Tuesday, August 02, 2005
MAKALA HII ILICHWAPWA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2005
KUTOKA TANGANYIKA KWENDA TANZANIA.
Ninaandika makala hii nikiwa Tanganyika! Nisieleweke vibaya. Mimi siko kwenye kikundi cha wale wanaotaka serikali tatu: Ya Muungano, Ya Tanganyika na ya Visiwani. Mimi ni mfuasi wa wale wanaotaka serikali mbili, ya Muungano na ya Visiwani. Pamoja na msimamo wangu huo, ukweli ni kwamba sasa hivi niko Tanganyika! Nimemaliza juma zima bila kusikia radio yoyote ile ya Tanzania! Si kwamba mimi sina uzalendo, hapana, hata ningetamani vipi kusikiliza RFA, Radio Tanzania na nyinginezo, isingewezekana! Ni bahati kwamba ninaweza kunasa radio za Rwanda na Uganda! Wale wenye uwezo kidogo, wanaweza hata kunasa luninga za Rwanda na Uganda. Kwa njia hii mtu akiwa Tanganyika, atapata habari za nchi jirani kuliko habari za nchi yake mwenyewe! Ikiwa bahati magazeti yakafika Tanganyika, basi yatakuwa ni ya siku tatu au nne zilizopita! Inawezekana kupata gazeti la siku hiyo la nchi ya jirani, lakini ndoto kupata gazeti la siku hiyo katika maeneo ya Tanganyika. Mtandao wa Voda na Celtel unapatikana kwa kupanda juu ya mti au kusimama kwenye vichuguu! Ni bahati kwamba sikuuugua, ningeshambuliwa na malaria, labda ungekuwa ni mwisho wa maisha yangu. Nimeshuhudia vifo vya watoto wadogo ambavyo kama si kuishi Tanganyika, basi watoto hao wasingepoteza maisha yao! Umbali wa kilomita 40, nauli ni shilingi 1,500 hadi 2,000! Ukilinganisha na Tanzania, ambako kwa nauli hiyo mtu anatembea zaidi ya kilometa 150! Gari dogo lenye uwezo wa kupakia watu wanne tu, linapakia zaidi ya watu kumi!
Inawezekana ile Tanganyika ya kabla ya uhuru ilikuwa bora kuliko Tanganyika ya leo. Sina maana ya kuubeza uhuru tulioupata, lengo langu ni kubeza hali ya kuangalia maendeleo ya upande mmoja tu. Maendeleo ya Tanzania, maendeleo ya mijini, maendeleo ya watu wachache, bila kuangalia maendeleo ya taifa zima la Tanzania.
Si nia yangu kuweka chumvi, lakini soda inayonunuliwa kwa shilingi 200 Tanzania, hapa Tanganyika inanunuliwa shilingi 350! Chupa ya bia inayonunuliwa shilingi 900 hadi 1000 kule Tanzania, hapa Tanganyika, inanunuliwa 1,300!
Tanganyika hakuna maji. Hakuna umeme na hakuna huduma nyingi muhimu. Watu wanatembea zaidi ya kilometa 5 hadi 10 kutafuta maji. Wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, mbunge wa Tanganyika, alitoa ahadi ya kusambaza maji kwenye jimbo lake, sasa miaka kumi imepita bila ahadi hii kutekelezwa! Mbali na ahadi hii ya maji kuna ahadi nyingine zilizotolewa, ahadi ambazo zinafanana na nyingine zinazotolewa kwenye maeneo mengi ambayo yanajumuika kuitengeneza Tanganyika, iliyo tofauti na Tanzania.
Hakuna barabara ya lami Tanganyika. Sasa hivi wakati wa kiangazi ni vumbi mtindo mmoja. Udongo wenyewe ni mwekundu, hivyo sasa hivi kila kitu ni rangi nyekundu. Wakati wa mvua vumbi inageuka kuwa matope na kusababisha utelezi na kukwamisha usafiri.
Nimeongea na watu mbali mbali wa hapa Tanganyika. Maoni yao hayatofautiani na yale ya Watanganyika wengine wanaoishi maeneo mengine ya Tanganyika. Wengi wao wana maoni kwamba Tanzania, ni mijini na Tanganyika ni vijijini. Hata hivyo wale waliofanikiwa kutembea sehemu mbali mbali za nchi yetu wanatofautisha vijiji na vijiji. Wanasema huwezi kulinganisha vijiji vya mkoa wa Kilimanjaro na vijiji vya mikoa mingine mfano na vya Tanganyika, hii niliyomo. Lakini kwa ujumla vijiji vingi vya Tanzania, vinaishi Tanganyika! Havina tofauti kubwa, matatizo yanafanana: Ukosefu wa barabara, umeme, maji na huduma nyingine kama hospitali na shule bora.
Umeme, utaukuta mijini, ingawa miji mingine haina umeme wa uhakika, lakini unawaka. Maji ya bomba utayakuta mijini, ingawa pia, miji mingine usambazaji wa maji ni wa matatizo, lakini huduma hii inapatikana ukilinganisha na wale wanaoishi Tanganyika. Huduma ya hospitali zenye uhakika, unazikuta mijini. Shule zenye huduma nzuri unazikuta mijini. Jitihada zote za maendeleo zimeelekezwa mijini. Ingawa ukweli unabaki pale pale kwamba asilimia ya watanzania walio wengi wanaishi vijijini.
Kishawishi cha wale walio wengi ni kufanya safari ya kutoka Tanganyika kwenda Tanzania. Kutoka vijijini kwenda Mijini. Hii ni safari ambayo sasa hivi ni vigumu sana kuizuia.
Jambo linaloshangaza, ambalo mpaka sasa sina jibu lake ni kwamba, kule Tanzania, ambako kuna huduma za kila aina, kule ambako uchumi wake ni mzuri kiasi, kila kitu kinakuwa na bei nafuu. Lakini Tanganyika, ambako huduma ni mashaka, uchumi unachechemea, watu wana maisha magumu, kila kitu ni cha bei ya juu. Sukari bei juu, mafuta ya taa bei juu, soda bei juu, nauli bei juu! Inakuwaje wenye kipato wanunue vitu kwa bei ya chini na wale wasiokuwa na kipato walipe bei ya juu?
Ni nani atafika Tanzania, atamani kurudi Tanganyika? Sasa hivi kuna mipango ya kuwakusanya vijana wote wanaoishi mijini bila kazi kuwasukuma vijijini. Eti waende wakalime! Kwa maana nyingine watoke kwenye maisha nafuu na kwenda kwenye maisha ya juu. Watoke kule ambako vitu vinanunuliwa kwa bei ya nafuu, waende kule ambako vitu ni bei ya juu.
Kwa muda wa juma moja nilioishi Tanganyika, nitapinga kwa nguvu zangu zote nikisikia mpango wa kuwarudisha vijana vijijini. Warudi kule kufanya nini? Kwa nini tuwalazimishe vijana wetu kuendelea kuishi Tanganyika, wakati neema zote ziko Tanzania? Kwani vijana waendelee kuishi vijijini wakati maisha ya neema yako mijini?
Sasa hivi ni kipindi cha uchaguzi. Wale wote wanaotegemea kugombea nafasi za ubunge wanaikimbia Tanzania na kuelekea Tanganyika. Wanakuja na ahadi nyingi za maji, barabara, shule, mahospitali nk. Baada ya uchaguzi, wanaanza tena kukiikimbia Tanganyika na kuelekea Tanzania! Tanganyika, ni maandalizi ya Tanzania! Vijiji ndivyo vinavyoandaa maisha bora na yenye neema ya mijini. Na kwa bahati mbaya vijiji hivyo vinaendelea kuogelea katika dimbwi la umasikini!
Mtu yeyote kama yupo, atakayetaka kuzuia wakimbizi wa kutoka Tanganyika, kwenda Tanzania, ni lazima afanye jitihada kubwa ya kuitokomeza Tanganyika. Jitihada ya kueneza huduma muhimu nchi nzima. Jitihada za kuleta neema na maisha bora sehemu zote za nchi yetu, iwe vijijini na wala si mijini. Isitokee soda inayonunuliwa shilingi 200 sehemu moja ya nchi iuzwe shilingi 350 sehemu nyingine ya nchi ileile. Isitokee watu kufa kwa kushindwa kupata huduma ya hospitali. Isitokee sehemu moja ya nchi watu wanakula na kusaza na kutupa wakati sehemu nyingine ya nchi watu wanakufa kwa
njaa.
Hizi siku nilizomaliza hapa Tanganyika, nilijawa na mawazo mengi kichwani mwangu. Hivi viongozi wetu wanaotaka kuchaguliwa kuliongoza taifa letu wanafahamu kwamba nchi yetu bado imegawanyika katika sehemu mbili kubwa? Wanajua kwamba bado tuna Tanganyika na Tanzania? Wanajua kwamba kuna watanzania ambao bado hawana huduma ya maji, umeme, hospitali, mashule na hawana chakula cha kutosha? Wanajua kwamba watu wengine wanaishi kwenye neema kubwa wakati wengine wanaishi kwenye Jehanamu? Na je, wana sera gani ya kutokomeza matabaka haya ambayo yanaendelea kuongezeka? Na, je ni lini tutaimaliza safari hii ya kutoka Tanganyika kuelekea Tanzania? Ni lini Tanzania, itakuwa moja, yenye neema, amani na maisha tele?
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment