MAKALA HII ILICHAPISHWA KATIKA GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2005
NYERERE HAKUWA MALAIKA LAKINI………
Sina hakika kuwa kuna Mtanzania yeyote anayeamini kwamba Mwalimu Nyerere, hakufanya makosa katika maisha yake. Mwalimu, alikuwa binadamu kama binadamu wengine. Yeye hakuwa malaika. Shutuma za yule anayejiita Mzee Ludger Bernard Nyoni na Ambrose Mashaka, zilizoandikwa kwenye gazeti hili zikifuatana( Tanzania Daima ya Juni 12 na Juni 19) si za kweli. Hakuna aliyesema Nyerere hakufanya makosa. Alifanya makosa lakini heshima yake ikabaki hadi leo hii, alifanya makosa watu wakaendelea kumpenda. Hata baada ya kustaafu, aliendelea kupendwa na kupata heshima si Tanzania peke yake bali dunia nzima. Mwalimu ni marehemu, lakini bado tunaendelea kumpenda!
Mimi ninafikiri la kujiuliza ni kwa nini watu wengine wafanye makosa na kuandamwa hadi kaburini na wengine wafanye makosa, lakini wasiguswe kwa lolote. Heshima yao ibaki na mapenzi yao kwa watu yaendelee kuwa palepale? Hili ndilo la kujadili kwa kina. Mobutu, alifanya makosa na kila mtu anamlaumu hadi leo hii. Lumumba naye alikuwa na makosa yake, lakini hadi leo hii dunia nzima inamlilia na kumpatia sifa na upendo usiokoma!
Tutofautishe yule anayefanya makosa kwa kulishughulika tumbo lake, heshima yake na mali zake na yule anayefanya makosa akilitanguliza taifa lake mbele. Hawa wawili wakifanya makosa ni lazima yaangaliwe kwa macho tofauti. Mzee Kawawa, alifanya makosa hapa na pale, lakini hadi leo hii anapendwa na kuheshimiwa na watanzania wote. Kila mtu anampima mzee Kawawa kwa maisha yake, kwa uzalendo wake kwa uaminifu wake, uadilifu wake na mapendo yake kwa nchi. Hakujilimbikizia mali, hakuwa na mpango wa kuliuza taifa letu, hakuwa na uchu wa madaraka. Alilitumikia taifa letu kwa moyo wake wote – ingawa hapa na pale alifanya makosa, watu walimpima kwa moyo wake na nia yake njema.
Tutofautishe makosa ya kukusudia na kufanya kwa bahati mbaya. Tutofautishe makosa ya kufanya kwa hila na njama, na makosa ya kufanya kwa kuelekezwa vibaya au kudanganywa na watu wenye nia mbaya, wenye malengo ya kutafuta heshima, vyeo na madaraka. Mara nyingi watu wanaofanya makosa ya bahati mbaya wakati wakiwa kwenye utumishi wa Umma, wanaendelea kuishi maisha ya unyenyekevu na uadilifu hata baada ya kustaafu.
Mzee Ludger Bernard Nyoni katika makala yake anasema hivi: “ Profesa Mukandala anasema Malecela alikataliwa kugombea kwa sababu wajumbe walifuata ushauri wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, eti akiwa Waziri Mkuu, Malecela alimshauri vibaya Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi kuhusu Muungano. Kama hilo lilikuwa kosa, basi hata mzee Mwinyi mwenyewe anahusika na kosa hilo, na hakupaswa, kushiriki kikao cha kumhukumu Malecela. Si ni yeye aliyepokea ushauri huo unaoitwa mbaya? Iweje hakuna mtu hata mmoja leo anayemsema na kumhusisha na uamuzi mbovu?….”
Hili ndilo la kujadili. Kwanini Malecela alaumiwe na Mwinyi asilaumiwe? Watu wengine waliounga mkono serikali tatu mbona hawakulaumiwa? Na si hili tu wakati wa Mzee Mwinyi, kuna mambo ambayo hayakuenda vizuri sana, uchumi uliyumba na rushwa ikawa imepamba moto. Kwa vile kila Mtanzania, amegundua uadilifu wa Mzee Mwinyi, hakuna anayemgusa wala kumunyoshea kidole.
Hata kabla ya kuwa Rais wa Tanzania, Mzee Mwinyi, alifanya makosa kule Shinyanga. Hakuchelewa kuwajibika, (ni watu wachache wanaokubali kuwajibika, hata ukiwasema na kuwaandikia vitabu, bado wanakuwa kichwa maji!) na wakati anateuliwa kugombea Urais, hakuna aliyekumbuka makosa yake ya Shinyanga. Kwanini? Uadilifu wake, unyenyekevu wake, uzalendo na uaminifu wake kwa Taifa.
Hapo ndipo Bwana Ambrose achunguze hoja zake. Atokane na tabia yake ya kuwaita watu wajinga, atumie hoja kujibu hoja, si kutumia matusi kujibu hoja. Achunguze hoja hii: “ Sita, Nimewasoma wote ,na nakubaliana na hoja za Nikita Naikata. Bado ziko palepale; kwamba mgogoro kati ya Nyerere na Malecela, na ambao inadaiwa aliuandikia kitabu, ni juu ya mfumo wa serikali tatu.”
Basi kama anayoyasema Ambrose ni ya kweli watu wengi wangekuwa wakifuatwa na mzimu wa Mwalimu. Mbona mzimu huu haumwandami Mzee Mwinyi? Hata leo angetaka kugombea angepata kura! Mbona wale wote wa G 55 hakuna anayeandamwa kama Malecela?
Ndio maana mimi nikasema kwamba ugomvi wa Malecela na Nyerere, una chanzo kingine ambacho hakuna anayekijua isipokuwa Nyerere na Malecela. Ingawa Ambrose Mashaka, aliponda hoja hii kwa matusi, ukweli utabaki palepale. Bila Malecela, kusema, ukweli huo utakufa na kufunikwa na kaburi la Nyerere na Malecela! Na hii haina maana kwa vile hatujui kilichowagombanisha, tuache kujadili juu yake. Ni mambo mengi tusiyoyajua chanzo chake, lakini tunajadili juu yake na kwa kufanya hivyo tunachokoza na kuchokonoa hadi ajitokeze wa kusema ukweli na kwa hili ni Malecela, ambaye bado anaishi!
Hata kama Nyerere, alifanya makosa, leo hii kwa vile ni marehemu ndipo akina Mzee Ludger Bernard, ambaye ni mwasisi wa TANU/CCM, wanajitokeza kutuelezea makosa yake? Itusaidie nini? Walishindwa nini kumsahihisha mwalimu akiwa hai? Eti watu walikuwa wanamuongopa? Watu waoga hawezi kutusaidia kujenga Taifa letu. Walishindwa kusema Nyerere akiwa hai, sasa wakae kimya! Wakubali kuhukumiwa na historia. Kama Mwalimu alikosea basi nao waliyashiriki makosa hayo kwa kimya chao! Sisi tunamsema Malecela, kwa vile yuko hai na bado ana wajibu na mchango katika Taifa hili. Wengine wote wanaoheshimika kama Mwalimu Nyerere, Mzee Kawawa na Mzee Mwinyi, walirithisha utawala wa nchi hii wakiwa na umri wa chini ya miaka 65! Malecela, ana miaka mingapi, na bado anataka kuendelea kuwa Mbunge?
Juzi Malecela, alivunja ukimya. Kwa kile kilichoitwa kuvunja ukimya. Mbona hakuwaunga mkono wale wote wanaompigania? Amevunja ukimya kwa kuutengeneza ukimya mwingine. Amevunja ukimya kwa kutangaza kugombea Ubunge! Bado anataka kulitumikia taifa hadi kaburini, hataki kurithisha!
Huyu anayejiita Mzee Ludger Bernard Nyoni, anahoji aliyoyafanya Mwalimu, akiwa Rais, na kuuliza eti alitumwa na nani. Anajifanya haifahamu Katiba ya taifa letu inayompatia madaraka makubwa Rais. Katiba yetu ibara ya 33 hadi 46, zinaongelea madaraka ya Rais. Kama Nyerere, alifanya kinyume, basi angeshitakiwa kuivunja Katiba. Hadi anakufa sikusikia shitaka lolote juu yake la kuivunja katiba! Kumkaribisha Obote, ni kosa gani? Huyu alikuwa mkimbizi kama wakimbizi wengine. Hadi leo hii Tanzania, bado tunawatunza wakimbizi. Wakati Obote, anapinduliwa tulikuwa bado tuna Jumuiya ya Afrika Mashariki. Bila kukimbilia kwetu, angekimbilia Kenya. Hili nalo ni kosa gani? Sijasikia kwamba wanapokuja wakimbizi linaitishwa Bunge ili lifanye uamuzi wa kuwapokea au kuwakataa wakimbizi. Kuwapokea wakimbizi ni mikataba ya Umoja wa Mataifa. Tanzania ni mwanachama wa Umoja wa mataifa.
Ambrose Mashaka, anasema Nyerere, hakupinga utandawazi na Ubinafsishaji. Nisingependa kujiingiza kwenye mjadala huu bila kufahamu huyu Bwana Ambrose, anafahamu kiasi gani juu ya Utandawazi. Anafahamu kiasi gani juu ya Azimio la Arusha na Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Ni wazi Utandawazi ni ukoloni na utumwa katika sura mpya – lakini Mwalimu Nyerere alipinga vibaya sana ukoloni na utumwa na ndiyo maana aliendelea kupinga Utandawazi na ubinafsishaji. Ingawa Bwana Ambrose Mashaka, hapendi utafiti na uchambuzi wa kisayansi na kujifanya kuifahamu historia nina wasiwasi wa kutotaka kutumia matusi kama yeye, lakini mambo mengi yanampiga chenga.
Mfano, ni kweli kwamba Kingi, Mukandala na Nikita, wanatoka mkoa wa Kagera. Ambrose, haoni ni kwanini nitaje Mkoa wao kuhusiana na Malecela. Hiyo ni historia. Malecela, alipanda ngazi kutokea Mkoa gani? Ngome yake kubwa ilikuwa wapi? Hata hivyo hawa wanaomtetea na kumpinga si kwa vile wanataka kuchukua kiti chake cha Ubunge, hakuna atakayetoka Kagera na kugombea ubunge Dodoma! Wanamtetea na kumpinga kwa vile wanamfahamu vizuri kama Mtanzania na wala si kama Mhaya au Mgogo. Hilo Ambrose, halioni?
Wale wote wanaojitokeza kumtetea Malecela, ni bora wamshauri astaafu siasa na kubaki mshauri na mlezi wa viongozi chipukizi. Kwa njia hii heshima yake itabaki na kulindwa vinginevyo anatafuta mwisho mbaya.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment