ILANI INAYOJALI NI NYENZO YA MABORESHO

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2005.

ILANI INAYOJALI NI NYENZO YA MABORESHO

Mwezi huu mwanzoni zilifanyika sherehe za Serikali za mitaa. Sherehe hizi zilikuwa za pekee kwa vile ilikuwa ni mara ya kwanza kufanya tathimini ya mfumo wa maboresho unaoendeshwa katika Serikali za mitaa nchi nzima. Lengo kubwa la maboresho katika mfumo wa serikali za mitaa ni kuyapeleka madaraka kwa wananchi. Ni kulenga katika kubadilisha mfumo uliokaa kichwa chini miguu juu; ni jitihada za kuweka mambo sawa kwamba serikali inawajibika kwa wananchi. Mfumo wa maboresho unakazia utawala bora, ushirikishwaji, majadiliano, vita dhidi ya rushwa nk.
Bahati nzuri sherehe hizi zilifanyika katika kipindi ambacho nchi yetu inaelekea kwenye uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani. Ni wakati mzuri wa watu kujifunza na kujiandaa kufanya uchaguzi kwa uangalifu na kwa malengo ya kuliendeleza taifa letu.

Wakati sherehe za Serikali za mitaa zikiendelea, kijana mdogo Deusdedit Jovin, alitoa kitabu chenye jina la: Ilani ya Uchaguzi Inayojali 2005. Kitabu hiki kimechapwa na Ruvu Publishers ya Dar-es-Salaam, na hivi sasa kinauzwa kwenye duka zote za vitabu. Sina hakika kama Deusdedit, alikuwa anafikiria sherehe za Serikali za mitaa wakati akiandaa Ilani hiyo. Nijuavyo mimi na kama ambavyo mtu atakayesoma kitabu cha Ilani hii na kugundua ni kwamba madumuni ya Ilani hii ya Uchaguzi ni manne. Kwanza, inalenga kuwawezesha wapiga kura kutathimini historia ya kila mgombea katika nyanja zake kisiasa; kuwawezesha wapiga kura kutathimini usahihi wa sera za Ilani za Uchaguzi; kuwawezesha wapiga kura kujua na kuelewa haki, wajibu na majukumu ya raia katika nchi yao na kuwawezesha raia kujua na kuelewa haki na majukumu ya serikali katika dola. Malengo mawili ya awali ni ya muda mfupi kuelekea uchaguzi utakaofanyika mwezi wa Oktoba. Malengo mawili yanayofuata ni ya muda mrefu kuelekea majukumu ya uraia.

Inawezekana kitabu hicho kutoka wakati wa sherehe za Serikali za mitaa ilikuwa ni bahati tu. Ambalo halitiliwi shaka ni kwamba Deusdedit, analenga kwenye uchaguzi unaokuja. Uchaguzi mzuri ni nyenzo kubwa ya serikali za mitaa. Uchaguzi mzuri utayaboresha maboresho. Uchaguzi mzuri utayapeleka madaraka kwa wananchi bila mabishano. Kama tujuavyo hadi sasa hivi wale wanaokwamisha mpango huu wa maboresho ni watawala wanaofikiri kwamba wao ni viongozi!

Ingawa Katiba yetu iko wazi juu ya jambo hili la kupeleka madaraka kwa wananchi. Kwamba wananchi ndio wenye madaraka, hali haiko hivyo. Mwenye madaraka ni serikali na chama “tawala”. Chama kinachotawala na mtu anayetawala hawezi kupeleka madaraka kwa wananchi. Watawala wote wa dunia hii, hawakutawala kwa kupeleka madaraka kwa wananchi. Watawala hawana majadiliano, hawana mfumo wa ushirikishwaji. Daima watawala si watu wa demokrasia. Kama tujuavyo bila demokrasia ni vigumu kujenga jumuiya ya watu iliyo Uhuru. Bila Uhuru hakuna haki – bila haki ni vigumu kujenga jumuiya inayowajibika na kujali.

Kabla ya ujio wa wakoloni tulikuwa na watawala. Hawa walitawala bila demokrasia na kusema kweli watu hawakuwa huru. Uhuru wao ulikuwa mikononi mwa watawala. Hakuna ubishi kwamba watu hawa hawakuwa huru. Wakati wa ukoloni pia nchi yetu ilianguka mikononi mwa watawala. Wakoloni walikuwa watawala na wala hawakuwa viongozi, hawakuwa na demokrasia na watu hawakuwa huru.

Hata baada ya uhuru, tuliendelea kuwa chini ya watawala badala ya kuwa chini ya viongozi. Ndio maana hadi leo tuna chama tawala badala ya Chama - Kiongozi. Kutawala na kuongoza ni vitu viwili tofauti. Anayetawala anafifiza uhuru wa wananchi na anayeongoza anafunua mwanya wa ushirikishwaji na majadiliano. Kiongozi ndiye anayeweza kuleta uhuru wa kweli miongoni mwa wananchi wake. Hivyo Ilani inayojali inatuelekeza kuwachagua viongozi na wala si watawala.

Kwa kujenga hoja hii Deusdedit, anasema “ Tukichukulia kwamba familia za Tanzania ni wasafiri katika gari moshi linalotambaa katika reli ya historia kuelekea milele ijayo, basi gari moshi hili linayo mabehewa ya aina mbili, Kuna mabehewa ya abiria na mabehewa ya mzigo. Zile familia milioni tano ni abiria katika mabehewa ya mizigo, wakati familia milioni moja zilizobaki na abiria katika mabehewa ya abiria.

“Katika mabehewa ya mizigo hakuna viti! Kwa hiyo, familia milioni tano zinasafiri zikiruka kichura katika matope ya umaskini, zikipiga miayo ya njaa ya haki na kuhema kutokana na kiu ya maendeleo. Kwao elimu, huduma za afya, nyumba bora, mazingira safi na salama, maji safi na salama, mavazi, malazi, barabara na miundombinu mingine ni bidhaa adimu!

“Kwa upande mwingine, katika mabehewa ya abiria kuna viti! Hivyo, zile familia milioni moja zinapata kifungua kinywa cha chai ya maziwa na mikate iliyopakwa asali, zinakula kuku kwa mirija, na kusuuza koo kwa mvinyo baridi! Kwao elimu, huduma za afya, nyumba bora, maji safi na salama, nishati , na miundombinu mingine ni bidhaa ya kawaida. Na kwa sehemu kubwa madereva wa gari la moshi wanatokana siyo na abiria katika mabehewa ya mizigo, bali abiria katika mabehewa ya abiria!

“ Kwa kuutambua ukweli huu mchungu, tunapoelekea uchaguzi mkuu lazima tujiulize maswali ..”

Maswali haya ndio yanajitokeza katika Ilani Inayojali.

Kiongozi yoyote anayeongoza wananchi wenye madaraka, wananchi walio huru ni lazima ajue na kutambua kwamba wananchi hao wana haki zao za msingi. Kiongozi anayetambua hayo na kuyafuata ndiye kiongozi bora. Bwana Deusdedit, amejitahidi kwa kiasi alichoweza kuzitaja haki hizo na kuzielezea. Haki zenyewe ni kama: Haki ya kuheshimiwa kama binadamu, haki za kiutamaduni, haki za kuishi, haki za kisaikolojia, haki za kijinsia, haki za kijamii, haki za kiuchumi, haki za kisiasa, haki za kiakili, haki za kidini, haki za kimaadili, haki za mshikamano Kitaifa Na Kimataifa, haki za kisheria, Haki za kuwa huru dhidi ya rushwa, haki ya kuwa huru dhidi ya umaskini.
Kiongozi anayezifahamu haki hizi, hawezi kusita kuupokea mfumo wa kupeleka madaraka kwa wananchi. Hivyo jitihada zote zinazofanyika za kuboresha mfumo wa serikali za mitaa, ni lazima zizingatie Ilani hii ambayo imechomoza na kuwa na picha ya Ilani Inayo Jali.

Mfano mzuri wa yale ninayo yasema unapatikana katika kitabu hiki ukurasa 21: “ Tunataka mgombea anayeamini kwa dhati kabisa kwamba akili na utashi ndizo sifa pekee zinazomtofautisha binadamu na mnyama hayawani, na kwamba kwa sababu hii, kila mtu anastahili kupewa fursa ya kutumia akili na utashi wake bila kulaghaiwa wala kulazimishwa kwa namna yoyote ile. Kumdanganya au kumnyima mtu habari muhimu zinazomwezesha kufanya maamuzi sahihi ni kwenda kinyume na kanuni hii, kwani katika hali hii atakosa fursa ya kutumia akili yake vizuri, Vile vile kumlazimisha ni kwenda kinyume na uhuru wa utashi alio nao!”

Ukurasa wa 27, tunapata ujumbe mwingine “ Tunataka mgombea anayefahamu kwamba Tanzania ni dola inayopaswa kuongozwa, siyo kwa mujibu wa kanuni za kifalme au kiimla, bali kwa kufuta kanuni kuu nne: kanuni za demokrasi, kanuni za jamhuri, kanuni za utawala wa sheria na kanuni za shirikisho”

Kitabu chote kimesheheni ujumbe mzito. Ujumbe ambao ukizingatiwa kwa makini, si kwamba utasaidia tu katika Uchaguzi ujao, bali utakuwa nyenzo kubwa ya kuboresha Serikali za mitaa. Kilio cha Mtanzania hivi sasa ni kuwa na Serikali za mitaa zilizo imara na zilizo msingi wa Uongozi katika taifa letu.

Na
Padri Privatus Karugendo

0 comments:

Post a Comment