KUMBI ZA MUZIKI ZINA KASORO GANI?
Sitaki kabisa kulumbana na Mheshimiwa Samuel Sitta na hasa kwa hoja yake kwamba Mbowe ni mzoefu wa kuongoza kumbi za muziki hivyo si tishio la urais 2015; maana kama ni kulumbana na mzee huyu yako mengine ya msingi: Kwenye vyombo vya habari tumeshuhudia akisimikwa kuwa Mzee wa Kabila la Wanyambo. Tulipofanya tamasha la Wanyambo, Sitta, hakuonekana! Wanyambo wamesumbuliwa sana na Idara ya Uhamiaji, kwamba baadhi ni wahamiaji haramu, Wanyambo wana tatizo sugu la maji, wanyambo wana tatizo sugu la barabara, shule na hospitali, wanyambo migomba yao imeshambuliwa na ugonjwa hatari wa mnyauko. Wanyambo wana tatizo kubwa la soko la kahawa zao na wengi wao wanauza “Butura” na “Ebyenju” soko kubwa likiwa ni la Uganda kwa kuuza kahawa kwa magendo na kwa hasara kwa uchumi wa mtu binafsi na uchumi wa taifa. Ni nani mwenye Kumbuku yoyote ile ya Sitta kuonyesha mapenzi na kabila la Wanyambo? Amefanya nini zaidi kuwa Mzee wa Kabila la Wanyambo? Mtu makini kama anavyotaka tuamini, angefanya utafiti na kujipima kama anastahili “Cheo” hicho. Kama ametunukiwa na WanaCCM wachache, hana ubavu wa kubeza kumbi za muziki.
Mheshimiwa Sitta, ni mtu anayeheshimika katika taifa letu na hasa baada ya kuliongoza Bunge lenye kasi na viwango. Kazi zote alizozifanya huko nyumba hazikumjengea jina kama kazi yake ya Uspika. Ni bahati mbaya kwamba sasa anaanza kuvuruga heshima hii kwa kujiingiza kwenye mambo ya kijinga. Badala ya kujenga hoja zenye mantiki na zenye lengo la kulijenga taifa lenye umoja na mshikamano anaendeleza “matusi” na dharau za CCM. Anazitumia ziara za kiserikali kufanya kazi za CCM na kuzigeuza ziara hizo jukwaa la kuwashambulia wenzake. Kusimikwa kuwa Mzee wa Kimila wa Kabila la wanyambo ni sehemu ya kazi za serikali? Hili ni jambo binafsi ambalo mtu analifikia baada ya kutimiza masharti Fulani na kukubaliwa na asilimia kubwa ya kabila husika. Ikibainika kwamba sherehe za kumsimika Sitta kuwa Mzee wa Kabila la wanyambo zilitumia fedha na muda wa serikali, ni lazima Mheshimiwa Sitta, ashitakiwe kwa kutumia madaraka na mali za umma vibaya.
Baada ya kuona anasimikwa kuwa Mzee wa kabila la Wanyambo, niliwasiliana na wazee wa Karagwe, kutaka kujua vigezo walivyovitumia kumsimika Sitta. Asilimia 98 walijibu kwamba nao walisikia kwenye vyombo vya habari! Hivyo cheo cha Mzee wa Kabila la Wanyambo ni bandia. Kama sikosei amesimikwa kuwa Mzee wa makabila mbali mbali hapa Tanzania. Lengo la kufanya hivyo analifahamu yeye mwenyewe. Na wakati ukifika tutamwambia bila kificho.
Sasa turudi kwenye hoja yenyewe kwamba Mbowe ni mzoefu wa kuongoza kumbi za muziki hivyo si tishio la Urais 2015. Sitta, alivyokubali kusimikwa kuwa Mzee wa Kabila la wanyambo bila utafiti ndivyo anajisemea bila utafiti juu ya Mbowe.
Mbowe ni Mbunge wa Hai, na si kwamba ni mbunge mpya bali ni mbunge mzoefu. Anashinda kwenye jimbo lake kwa kujieleza na kuwashawishi watu wamchangue. Mchango wake mkubwa unaonekana kwenye jimbo lake na hata Bungeni.
Mbowe ni mfanyabiashara aliyefanikiwa na anafanya biashara zake wazi bila kificho. Ni tofauti na wale wanaofanya biashara wamejificha kwa kutumia majina ya watoto, shangazi, mjomba na wakati mwingine marafiki. Mtu ambaye anaweza kufanya biashara ndani na nje ya nchi kwa mafanikio, anabezwa kwa msingi gani?
Mbowe ni Mwenyekiti wa Chadema, chama kinachoinyima CCM usingizi. Aliposhika uenyekiti wa Chadema, chama hiki kilikuwa na wabunge wachache, leo hii chini ya Uongozi wake, Chadema kina wabunge wengi na ni chama cha Upinzani kinachoongoza kuwa na wabunge wengi. Mikakati ya kukijenga chama chake ambayo ina mafanikio makubwa kama vile Operation Sangara na M4C, imebuniwa chini ya uongozi wake.
Kwa kukubali kwama Dr.Slaa ni tishio kwa urais wa 2015, ni kukubali kwamba Chadema ina nguvu. Dr.Slaa, hawezi kusimama peke yake, maana yake ni kwamba yuko kwenye chama chenye sera safi na mfumo mzuri. Kukubali nguvu za Chama na kubeza uwezo wa mwenyekiti ni upuuzi uliopindukia. Chama kikiwa imara, maana yake ni kwamba mwenyekiti ni imara pia. Si kazi yangu kumjulisha Sitta, matokeo ya chama ambacho Mwenyekiti hana uwezo wa kuendesha chama, yeye anafahamu zaidi yangu.
Tumeshuhudia Chadema ikikumbwa na misukosuko mingi, lakini inatanzuliwa kwa busara na amani: Kifo cha Chacha Wangwe, kiliyumbisha Chadema, lakini chini ya uongozi wa Mwenyekiti Mbowe, chama kilijipanga upya na kuimarika zaidi. Kumekuwa na shutuma za mamluki ndani ya Chadema, lakini hatujasikia chama hiki kikisambaratika. Suala la Mheshimiwa Kafulila na vijana wenzake lilikiyumbisha chama, lakini tulisikia kwamba kwa hekima na busara za Mwenyekiti akisaidiana na viongozi wengine wa Chadema, chama kilisonga mbele. Suala ya kuwateuwa wabunge wa viti maalumu, nalo lilileta mtikisiko kwenye chama cha Chadema, lakini likaisha bila kukisambaratisha chama. Tunashuhudia misuguano ya Mheshimiwa Shibuda na wanachama wenzake kwenye Chadema, lakini hadi leo msuguano huu haujaleta ufa mkubwa kwenye Chama. Kuna mifano ya changamoto nyingine nyingi zinazojitokeza kwenye Chama Chadema na kushughulikiwa kwa ufanisi chini ya Mwenyekiti Mbowe. Hivyo kumbeza mtu ambaye ameonyesha uwezo mkubwa wa kukiongoza chama ni upuuzi wa kupitiliza.
Marehemu Remi Ongala, aliuliza swali kwamba kama muziki ni uhuni mbona watu wanajazana kwenye kumbi za muziki? Mbona muziki unaimbwa kanisani? Mbona watu wananunua vyombo vya muziki na kuviweka majumbani?Mbona Kapteni Komba, Mheshimiwa Mbunge wa CCM, anapanda majukwaani na kuimba? Maana yake naye uwezo wake mdogo? Mbona kampeni za CCM zinatawaliwa na muziki?
Labda Mheshimiwa Sitta, ni tofauti na wazee wengine tunaowafahamu kwa majina kwamba ni washabiki wa disko? Wanakwenda huko kufanya uhuni? Wanakwenda huko kwa vile uwezo wao ni mdogo? Kumbi za muziki si ni biashara kama biashara nyingine? Tumesikia waheshimiwa wenye makampuni ya kuzoa takataka; tuseme uwezo wao ni mdogo kwa vile wanazoa takataka? Tunasikia waheshimiwa wana makampuni ya vyombo vya habari; radio, tv na magazeti. Baadhi vyombo vyao vya habari ni muziki asubuhi hadi jioni, tuseme uwezo wao ni mdogo kwa vile vyombo vyao vinapiga muziki masaa yote? Kuna waheshimiwa wana makampuni ya uvuvi, tuseme wana uwezo mdogo kwa vile ni wavuvi?
Tishio la urais 2015, ni mtu atakayeweza kuwakamata vijana na kuwashawishi na kuwahamsisha maana vijana ni wengi na wanataka mabadiliko. Kama Mbowe ana uzoefu wa kuongoza kumbi za muziki, tena kumbi za kisasa ambaco hazina ajali ya vifo kama zile za Tabora kwa Sitta, basi huyu ni wa kuogopwa kwa wale wenye uchu wa urais, maana kuongoza kumbi za disko, Mbowe, atakuwa yuko karibu na vijana.
Sitta, anasahau kwamba watu wanafuatilia mijadala huko Bungeni; wanajua ni nani anatoa pumba na ni nani anajua kujenga hoja za kitaifa. Mbowe, amekuwa akijenga hoja na kufuatilia masuala muhimu kwa taifa bila kuelemea upande mmoja; amekuwa ni miongoni mwa wabunge wanaotembea na teknolojia. Wakati wabunge wengi wamekuwa wakiwasilisha hotuba zao kwa kulamba karatasi yeye anatumia teknojia ya kisasa ambayo si lazima kubebana na makaratasi.
Labda kama Sitta, ana chuki binafsi na Mheshimiwa Mbowe. Hoja za kutaka kutushawishi kwamba Mbowe si tishio, hazina mashiko. Kama anaamini kwamba Dr.Slaa ni tishio, maana yake ni kwamba Chadema ni tishio. Na kama Chadema ni tishio, basi anayetisha ni mwenyekiti anayekiongoza chama hicho.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 633122
www.karugendo.net
0 comments:
Post a Comment