Uchambuzi wa Kitabu cha Azimio la Arusha

UCHAMBUZI WA KITABU: AZIMIO LA ARUSHA.


1. Rekodi za Kibibliografia.

Jina la kitabu kinchohakikiwa hapa ni Azimio la Arusha na Siasa ya Tanu Juu ya Ujamaa na Kujitegemea.Kilitolewa na idaraya ya Habari ya TANU, Dar-es-salaam 1967. Kilipigwa chapa na kiwanda cha Uchapishaji cha Taifa. Kijitabu hiki kina kurasa 40, na anayekihakiki hapa ni Mimi Padri Privatus Karugendo.

11. Utangulizi

Tunakumbuka kifo cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa letu la Tanzania. Na mwaka huu, ni wa uchaguzi mkuu. Hivyo ni bora kujikumbusha mawazo ya Mwalimu kupitia kwenye maandishi yake na hasa hoja yake nzito iliyojipenyeza kupitia kwenye kitabu hiki kidogo cha Azimio la Arusha, ambacho yeye alikifananisha kama msahafu au ndugu yake na msahafu, maana alisema daima alitembea na vitabu hivyo viwili; Biblia na Kijitabu hiki cha Azimio la Arusha.

Kitabu hiki kimegawanyika katika sehemu kuu tano. Sehemu ya kwanza inaongea juu ya Imani ya TANU, Sehemu ya pili inaongea juu ya Siasa ya Ujamaa. Sehemu ya tatu inaongea juu ya siasa ya Kujitegemea. Sehemu ya nne inaongea juu ya uanachama na sehemu ya tano ndiyo inaongea juu ya Azimio la Arusha.

111. Mazingira yanayokizunguka kitabu

Baada ya Uhuru kulikuwa na changamoto nyingi kwa nchi changa za Afrika. Mapinduzi ya kila mara yalikuwa yakizikumba nchi hizi. Ubeberu ulikuwa ukikodolea macho Afrika, na wakoloni walitaka kuendendelea kuitawala Afrika utokea mbali. Wakati huo kukiwa na pande mbili zinazopingana. Upande wa mabepari ukiongozwa na nchi za Ulaya Magharibi na Amerika na Ukomunisti ukiongozwa na Urusi na China. Tanzania kwa kuamua siasa ya ujmaa, ilijikuta inawekwa kwenye kapu la wakomunisti, ingawa msimamo wa Mwalimu Nyerere ulikuwa wazi wa siasa za kutofungamana na upande wowote.

Viongozi wa Afrika walikuwa na uchu wa mali, na kutaka kuishi maisha kama ya wakoloni. Walitaka mishahara mikubwa, walitaka kuwa na hisa kwenye makampuni na walitaka kufanya biashara.

Mwaimu Nyerere, aliona hatari ya kuruhusu viongozi kuiga maisha ya wakoloni waliofukuzwa. Alifikiri njia pekee ya kuwahakikisha Tanzania, inaendelea kwa pamoja kwa kuwainua watu wa chini ni kuanzisha mfumo wa kuongoza mapambano hayo. Azimio la Arusha lililenga kujenga na kusimika Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea katika Taifa letu.

Azimio la Arusha, halikupata mafanikio makubwa, kwa vile halikuungwa mkono na watu wengi. Walio wengi walifanya kazi ya unafiki. Hawakufuata Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea kutoka moyoni. Hivyo juhudi zote za Azimio la Arusha, za kutaifisha njia kuu zote za uchumi kuwa mikononi mwa Umma, kwa kuanzisha Mashirika ya Umma, zilishindwa vibaya sana na uchumi ulididimia.

Bila mjadala wa Kitaifa Azimio la Arusha, lilikufa na kuzikwa kule Zanzibar. Kilichofuata hapo si Ubepari – bali Ubeberu wenye kunakishiwa na Utandawazi. Kilio cha leo ni kwamba turudishe saisa ya Ujamaa na Kujitegemea!

1V. Muhtasari wa Kitabu.

Sehemu ya kwanza ya kitabu hiki inaeleza Juu ya Imani na Madhumuni ya TANU. Imani zote ni muhimu, lakini kwa uzito wa uchambuzi huu ni bora tukataja ya (h) na (i) ambazo zinasema hivi; “ Kwamba ili kuhakikisha kuwa uchumi wa nchi unakwenda sawa. Serilai lazima iwe na mamlaka kamili juu ya njia muhimu za kuuza uchumi; na Kwamba ni wajibu wa Serikali, ambayo ni watu wenyewe kuingilia kati kwa vitendo maisha ya uchumi ya Taifa ili kuhakikisha usitawi wa raia wote na kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine au kikundi kimoja kunyonya kikundi kingine na kuzuia limbikizo la utajiri kufikia kiasi ambacho hakipatani na siasa ya watu wote kuwa sawa” (uk 2).

Na sehemu hii naungana na sehemu nyingine upande wa Madhumuni ya TANU, inayosema hivi: “ Kuona kwamba Serikali ya nchi yetu inasimamia barabara njia kuu za kuzalisha mali na inafuata siasa ambayo itarahisisha njia ya kumiliki kwa jumla mali za nchi yetu” (uk.4)

Sehemu ya pili ya kitabu hiki inaelezea juu ya Siasa ya Ujamaa: Kwamba katika Siasa ya Ujamaa hakuna Unyonyaji; “ Nchi yenye Ujamaa kamili i nchi ya wafanyakazi: Haina ubepari wal ukabaila. Haina tabaka mbele za watu: tabaka ya chini ya watu wanaoishi wka kufanya kazi, na tabaka ya juu ya watu wanaoishi kwa kufanyiwa kazi...” (uk.5)

Kwamba kwenye ujamaa njia kuu za uchumi ziko chini ya wakulima na wafanyakazi; “ Namna ya pekee ya kujenga na kudumisha ujamaa ni kuthibitisha kuwa njia kuu zote za uchumi wa nchi yetu zinatawaliwa na kumilikiwa na wakulima na wafanyakazi....” (uk.6)

0 comments:

Post a Comment