SIKU NILIPOKUBALIANA NA MHESHIMIWA RAIS JAKAYA KIKWETE
Nimekuwa miongoni mwa wakosoaji wa Rais wetu Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kwa ukimya wake na kile kinachojulikana kama “Rais wetu kushindwa kufanya maamuzi magumu”. Nimekuwa nikifanya hivyo si kwa chuki au kwa nia nyingine mbaya, bali ni kwa nia njema na kwa mapenzi ya taifa langu la Tanzania. Ni imani yangu kwamba hata na wengine wote wanaomkosoa Rais na Chama chake cha Mapinduzi hawana nia mbaya. Ni bahati mbaya kwamba tumejenga utamaduni wa kutovumiliana na kutoaminiana. Tunataguliza itikadi na mapenzi ya chama cha siasa badala ya kutanguliza utaifa wetu na uzalendo wetu; Pia nimekuwa miongoni mwa wale wanaomlalamikia rais wetu kukikumbatia chama chake cha mapinduzi zaidi ya kazi yake ya Rais wa taifa letu na wakati mwingine kutumia rasilimali za taifa kukijenga na kukiendeleza chama chake; Na wakati mwingine niliungana na wale waliofikiri rais wetu anashindwa kuwakemea marafiki zake waliokuwa wakimpotosha na kumpatia habari za uongo na kumsababishia kufanya maamuzi mabaya.
Nimekuwa miongoni mwa wale waliofuatilia kwa karibu hotuba za kila mwisho wa mwezi za Rais wetu. Ukiachia hotuba yake ya kwanza aliyoitoa kwenye Bunge alipochaguliwa mara ya kwanza, hotuba zilizofuata hazikuwa na mvuto wala ushawishi wowote ule. Zilikuwa ni hotuba za kichama zaidi, zilikuwa ni hotuba za kukandia vyama vya upinzani na kukitukuza chama cha mapinduzi, hotuba za kujigamba, hotuba za kuwapumbaza watanzania kuamini kwamba wao ni masikini wakati ni kinyume, hotuba za kuwaaminisha watanzania kwamba serikali yetu ni masikini wakati si kweli.
Hotuba ya mwisho wa mwezi wa nane mwaka huu ilikuwa tofauti kidogo. Hapana shaka kwamba Rais wetu amebadilisha washauri wake? Au Rais wetu amezinduka na kugundua kwamba amekuwa akidanganywa na wasaidizi wake? Ni ufunuo mpya au miujiza inaanza kutokea tunapoelekea kutunga katiba mpya na uchaguzi mkuu wa 2015? Kama hotuba zake za nyumba zingekuwa kama hii ya juzi, mambo mengi yangekuwa tofauti; migomo na maandamano tunayoyashuhudia leo hii yasingekuwepo. Hotuba hii ilikuwa na mvuto na ushawishi mkubwa. Ndo maana ninadiliki kusema kwamba Hatimaye nimekubaliana na Rais wetu. Katika hotuba hii Rais alielezea juu mambo mawili. La kwanza lilikuwa ni la Sensa, alilielezea vizuri; ni upuuzi mkubwa watu kukataa sensa hata kama lengo lao ni kuigomea serikali si kwa jambo kama hili ambalo ni muhimu kwetu na kwa vizazi vijavyo. Ninamuunga mkono Rais wetu kwa kutamka kwamba wale wote waliokwamisha zoezi la sensa sheria itatumika kuwabana; hivyo hivyo sheria itumike kuwabana wote wanaokwamisha maendeleo ya taifa letu. Sheria itumike kuwabana wote wanaoiba fedha za umma na kutumia vibaya madaraka.
La pili ambalo lilichukua muda mrefu katika hotuba hii ni lile la mgogoro wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi. Rais, alielezea vizuri mgogoro huu kiasi cha kila mtu mwenye akili timamu kuuelewa vizuri. Ametukumbusha marehemu Mwalimu Nyerere, aliyekuwa amezoea kuelezea mambo magumu kwa lugha nyepesi. Ndo maana nimeamua kuandika makala hii kumpongeza rais wetu kwa kazi nzuri aliyoifanya kwa kufafanua vizuri mgogoro huu kwa lugha nyepesi na ya kueleweka kwa kila mtanzania. Kama angekuwa anaelezea na mambo mengine yenye utata kwa ufasaha huu, kelele zingepungua. Kuna suala la Muungano, lina utata mkubwa; bahati mbaya Rais wetu hajalifafanua vizuri kama alivyofanya kwa hili la mgogoro wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi. Kuna wakuu wa mikoa ambao ni wabunge, tujuavyo wakuu wa mikoa ni sehemu ya serikali na kazi ya Bunge ni kutunga sheria, kuisahihisha serikali na kuishauri; sasa hawa wakuu wa mikoa ambao ni wabunge wanaweza kufanya kazi zote hizi mbili kwa uaminifu bila mgongano wa maslahi? Wakuu wa wilaya na wakuu wa Mikoa ni makada wa chama tawala; je kazi ya serikali ni kujenga chama au ni kuijenga nchi? Kama kazi ya serikali ni kuijenga nchi kwa nini wakuu wa wilaya na mikoa wasichaguliwe miongoni mwa watanzania wenye uwezo bila kuangalia itikadi za vyama vya siasa? Haya ni baadhi tu ya mambo yenye utata ambayo hadi leo hii Rais wetu hajaweza kuyafafanua vizuri kama alivyofanya juu ya mgogoro wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi.
Kuna mengi ya kusifia kwenye hotuba hii ya mwisho wa mwezi wa nane; Ni hotuba ya kwanza ya Rais Kikwete, ambayo tangia mwanzo wa hotuba hadi mwisho hakukitaja Chama Cha Mapinduzi; tuseme ni mara ya kwanza Rais wetu kuonyesha watanzania kwamba yeye ni Rais wa watu wote wa Tanzania; aliweka pembeni itikadi na mapenzi ya chama, na kuelekeza nguvu zake zote kufafanua suala muhimu kwa usalama wa taifa letu. Sote tunajua kwamba Rais akila kiapo cha kuilinda na kuitetea Katiba ya nchi anakuwa ni Rais wa Taifa na wala si wa chama chochote cha siasa.Tumekuwa tukishuhudia kinyume na wakati mwingine ilikuwa ni vigumu kutambua ni lini Rais ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na lini ni Rais wa Taifa, na huu ni utata mwingine ambao unahitaji ufafanuzi wa kina. Pili, katika hotuba hii ya mwishoni mwa mwezi wa nane, Rais hakuwa na kigugumizi juu ya ni nani ana mamlaka ya kutangaza vita. Alitukumbusha watanzania wote kwamba yeye ndiye Amiri Jeshi mkuu na bila yeye kutangaza vita hakuna haja ya watu kuwa na wasiwasi wowote ule. Tunaambiwa baada ya tamko la Mhesimiwa Lowassa na Mhesimiwa Membe, kwamba Tanzania tuko tayari kwa vita, watu wa mpakani mwa Tanzania na Malawi, walikuwa na wasi wasi mkubwa na wengine walianza kuyahama makazi yao. Tatu, kwa mara ya kwanza aliwakemea “Marafiki” zake kupotosha ukweli juu ya mgogoro wa Malawi kwa kutangaza vita. Tumekuwa tukimlaumu Rais wetu kwa kuwakumbatia “marafiki” hata wale ambao wanaonekana wazi wazi kuwa ni adui wa taifa letu.
Nampongeza Rais wetu kutamka wazi kwamba hatuko tayari kupigana vita na Malawi, bali mgogoro huu utashughulikiwa kwa majadiliano. Hoja zote alizozijenga rais wetu zinashawishi na kuleta matumaini ya majadiliano. Kama sheria za kimataifa zinaelekeza kwamba kama mpaka wa nchi na nchi unagusa maji ni lazima mpaka uwe katikati, na kama mpaka wetu na Malawi kwa upande wa mto Songwe mpaka uko katikati, na Kama mpaka wa Mzumbiji na Malawi uko katikati mwa ziwa Nyasa kwa nini mpaka wetu na Malawi uwe ufukweni mwa ziwa Nyasa, kwa upande wa Tanzania? Hapa ni lazima itumike busara, hekima, udugu na kuelewana. Hakuna haja ya vita, maana vita ni hasara zaidi ya faida.
Msimamo wa Rais wetu juu ya mgogoro wa Malawi, ndiyo tulitegmea awe nao kwenye migogoro mingine iliyolikumba taifa letu tangia alipochaguliwa kuliongoza taifa letu mnamo mwaka 2005 kama vile mgomo wa madaktari, mgomo wa walimu, migomo ya wanafunzi wa vyuo vya juu, wizi wa fedha za umma kama vile EPA, na watu wachache kuweka fedha nyingi kwenye akaunti zao nje ya nchi, mikataba mibovu kama ule wa Richmond na mingine mingi
Bahati mbaya au kwa kushauriwa vibaya rais wetu alishindwa kuishughulikia migogoro niliyoitaja hapo juu kwa busara kama ile aliyoionyesha juzi kwenye mgogoro wa Malawi. Ni aibu kubwa Rais mzima kutangaza kwamba serikali ya Tanzania haina uwezo wa kuongeza mishahara ya madaktari na walimu wakati dunia nzima sasa hivi inajua kwamba baadhi ya watanzania wameficha fedha nyingi nje ya nchi; wakati kuna watanzania (Ndani ya serikali) wanalipwa mishahara mikubwa; wakati matumizi ya serikali hayaonyeshi dalili zozote zile za umasikini.
Ni jambo la kusikitisha Serikali kujisifu kuzima mgomo wa madaktari na walimu wakati mgomo baridi na mbaya zaidi unaendelea kwenye hospitali zetu na shule zetu. Ni wazi maumifu yanakwenda kwa wananchi wa kawaida. Wagonjwa wanaokumbana na hasira ya madaktari waliolazimishwa kurudi kazini ni wananchi wa kawaida. Watoto wanaokumbana na hasira ya walimu kulazimishwa kurudi kazini ni watoto wa wananchi wa kawaida; hata baadhi ya walimu wanaogoma na kuendeleza mgomo baridi watoto wao wanasoma shule za binafsi. Kwa maneno mengine mgomo huu haugusi maendeleo ya watoto wao.
Kama Rais wetu anaamini kwamba mgogoro wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi, utamalizwa kwa majadiliano na kuelewana, kwa nini basi asiamini pia kwamba migogoro mingine kama vile mgomo wa madaktari na walimu itakwisha kwa majadiliano na kuelewana?
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 6331 22
www.karugendo.net
pkarugendo@yahoo.com
0 comments:
Post a Comment