MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA RAI 2005.
UKUAJI WA UCHUMI KWA AJILI YA NANI?
Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa uchumi wa Tanzania umeendelea kukua kwa kasi nzuri kwa kipindi cha muongo mmoja sasa. Kwa mfano, mwaka 1996, uchumi ulikuwa kwa asilimia 4.2, mwaka 1999 asilimia 4.7, 2001 asilimia 5.7, 2002, asilimia 6.2 na kufuatia hali mbaya ya hewa mwaka 2003 kasi ya ukuaji uchumi ilipungua na kukuwa kwa asilimia 5.6. Mwaka 2004 ulipanda tena na kukua kwa asilimia--------. Hii ni dalili njema kabisa na matarajio ni kwamba ukuaji huu utakuwa zaidi na zaidi.
Kwa upande mwingine, mfumuko wa bei umeshuka kwa kasi sana. Ulishuka kutoka zaidi ya asilimia 16 Desemba 1997 na kufikia asilimia 6.0 Novemba 2000 na kushuka zaidi hadi kwenye asilimia 4.5 kwa wastani hadi sasa. Hii tena ni dalili njema kabisa kwa kuwa hakuna atakayependa kuwekeza pesa zake katika uchumi ambao mfumuko wa bei unakimbilia asilimia 100.
Pamoja na jitihada hizi nzuri bado tunaambiwa kwamba ukuaji huu haujaweza kupunguza umasikini kwa kasi nzuri. Tunaambiwa ili umasikini uweze kupungua inatakiwa uchumi ukue kwa asilimia 8-10. Hii ni changamoto kweli kweli. Jambo moja la msingi ni kwamba ukuaji huu wa uchumi umekwenda sambamba na ongezeko la pengo la matajiri na masikini. Kwa mfano, takwimu zinaonyesha kwamba asilimia 20 ya matajiri kati ya Watanzania wote katika mwaka 2001 ilitumia kiasi cha asilimia 44 ya matumizi yote ya kaya ikilinganishwa na asilimia 43 mwaka 1991. Kukua kwa uchumi kunakoambatana na kuongezeka kwa pengo la walio nacho na wasio nacho pia kunaonyeshwa na kipimo kiitwacho Gini ambacho kwa Tanzania kilionyesha kuongezeka toka 0.34 hadi 0.35. Kadiri tarakimu inavyokuwa ndivyo pengo linavyozidi kukua. Kwa mfano jamii ambayo mgawanyo wa pato una uwiano mzuri sana tarakimu hii hupungua na kuwa ndogo na jamii au nchi yenye mgawanyo mbovu huwa ni kubwa sana. Kwa mfano tarakimu hii ikiwa 0 ni kwamba wote mnagawana pato sawasawa na ikiwa 1 inawezekana mtu mmoja anakuwa na pato lote. Kwa kawaida haiwezekani kwa tarakimu hii iwe 0 au 1. Hata Swaziland ambapo mfalme Muswati anaweza kuamka asubuhi na kununua Magari 12 ya kifahari au akafanya sherehe ya siku ya kuzaliwa kwake kwa kutumia mamilioni ya fedha bado tarakimu hii haiwezi kuwa na thamani ya namba 1. Kwa upande mwingine kwa mfano, Cuba ambapo kuna uwiano mzuri sana wa mgawanyo wa pato bado hawawezi kuwa na tarakimu yenye alama ya 0. Nchi za Afrika ya Kusini na Brazil kwa mfano ni kati ya nchi zenye mgawanyo ulio mbovu kabisa duniani licha ya kuwa na chumi bora na pato la wastani la kila mtu kuonekana kubwa zaidi ya nchi nyingi za Afrika. Ukiangalia utaona kwamba katika Afrika ya kusini, watu weupe ambao ni asilimia 14 wanamiliki asilimia 88 ya mali zote binafsi na asilimia 86 iliyobaki inamiliki asilimia 12 iliyobaki. Tukiiweka kwa lugha nyingine, kama ukiweza kuigawa Afrika ya Kusini iwe mataifa mawili; moja la weupe na lingine la weusi, basi lile la weupe litashika namba ya 24 katika utajiri duniani wakati la weusi litakuwa la 125. Lakini kwa pato la wastani wa kila mmoja nchi kama hii huhesabiwa ni ya kipato cha kati. Ili lugha ieleweke kirahisi, wastani wa pato la kila mmoja hupatikana baada ya kujumlisha pato la taifa na kuligawa kwa idadi ya watu wa nchi ile. Ina maana kwamba kila mwananchi anahesabika kuwa na mmiliki wa chochote kilichozalishwa katika uchumi kwa huo mwaka.
Dalili hii ya kukukua kwa uchumi na wakati huo huo kuongezeka kwa pengo la matajiri na masikini, inaendana na ubashiri wa Mchumi maarufu wa Urusi Simon Kuzinet ambaye alibashiri kwamba kadiri nchi zinavyoendelea mgawanyo wa pato huwa hauko sawia na huenda usawa ukaongezeka baadaye kadri pato la nchi linavyozidi kukua.
Kwa Tanzania, kinacholeta mchanganyiko huu wa kutopungua umasikini wakati ambapo uchumi umekuwa, ni ukweli kwamba, ukuaji wa uchumi kwa miaka 10 iliyopita haujagusa sekta kiongozi. Sekta ya kilimo. Sekta inayoimbwa kila siku kwamba ndio uti wa mgongo wa taifa letu. Licha ya Sekta ya Kilimo kuchangia kiasi cha asilimia 45 katika pato la taifa, asilimia 85 ya mauzo ya nje na kuajiri asilimia 80 ya Watanzania wote katika mwaka 2004; ukuaji wa sekta hii umeonyesha dalili za kuzorota kwa kipindi cha miaka ya karibuni. Kwa mfano, sekta hii ilikuwa kwa silimia 5.5 mwaka 2001, asilimia 5.0 mwaka 2002 na asilimia 4.0 mwaka 2003. Hii inaonyesha kwamba vipato vya asilimia 80 ya waajiriwa wa sekta hii vimekuwa havikuwi kwa miaka mitatu, hivyo kutilia mashaka kama umasikini unaweza kupungua miongoni mwa watu hao.
Sekta ambayo imekuwa kwa kasi ni ya madini ambayo inaonyesha kwamba imekuwa toka asilimia 13.5 mwaka 2001 hadi asilimia 15.0 mwaka 2002 na asilimia 17.0 mwaka 2003. Hapa kuna swali la kujiuliza? Je sekta ya madini inakuwa kwa gharama za kufifisha sekta ya kilimo? Kwa jibu rahisi ni kwamba sekta ya madini ni mpya na imekuwa ikipata wawekezaji wengi siku za karibuni. Tatizo kubwa la sekta kama ya madini hasa katika nchi za Afrika ambazo husafirisha madini ghafi ni kwamba, haizalishi ajira zinaozikidhi haja na ambazo zingesaidia kupunguza umasikini kwa kasi. Hii inatokana na ukweli kwamba madini ghafi hupelekwa nje ya nchi na kukatwa katika maumbo mbalimbali tayari kwa uuzaji. Hivyo, sekta hii haina uhusiano wa karibu na sekta ya viwanda katika nchi zinazozalisha na kusafirisha madini ghafi. La pili ni kwamba sekta hii hutumia zaidi mashine za gharama kubwa kuliko watu kwa hivyo ajira inayozalishwa pia ni ndogo. Nchini Botswana kwa mfano ambako asilimia kubwa ya pato la Taifa hutokana na madini, kuna tatizo kubwa la ajira licha ya sekta hii kuzalisha kwa tija ya hali ya juu. Lakini kutokana na usafirishaji madini ghafi hakuna namna ambavyo inaweza kuzalisha ajira zaidi ukiondoa wachache wanaoajiriwa migodini. Matokeo yake ni kwamba, licha ya nchi hii kuwa na idadi ndogo sana ya watu, bado inakabiliwa na tatizo kubwa la ajira ambapo inakadiriwa kwamba asilimia 40 ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi wanakosa ajira. Hii inachangiwa pia na ukweli kwamba sehemu kubwa ya ardhi ni jangwa na hivyo haifai kwa kilimo.
Botswana sasa imeamua kuchukua hatua ya kijasiri kabisa. Imeanza kukataa kusafirisha madini ghafi inataka almasi zote zikatwe nchini mwao ili kuongezea madini thamani na kuzalisha ajira zaidi kuliko kwenda kuzalisha ajira nchi nyingine ilihali wao wakiteseka na tatizo la ajira nchini mwao. Kwao wanaweza hili kwa sababu wana umiliki mkubwa wa madini yanayozalishwa tofauti na kwetu ambapo wawekezaji ndio wenye kupanga cha kufanya. Lakini haidhuru, hata kama hatuna hisa katika kampuni hizo kwa maana ya fedha, bado tunayo ardhi yetu yenye madini na hivyo tunaweza kuwa na sauti katika kuwaelekeza hao jamaa cha kufanya. Tatizo letu kubwa tunadhani kwamba wao sisi ndio wenye shida sana nao, tunasahau kwamba na wao wana shida ya faida mno. Ni lazima tuanze hilo sasa.
Kwa upande wa Tanzania hali ya ardhi yetu si mbaya. Na njia pekee itakayoharakisha kupungua kwa umasikini wetu, pamoja na kuongeza thamani madini ni kuwekeza katika kilimo. Fedha zinazopatikana katika madini ziwekezwe kwenye kilimo ili kuwasaidia asilimia 80 ya watanzania waliojiriwa katika sekta hii. Kama hili lisipofanyika basi itakuwa ni ngumu na ni changamoto kubwa kwa Tanzania kufikia malengo ya milenia ya kupunguza idadi ya watu wanaoishi katika umasikini wa kupindukia ifikapo mwaka 2015. Ili malengo haya yatimie, inatakiwa uchumi ukuwe kwa wastani wa asilimia 3.8 hadi 4.8 kwa mwaka kati ya sasa na mwaka 2015. Wastani wa ukuaji huu ni mkubwa sana ikilinganishwa na ukuaji wa muongo uliopita. Ikitiliwa maanani kwamba ukuaji uchumi wetu unategemea sana hali ya hewa na kubadilikabadilika kwa bei katika soko la dunia, kuna wasiwasi kama tunaweza kufikia kiwango hicho.
Inabidi kuchukua tahadhari kwa misukosuko inayoweza kutokea kati ya sasa na mwaka 2015. Na njia rahisi ya kufanya hivyo, ni kuhakikisha kwamba kwa miaka ambayo hali ya hewa ni nzuri, uchumi ni lazima ukuwe kwa zaidi ya asilimia 7 kwa kuwa miaka mingine mibaya hali inaweza ikawa mbaya kabisa na kusionekane dalili yoyote ya ukuaji uchumi hasa ikitiliwa maanani kwamba kwa sasa hatujaweka mipango kabambe ya kupambana na uhaba wa mvua. Hakuna ubishi kwamba ili kufanya ukuaji wa uchumi usaidie kuondoa umasikini kwa Tanzania inabidi kuharakisha ukuaji wa sekta ya kilimo ambao ni uti wa mgongo wa nchi na kuiunganisha sekta hii muhimu na ile ya viwanda hasa vile vya kusindika vyakula kwa lengo la kuyaongezea mazao thamani.
Kuharakisha ukuaji wa sekta ya kilimo pia kutasaidia kupunguza tatizo la ajira ambalo limeonyesha kuongezeka kila mwaka. Ni muhimu vile vile kutilia mkazo katika elimu itakayowezesha watu kujiajiri wenyewe, kwani hii ni njia rahisi ambayo inaweza kumkwamua mtu katika umasikini mkubwa. Ni muhimu ikumbukwe kwamba nchi nyingi za Asia ya mashariki ambazo tunapenda kuiga namna zilivyoweza kukua kwa kasi, ziliweza kuua ndege wengi kwa jiwe moja; ukuaji wa pato la kila mwananchi kwa wastani ulikuwa kwa kasi ya kutisha, wastani wa umri wa kuishi uliongezeka, kuongeza kasi ya elimu na upunguzaji wa umasikini kwa kasi ya ajabu. Na cha maana kwao ni kwamba waliweza kufanya haya yote bila kufuta kama dini msahafu walioletewa na mabwana wa IMF na Benki ya Dunia. Walitilia mkazo elimu ya ufundi, utafiti na uwekezaji katika teknolojia sahihi.
Ukuaji wa uchumi ambao hauwezi kubadilisha maisha ya watu masikini hautakuwa na maana yoyote. Unaweza kuwa ni ukuaji wa uchumi wa takwimu zaidi kuliko kuongezeka kwa hali bora ya maisha ya watu. Haya ndiyo tumekuwa tukishuhudia katika nchi nyingi za Afrika na Latini Amerika ambapo takwimu huonyesha mambo kuwa mazuri lakini ukweli ukiwa kwamba ukiweza kuingia kwenye nyumba ya mtu wa kawaida kunawaka moto. Ukuaji wa namna hiyo hunufaisha kundi dogo la jamii na kujikita katika ukuaji wa vitu vichache ambavyo mara nyingi huwa na faida ndogo kwa jamii kubwa. Kwa mfano sekta ya madini ikikuwa kwa faida kubwa ya mwekezaji haitakuwa na maana kama watanzania wengi hawatafaidi matunda yake. Na matunda yanayozungumziwa hapa si viini macho vya wawekezaji kujenga madarasa ambayo siku hizi tunayaita shule au kujenga jengo ambalo litaitwa zahanati ambayo mara nyingi huwa na lengo la kuwadanganya wanakijiji wanaozunguka eneo la migodi. Kinachotakiwa ni maendeleo ya kweli yatakayoletwa na ukuaji wa sekta hii kwa maana ya kodi za kutosha na gawio linaloonekana. Tusidanganyane na michango ya shilingi milioni mia moja au madarasa yanayoitwa shule kwa kupoteza mamilioni ya fedha zetu za madini na ajira ambazo zingepatikana kwa kukata madini hapa nchini.
Unapofanya maamuzi ya kisera huwa yana gharama zake kubwa. Kama kubinafsisha migodi kwa kampuni kubwa na kuwafukuza wachimbaji wadogo, ni lazima uhakikishe kwamba pato litakalopatikana litaweza kuleta faida kubwa kuliko ambavyo wachimbaji wadogo walikuwa wakileta. Ni lazima izalishe ajira na fedha zitakazopatikana ziweze kutoa huduma za kijamii kwa watanzania. Kwa maneno mengine kama faida za kukaribisha wawekezaji wakubwa haziwezi kuonekana ni afadhali kuwaacha wachimbaji wadogo wadogo na kutafuta njia sahihi ya kuweza kupata pato la serikali toka kwao huku tukingojea kujenga uwezo wa wawekezaji wa ndani wazalendo kufanya kazi hiyo. Kama ukuaji wa uchumi haujapunguza makali ya maisha; je ukuaji uchumi ni kwa ajili ya nani?
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment