MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2005.
NYERERE NA UTAKATIFU.
Ni lazima tumpongeze Askofu Samba, wa Jimbo Katoliki la Musoma, kwa juhudi alizozianzisha za kufanya utaratibu wa kumtangaza Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, kuwa mwenye heri na hatimaye kutangazwa mtakatifu. Juhudi hizi ni za kuigwa na Maaskofu wengine kama yule wa Rulenge, wa Bukoba na Songea. Hakuna shaka kwamba Marehemu Askofu Christopher Mwoleka, aliyekuwa askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge, aliishi maisha ya kumpendeza Mungu, na alikuwa mtumishi mwaminifu. Alijulikana kama Askofu Mjamaa, aliishi kwenye vijiji vya ujamaa na kuunga mkono siasa ya Mwalimu Nyerere ya Ujamaa na Kujitegemea.
Watu wengi wa nje na ndani ya nchi wamekuwa wakimlinganisha Marehemu Askofu Mwoleka na Marehemu Mwalimu Nyerere. Marafiki wa Mwoleka wa Ujerumani, walitengeneza Jarida lenye ukurasa 45,wakielezea maisha ya Mwoleka na Nyerere. Hivyo njia ya kumtangaza Nyerere, kuwa mtakatifu haiwezi kumtupa nje Marehemu Askofu Mwoleka. Kama kuna nia, hekima na busara aliyoionyesha Askofu Samba, jambo hili linawezekana kabisa.
Hapa Tanzania tuna marehemu wengi ambao wanaweza kutangazwa watakatifu kama juhudi zingekuwepo. Mtu wa kwanza katika jimbo kuanzisha juhudi hizi ni Askofu wa jimbo. Askofu ndiye kiongozi na msimamizi wa Jimbo. Yeye ndiye anayeelekeza, kushauri na kuisimamia imani katika Jimbo lake. Kwa muda mrefu maaskofu wetu wa hapa Tanzania wamekaa kimya kuhusiana na jambo hili la watakatifu. Ni kwa makusudi, kusahau au ni bahati mbaya, inakuwa vigumu kuelezea. Marehemu Kardinali Rugambwa, mbali na kuwa Kardinali wa kwanza Mwafrika kusini mwa Jangwa la Sahara, ni mtu aliyefanya mambo mengi ya kuliendeleza kanisa la Afrika na kuchangia maendeleo ya watu kwa kujenga mashule, mahospitali na huduma nyinginezo za jamii. Amefanya kazi hizi kule kwao Bukoba , Dar-es-Salaam na sehemu nyinginezo katika Taifa letu.
Kuna wamisionari wengi waliofanya kazi hapa Tanzania na kuzikwa hapa au nchi jirani kama Rwanda. Hawa walifanya kazi kubwa. Kutowatangaza watakatifu ni kuisaliti kazi yao yote waliyoifanya. Askofu Hirth, alianzia Kagera akieneza dini na maendeleo ya binadamu hadi akafika Rwanda. Alikufa na kuzikwa nchini Rwanda. Huyu, kama kungekuwa na jitihada za pekee za Askofu wa Bukoba, basi naye angekuwa katika mchakato wa kutangazwa mtakatifu. Wanahistoria wengi akiwemo Askofu Methodius Kilaini, ambaye anaonyesha uelewa mkubwa na kipaji cha hali ya juu cha kuyachambua matukio mbali mbali ya kihistoria, wameandika mengi kuhusiana na maisha ya Askofu Hirth, inashanaza kuona hadi leo hakuna jitihada zilizofanyika kufuatilia maisha na kazi za Askofu Hirth.
Wako na walei wengi waliojitolea kufanya kazi za kueneza Injili na kuchangia kukua kwa maendeleo ya binadamu. Mzee Kazigo, aliyetoka Bukoba, kwenda Karagwe, ni mtu aliyeacha historia ya imani, mapendo na uvumilivu. Mtu kama huyu, ni muhimu katika historia ya kanisa. Lakini pia wapo walei wengine waliokataa kuipokea imani, ila wakalazimishwa kuipokea ili wapate huduma za kijamii kama shule, matibabu na ustaarabu wa kigeni, lakini kwa kufanya hivyo wamekuwa chanzo na kichocheo cha imani na maendeleo. Hawa walipata nafasi ya kuwapeleka watoto wao mashuleni, ambao sasa hivi ni madaktari, maprofesa, wanasheria, mapadri, masista nk. Waliipokea imani kwa uchungu, walifanyishwa kazi na kulazimika kutembea mwendo mrefu na wakati mwingine kuyapoteza maisha yao. Hawa wote wakifanyiwa utafiti wanaweza kupata heshima ya utakatifu.
Tuna mama zetu wanaopigwa hadi kufa wakizitetea ndoa zao. Wanavumilia mateso, hadi kufa ili kulinda sakramenti ya ndoa. Ipo mifano mingi ya akina mama waliokatwakatwa au kupigwa risasi au kwa mauaji ya aina nyingine. Wanawake hawa wanakufa wakitetea imani yao. Hivyo si haki kabisa akina mama kama hawa kuwanyima nafasi ya kukumbukwa katika kanisa.
Mwanamke Daktari wa Italia, alifanywa mtakatifu kwa vile alichagua kufa kuliko kuitoa mamba. Alikuwa na nafasi ya kuendelea kuishi kama angekubali kuitoa mamba. Hapa Tanzania, tunao akina mama wengi ambao wanapoteza maisha kwa kukataa kutoa mimba. Wanakuwa na nafasi ya kuendelea kuishi, lakini kwa kutetea imani yao wanachagua kufa kuliko kutenda dhambi na kulisaliti kanisa. Wanawake hawa hakuna kumbukumbu zao. Wanakufa na kupita tu!
Ni bahati mbaya au ni uzembe wetu kwamba baada ya miaka 100 ya Ukristu hapa Tanzania, hatujatunukiwa Mtakatifu Mtanzania au yule aliyefanya kazi hapa Tanzania. Wengine wana mawazo kwamba watakatifu wanadondoka kutoka mbinguni au si watu kama sisi. Kama mpango wa kumtangaza Mwalimu nyerere ukifanikiwa, itasaidia kuonyesha kwamba watakatifu ni watu kama sisi na wanazaliwa na kuishi miongoni mwetu. Wanakuwa na mapungufu kama sote tulivyo, lakini wanajiweka mikononi mwa Mungu, na kukubali kuongozwa naye!
Kila mtu anaruhusiwa kutoa ushuhuda kwa yule anayetajwa kwamba anastahili kuwa mtakatifu. Mfano sasa hivi kanisa limeruhusu watu kujitokeza na kusema walivyomjua mwalimu. Imani yake na upendo wake kwa Mungu na watu.
Kitu muhimu ni miujiza inayojitokeza ili kuonyesha kwamba kweli marehemu ni mtakatifu. Miujiza kama ya umoja wetu wa wanatanzania, miujiza kama amani yetu, miujiza ya watawala kukubali kufuata mifano ya mwalimu ya kuachia madaraka. Hizi ni kazi alizozifanya mwalimu. Kama tuna amani, ni kwa vile mwalimu alijenga misingi ya amani. Kama tuna umoja ni kwa vile mwalimu alijenga misingi ya umoja. Kama viongozi wanakubali kuachia madaraka ni kwa vile mwalimu alijenga misingi imara ya kupokezana uongozi! Mwalimu alishiriki kikamilifu kuzikomboa nchi za Afrika. Huu ni muujiza mkubwa. Pia mwalimu alianzisha mazungumzo ya Burundi. Leo hii Burundi, ina serikali iliyochaguliwa na wananchi wenyewe. Huu pia ni muujiza mkubwa. Miujiza ya mwalimu ni mingi kiasi kwamba kama ikifanyiwa kazi kwa makini, haitachukua muda bila ya kumtangaza Mwalimu Nyerere kuwa ni mwenye heri na hatimaye Mtakatifu.
Juhudi hizi zikienda sambamba na zile za kufanya utafiti wa marehemu wengine kama Mwoleka, Rugambwa, Komba na wengine wengi, tutajikuta tunapata tunu ya kuwapata watakatifu wengi. Jambo hili litachangia sana kukua kwa imani, kukua kwa uchumi wetu na kuacha kuliangalia kanisa kama chombo cha mataifa makubwa.
Kama yalivyo mawazo ya wanateolojia wengine, kwamba Baba Mtakatifu Benedict wa 16, hawezi kuwa na mengi mapya kwa nchi masikini kama Tanzania, zaidi ya kuwatangaza watakatifu wengi kadri awezavyo. Si Papa, wa kuleta mabadiliko, si Papa wa kukubali Theolojia ya ukombozi iliyo kilio kikubwa cha nchi maskini. Ni Papa wa kufanya yale yasiyoweza kumlazimisha kwenda kinyume na imani yake ya kale. Amepambana na theolojia ya ukombozi kabla ya kuwa Baba Mtakatifu, hawezi kuikumbatia wakati amepanda ngazi kuliko zote katika kanisa katoliki. Anaweza, na hili ni la uhakika, kwamba anaweza kutupatia watakatifu. Hii ni changamoto kwa maaskofu wetu!
Na,
Padri Privatus Karugendo
0 comments:
Post a Comment