AFRICARE NA MCHANGO WAKE KATIKA JAMII: TANZANIA.( 1)
AFRICARE, ni shirika lisilokuwa la kiserikali, la kimataifa linalofanya kazi zake dunia nzima na linajishughulisha na maswala ya kijamii. Shirika hili linafanya kazi pia hapa Tanzania, makao makuu yakiwa Dar-es-Salaam na matawi yake kule Manyara, Mara, Mwanza, Iringa, Dodoma nk.
Mwandishi wa makala hii amebahatika kufanya kazi na AFRICARE kwenye miradi miwili tofauti. Mradi wa kwanza ulikuwa ni utafiti juu ya Huduma Majumbani katika mikoa ya Manyara na Mara; utafiti ulifanyika mwaka jana mwezi wa sita. Na mradi wa pili ni ule Changamoto za Milenia wa kusogeza huduma ya umeme katika mikoa sita ya Tanzania bara; Tanga, Morogoro, Iringa, Dodoma, Mbeya na Mwanza, kazi iliyofanyika kwezi Januari na Februari mwaka huu.
Lengo la makala hii ni kuishukuru AFRICARE kwa mchango wake katika jamii ya watanzania. Mbali na huduma za moja kwa moja wanazoelekeza kwa walengwa wao kule vijijini; kuna huduma nyingine zisizokusudiwa moja kwa moja kama kuwawezesha watafiti na wafanyakazi wake wa muda mfupi kupata fursa hadimu ya kuitembelea mikoa mbali mbali ya Tanzania. Huu ni mchango mkubwa maana kama mtu angeamua binafsi kuizungukia mikoa hiyo, angetumia gharama kubwa na wakati mwingine haiwezekani. Kwa wengine fursa hii inakuwa ni kibarua cha kupata fedha na aina Fulani ya utalii wa ndani. Kwa mwandishi, mchambuzi na mchokonozi, hii ni fursa hadimu ya kuchota mengi na kuyasambaza kwa manufaa ya watanzania wote.
Matokeo ya utafiti wa Huduma Majumbani, ni jukumu la AFRICARE, kuyaweka wazi. Makala hii, si taarifa rasmi ya utafiti ule, bali ni maoni ya mwandishi aliyepata bahati ya kufanya kazi na AFRICARE. Bahati hii ya kuzunguka mikoa minane: Manyara, Mara, Tanga, Mbeya, Morogoro, Iringa, Dodoma na Mwanza; itunufaishe wote kwa kupata habari na kujifunza mambo mapya kutoka mikoa hii.
Hivyo makala hii itakuwa na sehemu mbili kuu; kwanza ni utafiti wa Huduma majumbani uliofanyika mwaka jana kwenye mikoa miwili na sehemu ya pili itakuwa juu ya Mradi wa Changamoto za Milenia wa kusogeza huduma ya Umeme vijijini.
HUDUMA MAJUMBANI: MAFANIKIO NA CHANGAMOTO
Hadi leo hii mwongozo wa Serikali kuhusu Huduma Majumbani ni ule uliotolewa mwaka 2005. Hata hivyo serikali iko mbioni kutoa mwongozo mwingine. Ni matumaini yetu kwamba mapungufu na changamoto zinazojitokeza kwenye huduma hii zitapata majibu chanya kwenye mwongozo mpya.
Huduma Majumbani, ni huduma inayowalenga wagonjwa wenye magonjwa ya kusendeka. Magonjwa haya ni kama vile Kifua Kikuu, Kisukari, kifafa na Ukimwi. Serikali kwa kushirikiana na mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali imekuwa ikijitahidi kuhakikisha huduma hii inawafikia walengwa.
Kwa kutumia wahudumu wa Kata, ambao kwa kawaida ni kumi na na wanne huduma hii imekuwa ikisambaa hadi vijijini na kwenye kaya zenye wagonjwa wanaosumbuliwa na magonjwa ya kusendeka. Huduma hii ambayo ni pamoja msaada wa kisaikolojia na kijamii, unasihi na ufuasi, ushauri nasaha, habari za virusi na ukimwi, msaada wa kisheria, elimu ya lishe, elimu ya usafi, elimu ya miradi ya kukuza na kuongeza kipato, elimu ya uzazi wa mpango, kuzuia maambukizo kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, rufaa kwenda vituo vya afya, rufaa ya kujiunga na vikundi vya watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi, rufaa kwenda kwenye Mashirika yanayotoa misaada, imekuwa ikitolewa na wahudumu wa kata wakishirikiana na wahudumu wa msingi kwenye kaya.
Utafiti uliofanyika mwezi wa sita mwaka jana kwa lengo la kutathimini utoaji huduma majumbani katika Mikoa ya Manyara na Mara ulibaini mafanikio na changamoto katika huduma hii. Mwandishi wa ripoti hii alishiriki kikamilifu kwenye utafiti huu uliochukua muda siku kumi na nne. Kwa kuheshimu matakwa ya walioshiriki utafiti huu; wahojiwa na wadodosaji, sitataja majina. Nitaelezea mafanikio na changamoto na ikibidi kutaja maeneo.
Katika Mkoa wa Manyara, utafiti ulifanyika katika wilaya za Babati Mjini na Babati Vijijini, Hanang, Simanjiro na Mbulu. Babati Mjini zilitembelewa kata za Babati mjini, Bagara na Bonga. Babati vijijini zilitembelewa kata za Galapo, Magugu na Mamire. Kwa upande wa wilaya ya Hanang, kata zilizotembelewa ni Katesh, Nangwa, Ganan na Endasaki. Wilaya ya Simanjiro, utafiti ulifanyika katika kata za Orkesumet, Mererani na Emboret. Na Wilaya ya Mbulu, utafiti ulifanyika katika kata za Mbulu Mjini, Daudi na Haidom.
Mkoa wa Mara, utafiti ulifanyika katika wilaya za Musoma mjini, Musoma Vijijini na Rorya. Musoma mjini kata zilizotembelewa ni Makoko, Nyasho na Nyakato. Upande wa Musoma vijijini, zilitembelewa kata za Kiriba, Kukirango na Suguti. Wilaya mpya ya Rorya, zilitembelewa kata za Korio, Nyamtinga na Nyamunga.
Katika kata zote zilizotajwa, walengwa walihojiwa kwa kutumia dodoso la kaya, dodoso la mlengwa na baadaye kulikuwa na mikutano ya majadiliano na walengwa, wahudumu wa msingi na wahudumu wa Kata. Pia yalifanyika majadiliano na wakuu wa vituo vya afya vya serikali na vya kidini.
Mafanikio makubwa yaliyojitokeza kwenye wilaya zote tulizozitembelea ni huduma ya dawa. Wagonjwa wa magonjwa ya kusendaka wanapata dawa. Kwa wale wanaoishi na virusi vya UKIMWI, wamepata afya tena na wanaweza kufanya kazi. Ni matukio machache sana tulipomkuta mgonjwa amelala. Na pia ni matukio machache tulipomkuta mgonjwa wa VVU, kuugua ndani ya miezi mitatu kiasi cha kushindwa kufanya kazi.
Mafanikio mengine ni mafanikio ya mfumo wa huduma majumbani kuanzia Wilayani kwenda kwenye vituo vya Afya kupitia kwa mhudumu wa kata kwenda hadi kwenye wahudumu wa msingi na hatimaye kumfikia mlengwa. Ingawa kuna kasoro za hapa na pale, mfumo umesukwa vizuri.
Pia elimu ya unasihi na ufuasi, elimu ya ushauri nasaha, elimu ya lishe na usafi, elimu ya kujikinga na Virusi vya Ukimwi, elimu ya unyanyapaa, imeenea hadi vijijini. Haya ni mafanikio makubwa sana na ya kupongezwa.
Ushirikiano wa serikali na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali ni mafanikio makubwa maana uhai wa mwanadamu ni kazi yetu sote na ni lazima vita dhidi ya adui anayetishia uhai wetu tupambane kwa pamoja. Mashirika mengi yamejitokeza kutoa misaada ya kufanikisha mpango wa huduma majumbani.
Watu wengi tulioongea nao walikuwa wamepima afya zao. Wengine wamepima na kutoa majibu kwa ndugu, jamaa na marafiki, na wengine wamepima na imebaki ni siri yao. Tulichoambiwa ni kwamba wahudumu wa huduma majumbani wamefanya kazi kubwa ya kuwashawishi na kuwaelekeza kwenda kupima.
Kuna vikundi mbali mbali vya walengwa wanaoishi na virusi vya UKIMWI vilivyoanzishwa kwa lengo la kusaidiana kiuchumi, kuhimizana kufuata ratiba ya dawa, kufarijiana, kuelimishana na kushirikiana kupambana na unyanyapaa. Vikundi hivi vimesaidia pia utekelezwaji wa huduma majumbani na vimekuwa vikiungwa mkono na mpango huo wa Huduma Majumbani.
Kila mhudumu wa Kata, anapata mfuko wa dawa (Kit) , hivyo anaweza kuwasambazia dawa wagonjwa wasiokuwa na uwezo wa kusafiri kufika kwenye vituo vya afya. Pia mhudumu huyu anasaidia kuwaibua wagonjwa wengine na kuwaorodhesha ili wapate huduma..... Itaedelea.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0754 633122
pkarugendo@yahoo.com
www.karugendo.com
0 comments:
Post a Comment