“ LIWALO NA LIWE” ULIMI ULITELEZA?
“Liwalo na Liwe” ni maneno ya kukata tamaa? Kama Waziri mkuu anafikia hatua ya kukata tamaa, ni bora kusema ameshindwa kazi na kuachia ngazi kabla ya kuleta vurugu na maisha ya watu yakapotea bure; je wananchi nao wakikata tama na kusema “Liwalo na liwe” tutafika wapi? Vurugu na vita popote duniani zinaanza pale viongozi na wanaongozwa wakikata tama na kusema “Liwalo na Liwe”. Au tuseme tu kwamba “Liwalo na liwe” ni maneno ya mtu mwenye kiburi cha madaraka? Ni maneno ya mtu mwenye busara? Ni maneno ya mtu anayeongoza nchi katika mfumo wa kidemorasia? Ni maneno ya kulipenda taifa? Au ni maneno ya mtu asiyejali ambaye kwake kufa na kuishi ni mapacha? Au tuseme ni maneno ya mtu ambaye yuko tayari kupambana akijiamini kwa nguvu alizo nazo na kujiaminisha kwamba hakuna la kumtisha wala kumtikisa? Kiongozi aliyechanguliwa kwa kura za wananchi anaweza asiogope kutikiswa na wale waliomwajiri? Hicho ni kiburi au ni…..?
Kama Waziri Mkuu angekuwa kilabuni anakunywa pombe akajisemea “Liwalo na liwe” tunaweza kusema ulimi kumeteleza! Au Waziri Mkuu akiwa nyumbani kwake, anaongea mambo ya kifamilia na kusema “ Liwalo na liwe” hakuna atakayejali maneno hayo isipokuwa ladda familia yake hata kama maneno hayo yakiwekwa kwenye vyombo vya habari. Au Waziri Mkuu, akiwa na viongozi wenzeke wanachapa michapo, akajisemea “ Liwalo na Liwe” hakuna atakayejali.
Lakini Waziri Mkuu akisema “Liwalo na Liwe” akiwa amesimama Bungeni; kwenye Jumba tukufu la taifa letu la kutunga sheria na kuishauli serikali; akiwa na akili timamu, akiwa anatoa hoja juu ya jambo linalogusa maisha ya kila mtanzania: Mgomo wa Madaktari, akajisemea “ Liwalo na Liwe”, ni vigumu kuamini kwamba ulimi uliteleza au kwamba alikuwa na maana nyingine ya neno “Liwalo na Liwe”.
“Liwalo na liwe” hata kama watu wanakufa hakuna shinda! Mtu mwenye akili nzuri na ambaye anaweza kuchambua mambo vizuri ni lazima afikiri hivyo. Mjadala ulikuwa juu ya mgomo wa madaktari. Serikali ilitakiwa kutoa tamko juu ya mgomo huo: Kwa maana ya itafanya nini ili mgomo huo ufikie mwisho. Madaktari walipogoma mara ya kwanza, walikaa chini na serikali na kujadiliana na kukubaliana lakini serikali ya “Liwalo na liwe” haikutekeleza makubaliano. Uamuzi wa madaktari ukawa ni kugoma tena ili kuishinikiza serikali kutekeleza ahadi zake. Mgomo huu umeshika kasi, huduma kwenye hospitali za serikali unasuasua. Wenye fedha wanawakimbiza wagonjwa wao kwenye hospitali za watu binafsi. Wale ambao hawatibiwi ndani ya nchi (Na waziri mkuu akiwemo) wala hawana habari na linaloendelea. Wananchi wa kawaida wanateseka na wengine wanakufa kwa kutopata huduma. Ni wakati ambao kila mtanzani anasubiri kusikia hatua za haraka za serikali kumaliza mgomo huu. Na mara waziri mkuu anasimama Bungeni na kusema serikali itatoa uamuzi “Mgumu” juu ya mgomo wa madaktari “Liwalo na liwe”.
Wakati Waziri Mkuu anatoa maneno hayo, Kiongozi wa mgomo wa madaktari anakamatwa, anapigwa, anateswa na kutupwa kwenye msitu kama ilivyotokea kwa wafanyabishara wa Mahenge. Je hii ndo maana ya “Liwalo na Liwe”? Au Serikali itajikosha na kusema haina habari zozote juu ya tukio hilo?
Kuwateka watu, kuwapiga na kuwaumiza na wakati mwingine kutoa uai wao ni matukio yanayotokea kwenye nchi zinazotawaliwa kimabavu. Iddi Amin Dada, aliyekuwa Rais wa Uganda enzi zile, ambaye sisi tulimbatiza jina la Nduli, alikuwa akiwatesa na kutoa uai wa wapinzani wake. Dunia nzima ilimchukia baada ya vyombo vya habari kuonyesha picha za watu aliokuwa akiwatesa na kuwapiga risasi mchana kweupe mbele ya umati wa watu. Baada ya kuona unyama wake, dunia nzima ilimchukia. Picha za Kiongozi wa mgomo wa madaktari zilizosambaa kwenye magazeti na kwenye mitandao ya kijamii, zinaonyesha unyama kama ule wa Iddi Amin. Ingawa hadi sasa hivi serikali inajikosa kutoshiriki; bado kuna kishawishi kikubwa cha kuamini kuwepo mkono wa serikali. Nduli Iddi Amin aliyekuwa jirani yetu, sasa ametuingilia mpaka ndani!
Kama “Liwalo na liwe” ina maana yenyewe, basi Serikali ina mpango wa kuwafukuza kazi madaktari waliogoma au kuwakamata na kuwaweka kizuizini? Au kuwakamata na kuwatesa kama ilivyotokea kwa kiongozi wa mgomo? Kwa vyo vyote vile “Liwalo na liwe” si neno lenye nia njema.
Tanzania tuna madaktari wachache. Na hao tulio nao, serikali imewasomesha kwa shida. Hadi leo hii tunashuhudia vita katia ya serikali na wanafunzi juu ya mikopo. Wakati tunashindwa kuindesha serikali kwa fedha zetu wenyewe mbaka tupate msaada kutoka nje, tunaweza kupata wapi kiburi cha kuwafukuza kazi madaktari? Ina maana tukiwafukuza, kesho tunawapata wengine?
Waziri Mkuu anasema tutatumia hospitali za jeshi. Ziko ngapi hospitali hizi kuweza kutoa huduma kwa watanzania wote? Eti watawarudisha kazini madaktari walioshtaafu! Hili linawezekana, lakini je wakiwarudisha madaktari wastaafu kazini, watanunua na vifaa vipya na vya kisasa? Ugomvi wa madaktari si mshahara na posho bali ni vifaa pia. Lakini hili la vifaa linawekwa pembeni ili kuonyesha kwamba madaktari wana roho mbaya.
Madaktari ni watanzania na wanaishi hapa. Wanashuhudia jinsi fedha ya serikali inavyofujwa. Mfano mzuri ni Bunge letu. Kwanza lina wabunge wengi ambao kazi yao haionekani! Bunge linatumia fedha nyingi kuwalipa wabunge wanaoshangilia kila kitu hata mambo ambayo ni hatari kwa taifa letu. Mfano mbunge anayeunga mkono hoja asilimia miambili, kwanini apewe tena muda wa dakika 15 kuongea? Asilimia kubwa ya wabunge wetu wanaunga hoja zote mkono. Hivyo hao wanaounga mkono, kama wangekaa kimya bila kupoteza muda wa kuongea, Bunge la bajeti lingekuwa linakaa siku chache sana na kuokoa fedha nyingi zinazoteketea kule Dodoma. Fedha hizo zingeelekezwa kwenye Afya na kupunguza kelele na migomo ya madaktari.
Kuna mambo mengine mengi ambayo yanatumia fedha nyingi bila sababu za msingi. Tuna sherehe za kitaifa ambazo hata bila kuzisherehekea, taifa litasonga mbele. Matumizi makubwa ya viongozi wetu kuanzisa kwa Rais hadi kwa wabunge, yanaweza kusitishwa na taifa likasonga mbele. Hivyo madaktari wanapopiga kelele kutaka vifaa vipya na vya kisasa, wanapotaka waongezewe mshahara, wanafahamu fika kwamba serikali ina fedha.
Tumesikia wabunge wakilalamika kwamba Serikali inatuma fedha nyingi kwenye Halmashauri za wilaya, lakini fedha hizi zinapotelea njiani! Fedha hizi zinaingia shimo gani? Tunashuhudia wafanyakazi wa Halmashauri hizi wakijenga majumba makubwa, wanaendesha magari ya kifahari, wana mashamba makubwa, wana mifugo wengi, wanasomesha watoto wao nje ya nchi, wanatibiwa nje ya nchi, wanakwenda kupunmzika na kufanya manunuzi nje ya nchi. Serikali imekaa kimya, sauti yake inasikika kwa madaktari “Liwalo na liwe”.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment