DIRA YA UCHAGUZI: KUJALI MANUFAA YA WOTE

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2005

DIRA YA UCHAGUZI: KUJALI MANUFAA YA WOTE.

Maaskofu wa Kanisa katoliki la Tanzania wametoa barua yao ya kiuchungaji ikilenga uchaguzi mkuu ujao. Kwa lugha nyingine wametoa Ilani yao ya uchaguzi. Ilani hii inaungana na nyingine nyingi ambazo zimekwisha kutolewa na makundi mbali mbali, dini mbali mbali, vyama vya siasa na watu binafsi. Ni jambo la kutia moyo kuona kwamba watanzania wengi wanalitakia mema taifa letu. Maana Ilani zote zinasisitiza utawala bora, utawala wa kidemokrasia, ushirikishwaji, mshikamano nk.

Ningependa kuamini kwamba wale wote wanaotunga Ilani hizi wanakuwa hawalengi kitu Fulani kinachoitwa “Serikali”, wanakuwa wanaelekeza Ilani zao kwa watanzania wote na wao wakiwemo! Wakisisitiza demokrasia, basi wao watakuwa wa kwanza kuhakikisha demokrasia inafuatwa. Litakuwa jambo la kushaganza wakihubiri demokrasia wakati wao wanaishi kinyume na demokrasia, Wakihubiri rushwa, basi wao wawe mstari wa mbele kuipinga rushwa na matunda yake: Wazikatae sadaka zinazonuka harufu ya rushwa, na waikatae misaada inayoelekea kupatikana kwa njia za rushwa. Wakiongelea kupiga vita umasikini, wawe ni watu wanaoufahamu vizuri umasikini, mtu anayetembelea VX, usafiri wa ndege na nyumba ya kifahari atakuwa si mkweli akiongelea umasikini. Wakiongelea kutetea ukweli, basi wao wawe wa kweli kiasi cha kutotia shaka: Si ukweli wa CCM, CHADEMA, TLP, Kanisa Katoliki, Anglikana au Islam, uwe ukweli wa watanzania wote!

Kwamfano Maaskofu wetu wanasema:
“ Sisi Maaskofu wa Kanisa Katoliki la Tanzania, tukiongozwa na Imani, tunao wajibu na mwito wa kudhihirisha hazina ya Mungu iliyo ndani mwetu katika utukufu wa Mungu Baba. Hii ni pamoja utayari wetu wa kupigania ukweli siku zote tukiamini kuwa Mungu yuko upande wetu kila tunapobaki waaminifu kwake” (Ufu 2: 10,11; Ybs 4:23).

Kwa vile barua hii ya kiuchungaji imeelekezwa kwenye uchaguzi mkuu, ninakuwa na kishawishi cha kufikiri kwamba ni ya watanzania wote. Hivyo basi Ukweli wanaosema kwamba wako tayari kuupigania ni ukweli wa namna gani? Ni ukweli unaokubaliwa na watanzania wote? Waislamu, Wakristu, Wahindu na wale wa dini za jadi. Je ni ukweli ambao wangependa watu wengine waushike na kuufuata, au ni ukweli ambao ni wajibu nao kuufuata? Hata Kibwetere, aliwachoma waumini wake moto akitetea ukweli kwamba muda wao wa kuishi duniani ulikuwa umefikia kikomo, na Mungu, aliwahitaji watu wake kule Mbinguni!

Maaskofu wanataja wasia waliopewa na Marehemu Baba Mtakatifu Papa Yohana Paulo wa pili:
“ Ushirikiano kati ya Kanisa na Serikali katika mambo mhimu yahusuyo jamii unapaswa kuongezwa; na ni matumaini yangu kwamba wengine watafuata njia mliyoonyesha katika jambo hili. Nina hakika kwamba wataendelea kuhimiza kwamba hatua madhubuti zinaandaliwa ili kupunguza umaskini na kuongeza utoaji wa elimu kwa madhumuni ya kuwawezesha maskini kusaidiana wao kwa wao” (Vatikani Machi 11, 2005).

Je, ni nani atawafanya maskini wasaidiane wao kwa wao? Matajiri wanaweza kuwasaidia maskini Je, maaskofu wetu wako kwenye kundi gani? La matajiri au maskini? Je, elimu inatolewa? Kanisa linawasaidia vipi wale wasioweza kulipia elimu? Je Kanisa linatoa elimu ya Mungu (Theolojia) kwa watu wote? Bila theolojia, watu watapata mwanga mzuri wa maadili, imani na umaana wa maisha ya hapa duniani? Tuangalie hali yenyewe. Kama Ilani hii ni ya watanzania wote, ni bora kutafakari kwa makini juu ya maneno haya ya Marehemu Papa Paulo wa Pili. Kama hii ni ilani tunayoiweka mbele yetu, maana yake nini? Ni lazima tujue maskini ni nani, na ni nani wa kuhimiza maskini kusaidiana, kwa hali ya kawaida ni vigumu tajiri kuhimiza maskini kusaidiana! Na ni vigumu mtu asiyekuwa na mwanga wa elimu, kutoa mwanga kwa wengine.

Ukurasa wa sita wa Ilani hii, maaskofu wanasema hivi: “ Uchaguzi wa tarehe 30 Oktoba, 2005 ni nafasi pia kwa watu kutoa maoni yao, kueleza mahitaji yao na kupendekeza mambo yanayopaswa kufanyika katika eneo lao wanamoishi. Kwa hiyo, uchaguzi sio tu kwenda kupiga kura bali ni kushiriki pia katika mikutano ya kampeni ili kupata fursa ya kuuuliza wagombea maswali juu ya maoni na mapendekezo yao katika kutengeneza na kutekeleza sera za nchi.”

Ni kiasi gani maaskofu wetu wanawaruhusu waumini kutoa maoni yao, kuelezea mahitaji yao au kutunga sera juu ya mambo mbali mbali katika imani yao. Wanafamilia wanashirikishwa na kusikilizwa kiasi gani? Maana kama maaskofu wetu wanashinikiza ushirikishwaji ni lazima wawe mstari wa mbele kuonyesha ushirikishwaji kwa matendo!

“ Tunapaswa kulinda kwa uangalifu maisha ya familia. Huo ndio msingi wa jamii yetu ambayo leo hii inakabiliwa na mabadiliko mengi yanayodhoofisha uhai wa familia. Sera za umma lazima ziwe makini ili kuweka miongozo na taratibu za kuimarisha na kulinda ndoa, kutoa fursa ya elimu kwa watoto na vijana wetu, kushughulikia vema matatizo ya afya na magonjwa ambayo kwa watu wetu ni ya hatari na nje kabisa ya uwezo wao kugharimia tiba yake; kuweka sera safi ya upatikanaji makazi bora kwa familia changa na kuwezesha kila mwananchi apate pato la uishi maisha ya kiutu. Virusi vya UKIMWI (VVU) na maradhi ya ukimwi yamesababisha hali tete ya familia kwa kiasi kibaya vile kwamba akina mama na watoto ndio wahanga wakuu wa janga hili”.

Je, maaskofu wetu wenyewe wanazishughulikia kiasi gani ndoa hizi? Maana hakuna kitu kinachohofisha uhai wa familia kama maandalizi mabovu. Msimamo wao juu ya matumizi ya Kondomu, umeziingiza ndoa nyingi kwenye matata na hatari kubwa. Familia nyingi ziko hatarini kufyekwa na ugonjwa huu wa UKIMWI. Ilani yao hii inakuja na msimamo gani? Ni kutetea uhai au kupinga uhai? Ni kutetea ukweli au kipinga ukweli. Wengine wanasema kwamba ukweli ni kwamba Kondomu inazuia asilimia 98 maambukizo ya virusi vya UKIMWI. Maaskofu wanasema ukweli ni uaminifu na kuacha kabisa. Ukiingia kwenye ukweli wenyewe ni kwamba uaminifu na kuacha kabisa ni vitu ambavyo havijulikani hapa duniani!

Hata tukiachana na UKIWMI, na kuliangalia swala lote na ndoa na familia. Ni kiasi gani Maaskofu wetu wanajihusisha na maandalizi ya ndoa. Mafundisho ya siku tatu wakati vijana wanajiandaa kufunga ndoa yanatosha kuiandaa familia ili ipokee changamoto za kijamii na kuweza kuwa msingi imara wa jamii? Ni wapi vijana wetu wanafundishwa mahusiano? Je, tutazilinda vipi hizi ndoa kama hakuna maandalizi ya kuzijenga? Maaskofu wetu hawana familia, wanaishi nje ya familia, hawayajui matatizo na changamoto ya familia, wanawezaje kuziongelea familia? Ni kujidanganya kutoa Ilani ya kitu mtu asichokifahamu vizuri wala kukiishi. Waumini, wanaweza kutoa Ilani inayogusia familia, si Maaskofu!

Maaskofu wetu wanasema hivi:
“ Ni ukweli usiofichika kwamba mfumo huo wa soko huria unawanufaisha tu wale walio katika uchumi rasmi mkubwa kutokana na kukua kwa uchumi. Wengi wa watu wetu wamo katika shughuli ndogondogo za uzalishaji mijini na wengi mno wako vijijini wakijishughulisha na shughuli ndogo za ufugaji, uvuvi na kilimo cha kujikimu tu. Mipango yetu ya uchumi haiwajali vya kutosha hao wote. Katika ziara zetu za kiuchungaji tunakutana na hali ngumu za maisha ya watu wetu vijijini na miji. Kama Taifa tunapaswa kuliangalia tatizo hili kwa makini zaidi na kulitafutia marekebisho ya haraka”.

Ni kweli kwamba Maaskofu wetu wanaijua hali ngumu ya watu kule vijijini? Wanajua maana mtu kwenda kuteka maji zaidi kilomita tano? Wanajua matatizo ya usafiri? Wanajua matatizo ya kukoswa matibabu? Mbona watu hao maskini wa vijijini hawakomi kutoa sadaka? Wanashindwa kuwatibisha watoto wao, lakini wanapata pesa za sadaka? Ni nani wa kuwaelimisha kwamba badala ya kutoa sadaka, wanunue dawa za watoto, maana maisha ya watoto ni muhimu sana kuliko sadaka. Je, hii ni kazi ya kitu kinachoitwa serikali?

Ni vyema kuandika Ilani. Ni imani yangu kwamba ni wajibu wa maaskofu wetu, lakini hoja ni je, maaskofu wetu wanaitekeleza Ilani hii kwa matendo? Je inawahusu nao pia au ni kitu wanachotaka kifanywe na wengine?

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment