HATUKO TAYARI KWA VITA YA NJE, TUPIGANE VITA YA NDANI KWANZA.
Mheshimiwa Lowassa na Mheshimiwa Membe wametoa tamko kali juu ya mgogoro wa mpaka kati ya Malawi na Tanzania, kwamba tuko tayari kwa vita. Sitaki kuingilia mjadala kwamba kazi ya kutangaza vita si ya waheshimiwa hawa hata kama kungekuwepo na ombwe la kutisha; Amiri jeshi yupo.Kutangaza vita na hali ya hatari ni kazi ya amiri jeshi mkuu na si vinginevyo. Hoja yangu kwenye makala hii ni maneno ya Mheshimiwa Lowassa na Mheshimiwa Membe kwamba Tanzania tuko tayari kwa vita; pamoja na ukweli kwamba wanaipatia diplomasia nafasi ya kwanza, hamu yao ya kutaka tuingie vitani ni lazima ihojiwe. Mimi na wengine wengi wanaojali, tunasema Tanzania hatuko tayari kwa vita ya nje, tupigane vita ya ndani kwanza. Kama Mheshimiwa Lowassa na Mheshimiwa Membe, wanafikiri vita ya nje ni muhimu watangulie mstari wambele wao, wake zao na watoto wao na kuachana na ndoto za kuliingiza taifa letu vitani.
Kuna sababu nyingi za Tanzania kutokuwa tayari kuingia vitani. Tamko la Mheshimiwa Lowassa na Mheshimiwa Membe, limetolewa bila kuwahoji watanzania. Tunajua sote kwamba tukiingia vitani watakao beba jukumu kubwa, watakaoteseka, watakaokimbia huku na kule na kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi, watakaokufa, watakaoumizwa na pengine kupata ulemavu wa kudumu ni wananchi wa kawaida na wanajeshi wetu na wala si hawa viongozi wa kisiasa wanaotoa tamko.Mara nyingi viongozi wa kisiasa wanaanzisha vita, hali ikiwa mbaya wanakimbilia nchi za nje. Ndo maana marehemu Ghadafi, ataendelea kuheshimika kwa kukubali kufia nchini mwake pamoja na uwezekano mkubwa wa yeye kukimbilia nchi za nje ulikuwa mkubwa; alikataa kukimbia kuacha nyuma yake vifo na mateso, akakubali afe akipigana. Ni wanasiasa wachache wenye roho kama hiyo ya Ghadafi. Wanawake na watoto ni kundi katika jamii linalopata machungu makubwa wakati wa vita. Ukweli huu unajionyesha kwenye nchi ambazo zimekuwa na migogoro ya vita mara kwa mara.
Siwezi kujua, labda Mheshimiwa Lowassa na Mheshimiwa Membe walijadiliana na wanajeshi wetu juu ya utayari wao wa kuingia vitani na Malawi. Nina mashaka makubwa kama waheshimiwa hawa wamepata nafasi ya kujadiliana na wanawake na wananchi wote wa Tanzania juu ya utayari wao wa kuingia vitani. Bila kujadiliana na wanajeshi; ambao ni Jeshi la Wananchi wa Tanzania, bila kujadiliana na wanawake ambao mara zote ndo wanabeba machungu ya vita kwa kuhakikisha usalama wa watoto, bila kujadiliana na wananchi wote juu ya utayari wao kuingia vitani, kutangaza vita ni kujitangaza Adui wa umma.
Sababu nyingine ambayo ni kubwa ya kutuzuia kuingia vitani ni umaskini wetu. Serikali yetu haina uwezo wa kuongeza mishahara ya walimu. Serikali yetu haina fedha ya kuongezea mishahara wa madaktari na kununua vifaa vingine vya hospitali. Serikali yetu haina fedha za kuendesha bajeti ya serikali kwa asilimia miamoja. Serikali yetu haina fedha za kununulia madawati, kujenga nyumba za walimu, kujenga vyoo, kununua vitabu na vifaa vingine vya kufundishia, itapata wapi fedha za kupigana vita na Malawi?
Watanzania tulishuhudia kilichotokea wakati wa vita ya Kagera. Vita isikie kwingine na si kwako. Wale waliokuwa wazima wakati ule, nina imani hawawezi kushabikia vita ya aina yoyote ile. Vita si kitu cha kushabikia kama wanavyofanya Mheshimiwa Lowassa na Membe. Pamoja na kwamba tuliishinda vita ya Kagera, Uchumi wetu haukutengamaa hadi leo hii. Hata wanajeshi walioumizwa wakati wa vita hiyo bado wanadai fidia yao hadi leo hii. Ukiweka kwenye mizani matokeo ya vita, ni vigumu kushabikia vita na hasa kama kuna nafasi ya kujadiliana na kumaliza mgogoro. Mipaka ya nchi zetu iliwekwa na wakoloni. Sisi wenyewe sasa hivi tunaimba umoja wa Afrika na umajumui wa Afrika. Tanzania inajulikana dunia nzima kuwa mstari wa mbele kupigania umoja wa Afrika. Muungano wa nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar pamoja na matatizo yake ni mfano wa kuigwa. Iweje leo hii tunatangaza vita kugombania Ziwa Nyasa? Kwa nini tusijadiliane na Malawi, jinsi ya kulitumia ziwa hili kwa pamoja? Huko nyuma, miaka mingi ya nyuma, babu zetu ambao hawakuishi kuushudia ukoloni walilitumia ziwa hili kwa pamoja; itakuwaje mipaka ya wakoloni ituzie kulitumia ziwa hili kwa pamoja? Na kwa upande wetu Tanzania, tumelitumiaje ziwa hili hadi leo hii? Watu wanaolizunguka wamesambaziwa maji kutoka kwenye ziwa hili? Tunalitumia ziwa hili kwa kilimo cha kumwagilia? Tunalitumia ziwa ili kuvua kisasa, kusindika samaki, kuwauza nje ya nchi na kuzalisha ajira? Tunalitumia ziwa hili kwa usafiri wa kisasa na kulitumia kwa utalii wa ndani na kuwavutia watalii kutoka nje? Au tunataka tulimiliki na kuishia kulitazama tu?
Ni wajibu wetu kupambana na adui wanaotisia usalama wa taifa letu. Hili wala halina mjadala. Kuna adui wa nje na adui wa ndani. Kwa maoni yangu wakati huu ninapoandika makala hii adui wa ndani wanatishia usalama wetu zaidi ya adui wa nje mfano hawa wa Malawi. Nguvu, hasira na uwezo wa kupambana na adui wanaouonyesha waheshimiwa Lowassa na Membe, utumike kupambana na adui wa ndani. Ni mchezo wa kuigiza kuonyesha Tanzania ina nguvu za kupigana vita na nchi jirani, wakati adui wa ndani wanaliteketeza taifa letu.
Tunao adui wengi wa ndani na baadhi wanajulikana kwa majina yao. Wameuza ardhi yetu kwa wawekezaji, wanauza rasilimali zetu na kujiwekea fedha mifukoni mwao au kuziweka kwenye mabenki ya nje.Tuna maadui wetu ambao wamekuwa wakihujumu uchumi wetu; tumeambiwa mgao wa umeme ulikuwa ni wa kutengenezwa na mgao huu umeliingiza taifa kwenye hasara kubwa na uchumi wetu umedorora kutokana na mgao wa umeme; fedha zinazolipwa kwa makampuni hewa ya umeme ni nyingi kiasi cha kushangaza: Wakati serikali yetu inatangaza kwamba haina fedha za kuwalipa walimu na madaktari, fedha nyingi zinatumika kuyalipa makampuni hewa ya umeme; Juzi tu amekamatwa mtu aliyekuwa na kampuni ya kuiba umeme, ameiba umeme kwa miaka saba! Inawezekana alikuwa akiiba bila kujulikana au alikuwa akishirikiana na aduni wengine wa taifa letu? Adui hawa wameliingiza taifa letu kwenye ufisadi na rushwa kubwa kama ile ya Rada. Mheshimiwa Membe, alitwambia anawajua waliohusika na rushwa hiyo ya rada na kwamba atawataja. Ameogopa kuwaja! Ameogopa! Huyu ndiye anataka tuamini anaweza kuongoza mapambano ya vita na nchi ya Malawi? Huyu ndiye ataweza kuiongoza Tanzania iliyotekwa na matajiri wenye fedha chafu? Rais tunayemtaka ni Yule ambaye ataweza kupambana na maadui wa ndani bila woga na bila kuwakumbatia hao maadui waliotufikisha hapa tulipo.
CCM ilitangaza vita ndani ya chama hicho.Ilitangaza vita ya kuvua gam ba. Maana yake ni vita ya kupambana na adui wa ndani. Vita hii imeshindwa kabisa! Mheshimiwa Lowassa na Mheshimiwa Membe, ni wanaCCM na wana nafasi ya juu ya kwenye chama chao. Kama chama chao kimeshindwa kupambana na adui wa ndani,wataweza kutushawishi kwamba wanaweza kuongoza vita ya nje? Kwa nini tusiamini kwamba ni mpango wao wa kutaka tuingia vitani na Malawi ili akili yetu yote iwe kwenye vita na kupiga kisogo “uchafu” unaoenelea kwenye taifa letu. “Uchafu” unaosabaishwa na CCM? Hizi ni mbinu ili tusahau ya Ulimboka, tusahau ya Richmond, Dowans, tusahau serikali kuitumia mahakama kama chombo cha kuzima sauti za wanyonge, tusahau serikali kuingilia uhuru wa vyombo vya habari, tusahau migono ya walimu wa madaktari, tuiweke akili yetu yote kwa vita ya Malawi.
Mheshimiwa Lowassa na Mheshimiwa Membe ni miongoni mwa wale wanaotajwa kutaka kugombea Urais 2015. Je hizi si mbinu za kutaka kutafuta umaalufu? Au mbinu za kutaka kukusanya fedha za kutosha kuwasaidia wakati wa uchaguzi? Inaaminika kwamba matumizi ya Jeshi na hasa kama ni wakati wa vita hayahojiwi! Baadhi ya viongozi wa Afrika wamekuwa wakitumia vita kama “kichaka” cha kujikusanyia fedha. Kuna mfano wa Uganda, batalioni moja iliyokuwa kule DRC, ikipigana, kipangiwa bajeni ya vifaa vya kivita, posho na mishahara ya wanajeshi na matumizi mengine mengi, haijaonekana hadi leo hii. Si kwambwa batalioni hiyo ilifyekwa hadi mtu wa mwisho, ilikuwa batalioni hewa!
Yawezekana mgogoro wa mpaka wa Malawi ni mbinu za kuingilia mchakato wa Kuandika katiba mpya? Ili tuingie kwenye uchaguzi tukiwa na katiba ya zamani au ikiwezekana uchaguzi ukasogezwa mbele? Tukiingia vitani, vitu vingi vitasimama. Uzoefu wa vita ya Kagera ulitufundisha. Inawezekana pia na uchaguzi wa 2015, ukasongezwa mbele ili CCM ipate nafasi ya kujijenga na kujisafisha na labda kutumia ushindi wa vita kama silaha ya kujigamba na kuonyesha kwamba bado chama kina nguvu na uwezo wa kuendelea kuiongoza Tanzania.
Tumeambiwa kwamba kuna makampuni yanafanya utafiti wa kuchimba mafuta kwenye ziwa Nyasa. Makampuni haya ni ya nani? Haiwezekani ni makampuni wa watanzania ambao baada ya kuona hawawezi kuiba mafuta haya kutoka upande wa Tanzania, wameibua mgogoro wa mpaka ili ziwa lirudi upande wa Malawi; wapate mwanya mzuri wa kuiba mafuta haya kutokea upande mwingine? Kama watanzania waliweza kusomba nguzo za umeme kutoka Mfindi, zikaenda Mombasa na baadaye sikarudishwa hapa kama mzigo unaotoka nchi za nje Afrika ya kusini na Ulaya, watashindwa kujigeuza kuwa ni makampuni ya Malawi yanafanya utafiti wa mafuta kwenye ziwa Nyasa ,kumbe ni watanzania wale wale?
Mgogoro wa Tanzania na Malawi, ni lazima uangaliwe kwa umakini mkubwa. Hakuna sababu za kutosha kutuingiza vitani hata kama tunalipoteza ziwa lote; umoja wa Afrika, umajumui wa Afrika na usalama, amani ya wananchi ni muhimu zaidi ya kulipata ziwa lote la Nyasa. Kama kuna dalili za kisiasa ndani ya mgogoro huu, utakuwa mgogoro mkubwa zaidi ya kutanvyofikiria. Tanzania ina watu wenye uchu wa madaraka kiasi cha kutojali matokeo ya vita; wako tayari kutumia mbinu zote; chafu na nzuri ili waingie madarakani.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 6331 22
www.karugendo.net
0 comments:
Post a Comment