imani yangu kwamba tukiukataa, hakuna atakayedhubutu kuleta hoja hii ya kizembe tena.
Jana Jiji la Dar-es-salaam limeshinda na kelele za jenereta. Hakuna mwenye uhakika zamu hii ni tatizo gani limesababisha mgawo wa umeme. Nilipopita Kariakoo, nilikuta wafanyabishara wakiendelea na biashara zao huku jenereta zikiwa zinawaka na kupiga makelele kiasi cha watu kushindwa kusikilizana. Mbali na makelele jenereta nyingi zinatoa moshi mweusi na kuchangia uchafuzi wa mazingira. Watanzania kwa kupole wao, wanafikiri ni jambo la kawaida umeme kuzimika. Wanafikiri hawana la kufanya. Hata ungezimika mwaka mzima, kuna ambao jambo hilo halitawagusa. Si kwamba hawaitaji umeme, ila walishafanywa mazezeta nao wakakubali. Tulikuwa tukielezwa kwamba mgawo wa umeme unasababishwa na kina cha maji kupungua kwenye mabwawa ya kuzalisha umeme. Baada ya mvua kunyesha na mabwawa haya kujaa hadi kupita kiasi, mgawo wa umeme ulitokomea kusiko julikana. Na kila mtu aliamini hatuwezi kupata tatizo hili tena. Lakini juzijuzi mgawo ukarudi kwa kisingizio cha mitambo ya kuzalisha gesi kupata hitilafu pale Ubungo. TANESCO, walitutangazia kwamba wataalamu wa kutengeneza mitambo hiyo waliangizwa kutoka Amerika, lakini Songas, wakakanusha habari hizo. Kama hakuna hujuma, kama hakuna ufisadi, ni kwanini Songas na TANESCO wawe na lugha mbili tofauti wakati wote wana lengo la kumsaidia na kumwendeleza mwananchi wa Tanzania? Kwanini wawe na lugha mbili tofauti wakati wote wanaitumikia Serikali ya Tanzania. Utofauti huo unaonyesha kwamba kuna kitu kisichokuwa cha kawaida katika zoezi zima la mgawo wa umeme. Kuna mtu anayepanga hujuma hizi na ni lazima mtu huyu atafutwe ili afikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Tunaambiwa kwamba mgawo huu wa umeme umesababishwa na ubovu wa mitambo ya kuzalisha gesi pale Ubungo. Sababu hii haitoshi! Ubovu huu umejitokeza lini? Ina maana mitambo hii haifanyiwi ukarabati wa mara kwa mara? Kwanini pasiwepo na mitambo ya dharura? Kwanini wanaohusika wasipange mapema kuwa na mitambo ya dharura? Kwanini kusiwepo na njia nyingine za kuzalisha umeme pale panapotokea tatizo? Baada ya tatizo la umeme lililochukua muda mrefu tungejifunza kwamba ni lazima kuwa na mitambo ya dharura. Kwanini tusubiri tatizo ndo tuanze kufikiri la kufanya wakati wananchi wanaumia? Tatizo liko wapi? Labda tutaambiwa kwamba serikali haina fedha za kununua mitambo ya dharura. Tutaambiwa serikali haina fedha za kuwekeza kwenye umeme ili kuhakikisha kuna umeme wa huhakika siku zote. Wimbo huu wa kwamba serikali haina fedha umezoeleka sana. Lakini si kweli kwamba serikali haina fedha. Nchi tajiri kama Tanzania, serikali yake haiwezi kukoswa fedha za kuwekeza kwenye umeme. Wanaoufahamu utajiri wa Tanzania, wanatucheka na kutudharau. Wanasema wajinga ndio waliwao, wanaitumia Tanzania kujitajirisha, wakati watanzania wanaendelea kudidimia kwenye umaskini.
Mimi nafikiri mgawo wa umeme ni uzembe na kutojali. Lakini pia ni upole wa Watanzania. Ni amani na utulivu. Mambo yanaharibika, uchumi wetu unavurugwa, wajanja wanapora rasilimali zetu, sisi tunaangalia na kuendeleza upole na utulivu. Kama tungekuwa na mfumo wa kuwawajibisha viongozi wetu na watumishi wa serikali kila panapotokea uzembe kama huu wa mgawo wa umme, kungejengeka umakini na kujali katika kazi. Lakini sasa hivi kila mtu anafanya anavyotaka maana anajua hakuna wa kumwajibisha. Hata hivyo wanaona jinsi watu wanavyofanya uzembe mkubwa bila kuchukuliwa hatua yoyote ile.
Ndo maana mimi ninasema tuukatae mgawo huu wa umeme. Kama ni tatizo kubwa lilio juu ya uwezo wa watendaji wetu, tutaelewa. Lakini hili la mitambo mibovu liko kwenye uwezo wa watendaji wetu.Kinachofanyika ni uzembe. Tuukatae uzembe huu ambao nina imani hata na Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, haukubali. Ni lazima kila Raia Mwema amsaidie Rais wetu kupambana na watendaji wazembe. Hivyo ni lazima tuukatae mgawo huu wa umeme. Na njia ya kuukataa mgawo huu ni kuwashinikiza viongozi wa juu katika shirika la Umeme TANESCO kujiuzulu. Hawa wakiachia ngazi, wale watakao shika nafasi zao, watakuwa makini katika mipango yao. Watahakikisha wana mitambo ya dharura, watahakikisha wanabuni njia mbali mbali za kuzalisha umeme.
Kama TANESCO, wana mipango mizuri na labda wanakwamishwa na serikali tutaambiwa tutakapokuwa kwenye harakati za kuwashinikiza wajiuzulu. Ikitokea hivyo basi ni lazima tuigeuzie kibao serikali. Na huko tupambane na watendaji wazembe. Ni lazima tufike mahali tubadilike, vinginevyo mambo hayawezi kwenda. Ni lazima tutengeneze mifumo ya kuwajibishana. Nchi zote zilizoendelea zimefanikiwa kwa kuwa na mifumo ya kuwajibishana. Mifumo hii wakati mwingine ni michungu na haifurahishi hata kidogo; panahitajika uamuzi wa kumeza machungu ili kupiga hatua.
Tangia tuanze kupata tatizo la mgawo wa umeme katika taifa letu, hakuna sababu za msingi zinazotolewa kuhusiana na tatizo hili. Kwamba mabwawa ya kuzalisha umeme yanakauka ni uzembe. Kwamba hatujaweza kufanikiwa kuzalisha umeme wa kututosha ni uzembe. Kuna njia nyingi za kuzalisha umeme na kuunganisha kwenye gridi ya taifa. Jua linazalisha umeme, upepo unazalisha umeme, miti inazalisha umeme nk. Kuna njia nyingi za kuzalisha umme. Tungekuwa na watu makini, watu wanaowajibika na kulipenda taifa letu, umeme usingezimika hata siku mmoja. Tungekuwa na wasomi waliosoma na kuelimika, umeme wetu usingekuwa unakatika ovyo ovyo na kufikia hatua ya mgawo. Je, ni kweli kwamba wasomi wetu hawakuelimika? Au ni wazembe? Kama hawajaelimika kuna haja ya kuwarudisha vyuoni ili waelimike. Kama ni uzembe, basi watu hawa wawajibishwe! Watimuliwe, na nafasi zao zichuliwe na wengine. Nchi zote ambazo umeme unawaka muda wote, zinatumia njia mbali mbali za kuzalisha umeme. Wasomi wa nchi hizi wanatumia elimu yao kuzalisha umeme kwa kutumia njia mbalimbali kama nilizozitaja hapo juu.
Tumekuwa tukishuhudia uzembe mkubwa wa TANESCO. Umeme unakatika ovyo ovyo bila taarifa. Haiwezekani umeme ukawaka siku mbili bila kukatika. Vyombo vya watu vinaharibika. Watanzania kwa upole wao, hakuna anayelalamika. Kama TANESCO wangelazimishwa kulipa hasara zinazojitokeza wanapozima umeme ovyo ovyo, wangekuwa makini kuzima umeme bila taarifa. Wangekuwa makini kuhakikisha umeme unakuwa wa uhakika kila wakati. Au kama wateja wa TANESCO, wangefungua kesi mahakamni kuishitaki TANESCO, kuendesha zoezi la mgawo, shirika hili lingekuwa makini katika mipango yake. Kila mteja wa TANESCO ana mkataba na shirika hilo la kupata hudu ya umeme. Hivyo TANESCO inapokatisha huduma hiyo bila ya taarifa, ni lazima mteja aiwajibishe.
Waigizaji wa Ze Komedi, katika baadhi ya vipindi vyao vya vichekesho waliigiza jinsi mafundi wa TANESCO Dar, wanavyofanya njama za kuzima umeme maeneo fulani fulani na hasa yale yenye sherehe ili wapate kitu chochote kutoka kwa waandaaji wa sherehe husika. Ingawa hivi vilikuwa vichekesho, lakini mara nyingi viligusa mambo yanayotendeka katika jamii.
Hoja ninayojaribu kuijenga hapa ni kwamba, inawezekana kabisa tukatangaziwa mgawo, wakati hakuna mtambo mbovu. Kama Richmond, walilipwa fedha bila kuzalisha umeme, kwanini umeme usizimwe kifisadi? Dawa peke yake ni wananchi kuwa wakali! Dawa peke yake ni wananchi kushikamana na kuukataa mgawo huu wa umeme.”
Na,
Padri Privatus Karugendo.
www.karugendo.net
0 comments:
Post a Comment