MWANA MAMA. TATU BINTI MZEE. Karibu tena kwenye safu hii ya Mwana Mama. Juma lilopita tulikuletea Mwana Mama Elieshi Lema, ambaye ni mwanaharakati, mwandishi na mchapishaji wa vitabu. Leo tunakuletea Mwana Mama Tatu Binti Mzee, mwanaharakati aliyepigania uhuru wa Tanganyika na kukiimarisha chama cha TANU kwa kuwaingiza wanachama wengi. Mwana Mama huyu ni kati ya wanawake wengi waliojulikana kama Wanawake wa TANU. Wanawake hawa walifanya kazi kubwa, walijitoa, walitumia rasilimali zao kupigania uhuru. Walivumilia mengi, maana jamii iliyowazunguka waliwachukulia ni “Malaya”. Lakini wao walisonga mbele maana walijua wanachokitafuta kama anavyosema Salima Ferouz kwenye kitabu cha Wanawake wa TANU: “ Niliuza vitumbua kupata fedha ya kununua kadi. Nilijiunga kwa sababu nilitaka uhuru na kuondokana na utumwa…Ukoloni ulikuwa mgumu. Tuliwekwa ndani, au tuseme tuliolewa. Unakaa ndani na kuletewa kila kitu… kinachoendelea nje hukijui, hujui kinachoendelea duniani. Kwa hio tulifikiria, kama tusipopata uhuru sisi ,watoto wetu wataupata, lakini tufanye kazi tuondokane na utumwa… “Sisi wanawake tulikuwa na nguvu… tuliongoza njia kwa sababu ya uonevu wa watoto wetu na jinsi tulivyowekwa ndani… tulifanya kazi pamoja, tukajiunga na Kitengo cha Wanawake na kutumikia TANU, tukichangisha fedha na kuwahamasisha wengine wengi wajiunge..” (Wanawake wa TANU). Ukisoma Historia ya Taifa letu, mchango wa wanake wakati wa kupigania huru umeachwa! Inawezekana umeachwa kwa bahati mbaya, lakini pia inawezekana ni kwa makusudi? Au ushauri wa Bwana Mgonja ulifuatwa vizuri? Katika kitabu cha Wanawake wa Tanu, tunausikia ushauri wa Bwana Mgoja: “ Waziri wa Maendeleo ya Jamii Bwana Mgo nja, alizungumza katika njia iliiyofiifisha ari ya siasa kwa wanawake na kuimarisha mamlaka ya serikali. Wakati kitengo cha wanawake kilikuwa kinahamasisha wanawake wajiunge harakati za kujenga taifa, Mgonja aliwaambia wanawake kwamba wakilea watoto watakuwa wamelea taifa zima. Aliwasifu wanawake kwa juhudi zao katika kupigania uhuru, lakini kwa sasa walichotakiwa kufanya ni kulima, kufuga kuku, kuchimba visima na kupanda miti pamoja na kushiriki katika kisomo cha watu wazima. Mgonja alionya kwamba itabidi utamaduni wa Kiafrika ukuzwe, kwani wakoloni waliudharau.” (Wanawake wa Tanu uk 110). Kufuata utamaduni wa Mwafrika ni kumrudisha mwanamke jikoni! Ni kuhakikisha mwanamke anafanya kazi ya kulea watoto na kuachana na siasa au kazi nyingine za serikali. Ni utamaduni mbaya wenye kunyanyasa na kugandamiza haki za wanawawake. Na kusema kweli, ushauri wa Mgonja, ulizingatiwa, maana baada ya hapo wanawake walikwenda jikoni na kutunza watoto. Mbaya zaidi hata na jitihada zote zilizoendeshwa na wanawake wake hawa wakati wa kupigania huru zilifutwa kwenye kumbukumbu. Majina makubwa yaliyosikika wakati wa kupigania Uhuru kama vile Bibi Titi Mohamed na Tatu Binti Mzee hayakusikika tena! Baadhi ya wanawake wapigania uhuru wa Tanganyika, walipohojiwa kwenye kitabu cha Wanawake wa Tanu, walikuwa na haya ya kusema: “Nikwambie ukweli, wanawake ndio walioleta TANU. Ukweli ni kwamba wanawake ndio waliofanya hivyo. Wanaume wengi waliogopa kufukuzwa kazi. Waliambiwa na waajiri wao kwamba yeyote atakyejiunga na TANU atakufkuzwa mara moja…Lakini wanawake walikuwa mashabiki wa nguvu wa TANU na wengine waliachika kwa sababu ya shughuli zao za siasa” ( Mashavu binti Kabonge- Wanawake wa TANU) “Nilisaidia kujenga ofisi ya chama ya Mabogini, ilikuwa nyumba ya Abddi Nuru aliyoitoa kwa chama.Nyumba nyingine ilikuwa ya bi Muhogo, alitoa chumba kimoja amacho nilikarabati mwenyewe…nilitoa mali na rasilmali zangu kwa Tanu…” (Elizabeth Gupta – Wanawake wa Tanu) ‘Tulitembea kw amiguu siku nzima bila chakula. Ukichukua chai nyumbani na ukijaliwa kupata karanga, unanunua. Wakati mwingine tuliweza kupata fedha za chakula kutoka ofisi ya TANU, lakini ilibidi wapige hesabu kwa makini. Wakati mwingine tulipewa shilingi mbil tu..” (Halima Hamisi- Wanawake wa TANU). “Tulikuwa tunatafuta maisha bora ya baadaye kwa watoto wetu na tulitaka uhuru, uhuru wa kuamua tulichotaka… Tulitarajia uhuru ulete amani…usawa, tuwe pamoja na tuishi kw aamani. Hatukutarajia kupata fedha. Hata kama sio matajiri, hatuna nyumba kubwa, tunapaswa kuwa na umoja na tuheshimiani…” ( Halima Hamisi – Wanawake wa TANU”. Kuna ushahidi wa kutosha na usiopingika kwamba wanawake walishiriki kikamilifu kuleta uhuru wa Tanganyika, lakini majina yao yamefukiwa na mifupa yao kaburini. Miongoni mwa wanawake hawa waliopigania uhuru na kufanya kazi kwa karibu na Bibi Titi Mohamed ni Tatu Binti Mzee. Tatu Mzee alizaliwa katika mji wa Kikale uliopo Rufiji, wakati vita Kuu ya Pili ya Dunia ilipokuwa inakaribia kuisha. Baba yake, Mzee bin Abad alikuwa Mnyao kutoka Kilwa na alifanya kazi New Africa Hotel, na baadaye akafanya kazi ya udobi. Mama yake Tatu, Hadija binti Fundi, alikuwa dada wa mke wa kwanza wa baba yake Bibi Titi. Baba yake Tatu alipopata kazi, familia ilihamia mjini na Tatu aka baki na bibi yake. Baada ya kutoka ndani kama mwali, aliolwa na mume wake wa kwanza Hamisi bin Suleiman, aliyekuwa mhandisi wa maji. Baadaye Tatu alisikia juu ya TANU kupitia kwa Bibi Titi Mohamed. Tatu alikaa na kadi ya uanachama bila kujua la kufanya mpaka Sheneda, mwanachama wa TANU alipokuja kuwaambia “ Nyie wanawake mnahitajika na chama. Tupo wanaume tu. Wanawake wanahitaji wawahasishe wengine kujiunga na katika TANU” Hivyo Tatu Binti Mzee, alifanya kazi ya kwenda nyumba kwa nyumba kuandikisha wanachama wa TANU. Hata hivyo baadaye waliona zoezi la kwenda nyumba kwa nyumba ni gumu, hivyo waliamua kuviendea vikundi. Walitafuta vikundi vya Lelemama na wapika pombe kwa sababu sehemu hizo zilikuwa na mkusanyiko wa watu, ambao waliendeleza kusambaza ujumbe wa kujinga na TANU. Hivyo, wanawake walikuwa muhimu, sio tu kwa kuandikisha wanawake wenzao, lakini pia kuandikisha wanaume wa mjini Tatu Mzee alisafiri nje ya Dar-es-salaam kwa shughuli za uhamasishaji, lakini zaidi alisafiri sehemu za pwani. Pamoja na Bibi Titi Mohamed, Tatu Mzee alikuwa mmoja wa wajumbe wanawake wa kwanza katika chombo muhimu cha maamuzi, yaani Kamati Kuu ya Chama. Leo hii Tatu Binti Mzee, hasikiki popote, ndani ya CCM, chama kilichotokana na TANU na ndani ya historia ya taifa letu. Mwenzake Bibi Titi, anasikika ingawa ni pamoja na doa alilolipata la uhaini na baadaye kusahaulika kabisa. Ndo maana jitihada za sasa hivi pamoja na uanzishwaji wa ukrasa huu wa Mwana Mama, ni kulenga kufufua historia hii ya wanawake wapigania uhuru iliyozikwa. Watafikti, waanze kazi ya kutafuta ukweli juu ya suala hili. Watafiti juu ya Mwana mke huyu Tatu Binti Mzee, ambaye Bibi Titi anakubali kwamba alikuwa msaidi wake wa karibu na alifanya kazi nyingi ya kuwaingiza wanachama wa TANU, kwa kutembea nyumba kw nyumba na kutafuta vikundi vya ngoma na pom be. Hii haikuwa kazi ndogo,ni mchango mkubwa kuliko hata mchango wa majina makubwa ya wanaume tunayoyaskia sasa hivi na kuyatukuza. Bila kuwatafuta wanachama na kujenga chama imara chenye wanachama, harakati za kupigania uhuru zingekuwa ngumu. Hivyo kuna hitaji la lazima na la haraka kuwakumbuka mashukaa hawa waliopigania uhuru wa taifa letu kwa uaminifu mkubwa. Na, Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment