JABIR IDRISSA

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2005.

JABIR IDRISSA

Nimeshangazwa sana na mahojiano baina ya Waziri wa Habari wa Zanzibar na BBC kuhusiana na mwandishi Jabir Idrissa. Waziri wa Habari wa Zanzibar, anasema Jabir, amezuiwa kuandika makala zake kutoka Zanzibar, kwa vile hana cheti, kibali au kwa maneno mengine hayuko kwenye orodha ya waandishi wa habari wa Zanzibar, wanaotambulika! Kufuatana na maelezo yake Jabir, amekuwa akiandika kwa kuvunja sheria ya habari ya Zanzibar. Sheria hiyo ilitajwa na kifungu chake, mimi sikuona umuhimu wa kuikumbuka!

Sitaki kujifanya mtaalam wa sheria. Inawezekana kweli Jabir Idrissa, amevunja sheria ingawa si kwamba ameanza kuandika leo! Amevunja sheria au hakuivunja sheria hiyo ni kazi ya mahakama! Ukweli ni kwamba mtu yeyote aliyesikiliza mahojiano hayo atakubaliana na mimi kwamba sababu zilizotolewa hazijitoshelezi. Zilielekea kuwa sababu za kisiasa zaidi ya sababu za kulisaidia taifa letu na watu wake!

Kinachonishangaza ni kuona Waziri wa habari, anashindwa kutofautisha kati ya mwandishi wa habari anayetoa “Hard story” na mwandishi anayeandika kuchambua mambo Fulani katika jamii. Hili ndilo ninataka kuongelea. Hivi ni vitu viwili tofauti. Kuandika habari na kuchambua habari si kitu kile kile. Ninafikiri hapa tunahitaji msaada wa wataalam waliobobea katika uandishi wa habari ili watusaidie kuondoa utata huu ambao inaelekea utakwamisha maendeleo ya Taifa letu na kurudisha nyumba demokrasia na uhuru wa vyombo vya habari.

Unajua Kiswahili chetu ndio hivyo bado kina misamiati michache. Watu wamekuwa wakichanga mambo haya. Mwandishi wa habari na mwandishi wa makala wote wanaitwa waandishi wa habari. Ni kweli kwamba wote ni waandishi, lakini uandishi una aina mbali mbali na sheria mbali mbali. Huwezi kumlinganisha mwandishi wa habari (hard story) kwenye gazeti na mwandishi wa vitabu au mwandishi wa mashairi, tenzi, barua na nyimbo.

Jabir, alikuwa akiandika makala na wala si “Hard Story”. Yeye alikuwa hafanyi kazi ya kutoa ripoti juu matukio, bali alikuwa akichambua, akichokoza mawazo na kuchochea watu kufikiri na kutafakari juu ya matukio mbali mbali katika jamii yetu. Mtu kufikiri, kutafakari na kushirikisha wengine yale aliyoyatafakari anahitaji cheti gani, kibali gani, orodha gani na sheria gani? Kuandika makala ni sawa na kuandika kitabu. Tuna vitabu vingi vya hadithi vyenye mafundisho na uchambuzi wa mambo mbali mbali. Waandishi wa vitabu hivi wanapata kibali gani na kuifuata sheria gani?

Kuandika makala ni sawa na kutunga mashairi. Tuna watu wengi wanatunga mashairi mbalimbali kuhusu siasa, uchumi, dini, maadili, malumbano na wakati mwingine matusi. Washairi hawa ni wengi na wanaandika kwenye magazeti mbali mbali. Wanapata kibali gani na kuifuata sheria gani?

Kuandika makala ni sawa na kutunga mchezo wa kuigiza kama ile tunayoiangalia kwenye Luninga, mfano kama Wingu, Sayari, Taswira, Uhondo wa Ngoma, Jakamoyo nk. Watunzi wa michezo hii wanapata vibali gani na kuifuata sheria gani?

Kuandika makala ni sawa kutunga wimbo unaochambua mambo mbali mbali katika jamii. Saida Karoli, anapotunga nyimbo zake, anapata kibali gani na kufuata sheria gani? Kuna nyimbo mpya za kizazi kipya zinachipuka kila kukicha na zimesheheni ujumbe na uchambuzi mzito. Nyimbo hizi zinaimbwa kwenye redio, kwenye luninga – zinawafikia watanzania wote. Vijana hawa wanapata kibali gani na wanafuata sheria gani.

Kuandika makala ni sawa na kutunga wimbo wa taarabu. Zanzibar inajulikana kwa taarabu. Tujuavyo taarabu zina ujumbe mwingi, vijembe, matusi, siasa, uchambuzi, kusifia serikali, kuibeza serikali nk. Watunzi wa taarabu wanapata vibali gani na wanafuata sheria gani?

Kuandika makala ni aina fulani ya usanii kama vile kuchonga vinyago au kuchora picha. Jinsi makala inavyotoa ujumbe ndivyo hivyo hivyo vinyago na michoro vinatoa ujumbe. Vinyago vingi vinabeba ujumbe mzito. Kwa mtu anayeguswa na usanii atapata ujumbe sawa na yule anayesoma makala kwa kuangalia tu kinyago. Watu wengi wanapenda kuangalia katuni kwenye magazeti – mara nyingi katuni zinabeba ujumbe mzito, nyingine zinasifia serikali, nyingine zinaichambua serikali, nyingine za kuchochea na nyingine za kuunga mkono jitihada za serikali. Hawa wanaochora katuni wanapata vibali gani na kufuata sheria gani?

Kuandika makala ni sawa na mtu kutoa maoni yake kwenye redio au luninga. Tunasikia watu wakihojiwa kwenye redio mbali mbali. BBC, VOA, Sauti ya Ujerumani nk, hawa wanapata vibali gani na wanafuata sheria gani. Barua za maoni tunazozisikia kwenye redio mbali mbali zinaandikwa kwa kibali gani na kwa sheria gani?

Makala ni barua ya maoni iliyoandikwa kwa urefu, kwa kuzingatia utafiti, ukweli na umuhimu wa mada inayozungumziwa. Katika gazeti la RAI, makala ya Jabir Idrissa, inaitiwa Waraka Kutoka Unguja. Makala ni barua ya wazi kwa jamii. Ni kibali gani na sheria gani inahitajika kwa mtu kuandika barua kwa rafiki zake, ndugu zake na watanzania wenzake?

Kuandika makala kwenye gazeti ni sawa na kuandika makala kwenye Blogu ndani ya mtandao. Watu wanaoandika makala kwenye Blogu zao ndani ya mtandao wanapata kibali gani na wanafuata sheria gani? Jabir, anazuiwa kuandika kwenye magazeti, lakini makala zake zitawekwa kwenye mtandao. Ni vigumu kuingia kwenye mtandao na kuzizuia makala za Jabir. Ni imani yangu kwamba watanzania wengi sasa hivi wanasoma habari ndani ya mtandao. Hali hii ya kumzuia Jabir, kuandika inaonyesha jinsi Serikali ya Zanzibar ilivyobaki nyuma ya wakati na bado inakumbatia mifumo ya kizamani.

Kama kuna sheria ya kumzuia mtu kufikiri, kutafakari kuwa mbunifu na kuwashirikisha wengine, tafakari zake na ubunifu wake, basi sheria hiyo ni batili na imepitwa na wakati. Si sheria ya kuitumia wakati huu. Tutachekwa na dunia nzima!

Wito wangu ni kwa vyombo vya habari vyote kushirikiana kumtetea Jabir. Kuruhusu hili litendeke Zanzibar, ni kuliruhusu litendeke bara pia. Kuliruhusu hili litendeke kwa Jabir, ni kuliruhusu litendeke kwa mwingine pia. Vyombo vya habari vionyeshe ushirikiano wa kutetea uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa watu kutoa maoni bila vitisho.

Siwezi kushangaa kusikia kwamba Jabir Idrissa, si Mzanzibari. Hizi ndizo silaha za watu walifilisika kisiasa, watu wasioheshimu uhuru wa vyombo vya habari na haki ya mtu kujieleza na kutoa mawazo.

Leo ni Jabir Idrissa, jana ilikuwa Nabwa na kesho ni mwingine. Ni lazima tufikie mahali tukue, tutoke katika utoto na ujinga wa kisiasa. Dunia yetu imeingia kwenye utandawazi kiasi ni vigumu kuendelea kucheza michezo ya kitoto. Utamzuia mtu kuandika kwenye gazeti, lakini huwezi kumzuia kuingia kwenye mtandao na kuendelea kueneza mawazo yake dunia nzima.

Binafsi ninaona, badala ya kumfungia Jabir, kuandika, kitu ambacho hakina maana yoyote ile zaidi ya kuonyesha ulimwengu kwamba sisi bado tuko gizani, ni bora angejitokeza mtu kule Zanzibar, wa kukanusha yote anayoyaandika Jabir. Kwa njia hii kutazuka mjadala na majadiliano na mwishowe ukweli utajitenga na Uongo.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment