MAKALA HII ILICHAPWA KWENYE GAZETI LA RAI 2005.
JE, NA HILI NI KOSA LENYE HERI?
Isieleweke kwamba ninasimama kumtetea padri aliyelawiti. Kama kuna utetezi wa aina yoyote ile juu ya padri huyu, mimi nitakuwa mtu wa mwisho kujiingiza kwenye utetezi huo. Punguani peke yake ndiye anayeweza kujiingiza kwenye utetezi wa mtu aliyemlawiti na kumdhalilisha kijana aliye chini ya miaka kumi na minane. Kumtetea mtu aliyelawiti, ni sawa na kumtetea mtu aliyefanya tendo la ngono na binti yake au mtoto wa kiume kumlala mama yake; ni sawa na kumtetea mtu aliyefanya tendo la ngono na ndugu yake wa damu au kumtetea mtu aliyempanda mbuzi au mnyama yeyote yule kwa lengo la kutuliza hamu na tamaa zake za kimwili. Kulawiti ni kinyume na maumbile, ni kinyume na maadili, ni kinyume na utamaduni wetu, ni uzinzi, ni dhambi, ni aibu nk.!
Ingawa mimi si mtetezi wa padri aliyelawiti, siwezi kukaa pembeni na kushangilia. Siwezi kusema ngoja apate, siwezi kusema ngoja aumbuke. Mwenzako akinyolewa, wewe tia maji. Kilichompata padri huyu kinaweza kumtokea kila mtu. Ni sawa na mwizi wa usiku, ni sawa na kupitiwa, kulewa na kutenda yasiyokubalika katika jamii, kuchanganyikiwa au kupagawa. Kwa mtizamo huu, hakuna shujaa, hakuna wa kumteta mwenzake. Unabaki ukweli kwamba anayekamatwa ndiye mwenye kosa! Maana kama mtu hakukumbwa na kashfa ya kulawiti, anaweza kukumbwa na kashfa ya kusagana, au kutomasa matiti, kuingilia ndoa za watu, kuwa na kibustani, kuzaa watoto na kuwatelekeza au kufanya matendo mengine yasiyokubalika katika jamii. Kila mtu ana tabia ambayo kama si kuitekeleza kwa siri, haiwezi kukubalika katika jamii. Hata na padri huyu alikuwa na tabia yake hii ya kulawiti zaidi ya miaka mitatu. Aliendeleza bila kugundulika. Kama si kupitiwa na kufanya mambo yake kwenye gari, labda angeendelea miaka mingi tu. Hivyo ndivyo kila mmoja wetu anavyotunza tabia zake mbaya rohoni mwake. Mwenye bahati mbaya kama ya huyu padri anakamatwa. Mwenye bahati nzuri anaendelea na tabia zake mbaya hadi kaburi linapoteza ushahidi!
Lakini pia isieleweke kwamba mimi ninasimama kumlaumu, kumhukumu na kumlaani padri aliyelawiti. Kama kuna haja ya kumuhukumu, kumlaumu na kumlaani, mimi nitakuwa wa mwisho kufanya hivyo. Unajua anapokamatwa mwizi, wale wanaompiga hadi kufa ni wezi wenzake. Mwizi au kibaka anachukia sana mwizi mwenzake anapokamatwa: Kuna hatari ya kuwataja wezi wengine, kuna hatari ya kufichuliwa mipango ya wezi na kuvuruga zoezi zima la wezi; ili kufunika yote hayo, akikamatwa mwizi, wezi wenzake wanaona njia bora ya kuendelea kutunza siri ni kuyamaliza maisha ya mwenzao aliyekamatwa! Anapigwa hadi kufa bila huruma. Mwizi hodari hakamatwi, kukamatwa ni uzembe na kutowajibika ipasavyo. Hivyo akikamatwa mwizi anahukumiwa kifo na wezi wenzake!
Akikamatwa mchawi, wanaokuwa wa kwanza kumlaumu na kumlaani ni wachawi wenzake na wakipata nafasi nzuri wanayamaliza maisha yake kabla hajapata nafasi ya kuelezea mengi juu ya uchawi.
Akifumaniwa mtu, wanaojikusanya haraka kumzomea na kusambaza habari ni wale ambao tabia yao ni kuziingilia ndoa za watu. Ili wasishukiwe, wanakuwa mstari wa mbele kulaani kitendo na waliokitenda. Utawasikia wakisema kwa hasira:
“Mwalimu! Mwanamke huyu alifumaniwa katika uzinzi. Katika Sheria yetu Musa alituamuru mwanamke kama huyu apigwe mawe. Basi, wewe wasemaje”. Sawa na wezi au wachawi, ukiwahoji wale wanaotoa hukumu kwa mtu aliyevumaniwa:
“ Mtu asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza kumtupia jiwe”.
Nafsi zao zitawasuta, hakuna atakayekuwa na nguvu za kuamsha mkono na kutupa jiwe, hakuna atakayeendeleza hukumu wala kusema chochote, wote watatawanyika na kupotea kiasi cha kuacha swali:
“ Mama, wako wapi wale watu? Je, hakuna hata mmoja aliyekuhukumu?”
Na hapo hakutakuwa na kitu kingine zaidi ya yale maneno:
“ Wala mimi sikuhukumu. Nenda zako; na tangu sasa usitende dhambi tena.”
Kwa ufafanuzi zaidi soma Yohana 8:1-11.
Kama mimi si mtetezi wa padri aliyelawiti na wala si shabiki wa kukaa pembeni na kushangilia yaliyotokea. Na kama mimi siko upande wa wanaohukumu, kulaumu na kulaani ni kwa nini niandike? Kwanini basi tukio hili liniguse kiasi cha kushika kalamu na kuandika. Kwanini linipotezee muda wangu wa kufikiri na kutafakari?
Ninaandika kuuliza maswali. Ninaandika kutafakari! Ninaandika kuchokoza mawazo na kuchochea majadiliano: Je, kosa la padri kumlawiti kijana ni kosa lenye heri? Je, wakati umewadia wa kujadili useja wa kanisa katoliki na kutafuta maana yake na faida yake katika jamii ya Kitanzania? Je, wakati umefika wa kufikiria muundo mpya wa maisha ya mapadri ;mapadri waishi miongoni mwa jumuia na kuchanganyikana na watu ili kuufukuza upweke unaowazunguka katika nyumba zao? Je, wakati umefika wa kulijenga kanisa kama familia? Kulijenga kanisa linalosikiliza, linalojali na kuwakumbatia watu wote katika udhaifu wao? Je, wakati umefika wa kuacha tabia ya kulaumiana, kushitakiana, bali kuchukuliana na kuvumiliana? Tunajifunza nini kutokana na tukio hili la padri kulawiti?
Ninajua mada hii ilivyo nyeti. Ninajitahidi kuandika kwa uangalifu mkubwa na kwa kupima kila neno. Kabla ya kuandika makala hii nimepitia kwa makini maoni ya Herbert Thurston, kwenye “The Catholic Encyclopaedia” juu ya “History of Clerical Celibacy”. Pia nimepitia aliyoandika Papa Paulo wa sita, mwaka 1967 mwezi wa Juni tarehe 24 juu ya “On the Celibacy of Priest”, “Celibacy Isn’t a problem”, iliyoandikwa na Kadinali John.J. O’connor na yale aliyoyaandika Kadinali Ratzinger 1986, ambaye sasa hivi ni Papa Benedict wa 16: “On The Pastoral Care of Homosexuals”.
Maandishi yote hayo hayakunipatia jibu la swali langu la tunajifunza nini kutokana na tukio la Padri Kulawiti. Nina maana jibu ambalo linaweza kumsaidia Mtanzania. Jibu linaloendana na maisha yetu ya kila siku, katika utamaduni wetu, mila zetu na imani zetu. Jibu la kuzingatia maadili na makuzi yetu ya leo na ya vizazi vijavyo. Jibu linaloweza kuwa kitulizo kwa familia ya Padri na kijana aliyelawitiwa. Jibu linaloweza kuwa kitulizo na kurudisha imani na amani ya waumini waliokwazwa na tukio hili. Jibu ambalo linaweza kuitibu na kuirekebisha roho ya padri na kuirudisha heshima ya kijana aliyelawitiwa. Jibu lenye busara, hekima, wema na huruma.
Watu walio makini katika jamii, watu wanaoongozwa na tukio baada ya tukio, hawapuuzii tukio lolote katika jamii. Kila tukio lina fundisho na kila tukio ni chanzo cha kupiga hatua katika maisha. Kuna ukweli kwamba hakuna tukio katika jamii linalosimama peke yake bila kuwa kwenye mchakato mzima wa msuko wa maisha ya jamii. Kama wasemavyo Waswahili kwamba hakuna msiba usiokuwa na mwenzie.
Watu walio makini katika jamii, wana tabia ya kujifunza kutokana na matukio. Mfano matukio kama wizi, uchawi na kufumaniwa katika jamii, yanasaidia kuonyesha udhaifu wa jamii. Yanasaidia jamii kuona pale inapokwenda tenge. Kama kuna mwizi katika jamii, kutakuwa na watu wengi wanaouzunguka wizi huu. Kuna wanaonufaika kutokana na wizi. Kuna ambao ni chanzo cha wizi katika jamii. Kuna ambao kama wangewajibika ipasavyo wizi usingetokea. Kama kuna nafasi ya kutafakari na kuhoji utakuta watu wengi wanahusika kwa namna moja ama nyingine katika matendo ya wizi katika jamii. Kwa bahati mbaya jamii zetu zimeendelea kuwa ni jamii za watu wasiokuwa makini vya kutosha. Mwizi ni mwizi, na nafasi yake ni magereza. Hatujawa na muda wa kutafuta chanzo cha wizi. Kwa vile mwizi anakuwa amezungukwa na watu wengi na kwa vile vyanzo vya wizi haviwekwi wazi, mwizi anakwenda gerezani lakini wizi unaendelea!
Tunakuwa wepesi wa kuhukumu, kulaumu na kulaani bila kufanya jitihada ya kutafuta chazo cha matatizo yaliyo katika jamii na kutafuta dawa ya kuponya matatizo hayo. Matokeo yake matatizo yanaendelea kuwa mengi katika jamii yetu. Wizi, ujambazi, rushwa, kulawiti, kusagana, uzinzi wa aina mbalimbali n.k. vinaongezeka kila kukicha.
Mfano padri wetu waliyelawiti yuko mahabusu, labda atahukumiwa kifungo cha maisha, amesimamishwa kuendesha ibada, lakini huku nyuma yake, kulawiti kunaendelea. Kwa maana nyingine kule kumfunga na kumsimamisha kazi za uchungaji wa roho za waumini si msaada wa tatizo lililo mbele yetu katika jamii. Au kumfunga na kumsimamisha utumishi wa kiroho kunasaidiaje kuponya makovu na aibu iliyozikumba familia za padri na kijana aliyelawitiwa, inasaidiaje kurudisha imani na amani ya waumini waliokwazwa na tukio hili? Huyu Padri, ana kilema. Anahitaji msaada wa pekee. Anahitaji mtu wa kuwa karibu naye na kuingia moyoni mwake na kumbadilisha. Kazi hii haiwezi kufanywa na gereza wala adhabu ya kumsimamisha kazi za kutoa huduma za kiroho. Kazi hii inahitaji upendo, uwazi na huruma. Hii si kazi ya mtu mmoja, ni kazi ya jamii nzima. Ni kazi ya waumini wote wakishirikiana na viongozi wao.
Ndio maana mimi ninauliza kama kweli hili ni kosa lenye heri. Anayefanya kosa si mtu wa kulaumiwa, bali ni mtu wa kushukuriwa. Yeye kwa kufanya kosa, macho yetu yanafumbuka. Mfano sasa hivi hakuna ubishi tena kwamba kulawiti ambako ndio kunaelekeza kwenye ndoa za mashoga ni jambo ambalo limeota mizizi katika jamii yetu. Kama Padri ameweza kufanya hivyo, itakuwaje kwa waumini? Ni wazi sasa kwamba tatizo hili tunalo. Hatuwezi kukwepa kuliongelea na kulijadili. Hatuwezi kulifunika tena. Liko wazi mbele ya macho yetu.
Je, hili ni kosa la padri peke yake? Hakuna watu wengine wanaolizunguka kosa hili? Haiwezekani hili likawa kosa la padri na kinaja aliyelawitiwa. Kama padri huyu alikuwa akiuungama, na ni lazima tuamini kwamba alikuwa akiungama maana haya ndio alikuwa akifundisha na kuyaishi, alisaidiwa vipi na huyu aliyekuwa akimwongoza kiroho? Hapa ni lazima kuhoji umaana na umuhimu wa sakramenti ya kitubio. Mwenye makosa anafumbua mdomo na kutoa yote yaliyo moyoni mwake, lakini anayeungamisha na kusamehe dhambi anafumba mdomo wake. Anasafisha dhambi bila kufanya kazi ya kurekebisha, anasafisha dhambi bila kuleta mabadiliko. Anasafisha dhambi bila ya kumkabidhi mwenye dhambi mikononi mwa jumuiya nzima ili imsaidie. Matokeo yake mwenye dhambi, anasafishwa, lakini anaendelea kutenda dhambi kwa matumaini ya kurudi kule kule kwa mwenye uwezo wa kusafisha dhambi – kinachoendelea ni mwenye dhambi kuendeleza matendo yake hadi anapoumbuka na kudhalilika mbele ya jumuiya kama ilivyokuwa kwa padri wetu.
Hivyo dhambi ya mtu mmoja inawagusa watu wengi. Kwa swala la huyu padri, kuna wengi wanaohusika: Mapadre wenzake, Askofu wake na waumini. Padri huyu ni muhanga wa mifumo isiyokubali kubadilika na kuukubali ukweli. Mfano, kama sakramenti ya kitubio ingefanya kazi ya kusafisha, kurekebisha na kushughulikia chanzo cha dhambi, basi padri wetu aliyelawiti asingefikia hatua aliyoifikia.
Mimi ninaliona kosa hili la kulawiti, kama kosa lenye heri, ni lazima sasa kanisa lijifunze kwamba kuna ulazima wa kujenga mifumo ambayo waumini na viongozi wao wa kiroho wanaweza kusaidiana na kuelekezana katika maisha. Kuna haja ya kutengeneza mifumo iliyo wazi zaidi. Mifumo ambayo itasaidia kuongoza uhusiano wa mtu na mtu, jirani na jirani na familia kwa familia. Ni lazima ibuniwe mifumo ya kuufukuza upweke katika mioyo ya watu, upweke katika familia na upweke katika jamii nzima.
Upweke, ukimkumba mtu ni lazima afanye na kutenda yale yasiyotarajiwa katika jamii. Upweke, ukiikumba familia, ni lazima familia hiyo isambaratike. Na upweke ukiikumba jamii, ni vita na kumwaga damu kama vile ilivyotokea Rwanda mwaka wa 1994. Upweke ni adui mkubwa wa mwanadamu. Ndio maana theolojia ya Kikristu inakazania Mungu, asiyekuwa mpweke. Mungu wa utatu mtakatifu. Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu. Kwamba, anachokifanya Mungu Baba, anakijua Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu. Na kwamba nafsi hizi ni tofauti na zina kazi tofauti lakini ni kitu kimoja na zinafanya kazi kwa ushirikiano, ni Mungu Mmoja.
Lakini pia ni wakati wa Kanisa Katoliki kuona kwamba kuna haja ya kufanyia mambo mbali mbali mabadiliko. Mfano sakramenti ya kitubio ni lazima irekebishwe kiasi kwamba inaweza kumsaidia mtu kiasi kizima na kuisaidia jamii.
La msingi zaidi ni ile haja ya kufungua milango ya theolojia na majadiliano ya wazi juu ya imani. Ni wakati wa kuifanya imani ikajisikia nyumbani hapa Tanzania. Mambo mengi yanayoleta maswali na utata yaelezwe kwa lugha ya kawaida inayoweza kueleweka kwa watu wote. Mfano useja wa mapadri uelezwe vizuri. Kwamba mapadri waruhusiwe kuoa si jibu la tatizo. Maana hata wale waliofunga ndoa kanisani wanashindwa kujifunga kwenye sheria ya mke mmoja mme mmoja. Tatizo si useja na wala jibu si ndoa. Kinachogomba hapa ni swala zima la uhusiano kati ya mtu na mtu. Ni kiasi gani jamii yetu inamruhusu mtu kuhusiana na watu wengine. Uhusiano unaanzia wapi na kuishia wapi? Ni uhusiano upi unakubalika na ni uhusiano upi haukubaliki? Hili ni lazima liwe ni jambo la kujadiliwa na jamii nzima kwa uwazi na uhuru unaoigusa roho ya kila mwanajamii.
Ni wakati wa kutambua kwamba sote ni binadamu, sote ni dhaifu na ni lazima tusaidiane ili tuweze kusimama imara katika kulinda maadili, imani, utu wetu na kumtukuza muumba wetu.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment