MADAKTARI WASIGOME LAKINI.....

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2005.

MADAKTARI WASIGOME LAKINI PIA WASIPUUZWE!

Mgomo wa Madaktari umekuwa gumzo, kero, aibu na kwa upande mwingine ushindi wa aina Fulani! Inawezekana Serikali ikajiona mshindi kwa kufanikiwa kupambana na madaktari na kuwashinda kwa kuwafukuza kazi. Na inawezekana madaktari wakaonekana washindi pale serikali itakapolazimika kuajili madaktari kutoka nje ya nchi na kuwalipa pesa nyingi mara tatu ya zile walizokuwa wakidai madaktari. Ipo mifano mingi ambapo mtaalam kutoka nje analipwa zaidi kuliko mtaalam wa ndani, hata kama ujuzi wao na kisomo vinalingana.

Wamejitokeza watu mbali mbali kuandika juu ya mgomo huu. Mfano Tanzania Daima Jumapili, iliyopita ilikuwa na makala mbili zinazopingana juu ya mgomo huu. Makala moja ilikuwa inasema kwamba madaktari sheria inawazuia kugoma. Imeandikwa vizuri na hoja ni nzito. Mwandishi wa makala hii alienda mbali zaidi kwa kuwaweka madaktari waliogoma kapu moja na wauaji, maana vifo vilitokea wakati madaktari wakigoma. Makala ya pili ilikuwa ikiwasifia madaktari kwa kugoma kwao, na kwamba hawa ni wazalendo, maana badala ya kuikimbia nchi na kwenda kufanya kazi nchi za nje ambako wangepata mishahara mikubwa, wameamua kubaki hapa nchini. Na ili kuonyesha uzalendo wao, wameamua kutumia njia ya amani kudai kile wanachokiita haki yao. Mgomo unachukuliwa kama njia ya amani ya kushinikiza mambo katika serikali inayoelekea kukwepa wajibu wake.

Mbali na makala hizi mbili, majadiliano yanaendelea kila sehemu, vijiweni, kwenye daladala, kwenye vikao vya pombe na wakati mwingine kwenye mijadala ya kisomi inayoendeshwa sehemu mbali mbali kama kwenye redio na kwenye luninga. Kama nilivyosema hapo juu, watu wamegawanyika, wengine wanawatetea madaktari na wengine wanawalaani.

Binafsi nisingependa kuwatetea wala kuwalaani. Lengo la makala hii ni kuwakumbusha watanzania kwamba mgomo wa madaktari usichukuliwe kama mgomo wa madaktari. Mgomo huu ni kielelezo cha mambo mengi ambayo hayajapata ufumbuzi. Yapo mambo mengi ambayo yanahitaji majadiliano na hasa tukigusa keki ya taifa na ustawi wa jamii.

Mfano, siku hizi umekuwa utamaduni kwamba bila mgomo mambo hayafanyiki. Mheshimiwa Mkono, alisema kwamba Bodi ya Mkopo, ina pesa nyingi. Pesa hizi hazikutoka hadi wanafunzi wa Chuo Kikuu, alipogoma kwenda madarasani. Juzi tena wanafunzi wa uandisi walilazimika kugoma ili wapate haki zao. Ni imani yangu kwamba baada ya mgomo wa madaktari utafuata mgomo mwingine, sitaki kuwa mtabiri, lakini unaweza kufuata mgomo wa walimu.

Kabla ya kuwalaani au kuwatetea madaktari, ni lazima tujiulize ni kwa nini madaktari hawa waliamua kugoma siku hizi za kampeni? Kwanini waliamua kugoma siku ambazo kila Mtanzania anaona wazi jinsi serikali inavyotumia pesa nyingi kwenye zoezi zima la uchaguzi na kampeni zinazoendelea? Ukimwambia mtu kwamba Taifa letu ni masikini atakuita mwendawazimu. Mabango yote ya kampeni yametengenezwa kwa pesa, kofia na t-shirts ni pesa, magari yanatumia mafuta kuzunguka nchi nzima. Nchi masikini haiwezi kumudu kufanya yote hayo.

Inawezekana kabisa kwamba madaktari wetu waliamini kwamba nchi yetu ni masikini, hivyo ilikuwa ni wajibu wao kama watanzania kushikamana na kufanya kazi kwa kujitolea zaidi ya kuangalia mishahara mikubwa. Ninasema walifikiri hivyo maana karibu kila Mtanzania anafikiri na kuamini kwamba nchi yetu ni masikini. Lakini baada ya kuona yale tunayoyaona, pesa zinavyotumiwa kwa mambo ambayo si muhimu, madaktari nao kama binadamu ni lazima waanze kuhoji. Ndio maana ninasema ni jambo la msingi kujiuliza ni kwa nini mgomo huu uje wakati ambapo taifa letu linaonyesha dalili za kuwa na pesa nyingi. Kwanini mtu aendelee kufanya kazi kwa kujitolea wakati taifa lina pesa nyingi na za kumwaga? Kwanini mtu aendelee kujitolea wakati yeye anafanya kazi nyingi hadi kukesha na kutembelea daladala, wakati wale wasiofanya kazi yoyote wanatembelea mashangingi? Wanasomesha watoto wao nje ya nchi na kuishi maisha kifahari? Wana majumba makubwa na wala hawana kitu chochote kinachosumbua akili yao.

Jambo la pili ambalo ningependa watanzania wazingatie juu ya mgomo huu wa madaktari ni neno uzalendo. Mtu mzalendo analipenda taifa lake na kulitumikia na taifa linampenda na kumtumikia. Mzalendo anawajibika kulitumikia taifa lake, na taifa linawajibika kumtunza na kumjali raia wake. Taifa linalojali linajua kwamba madaktari wanashughulikia maisha ya watu, daktari akifanya kosa, maisha yanapotea. Hivyo ni lazima daktari awe kwenye mazingira mazuri ya kumwezesha kutulia kiakili. Kama daktari ana wasiwasi na karo ya mtoto, kama daktari ana wasiwasi na kodi ya nyumba, pesa za chakula, hawezi kutulia kiakili na kufanya kazi zake ipasavyo. Jinsi daktari anavyowajibika kuyatunza maisha ya raia kwa gharama yoyote ile, ndiyo taifa linavyopaswa kuwajibika kuhakikisha daktari anaishi kwenye mazingira yanayomwezesha kufanya kazi vizuri. Na daktari anayejali akishindwa kufanya kazi kwa matatizo yanayosababishwa na taifa, ni lazima atasema. Kwa maana nyingine, kile kinachoonekana kuwa mgomo, hadi wengine wanataja sheria inayozuia mgomo wa madaktari, si mgomo, ni njia ya kufikisha ujumbe kwa wanaohusika kwamba madaktari hawawezi kuendelea kufanya kazi katika mazingira yasiyokuwa na utulivu, vinginevyo watasababisha vifo badala ya kuokoa maisha.

Hii ni kinyume, kwa mfano madaktari wangeamua kufanya mgomo baridi. Wanakwenda kazini, lakini hawafanyi kazi. Mwisho wa mwezi wanapata mshahara. Tuna mifano mingi ya watanzania ambao, hawajagoma, lakini hawafanyi kazi ipasavyo. Wanashinda kazini, lakini hakuna wanachokifanya. Mtu mwenye akili nyingi, anaweza kusema ni bora hao, maana hawakugoma, kitu kibaya ni mgono na sheria inazuia mgomo. La msingi ni kuitii sheria! Madaktari wetu wangefanya hivyo, hakuna ambaye angepiga kelele. Jinsi ilivyo tunatawaliwa na giza la unafiki uliofungamana na ujinga mkubwa!

Mwandishi aliyewaweka madaktari kwenye kapu moja na wauaji, amewakosea kabisa. Maana kamani kuangalia kwa mtazamo huo, basi watu wengi hapa Tanzania wanashiriki mauaji. Mfano, ni watu wangapi hapa Tanzania, wanakufa kwa kupotoshwa kutotumia kondomu? Ni watu wangapi wanakufa kwa kutoweza kununua dawa ya malaria? Ni watu wangapi na hasa akina mama wanakufa kwa kushindwa kusafiri hadi kwenye zahanati au hospitali wakati wa kujifungua? Wanakufa bila sababu yoyote. Mbona hatupigi kelele na kusema kwamba Serikali kushindwa kusambaza huduma za jamii inashiriki katika mauaji?

Pia ninashindwa kukubaliana na mwandishi huyu anaposema kwamba Madaktari walicheza ndombolo mbele ya wagonjwa. Huku ni kuweka chumvi. Madaktari hawakuwa na magomvi na wagonjwa, itakuwaje wawachezee ndombolo. Kama walicheza, waliilenga Serikali, na wala si wagonjwa. Ni bora kueleza ukweli kuliko kupotosha. Si busara kuongeza chumvi kwenye swala nyeti kama hili.

Madaktari ni watu wanaofanya kazi kubwa na kwa kujitolea na kuyaweka maisha yao hatarini. Madaktari walio wengi wanakesha kwa kufanya kazi masaa mengi zaidi ya watanzania wengine. Ni vigumu kuwalipa kwa kile wanachokifanya. Kama wanadai nyongeza ya mshahara, maana yake ni kwamba wanataka wafanye kazi akili yao ikiwa imetulia. Wanataka wafanye kazi wakijua kwamba nyumbani watoto wanakwenda shule, wana chakula cha kutosha na wana nyumba ya kulala. Si vibaya pia wakiwa wanajua kwamba wana usafiri wa kuaminika na wana pesa ya akiba kwa tatizo lolote linaloweza kujitokeza kama mwizi wa usiku!

Madaktari wetu wanaishi ndani ya jamii. Wanaona jinsi watu wengine wanavyotesa tena bila ya kuwa na kazi wala biashara inayoonekana. Wanaona jinsi viongozi wa serikali wanayoyafurahia maisha, na wakati mwingine wale wanaofurahia maisha na kuishi maisha ya starehe ni watu ambao hawakusoma sana kama madaktari. Binadamu yeyote ni lazima aguswe na hali kama hii.

Tusiwalaumu madaktari na wala tusiwatetee. Jambo la msingi ni kuchunguza chazo cha mgomo wao. La muhimu ni serikali kukaa chini na kuzungumza nao na kuyachunguza madai yao. Pesa wanayoidai si nyingi ukilinganisha kazi nzito wanayoifanya. Pesa wanayoidai si nyingi ukilinganisha na pesa zinazotumika sasa hivi kutengeneza kofia, t-shirts na shughuli nyingine za uchaguzi. Kama hizo pesa zinapatika, kwa nini zisipatikane pesa za kuwahudumia madaktari wetu ili waweze kufanya kazi kwa utulivu?

Kule tunakoelekea panahitaji majadiliano zaidi ya kutumia nguvu na mabavu katika maamuzi mbali mbali katika jamii yetu. Panahitaji hekima na busara badala ya kutumia madaraka na majigambo. Ni kweli kwamba si halali madaktari kugoma, lakini pia si halali serikali inayowajali raia wake kuwafukuza madaktari.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment