AFRICARE NA MCHANGO WAKE KATIKA JAMII: TANZANIA.( 3)
Baadhi ya vituo vya afya viko mbali na walengwa. Hii ni changamoto kubwa kwa wahudumu wa huduma majumbani. Lakini pia kuna swala zima na dawa za magonjwa nyemelezi. Serikali inatoa bure za kurefusha maisha kwa wagonjwa wanaoishi na virusi vya UKIMWI na wale wenye magonjwa mengine ya kusendeka. Upatikanaji wa dawa za magonjwa nyemelezi linabaki ni jukumu la mgonjwa mwenyewe. Kama dawa hizo hazipatikani kwenye Zahanati au vituo vya afya vya serikali unakuwa mzigo mkubwa kwa mgonjwa. Wahudumu wa kata, walilalamikia swala hili na kupendekeza kwamba serikali itoe pia huduma ya magonjwa nyemelezi kwa wagonjwa wenye magonjwa ya kusendeka.
Maambukizi mapya ni changamoto kubwa katika mpango mzima wa huduma majumbani na harakati za kupunguza kuenea kwa virusi vya Ukimwi. Kata ya Mererani, ni mfano mzuri. Wanaapolo, wakitoka machimboni na kujipumzisha kwenye mji mdogo wa Mererani na hasa maeneo ya Burudani kama vile Songambele, wanakuwa na kazi moja: Kupumzika na kustarehe. Wanakuwa na fedha na wanakuwa na uhakika wa kupata fedha nyingine kwa muda mfupi. Hivyo wanaitumia fedha: Wanakunywa pombe, wanatumia madawa ya kulevya na kufanya mapenzi. Tulishuhudia mirungi ikiuzwa waziwazi.
Binti, mhudumu wa kwenye Bar pale Songambele, alituelezea huku machozi yakidondoka; “ Wanaapolo wana fedha kweli. Wao kutoa laki tatu hadi tano si kitu, lakini sharti lao ni moja tu, kufanya mapenzi bila kinga. Umaskini wetu unatuponza. Mimi nikipata virusi vya UKIMWI, nitalaumu umaskini wa nchi yangu na serikali yetu inayoshindwa kupambana na Umasikini. Nikifikiria kulipa kodi ya nyumba, kulipa karo ya mtoto, kuwatunza baba na mama yangu, nashindwa kupambana na kishawishi cha wanaapolo.... nazipokea fedha zao na kusubiri matokeo!”
Mifano kama ya binti huyu ni mingi pale Mererani. Wanaapolo wanakwenda mbali hadi kuzisambaratisha familia za Mererani. Wanatumia nguvu ya fedha kuwarubuni wanawake na kuhakikisha wanawatenga na waume zao. Si kweli kwamba kila mwanaapolo ana virusi vya UKIMWI, lakini katika mfumo huu wa kufanya mapenzi kwa jeuri ya fedha ni vigumu kuhakikisha usalama wa wale wanaopenda kujikinga na maambukizo ya virusi vya UKIWMI.
Watoto wa kike na hasa wale wanasoma Sekondari za kutwa wanajikuta katika wakati mgumu. Tatizo la usafiri, maisha magumu kwenye familia zao, vishawishi vya kuishi maisha ya kileo: kutengeneza nywele na kuwa na simu za kisasa vinawasukuma kuzikubali fedha za Tanzanite. Matokeo yake ni mimba za utotoni, kukatisha masomo na kuanza kufanya kazi kwenye Nyumba za starehe pale Mererani. Mabinti wadogo tuliohojiana nao pale Mererani na ambao ni walengwa, wana historia ya kusikitisha. Wanaambukizwa katika umri mdogo na vurugu za Mererani haziwezi kuwaruhusu kujikinga na maambukizi mapya.
Umasikini umetajwa pote, Manyara na Musoma, kama changamoto kubwa kwa maambukizi ya UKIMWI. Maana imejidhihirisha wazi kwamba kuna wanaoanguka kwenye mtego kwasababu ya umasikini. Yule binti wa Mererani alitwambia kwamba akiambukizwa virusi vya UKIMWI, ataichukia serikali yetu inayoshindwa kupambana na umaskini. Wakati wa utafiti wetu tulitafakari sana juu ya swala hili la umasikini na kushindwa kuelewa ni kwa nini Tanzania ni masikini hivyo na watanzania tunaamini kwamba sisi ni masikini.
Wakati tunatoka Mererani kwenda Arusha, tulipitia ile njia ya kutokea Kijenge. Tulishuhudia ardhi nzuri na yenye rutuba, mashamba mazuri na makubwa yenye mfumo wa umwagiliaji. Mashamba ya kahawa ambayo sasa hivi yanabadilishwa kuwa mashamba ya maua. Tulielezwa kwamba maua haya yanauzwa nchi za nje na kuingizia Tanzania fedha za kigeni. Tulishuhudia idadi kubwa akina mama walioajiliwa kwenye mashamba haya ya maua wakitoka kazini kuelekea kwenye majumba yao. Ni imani yetu wanalipwa mshahara, labda kama ni ule wa kima cha chini unaolalamikiwa na chama cha wafanyakazi wa Tanzania.
Tulipokwenda Babati, Hanang na Mbulu, tulishuhudia pia mashamba makubwa na ardhi nzuri na yenye rutuba. Mbali na utajiri wa madini ya Mererani, Mkoa wa Manyara una utajiri mkubwa. Kilimo peke yake ni utajiri mkubwa ambao unaweza kuinua kipato cha Tanzania nzima. Mtu unabaki kushangaa, zimwi hili la umasikini linatoka wapi?
Safari ya kwenda Musoma, tulikatisha katika mbuga za wanyama; Ngorongoro na Serengeti. Tulishuhudia magari ya watalii yakiingia na kutoka kwenye mbuga hizi za wanyama. Ni wazi watalii hawa wanaingiza fedha nyingi kwenye mfuko wa taifa. Kila anayekatisha mbuga za wanyama ni lazima kulipa. Hata sisi tulilipa. Hizi fedha zinakwenda wapi? Kwa nini zisichangie kupunguza au kulitokomeza zimwi hili la umasikini wa Tanzania?
Wakati Mkoa wa Manyara ,kuna tishio la Wanaapolo na jeuri ya fedha katika kufanya mapenzi kuhusiana na maambukizi ya virusi vya UKIMWI. Mkoa wa Mara unatishiwa na utamaduni wa mfumo dume kwa upande mmoja na utamaduni wa Nyumba ntobu kwa upande mwingine. Ni vyema kutaja hapa kwamba Unyanyapaa uko juu sana mkoa wa Mara. Uwazi wa mtu kujitaja kwamba ana virusi vya Ukimwi tulioukuta Manyara, ni mdogo sana kule Mara. Walengwa wengi wa Mara, walitaja magonjwa ya kisukari, kifua kikuu na kuogopa kutaja UKIMWI, ingawa baadaye tuligundua kwamba karibia wote tuliohojiana nao walikuwa wakitumia madawa ya kurefusha maisha. Wanaogopa kujitangaza, wasitengwe na jamii. Ugonjwa huu wanauangalia kama laana na kwamba ni ugonjwa wa aibu. Elimu juu ya ugonjwa huu bado inahitaji katika Mkoa wa Mara.
Mfumo dume wa Mkoa wa Mara, ni kwamba baadhi ya wanaume wanapima afya zao kwa siri. Wakigundua wana virusi, wanaendelea kufanya tendo la ndoa na wake zao bila kinga. Lakini hata pale ambapo wanawake wanafanikiwa kufahamu hali ya afya ya waume zao, wanaume wanakataa kutumia kondomu. Wanawake hawana uamuzi juu ya afya zao na maisha yao. Huo ndio mfumo dume ambao unatishia juhudi za huduma majumbani.
Nyumba ntobu, utamaduni wa wanawake kuoa. Nao ni tishio kubwa. Mwanamke anaoa binti, anamtolea mahari, huyu binti anakuwa hana uhuru wa kufanya mapenzi na mwanaume anayemtaka. Mwenye uamuzi ni yule mwanamke aliyetoa mahari. Hivyo anaweza hata akaamua binti afanye mapenzi na mtu mwenye virusi vya UKIMWI, kama huyo mtu hajapima au amepima lakini ana mali nyingi. Utamaduni huu bado unaendelea katika Mkoa wa Mara na ni hatari kwa juhudi zinazofanyika za kuzuia maambukizi ya UKIMWI. Mfumo ambao unamzuia mtu kufanya uamuzi juu ya afya yake na maisha yake ni hatari kabisa kwa uhai wa mwanadamu.
Kwa kuhitimisha tunapendekeza Serikali iendelee na mradi huu wa Huduma Majumbani. Lakini pia Serikali iwasikilize walengwa. Kilio chao cha kuomba chakula kisikilizwe, kilio chao cha kuomba mitaji kifanyiwe kazi. Kilio cha kuomba usafiri kwenye vituo vya afya kishughulikiwe. Hakuna mashaka kwamba Serikali yetu inaweza kuyatekeleza yote haya. Mfano yale mabilioni ya Kikwete, kwa nini yasielekezwe kwa watu hawa ambao ugonjwa uliwanyang’anya mtaji wao na sasa dawa za kuongeza nguvu zimewarudishia uhai na nguvu na wako tayari kuchapa kazi. Kwa nini serikali isiwapatie mitaji kupitia usimamizi wa programu hii ya Huduma majumbani?
Pia ni muhimu Serikali kuyaelekeza mashirika ya yasiyokuwa ya kiserikali na hasa yale yanayotoka nje ya nchi ni maeneo gani yanahitaji huduma. Kuna hatari ya mashirika mengi kuelekeza huduma zao kwenye maeneo yale yale. Na inawezekana mashirika yakatoa huduma isiyokuwa kipaumbele cha walengwa. Kama walengwa wanahitaji mitaji, wanahitaji chakula, wanahitaji karo kuwasomesha watoto wao, wasipatiwe vipande vya sabuni na sukari. Asilimia kubwa ya bajeti ya mashirika haya ielekezwe kwa walengwa. Matumizi ya mashirika haya ya kununua magari na kuyatunza, kulipa mishahara ya watumishi, kuendesha semina na mengine mengi ni makubwa ukilinganisha na huduma inayotolewa kwa walengwa. Labda ndio maana walengwa wanalalamika na kudai kwamba wanafanywa mitaji?
Hapa ni mwisho wa sehemu ya kwanza juu ya miradi miwili ya AFRICARE, ambayo mwandishi wa makala hii alishiriki. Makala ifuatayo itaelezea juu ya mradi wa pili wa kusogeza huduma ya umeme vijijini.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment