MAKALA HII ILICHAPWA NA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2006.
BARUA YA WAZI KWA MHESHIMIWA MASHA.
Mheshimiwa sana L.Mashama, Mbunge wa Nyamagana na Naibu Waziri wa Nishati na Madini. Ninaona Tanzania tumeingia kwenye utamaduni mpya, utamaduni wa kuandikiana barua za wazi. Na ninaona barua hizi zinashika kasi wakati wa Serikali ya awamu ya tatu ambayo na wewe umetunukiwa kushiriki katika uongozi wake. Si utamaduni mbaya, maana ni njia ya kuwashirikisha na wengine yale ambayo ni muhimu kwa Taifa. Yale yanayoandikwa kwenye barua za wazi yanakuwa si mambo binafsi na wala si kuingilia mtu katika uhuru wa maisha yake ya binafsi. Nilitamani sana kukwambia haya siku za nyuma, lakini muda haukuwepo. Leo Mwenyezi Mungu amenipatia nguvu za kuweza kukaa chini na kukuandikia barua hii ambayo sitegemei iwe ndefu zaidi ya maneno elfu moja!
Tulipokutana Mwanza, mwaka jana mwezi wa nne au wa tano, siku chache kabla ya kura za maoni za kumchagua mgombea wa CCM, katika nafasi ya urais, nilifikiri ilikuwa ni mara yangu kwanza kukutana na wewe. Nimekumbushwa na kujikuta kwamba tunafahamiana siku nyingi. Lakini hili si lengo la barua hii fupi hayo tutakumbushana mbele ya safari.
Lengo langu ni kukumbusha tukio la siku hiyo tulipokutana. Tulikutana Rock Beach, wewe ulikuwa na wageni wako mnapata chakula cha mchana. Mimi pia nilikuwa na wageni wangu tukipata chakula cha mchana. Rock Beach, inaendeshwa na Mchina. Sina haja ya kukumbusha kwamba hata wapishi na baadhi ya wahudumu wengine ni Wachina, pia hili si lengo la barua hii fupi!
Nyinyi mlipomaliza kula chakula na vinywaji, ulienda kulipa. Kama sikosei ulilipa sh 87,000. Kwenye risiti yako walikuandikia pesa hizo, lakini kwa udadisi na umakini ulionao uligundua kwamba kwa copy yao ya kubaki nayo ambayo ndicho kielelezo cha kuisaidia TRA kukusanya mapato waliandika kwamba uliwalipa sh 7,000! Ninakumbuka vizuri ulivyopandisha na kuanza kubishana na Wachina hao. Ninakumbuka ulivyojitahidi kupiga simu kuwaelezea watu wa TRA, ujanja wa Wachina hao. Maana walionyeshe sh7,000 na kuzificha zile 80,000. Inaelekea huo ndio ulikuwa mchezo wao wa kuendelea kutuibia. Kwa njia hiyo ni lazima TRA, wangeamini kwamba watu hao hawafanyi faida kubwa na kwa njia hiyo kuwatoza pesa kidogo.
Sikufuatilia kujua mambo yaliishia wapi. Sikujua kama TRA, walisaidia, au wewe uliwasaidia kuwapatia ulaji, maana kama waligundua ujanja huo na kama kwa bahati mbaya ambayo ipo sehemu na sehemu, wakutwe si wazalendo wa kweli, basi kunyoosha tatizo hilo ni lazima matumbo yao yalijaa. Inawezekana badala ya kusaidia, ulikuwa unaongezea tatizo juu ya tatizo!
Wakati huo sikufahamu kwamba ulikuwa na mpango wa kugombea kiti cha Nyamagana. Mimi nilikuona tu kama Kijana mzalendo na mwanamapinduzi na kuna mtu alinidokeza kwamba wewe ni mwanamtandao. Sikujua zaidi ya hapo. Ningejua, ningekuwa mtu wa kwanza kukupigia kampeni. Hata hivyo umefanikiwa bila mchango wangu. Mungu, ashukuriwe maana Tanzania inahitaji vijana kama wewe!
Ujasiri uliouonyesha kupambana na Wachina hao, ulinifanya nikuone kama mtu asiyekuwa wa kawaida. Ni watu wachache wanaojali mapato ya serikali. Mtu mwingine angeenendelea na safari zake, maana risiti yako ilikuwa inaonyesha kiwango chenyewe, na kama na wewe ulikuwa unaenda kudai kurudishiwa kule ofisini kwako, basi haikuwa na tatizo. Lakini wewe ulisimama kidete na kuwaelezea Wachina wale wizi waliokuwa wakilifanyia Taifa letu. Ninakumbuka jinsi ulivyokuwa ukifoka kana kwamba mali za Mzee Masha na Mbuta Milando zimeguswa. Au labda Uzinza imevamiwa! Nilikushangaa na kukuheshimu sana tangia siku ile. Sikushangaa kusikia umechaguliwa kuwa Mbunge wa Nyamagana na baadaye kuteuliwa na Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini.
Wizara uliyopewa imekuwa ikilalamikiwa na watu wengi kwamba kuna ujanja kama ule uliougundua pale Rock Beach Mwanza. Yamesemwa mengi na yametolewa majibu mengi. Wengine wanasema mchanga unabebwa ukiwa na madini, wengine wanasema Taifa linapata faida ndogo kutokana na madini yanayochimbwa. Wakati wa kampeni Mheshimiwa Mbowe wa CHADEMA, alilieleza hili kwa utaalamu akilinganisha na nchi nyingine kama Botswana, lakini Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, alimjibu kwa utaalamu pia hadi tukabaki kuchanganyikiwa ni nani anasema ukweli. Wataalamu wengi hawakubaliani kwa hili, wengine wanasema tunaibiwa na wengine wanasema mambo ni poa tu! Ni imani yangu na wale wote wanaokufahamu vizuri kwamba utatumia wakati wako na nguvu zako kupambana, kufoka na kuonyesha uzalendo katika Wizara ya Nishati na Madini zaidi ya ujasiri uliouonyesha pale Mwanza, wa kupambana na Wachina. Ni imani yangu kwamba Wachina wale wanaiba, lakini si kiasi kikubwa kulinganisha na mashaka ya watu waliyo nayo kuhusu madini yetu.
Bahati nzuri Wizara ya Nishati na Madini, imekuwa ikisifika kuwa na Katibu Mkuu mzalendo, mchapakazi na adui mkubwa wa rushwa. Ni imani yangu kwa kushirikiana naye na wengine mnaweza kufanya mabadiliko makubwa.
Madini ni chanzo kikubwa cha uchumi wetu, ni chanzo ambacho kinaweza kuleta mabadiliko makubwa sana. Wewe ni mzaliwa wa Mkoa wa Mwanza na Kanda ya Ziwa. Unajua utajiri mkubwa wa madini ulio katika maeneo haya. Pia unajua jinsi hadi leo hii watu wa mikoa hii hawajafaidi vizuri madini yao.
Wewe ni kijana kwa maana ya neno kijana. Bado una muda mwingi wa kuishi katika taifa hili, Mwenyezi Mungu, akikuwekea mkono. Ni lazima utumie wakati huu kupanga mipango ya mbele ya kuendeleza Wizara yako ili watu wa Mwanza na Tanzania nzima wafaidi utajiri wa madini yao.
Wewe ni mwanasheria, ujuzi huu utakusaidia kuiangalia vizuri mikataba ya madini na kujitahidi kuondoa utata unaojitokeza na kuwakwaza wananchi.
Sikuombei ushindwe. Lakini ikitokea, nitakuwa mtu wa kwanza kukuandikia barua ndefu. Nitakuwa wa kwanza kukusuta. Sitegemei Unaibu Waziri utakubadilisha na kukuletea tabia ambazo hukuwa nazo. Sitegemei usimame pale Nyamagana na kuwaonesha watu kwamba wewe ni mbunge na ni waziri kwa kuwatupia watu pesa, sitegemei utafunga madirisha ya gari lako na kuwapita wapiga kura wako bila kuwasalimia.
Nina imani utashirikiana na wabunge wengine wa Mwanza, kusukuma maendeleo ya Mkoa wa Mwanza mbele. Badala ya kuwatupia watu pesa, uwawezeshe ili watu waweze kujitegemea. Haina maana kuwatupia watu pesa, wakati hawana maji, hawana nyumba bora, hawana barabara na hospitali zao ni za wasiwasi. Utajiri wako ubunge wako na uwaziri wako uwe ni kuwawezesha na kuwatumikia watu. Hata hivyo wamekuchagua wenyewe na wewe ni mtumishi wao. Watu ndio waheshimiwa na wewe ni mtumishi tu! Heri mtumishi mwaminifu na mwenye busara!
Wewe ni mwanamtandao wa nguvu, hivyo sitegemei utamwangusha kiongozi wa wanamtandao na watanzania wote, Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete. Ukimwangusha, ujue nitakuwa mtu wa kwanza kukusuta na kwa hili sitakuandikia barua bali tutaongea ana kwa ana.
Kama alivyosema Mheshimiwa Rais Kikwete, Uwaziri hauna shule. Hivyo usiwe na wasiwasi, uanze kazi kwa kujiamini na kuendelea kuwa mzalendo wa kweli. Mungu akubariki!
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment