MAKALA HII ILICHAPWA KWENYE GAZETI LA HEKO LA MAREHEMU BEN MTOBWA (Mungu amlaze mahali pema peponi) 2005.
PADRI KULAWITI; TUNAJIFUNZA NINI?
Kashifa za mapadri wa Amerika kuwanajisi watoto zilipolikumba kanisa katoliki la Amerika, Askofu Kilaini, alisikika akisema kwamba hayo ni matatizo ya Wazungu na wala si matatizo ya Kanisa la Afrika! Ndoa za mashoga zilipolitikisa kanisa la Agilikana kule Uingereza na Amerika, Askofu huyo huyo ambaye ndiye msemaji mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar-es-Salaam, alisikika tena akisema kwamba hayo ni matatizo ya Wazungu na kwamba hayo ni matatizo ya watu binafsi na wala si matatizo ya kanisa!
Wachambuzi wa mambo ya kanisa, wanajua fika jinsi Askofu Kilaini, anavyojitahidi kulitetea kanisa hata pale ambapo mambo ni wazi kiasi cha kueleweka hata kwa mtoto mdogo. Kwa mfano Askofu Kilaini, anapinga matumizi ya KONDOMU, kwa kusisitiza kwamba, mtu anayeugua ugonjwa wa kisukari ni lazima kuacha kutumia sukari, mwenye matatizo ya ugonjwa wa miguu, ni lazima kuacha kula nyama ya mbuzi, hivyo na mgonjwa mwenye virusi vya UKIMWI, ni lazima kuacha tendo la ngono!
Mungu, kwa kutaka kuonyesha ukweli, Padri wa kanisa katoliki, amefanya kitendo cha kulawiti katika Diocese iliyo chini ya uongozi wa Askofu Kilaini, Jimbo Kuu la Dar-es-Salaam. Hili ni pigo kubwa na ni fundisho. Ni wazi kama kawaida yake Askofu Kilaini, atajitahidi kupuuzia tukio hili, lakini nguvu zake za kuufunika ukweli zimepungua! Sasa ni wazi kwa watanzania wote kwamba kuwanajisi watoto si tatizo la Wazungu peke yao, ni tatizo la kibinadamu. Ndoa za mashoga si tatizo la kanisa la Anglikana peke yake, ni tatizo la dunia nzima. Pia tukio hili la padri kulawiti, limekuwa fundisho kwa Askofu Kilaini, kwamba kuachana na tendo la ngono si rahisi hivyo kama yeye anavyofikiri na kufundisha. Kama padri wake amefikia hatua ya kufanya ngono kinyume cha maumbile, itakuwaje kwa watu ambao ngono ni sehemu ya maisha yao, ni kitulizo, ni furaha, ni ubinadamu na ni msingi wa uhusiano kati ya mtu na mtu?
Watanzania wanasubiri kwa hamu kuona kama padri huyu atafikishwa mahakamani na kupata hukumu kama ile ya Babu Sea. Je, padri huyu atafungwa maisha? Mbona usiri na ukimya unaanza kulizunguka tukio hili la mtumishi wa Mungu? Mbona Tibaigana, mtu tuliyemzoea kwa kuelezea ukweli wa matukio yote ya Dar-es-Salaam, anaanza kupatwa na kigugumizi juu ya tukio hili? Au ameanza kutanguliza dini na heshima ya Kanisa Katoliki?
Watanzania wamemzoea Askofu Kilaini, Kashifa ikilikumba Kanisa Katoliki, wanafahamu majibu yake hata kabla hajaongea. Sasa hivi karibu kila mtu , Mkristu na asiyekuwa Mkristu, hata na mtoto mdogo, anajua atakavyosema juu ya Padri aliyelawiti: Kwamba hilo ni tatizo la mtu mmoja na wala si tatizo la kanisa zima! Kanisa haliwezi kufanya makosa! Na ikitokea likafanya makosa, basi makosa hayo yanalisaidia kuendelea kuwepo. Yeye kama mwanahistoria, anazoea kusema kwamba kanisa limepitia uchafu mwingi, lakini hadi leo hii bado lipo.
Hayo ndiyo majibu ya mheshimiwa Askofu Kilaini. Anatufanya tusahau kwamba kanisa linajengwa na watu! Bila watu, kanisa si kanisa! Kama watu wana shida na matatizo, ni lazima kanisa liwe na shida na matatizo. Kama watu wana furaha na neema, ni lazima kanisa liwe na furaha na neema.
Tumemsikia Askofu Kilaini, akisema kwamba Padri aliyelawiti, amesimamishwa kutoa huduma za kiroho na kuendesha ibada. Kwa maneno mengine amepata adhabu na kuwajibishwa. Lakini adhabu hii haimsaidii padri huyu, haimsaidii kijana aliyelawitiwa, haisaidii familia ya padri na kijana zilizoumbuliwa na kuathiriwa na tukio hili la aibu na wala adhabu hii haiwasaidii waumini waliokwazwa na kitendo hiki. Padri anahitaji msaada wa kiroho na wala si adhabu. Kijana aliyelawitiwa anahitaji pia msaada wa kiroho na kiakili ili kumrudisha katika hali ya kawaida. Familia za pande zote mbili zinahitaji msaada wa kiroho, kiakili na kiimani. Waumini wote na wale wote walioguswa na tukio hili kwa namna moja ama nyingine ni lazima washirikishwe katika mchakato wote wa kutibu makovu ya aibu hii ili kurudisha imani na utulivu wa kiroho katika jamii yetu.
Adhabu aliyoipata padri huyu ni utamaduni wa kanisa Katoliki wa kumthamini mtu pale tu anapotoa huduma. Ni utamaduni wa kumtumia mtu kama chombo. Katika Kanisa katoliki, padri akizeeka, akapata kilema au kuchafuka kiroho, anatelekezwa kwenye matope ya dhiki bila ya msaada wala huruma ya aina yoyote ile. Kanisa linalofundisha upendo, haki, wema, huruma na msamaha, linageuka kuwa bubu saa ya kutoa mfano inapowadia.
Hatuwezi kusema tabia hii ya padri huyu aliyemlawiti mtoto, imenyesha kama mvua. Tunasikia uhusiano wake na huyo kijana ni wa miaka mitatu. Tunaamini padri alikuwa akiungama dhambi hii kwa mapadri wenzake. Swali ni je mapadri hawa walimsaidia vipi au walikuwa wanafanya kazi ya kusafisha dhambi na kumpatia baraka kuendelea na tabia yake ya kulawiti. Walikuwa wanafanya kazi ya kumruhusu padri afumbue mdomo wake na kusema yaliyo moyoni mwake wakati wao wanaifumba midomo yao na kuzifunga roho zao? Swali jingine ni je, huyu ni padri peke yake mwenye tabia hii? Kama yeye ameweza kudumu miaka mitatu katika uhusiano huu, haiwezekani kuna wengine, lakini hawajanaswa? Kama yeye aliweza kufumbua mdomo wake na kuungama na ukweli wake ukafungwa katika giza nene la siri ya maungamo, si itakuwa ni hivyo kwa mapadri wenzake ambao wanaishi maisha kama yake, lakini hawajapata bahati ya kunaswa?
Binafsi siwezi kumlaumu padri huyu. Ametenda kosa lenye heri. Ametusaidia kugundua udhaifu ulio katika jamii yetu. Ametusaidia kutambua madhara ya upweke katika jamii na katika kanisa. La msingi ni je tumejifunza nini na tufanye nini ili tukio kama hili lisitokee tena. Tunafanya nini kusaidia padri wetu na kijana wetu aliyelawitiwa. Tunafanya nini kuzituliza na kuziliwaza familia za pande zote mbili zilizoguswa na aibu hii. Tunafanya nini kusafisha hewa mbaya katika jamii yetu. Hili liliomkuta padri linaweza kumtokea kila mtu – hakuna shujaa wa kuweka kifua mbele kwamba hawezi kuguswa na hili lililompata padri wetu. Kama si kulawiti, mtu atayatomasa matiti ya wasichana, atawanyanyasa kijinsia wafanyakazi wa kike, atafumaniwa, atakuwa na kibustani, ataingilia ndoa za watu nk. Padri huyu hayuko peke yake!
Badala ya kumsimamisha kazi, kumlaani na kumtupa kwenye shimo la wenye dhambi, ni bora tuanze kutafakari kwa kina juu ya Uhusiano wa mtu na mtu. Jambo hili linachukuliwa kijuu juu tu na wala hakuna jitihada za pekee zinazofanyika kulifundisha na kuliishi kwa pamoja kama jamii.
Uhusiano wa mtu na mtu unaanzia wapi na kukomea wapi? Je, unaweza kuhusiana na mtu kiakili bila kuhusiana naye kiroho? Je, unaweza kuhusiana na mtu kikazi bila kuhusiana naye kiakili na kiroho na bila kugusa hisia zozote mwilini mwako? Je, unaweza kuhusiana na mtu kimichezo bila kuhusiana naye kiakili, kiroho na bila kuamsha hisia zozote za kimwili? Je, unaweza kujifunua wazi kwa mtu, ukamweleza furaha yako, matatizo yako, matumaini yako na siri nyingine za moyo wako, bila kuguswa au kuamsha hisia za aina yoyote ile mwilini mwako? Je na ikitokea hisia kama mvuto wa…. Kuna kuwa na tofauti gani na kuhusiana kiakili, kiroho, kimichezo, kushikana mikono, kukumbatiana na kikazi? Je mipaka ya uhusiano ni ipi? Inawekwa na nani na inalindwa na nani? Na ni kwa nini kuwepo mipaka katika uhusiano? Je, mtu binafsi anaweza kujiwekea mipaka ya uhusiano na kuilinda au ni lazima asaidiwe na jamii inayomzunguka?
Tuchukue mfano wa padri wetu aliyeanguka kwenye tendo la kulawiti. Je uhusiano wake na huyo kijana ulianza ukiwa hivyo tangia siku walipokutana siku ya kwanza? Au walianza polepole, kwa kuhusiana kikazi, kimichezo kiakili na kiroho na hatimaye kimwili? Je, haiwezekani kwamba upweke wa padri ndio ulimsukuma kushindwa kuweka mpaka wa uhusiano kati yake na huyo kijana? Je, si ukweli kwamba padri huyu alihitaji msaada wa jumuiya iliyokuwa ikimzunguka ili imsaidie kuweka mipaka? Angejifunua wazi kwa marafiki, angeuweka wazi udhaifu wake, si angepata msaada?
Kuna ile tabia ya woga kwamba watu wakijua udhaifu wako wanakudharau na kukutenga. Lakini mfano mzuri ni wa mama zetu. Kila mama anafahamu vizuri udhaifu wote wa mtoto wake, lakini hakuna anayempenda mtu na kumthamini kama mama yake mzazi. Mtu akikufahamu vizuri anakupenda sana na kukuthamini zaidi.
Au tukiangalia upande wa ndoa. Kile kinachoitwa uaminifu katika ndoa, ni hali ya wanandoa kujenga mipaka ya uhusiano kati yao na watu wengine wanaowazunguka. Maana mtu akiolewa au kuoa, anaendelea kuhusiana na watu wengine katika jamii inayomzunguka. Atakuwa na uhusiano na wafanyakazi wenzake, wanamichezo wenzake, wanakikundi wenzake, marafiki wenzake nk. Hoja ni je anaendelea kuhusiana nao kwa kiasi gani? Ugumu unaojitokeza hapa ni kuendeleza uhusiano bila mvuto, na kama mvuto ukitokea usiambatane na kitendo! Kwa maneno mengine ni kuendeleza uhusiano na watu wengine nje ya ndoa, bila kuvunja uaminifu wa ndoa. Lakini utata mwingine unaojitokeza hapa ni je uhusiano wa mtu na mtu katika ndoa unamaanisha kummiliki mtu, kumiliki akili yake, roho yake, mwili wake, hisia zake nk.? Kiasi kwamba hisia zenu, na mvuto kwa watu wengine nje ya ndoa yenu utafanana?
Uhusiano wa mtu na mtu kiakili, kiroho, kikazi, kichama, kiurafiki nk. bila kuvunja uaminifu, bila kushirikisha sehemu zote za mwili, mikono, miguu, midomo na nyeti nyingine ni kitu kigumu ambacho mtu binafsi hawezi kukimudu. Uhusiano wa mtu na mtu ni lazima ulindwe na jamii nzima. Wale wanaojaribu kufanya kitu hiki bila kuishirikisha jamii, wana kwama. Mfano ndoa zile ambazo wanandoa wanajifungia kwenye ndoa yao, bila ya kuwa na washauri, bila kuyaweka matatizo yao wazi mbele ya ndugu na jamaa wa karibu au mbele ya waumini wenzao, wanaingia matatani. Ndoa ambazo zinatawaliwa na upweke, zinaingia matatani. Baadhi ya matata haya ni kutembea nje ya ndoa au wakati mwingine baba kufanya mapenzi na binti yake!
Hata na mapadri wanaoukumbatia upweke na kuifunga mioyo yao wanaingia kwenye matata makubwa kama yale yaliyomkumba huyu padri aliyemlawiti kijana. Tutake tusitake, ni lazima mtu ahusiane na watu wengine. Na watu hawa hawana mwisho, kwa maana kusema, sasa hesabu aliyonayo mtu inamtosha. Mungu, anaendelea kuumba, na mwanadamu ana tabia ya kuhama kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine, na kila sehemu kuna watu wapya, wenye akili mpya, roho mpya na mvuto mpya, hivyo mahusiano na watu hayakomi hadi mtu anapoingia kaburini.
Matatizo yanayojitokeza katika jamii yetu ya watoto wa mitaani, ndoa kuvunjika, ukosefu wa uaminifu katika ndoa, nyumba ndogo, vibustani, changudoa, ushoga, usagaji, kulawiti, kutoa mimba, UKIWMI na matumizi ya kondomu, chimbuko lake ni Uhusiano wa mtu na mtu! Na dawa yake si wimbo wa “sheria” kama anavyoimba siku zote Askofu Kilaini. Dawa si kuimba mafundisho ya kanisa na kwamba Kanisa Katoliki, halibadiliki. Haya ya kukazania sheria na mafundisho bila tafakuri ya kina, hayasaidii kitu, hayakusaidia juzi na jana na wala hayatasaidia leo, kesho na keshokutwa.
Msaada mkubwa ni kutengeneza mifumo ya kijamii inayoruhusu mijadala ya pamoja. Mijadala ambayo kila mtu anaweza kutoa mawazo yake, wasiwasi wake, udhaifu wake na mchango wake katika kuwasaidia wengine. Tunahitaji kutengeneza mifumo ya kuufukuza upweke mioyoni mwa watu, kuufukuza upweke kwenye ndoa, kwenye familia na kwenye jamii nzima. Bila kufanya hivyo tutamezwa na matatizo haya yanayojitokeza. UKIMWI, utatushambulia bila ya huruma, ushoga, usagaji, ndoa kuvunjika, kutoa mimba vitaenea na kuzagaa katika jamii yetu. Matatizo haya hatamwangalia padri, sista mchungaji, shehe, askofu au wenye ndoa, yatatumeza sote, vijana, wazee hata na watoto! Mwenye masikio na asikie!
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment