MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA RAI 2005.
MTWARA, KOROSHO NA OMBA OMBA
Ninaandika makala hii nikiwa Mtwara. Mji wa Mtwara ni wa kihistoria, ni kati ya miji ya zamani iliyoshuhudia historia ya biashara ya watumwa na maendeleo ya kujenga nyumba imara ambazo nyingine sasa hivi ni magofu. Ukiondoa barabara ya lami inayoingia mji huu kutokea Dar, na ile inayokatisha Bima, Sokoni na kurudi tena kwenye makutano ya Uwanja wa mashujaa, hakuna barabara nyingine ya lami katika mji huu. Barabara nyingine kama za kwenda Shangani, Ligula na maeneo mengine ya mji zimetengenezwa na magari yanayopita mara kwa mara. Leo jioni nilitembelea Bandari ya Mtwara yenye kina kirefu kuliko cha Dar na Tanga. Ni bandari kubwa yenye shughuli kidogo kulinganisha na ukubwa wake. Inakuwa na shughuli nyingi kidogo wakati wa msimu wa korosho. Vinginevyo ni bandari iliyolala usingizi! Si lazima nikumbushe kwamba bandari zimechangia sana katika maendeleo ya nchi nyingi duniani.
Meli kubwa ambazo haziwezi kutia nanga kwenye Bandari za Dar na Tanga zinatia nanga kwenye Bandari ya Mtwara. Zilizo nyingi zinakuja kusomba korosho. Zinasomba utajiri mkubwa wa Mkoa wa Mtwara na kuacha nyuma umaskini na ufukara unaonuka. Hata kama mtu hakusoma uchumi, vipo vipimo vya kupima maendeleo ya neema ya watu: Nyumba imara na bora, mavazi wanayovaa watu, afya, barabara nzuri na imara, huduma ya maji nk.
Sikuwa na nia ya kuzungumzia bandari ya Mtwara, hapana, nimeigusia tu kwa vile nimeitembelea leo. Nimeambiwa kwamba na uwanja wa ndege wa Mtwara, miaka ya nyuma ndio ulikuwa uwanja wa pili kwa ukubwa hapa Tanzania. Uwanja uliochangia kiasi kikubwa mapambano ya kusini mwa Afrika. Leo hii uwanja huu uko vipi? Hili nalo si nia yangu kuliongelea kwa leo, labda kesho ama keshokutwa!
Mjini Mtwara, kuna sehemu ijulikanayo kama Bima. Sikuuliza ni kwa nini panaitwa Bima. Lakini ukweli ni kwamba ukifika Bima, umefika Mtwara! Hiki ni kijiwe cha kila kitu, kuanzia siasa, ushabiki wa mpira, dadalada zote na mabasi ni lazima yapite Bima, kuna nyama choma na vinywaji vya kila aina. Unataka usitake baada ya kazi na joto la Mtwara, ni lazima utapumzika kidogo Bima kula au kunywa chochote. Sehemu hii na watu wa kila aina, matapeli, waandishi wa habari, wanasiasa, wahubiri, wafanyabiashara. Ni sehemu ambayo utasikia majina ya kila aina kuanzia Osama hadi Tarimo. Na ukisikia mtu anaitwa Tarimo, Mosha, Marandu au Macha, usifikirie ni Mchaga wa kutoka Moshi. Usishangae ukimkuta Mmakonde, anaitwa Marandu! Unaweza usiwaelewe watu hawa, lakini nilijitahidi kuwaelewa. Kama mimi ninaitwa Privatus, jina la Kiuulaya, kwa nini Mmakonde asiitwe Marandu, jina la kichaga?
Siku moja nilikaa pale Bima. Niliagiza kinywaji na kwa vile nilikuwa Mtwara, nilitamani kula Korosho. Mawazo yangu, nilifikri kwa vile Korosho, inalimwa Mtwara, basi bei yake itakuwa ya chini. Kumbe bei yake ya juu kuliko hata ile ya Dar-es-Salaam! Niliagiza Korosho za Elfu mbili. Kilo moja ni shilingi Elfu tano! Nilipoanza kula, watu wawili walikuja na kukaa karibu na mimi. Niliwakaribisha na kuwaagizia soda mbili. Hapo ndio maajabu ya Mtwara, yakaanza. Ile shukrani yao haikuwa ya kawaida. Walinishukuru hadi nikaguswa. Ni kawa na maswali mengi, kwa nini mtu ashukuru hivyo kwa kununuliwa soda na kukaribishwa korosho? Mtu wa Mtwara, anayelima korosho, atoe shukrani nzito kwa kukaribishwa Korosho? Au mtu ashukuru hivyo kwa kununuliwa soda, ingawa tunashauriwa kushukuru kwa jambo.
Nilikuwa na hamu ya kuongea na marafiki hawa wa Mtwara, ili niweze kujua kiini cha shukrani zao. Kabla sijaanzisha maongezi, mhudumu alileta bili ya soda tatu, shilingi elfu moja miatano. Maana yake kila soda shilingi miatano. Baadaye niliambiwa wengine wanauza mianne. Ninakumbuka nikiwa Mwanza, nililalamika kunywa soda ya shilingi miambili hamsini, nilikuwa nimezoea za miambili kule Bukoba. Wakati wa mongezi, na hao marafiki zangu nikagundua kwamba kwa kipato cha kawaida hapa Mtwara, inamchukua mtu zaidi ya miezi miwili bila kupata shilingi miatano. Hivyo wanaokunywa soda ni watu wenye kipato cha juu! Kilo moja ya korosho, inanunuliwa shilingi mia sita kwa mkulima! Hivyo kwa soda tatu ni lazima kuuza zaidi ya kilo tatu! Ndio nikaelewa ni kwa nini marafiki zangu walishukuru kwa soda.
Na korosho je? Wao si wakulima wa korosho? Kumbe walikuwa na hamu ya korosho? Na kweli hawakuweza kuificha hamu waliyokuwa nayo. Mmoja wao alisema alikuwa na zaidi ya mwaka bila kuonja korosho. Si kwamba hapendi kula korosho, bali bei yake ni ya juu. Mtu anayeshindwa kupata shilingi miatano kwa kipindi cha miezi miwili, atapata wapi za kununua korosho ambazo kilo moja ni shilingi elfu tano, tena hizo ni zile za Grade ya chini, ukitaka za Grade ya juu inayosafirishwa kwenda nchi za nje, kilo tano ni shilingi elfu kumi! Haya ndio maajabu ya Mtwara. Mtu analima korosho, lakini hawezi kula korosho.
Niliongea mambo mbali mbali na hao marafiki zangu, ingawa maongezi yetu yalikuwa yakikatishwa mara kwa mara na watu wanaopitapita wakiomba. Ukiwa mgeni huwezi kuwafumbia macho. Wakiomba unashawishika kuingiza mkono mfukoni na kutoa chochote kuwapatia. Tatizo ni je, utawasaidia wangapi, maana ni wengi. Siku hiyo tu nilifanya mahesabu kwa kumpatia kila aliyeomba shilingi 200 tu, ningetoa shilingi elfu ishirini! Wenyeji wamezoea, wakipita wanaomba, wanawaambia warudi kesho. Ndio hivyo na mimi nikajifunza, nikawa ninawaambia warudi kesho. Tatizo la omba omba si la Bima tu, hili ni taitzo sugu la mji wa Mtwara. Nimetembelea miji mbali mbali hapa Tanzania, lakini tatizo hili nilikuwa sijakumbana nalo. Ndiyo wapo omba omba katika miji yetu, lakini ninaona hapa ni utamaduni uliojengeka na kukubalika! Huwezi kukaa sehemu yoyote ile ya starehe, ya ibada au shughuli nyingine, bila kuwaona watu wakipita na kuomba omba. Si mmoja wala wawili ni zaidi ya kumi. Wanaomba kila siku ya Mungu. Sehemu nyingine tumezoea watu kuomba siku ya Ijumaa, lakini Mtwara, kila siku ya Mungu, ni ya kuomba!
Wengine ni walemavu, lakini linaloshangaza namba kubwa ni watu ambao hawana tatizo lolote kimwili la kuwazuia kujishughulisha na kupata chochote. Ni watu ambao wakipata wa kuwaelekeza na kuwasaidia kidogo wanaweza kujitegemea. Bahati mbaya tatizo hili haliingii kwenye sera za watanzania wanaojali!
Marafiki zangu niliokaa nao pale Bima, waliwatetea hawa omba omba, kwamba hawana la kufanya. Korosho ndio hivyo bei yake ya chini, ajira haipatikani na ikipatikana, mtu anafanyishwa kazi kama punda na kulipwa mshahara kidogo. Walitoa mfano wa kiwanda cha Korosho. Kiwanda hiki kinatoa ajira nyingi na hasa kwa akina mama, kazi ya kubangua korosho ni kubwa na inatesa. Lakini wanacholipwa akina mama hawa ni kidogo hivyo kiasi wengine wanalazimika kufanya kazi ya omba omba ili waongezee kipato chao. Kila anayeomba anasema “saidia masikini”. Na kweli ukimwangalia anayeomba, unaona amepambwa kwa ufukara na afya mbaya, anakuwa ni maskini katika nchi inayojigamba kupiga hatua kubwa katika kukuza uchumi. Watu wa nje wanayaona maendeleo, lakini hawa omba omba wa Mtwara, wakiyaona, basi watakuwa ni vipofu wanaojifanya kuwa vipofu!
Hayo ndio maajabu ya Mtwara, mkoa wenye utajiri mwingi. Mtwara, ni kati ya Mikoa inayochangia kiasi kikubwa kwenye pato la Taifa. Mkoa unaolima korosho zao ambalo lina bei kubwa nchi za nje. Hata kule kwa wenyewe si kila mtu ana uwezo wa kununua korosho – bado mkoa huu unaongoza kwa omba omba na umaskini unaoonekana kwa vigezo vingi bila hata kuingia kwenye utaalam wa kimazingaombwe wa kuhesabu, takwimu na uchumi.
Mtwara, ni mkoa wenye maeneo mengi ya kuwekeza. Mfano mji mdogo wa Mikindani, ni sehemu nzuri iliyo chini ya usawa wa Bahari. Ni eneo zuri la kujenga mahoteli ya kisasa na ya kitalii – panavutia. Ingawa nyumba nyingi bado ni za makuti na zimejengwa kienyeji, bado panavutia. Bahati mbaya ni kwamba wenyeji wanaishi pale bila hati miliki, kesho na kesho kutwa wanaweza kutolewa mikindani na kuhamishiwa kwingine bila fidia yoyote ile.
Nimekaa Mtwara, zaidi ya miezi miwili. Sikusikia mtu akiongelea hili la mkulima wa korosho kuwa na hamu ya kula korosho, au mkulima korosho kufaidika na korosho. Kiasi kwamba Mtu, mgeni akiingia Mtwara, anuse maendeleo yaliyozalishwa na korosho. Kuna mataifa mengi ambayo hayajui kwamba korosho inatoka Tanzania. Wanajua inatoka India! Maana kuna korosho inayonunuliwa bila kubanguliwa, inabanguliwa kule India na kuuzwa Ulaya na Amerika. Wakiona ina nembo za India, wanafikiri inatoka India, kumbe ni ya Mtwara.
Nimekaa Mtwara, miezi miwili sikusikia mtu anayeongelea tatizo hili la Omba omba. Kusikia mtu anapanga mpango wa kuliondoa tatizo hili.
Nimekaa Mtwara, miezi miwili sikusikia mtu akinung’unika juu ya bei ya vitu. Tanzania yetu ni moja, kwa nini soda inunue shilingi miambili sehemu moja na miatano sehemu nyingine? Eti tatizo ni usafiri! Mji wenye Bandari, utakuwa na tatizo la usafiri? Ninasikia kuna mwekezaji aliyeleta meli nzuri na ya kisasa, kufanya safari za Dar- Mtwara, lakini akaihamisha kwa kutokuwa na wateja!
Kila kitu ni bei ya juu Mtwara. Wakorofi, wasioheshimu usawa wa kijinsia, wanasema kitu kisichokuwa na bei Mtwara ni chumvi na wanawake! Eti Mtwara, mwanamke, hajui neno hapana! Ni ukweli si ukweli, kwangu si hoja, ila wasiwasi wangu, ni kwamba sikuona wala kusikia aina yoyote ile ya kampeni juu ya ugonjwa wa UKIMWI, labda nimeweka chumvi, ila ukweli ni kwamba UKIMWI si agenda ya wanasiasa wa Mtwara. Nimetaja wanasiasa, maana nimekuwa Mtwara, wakati wa kampeni za uchaguzi, nilitegemea, kama unavyotegemea wewe msomaji wa makala hii kwamba korosho, omba omba, umasikini na UKIMWI, ni mambo ambayo yangekuwa kwenye agenda za wanasiasa wa Mtwara, lakini ni kinyume. Nilifikiri wanasiasa wana majibu ya maswali mengi yanayowasumbua watanzania wa Mtwara, kumbe si kweli. Lakini la kushangaza zaidi ni kwamba hata maswali ya wananchi si yale ambayo mtu angetegemea. Wale wakorofi walionielezea kwamba kitu chenye bei nafuu Mtwara ni chumvi na wanawake, waliongezea kwamba kisomo si hoja kwa wananchi wa Mtwara. Swali kubwa, kama unataka kufanya siasa au kama unataka kuwa kiongozi wa kisiasa, utaulizwa kama una uwezo wa kupika pilau, kama unashiriki mazishi, kama unawasalimia wafiwa, kama unasali na kama una uwezo wa kutoa misaada mbali mbali katika jamii. Hayo ndio ninayataja kama maajabu ya Mtwara, mkoa wenye utajiri mwingi lakini bado kuna kigugumizi cha maendeleo. Mfano uvuvi tu, ungeweza kubadilisha maisha ya omba omba wengi. Hata hiyo chumvi ambayo ina bei nafuu kuliko kila kitu, ingefanyiwa mpango mzuri na kutengeneza viwanda vya kisasa tofauti na inavyovunwa sasa hivi kwa njia za kienyeji, ungekuwa ni mradi wa kupunguza au kukomesha omba omba wa Mtwara. Kazi za mikono, Wamakonde, ni mafundi wa kuchonga vinyago, wangepata mpango mzuri wa kusafirisha vinyago hivi hadi nchi za nje. Meli zinazosomba korosho zingeweza kusomba na vinyago. Bandari tu ya Mtwara ni utajiri ambao vizazi vijavyo vitauliza mengi juu ya matumizi yake. Nimeondoka Mtwara, nikiwa na maswali mengi kichwani. Ni nani mwenye majibu ya maswali kama haya? Nina hakika si wanasiasa wa leo wa Tanzania!
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment