TWAHUBIRI MAJI TUKINYWA MVINYO?

MAKALA HII ILICHAPISHWA KWENYE GAZETI LA RAI 2005

TWAHUBIRI MAJI TUKINYWA MVINYO?

Kongamano la Kimataifa la ‘Kiswahili na Utandawazi’ la maadhimisho ya Jubilii ya Miaka 75 ya Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) lililofanyika tarehe 4 hadi 7 mwezi huu Jijini Dar-es-Salaam, limeacha changamoto nyingi nyuma yake.

Changamoto ya kwanza ni kwamba nchi zaidi ya 21 ziliwakilishwa kwenye kongamano hilo. Na si kuwakilishwa tu, bali washiriki walitoa makala kwa lugha ya Kiswahili. Nchi hizi zinafundisha na kufanya utafiti wa lugha ya Kiswahili. Na nchi nyingine zimeanza zamani. Mfano Amerika imeanza kufundisha Kiswahili mwaka wa 1945! Mwakilishi wa Nigeria, katika kongamano hilo, aliimba wimbo wa Kiswahili uliokuwa umejaa hisia kali: “Mrembo, Mrembo, Mrembo wa Moyo wangu”. Mrembo huyu ni lugha ya Kiswahili! Nigeria ni kati ya nchi yenye lugha za Kiafrika kongwe na zinazungumzwa na watu wengi, lakini bado mtu kutoka Nigeria, anakiita Kiswahili; “Mrembo wa moyo wake”!

Jambo lakushangaza zaidi, na ndio maana hii ni changamoto, ni kwamba wawakilishi wa kutoka nje ya Afrika, waliweza kujieleza na kuongea Kiswahili kizuri sana. Na si kuongea tu, bali kubuni maneno mapya ya Kiswahili na kujadili muundo mzima wa lugha Kiswahili kwa kujiamini. Mfano neno kama dolesha, likimaanisha “Index” limebuniwa na Profesa Hinnebush, kutoka Amerika. Profesa huyu amebuni maneno mengine mengi kutokana na lugha za Kiafrika kuingia katika Kiswahili.

Mfano wajumbe kutoka Amerika, Ujerumani, na Finiland, walielezea utaalamu wao wa kukiingiza Kiswahili katika kompyuta. Wamebuni na kutengeneza programu za Kiswahili. Binti mdogo kutoka Ujerumani, Raija Kramer, ambaye bado anasoma chuo kikuu kule Ujerumani, ametuachia msamiati wa Kamusi Mkondoni (Online-Dictionary). Maana yake ni kwamba kamusi na msaada wa kujifunza Kiswahili kupitia mtandao ni kitu kinachowezekana hivi sasa. Mtu anayetaka kuhakikisha anaweza kubofya kwenye: http://dictionary.it-swahili.org

Mbali na msichana huyu kulikuwa na wengine waliotoa makala juu ya matumizi ya Kiswahili kwenye mtandao. Hawa pia walijielezea kwa Kiswahili sanifu. Ukweli huu unapatikana:http:www.juasun.net/home.html
, http://www.yale.edu/swahili. Ipo na mitandao mingine mingi ambayo inatumia lugha ya Kiswahili. Hili ni jibu kwa wale wote ambao wamekuwa wakipiga kelele kwamba Kiswahili hakiwezi kuimudu teknolojia.

Profesa Hurskainen, kutoka Finland, aliwashangaza wanakongamano kwa kutumia SALAMA software kwenye Kompyuta yake kuitafsiri Hotuba ya Rais Benjamin Mkapa, kutoka kwenye Kiswahili kwenda kwenye Kiingereza kwa dakika zisizozidi tatu. Kama hii imewezekana, tunataka Kiswahili kiimudu teknolojia inayofanana vipi?

Changamoto kubwa zaidi kuhusiana na hili ninalolijadili ni kwamba washiriki hawa wa kongamano kutoka nchi za nje au niseme nje ya Afrika: Amerika, Ujerumani, Denmark, Poland, Italia,China,Korea, Japan, Finland nk, wamejifunza Kiswahili nchini kwao. Wamejifunza Kiswahili kama lugha. Si kwamba walikitumia Kiswahili kwenye masomo mengine. Lakini wanakiongea Kiswahili vizuri sana. Hivyo hoja inayotolewa kila siku kwamba watanzania watafahamu vizuri Kiingereza wakifundishwa masomo yote kwa Kiingereza, haina msingi wowote. Kama Mjerumani, anaweza kujifunza Kiswahili na kukiongea vizuri akiwa Ujerumani, kwa nini Mtanzania asijifunze Kiingereza, Kijerumani au Kifaransa kama lugha na kuiongea vizuri? Siri kubwa ya mafanikio ya hawa watu ni kwamba wanazitumia lugha zao kujifunza lugha nyingine. Wanaweza kujifunza lugha nyingine na kufanikiwa kuzifahamu vizuri kwa vile wanazifahamu vizuri lugha zao.

Tatizo letu sisi ni kwamba tunataka kutumia lugha za kigeni kujifunzia lugha za kigeni. Badala ya kutumia lugha yetu kujifunzia lugha za kigeni kama wafanyavyo watu wote duniani. Tunataka kutumia lugha za kigeni kujifunzia mambo yote ya Elimu dunia. Matokeo yake ni kwamba lugha za kigeni zinatushinda na Elimu dunia tunaipata nusu nusu. Ndio maana hata na vitu vile ambavyo viko chini ya uwezo wetu vinafanywa na watu kutoka nje ya nchi yetu. Tukizubaa zaidi hata na lugha yetu tutafundishwa na watu kutoka nje ya nchi yetu!

Changamoto ya pili kutokana na Kongamano hilo ni kwamba wale watu wanaojiita Waswahili, wale wanaosema kwamba Kiswahili ni lugha yao ya taifa, ndio wanaokiharibu Kiswahili na kukwamisha maendeleo yake. Kama alivyosema Sangai Mohochi, kutoka Chuo kikuu cha Egerton, Kenya, kwamba twahubiri maji tukinywa mvinyo! Wakati washiriki wa kongamano kutoka nje ya Afrika ya Mashariki walikuwa wanajitahidi kutoa makala zao kwa lugha ya Kiswahili, baadhi ya wajumbe wa Afrika ya Mashariki walishindwa au kukataa kutoka makala zao kwa Kiswahili. Walitumia Kiingereza! Na hawa ni watu wanaoongea Kiswahili kizuri tu. Lakini hawakupenda kutumia Kiswahili kwenye kongamano la kimataifa la Kiswahili! Profesa mmoja kutoka Kenya, alikataa kutoka makala yake kwa Kiswahili kwa vile yeye alikuwa ni mtaalamu wa lugha na makala yake ilikuwa inahusu lugha kama lugha na si Kiswahili. Lakini washiriki wengine kutoka nje ya Afrika ya Mashariki waliokuwa wanaongelea kompyuta na matumizi ya programu za kompyuta walitumia lugha ya Kiswahili!

Mfano mwingine ni kwamba hapa Tanzania baadhi ya magazeti yanatumia lugha ambayo inakiuka misingi ya Kiswahili sanifu tunachokielewa na ambacho tunawafunza wanafunzi wa Afrika ya Mashariki na ughaibuni. Mifano ni pamoja na matumizi ya lugha ifuatayo:

- Kumbe Bilali alikuwa anabip tu!
- Waziri kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ambaye pia alikuwa akibip..
- Chadema chatangaza kutafuta staa wa kupambana na Kikwete.
- Alifariki kitandani wakati akifanya mapenzi na demu wake
Mengine ni maneno kama vile sapoti, kumpiga sachi na kombaini.

Wakati akifunga Kongamano hilo, waziri mkuu Fredrick Sumaye, alitoa mifano mingi inayotumiwa na wabunge, kwa kuchanganya Kiswahili na Kiingereza na kuzalisha maneno ambayo si Kiswahili na wala si Kiingereza. Mfano neno kama “Kusupport” si Kiswahili na wala si Kiingereza. Haya yanafanywa na watu ambao ndio wangekuwa mstari wa mbele kukiendeleza na kukitetea Kiswahili. Bahati nzuri ni kwamba viongozi wa juu serikalini wamekuwa wakiuunga mkono matumizi ya lugha ya Kiswahili. Marehemu Mwalimu, Nyerere na Mzee Mwinyi, walikuwa mstari wa mbele. Ila lisiloeleweka hadi leo hii ni kwa nini hawakuhimiza jambo hili kuwekwa kwenye katiba, ikatambulika kisheria kwamba Kiswahili ni lugha ya Taifa. Labda hii ingesaidia zaidi kuipatia lugha hii heshima yake.
HH

Mfano mwingine ni ule aliouelezea Sangai Mohochi, kwamba Katika mkutano wa kwanza wa CHAKAMA uliofanyika mjini Arusha mwezi wa saba mwaka 2002, yalikuwepo majadiliano kuhusu maswala mbalimbali yanayohusiana na upendelezaji wa lugha. Miongoni mwa mambo yaliyotajwa na wajumbe ni uundaji wa msamiati katika lugha Kiswahili. Msemaji mmoja aliitaja istilahi moja ya Kiingereza kama pendekezo lake kuelezea dhana Fulani. Mjumbe mmoja ambaye ni profesa kutoka chuo kikuu kimoja wapo cha Afrika ya Mashariki alionekana kushangaa sana. Aliona istilahi iliyokuwa imetajwa haifai kwa dhana hiyo na akasema hivi “Waweza kuchezacheza na Kiswahili lakini si Kiingereza..” Maana yake ni kwamba Kiingereza ni muhimu sana na ni lazima kiheshimiwe zaidi ya Kiswahili au kwa maneno mengine Kiingereza ni lugha yenye misingi imara! Hayo ni matamshi ya profesa anayesema Kiswahili ni lugha yake ya taifa. Anahubiri maji akinywa mvinyo!

Mfano mwingine ni kwamba kila mwaka chuo kikuu cha Byreuth nchini Ujerumani huandaa kongamano la Kiswahili linalowakutanisha wasomi na wataalamu wengine wengi wa lugha ya Kiswahili kutoka sehemu mbalimbali za ulimwengu. Katika kongamano la 16 la Mei 2003, wajumbe walitoka sehemu nyingi, zikiwemo: Ubelgiji, Upolandi, Urusi, Uingereza, Marekani, Kenya, Tanzania, Uturuki pamoja na wenyeji wa mkutano huo Ujerumani. Makala zote zilitolewa kwa lugha ya Kiswahili isipokuwa mjumbe wa Kenya aliyetoa makala yake kwa lugha ya Kiingereza!

Mfano mwingine ni kwamba katika mkutano wa Chama cha Masomo ya Kiarika (African Studies Association) wa mwaka 2004 ulifanyika mjini New Orleans Marekani, kuliandaliwa jopo moja kuhusu lugha ya Kiswahili. Karibu washiriki sita walitoa makala kuhusu lugha ya Kiswahili. Makala zote isipokuwa moja ziliwasilishwa kwa lugha ya Kiswahili. Hiyo moja iliyotolewa kwa Kiingereza ilitolewa na profesa wa Kiswahili mzaliwa wa Afrika ya Mashariki! Hali hii ya wataalamu wa Kiswahili kutumia lugha ya Kiingereza wakati ambapo matumizi ya Kiswahili yangesaidia kudhihirisha kujitosheleza kwa lugha hiyo haijitokezi katika mawasilisho ya makongamano na mikutano mingine ya kitaaluma tu, bali pia katika uchapishaji kwa ujumla. Kwenye majarida ya kimataifa makala za kistahili zinaandikwa zaidi na wale waliojifunza Kiswahili kama lugha. Na Waswahili wenyewe wanaandika makala nyingi kwa kisingereza au Kifaransa au lugha nyinginezo za kigeni!

Changamoto ya tatu iliyojitokeza kwenye kongamano hili la Kiswahili ni kwamba kwa upande wetu hapa Tanzania, mjadala wa kutumia Kiswahili katika kufundisha ni lazima sasa ufike mwisho. Bila kufanya hivyo tutaaibishwa pale tutakapoletewa wataalamu kutoka nje ya nchi yetu, si tu kutufundisha kwa lugha yetu, bali pia kutufundisha lugha yetu! Maana kasi hii niliyoishuhudia kwenye kongamano ya wataalamu wengi wa lugha ya Kiswahili na matumizi yake katika mtandao kutoka nje ya Tanzania inatisha. Ingawa Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam, kimeonyesha jitihada ya kukiendeleza Kiswahili kwa kutengeneza programu ya kompyuta ya Kiswahili, uwiano na wale wanaofanya kazi hiyo ni ndogo. Mfano kwenye Kongamano hili tu tulikuwa na watu kutoka Amerika, Ujerumani na Finland, wanaoshughulikia programu za Kiswahili na kukiingiza Kiswahili katika kompyuta. Amerika peke yake ilikuwa na wajumbe watatu. Wote maprofesa na wote wanakifahamu Kiswahili vizuri kiasi cha kukifundisha.

Ni bahati mbaya kwamba watanzania hawakujitokeza kwa wingi kushuhudia miujiza ya lugha yao wakati wa sherehe za TUKI. Labda matangazo ya sherehe hizi hayakuwafikia wengi. Yaliweza kufika Nigeria, Uganda, Kenya, Botswana, Malawi, Rwanda, Burundi, China, Korea, Japan, Amerika, Finland, Poland, Italia, Germany, Sweden nk, yakashindwa kufika Buguruni, Tandika, Changanyikeni, Mwanza, Bukoba, Mbeya na Arusha? Ni imani yangu kwamba vyombo vya habari (kama kweli vilikuwepo) vitasaidia kusambaza ujumbe wa Kongamano kwa watanzania wote, ili wafahamu kwamba sasa hivi mjadala umefungwa. Na kama hawakubali kuufunga watalazimishwa kuufunga kwa nguvu za kutoka nje ya nchi yetu. Ni bora sasa kila Mtanzania amfahamu kwamba Kiswahili ni lugha ya kufundishia. Kazi iliyobaki ni kuliweka hili katika katiba yetu. Tukumbuke pia kwamba Titi la mama ni tamu hata kama ni la mbwa!

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment