TUMEKOSEA: TUJISAHIHISHE! Ndani ya juma moja tumeshuhudia mara mbili kwenye vyombo vya habari uchaguzi wa Vijana wa CCM ukivurugika. Vijana wamefikia hatua ya kurushiana viti na kutaka kupigana. Kuna manung’uniko kwamba fedha nyingi(za kuhonga) zinatumika katika kuwachagua viongozi wa umoja wa vijana. Tumeshuhudia pia vurugu kama hizo zikijitokeza kila panapokuwa na uchaguzi ndani ya vyama vya siasa. Jumuia zote za CCM haziwezi kufanya uchaguzi bila vurugu, kutuhumiana matumizi makubwa ya fedha na kuwahonga wapiga kura. Nyuma tulikotoka, hakukuwa na vurugu kama hizi. Watu waliendesha shughuli za vyama vya siasa kwa kujitolea. Watu walijitolea nguvu zao na mali ili kujenga na kuendeleza vyama vyao vya siasa. Wimbi jipya la kufikiri kazi ya serikali ni kutengeneza ajira, ndilo limetufikisha hapa tulipo. Kwa kuchanganyikiwa huku serikali yetu ikaifanya siasa kuwa ajira. Mawazo ya vijana na watu wote ambao wanataka ajira ya mtelemko wanakimbilia siasa. Tumeshuhudia jinsi watu wanavyopambana kuupata Ubunge. Wanatumia fedha nyingi, wakiamini baada ya kufanikiwa, fedha yao itarudi na watapata zaidi. Hivyo wakishashinda wakaingia Bungeni, kazi kubwa ni kuhakikisha fedha inarudi; kazi ya kuwawakilisha wananchi inawekwa pembeni. Si lazima kuelezea kwenye makala hii kwamba hata juzi juzi tuliwasikia wabunge wetu wakitaka kulipwa pensheni wanapomaliza kipindi chao cha kuwa bungeni. Kwa vile wanaamini Ubunge ni ajira, hawaoni sababu ya wao kutopata pensheni kama waajiriwa wengine wote. Siasa si ajira na kamwe kazi ya serikali si kuwatafutia wanasiasa kazi. Tunashuhudia serikali ikiongeza wilaya na mikoa na majimbo ya uchaguzi ili kuwatafutia wanasiasa kazi. Ndo maana tunasikia mtu mmoja anakuwa mkuu wa mkoa, pia mbunge na wakati mwingine ni mwenyekiti wa bodi. Kazi ya serikali si kuwaajiri watu bali ni kujenga mazingira mazuri ya raia wake kuweza kufanya kazi zao za kujipatia kipato ili waishi. Hii ndiyo kazi kubwa ya serikali zote duniani. Kinyume na hivyo ni vurugu kama tunazozishuhudia na kama tulizozishuhudia kwenye historia zikisababisha serikali kuanguka kwa kushindwa kufanya kazi yake. Serikali bora, serikali makini na serikali ya wananchi ni lazima ijenge mazingira bora ya wananchi kufanya kazi zao na kujipatia kipato ili waishi. Mazingira bora ni kama: Kudumisha amani na usalama. Ndiyo maana serikali inakuwa na Jeshi na vyombo vya ulinzi na usalama. Mwalimu Nyerere, alilibatiza Jeshi letu: Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Jina hili si la bahati mbaya; maana yake ni kwamba si Jeshi la Rais, si jeshi la viongozi, si jeshi la chama cha siasa, si jeshi la kidini,si jeshi la matajiri fulani au kikundi fulani cha watu, bali ni jeshi la kulinda usalama wa watu wote wa Tanzania. Uhalali wa kuwepo kwa jeshi hili unatokana ridhaa ya wananchi wote wa Tanzania. Kazi ya serikali ni kutoa elimu kwa wananchi wake. Kujenga shule bora na zenye viwango, kuwaandaa walimu na kuwalipa vizuri ili wafanye kazi nzuri ya kutoa Elimu. Wananchi wakipata elimu nzuri, wanaweza wenyewe kutumia elimu hiyo kuyaboresha maisha yao. Kazi ya serikali ni kujenga mifumo mizuri ya kujenga maadili ya kitaifa. Hakuna taifa linaloweza kusonga mbele bila kuwa na maadili ya kitaifa. Bila kuwa na miiko ya viongozi, bila kuwa na miiko ya wafanyakazi, bila kuwa na miiko ya familia, kuwa na miiko ya vijana nk. Kazi ya serikali ni kuhakikisha wananchi wana afya bora. Ni lazima serikali kujenga hospitali nzuri na zenye huduma ya kisasa. Kuhakikisha hospitali zina dawa na zina madaktari wenye viwango, kuwalipa madaktari vizuri na kuhakikisha wana vifaa vizuri na vya kisasa vya kutoa huduma nzuri kwa wananchi. Kazi ya serikali ni kutengeneza miundombinu ya barabara. Kuhakikisha barabara zote ni nzuri na zinapitika wakati wote . Wanachi wanaweza kusafirisha mazao yao kutoka shambani hadi kwenye masoko. Kazi ya serikali ni kutengeneza pia miundombinu ya maji na kuhakikisha wananchi wote wana maji safi na salama. Ziko huduma nyingine nyingi za kijamii ambazo ni kazi za serikali. Na kazi hizi zinaendeshwa kwa pato litokanalo na jasho la wanachi. Serikali ikiyaweka hayo niliyoyataja pembeni na kujiingiza kwenye mchakato wa kuwatafutia wanasiasa kazi; kuanzisha wilaya nyingi, kuanzisha mikoa mingi na kuanzisha majimbo ya uchaguzi mengi, kutengeneza bodi nyingi na kuwachagua wanasiasa kuwa wenyeviti na wajumbe wa bodi hizo, kuwa na baraza kubwa la mawaziri na kuhakikisha kila wizara ina naibu waziri, makatibu wakuu na manaibu wao, wakurugenzi na manaibu wao, makatibu tawala wa mikoa, wakurugenzi wa wilaya nk ni lazima serikali hiyo iwe kandamizi. Itatoza ushuru mkubwa na kuwakamua wananchi ili kupata mishahara ya wanasiasa na kuendesha shughuli nyingine ambazo hazina ustawi wa wananchi. Ni kuwa na serikali kubwa inayomeza bila kuzalisha! Tuna baraza kubwa la Mawaziri, kwasababu serikali inawatafutia wanasia kazi. Baraza hili la mawazi ni kubwa na ni mzigo mkubwa kwa walipakodi wa Tanzania. Tuna Bunge kubwa, ambalo nalo ni mzigo mkubwa kwa walipakodi wa Tanzania. Na tumefanya makosa makubwa kutengeneza mazingira yanayoufanya ubunge kuwa ajira. Hii imefuta dhana nzima ya uwakilishi. Ndo maana utakuta mtu anayeishi Dar-es-salaam, anapambana awe mwakilishi wa watu Magu – Mwanza. Kwa vile ni ajira yenye kipato kikubwa, mtu anaweza kuwa Dar-es-salaam na kuwakilisha mawazo na hoja za watu wa Magu! Tunawasikia wabunge wakijigamba wakati wa kampeni za uchaguzi kwamba wataleta maendeleo. Kwamba watajenga barabara, kwamba wataleta maji, kwamba wataleta umeme, kwamba watajenga shule, kwamba watajenga hospitali nk. Mbunge si serikali na Mbunge hana uwezo wa kufanya kazi hizo. Mbunge akifanya kazi ya kuleta maendeleo, kwaa maana ya yeye mwenyewe kuleta maendeleo ni lazima awe mwizi au fisadi! Maendeleo yanaletwa na watu wenyewe wakitengenezewa mazingira mazuri na serikali yao. Kazi ya mbunge ni kuwakilisha mawazo ya wananchi kwenye Bunge. Mfano hoja hii kwamba serikali imejiingiza kwenye kazi zisizokuwa zake za kuwatafutia wanasiasa kazi, ingefikishwa bungeni na Mbunge wangu mimi: Ikajadiliwa na kutafutiwa ufumbuzi. Nisingelazimika kuandika makala hii, nafanya hivyo kwa vile hakuna nafasi ya kukutana na Mbunge wangu; wabunge wetu wako kwenye ajira ya kupata mshahara na posho, hawako tena kwenye kazi ya uwakilishi. Mbunge anayewawakilisha watu wake hawezi kuiogopa serikali au chama chake cha siasa wakati wa kuchangia hoja ndani ya Bunge: Ni lazima awe huru maana daima hatoi mawazo yake bali ya wapiga kura wake. Mbunge anayewawakilisha wananchi hawezi kushangilia kila kitu kinacholetwa na serikali na kuunga mkono kila kitu hata wakati mwingine mambo ya ovyo na mengine ya hatari kwa watu wake kama vile bei ndogo ya mazao na kupanda bei kwa vitu muhimu kama vile mafuta ya taa. Tumekosea kukubali kuigeuza siasa kuwa ajira, tumekosea kukubali serikali kujiingiza kwenye mambo mengine yasiyokuwa na ustawi wa taifa letu, kama vile kuwatafutia wanasiasa ajira. Kosa hili bila kulisahihisha hatuwezi kupiga hatua ya maendeleo. Tunashuhudia jinsi wanasiasa wetu baada ya uchaguzi mkuu wanavyo tumia nguvu, fedha na muda wao mwingi kujiandalia uchaguzi ujao.Miaka mitano wanaitumia kutafuta fedha na kujiandalia uchaguzi unaofuata. Kwa vile siasa ni ajira ,basi wanasia wanataka kuhakisha wanalinda ajira yao kwa gharama yoyote ile. Maendeleo ya taifa yanawekwa kando na kushughulikia maendeleo ya mtu mmoja mmoja anayefanikiwa kupenyeza kwenye uwanja wa siasa. Vyovyote vile, tumekosea, ni lazima tujisahihishe. Na, Padri Privatus Karugendo. +255 754 633122 www.karugendo.net

0 comments:

Post a Comment