MAKALA HII ILICHAPWA NA GAZETI LA RAI 2005.
THE DA VINCI CODE
Mwezi wa pili mwaka huu gazeti hili(Toleo Na 593) kwenye ukurasa wake maarufu wa Kila Alhamisi lilitoa makala yenye kichwa cha habari: “ Uteuzi wa Waziri wazusha utata kuhusu taasisi ya Kikatoliki”. Sehemu kubwa ya makala hii ilikuwa imetafsiriwa kutoka kwenye gazeti la kila wiki la The Observer la London, Uingereza. Makala yenyewe ilikuwa ikijaribu kuelezea mambo matatu yenye uhusiano: Ruth Kelly, Waziri wa Elimu wa Uingereza aliyehusishwa na taasisi ya siri ya Kanisa Katoliki iitwayo Opus Dei, Kitabu kiitwacho The Da Vinci Code, riwaya ya Dan Brown, inayoeleza jinsi gani mwanachama katili wa Opus Dei alivyoendesha mauaji, ili kuficha na kulinda siri zake za kitakatifu (Riwaya hii pia inatoboa mbinu za kueneza itikadi kali za Ukatoliki) na jambo la tatu lilihusu Opus Dei yenyewe, taasisi ya Kanisa Katoliki inayodaiwa kuwa na usiri mkubwa na vitendo visivyoeleweka, mfano kuna madai kuwa wafuasi wa kikundi hiki hufuata desturi ya vitendo vya mateso ambako wanachama wanatakiwa kujiadhibu kwa kujichapa mijeledi ama kwa kujifunga minyororo miguuni ikiwa ni kujikumbusha mateso ya Yesu Kristo. Moja ya ujumbe mkuu wa Opus Dei ni kwamba imani yako inahusiana na kila kitu ambacho unafanya katika maisha. Hubadilishi nafsi yako unapoingia ofisini. Kila kitu kinafanyika mbele ya Mungu, na kila uamuzi unatakiwa kufikiwa kulingana na imani ya mtu. Ni muhimu kwa watu kujaribu kupata maana ya kazi zao kufuatana na imani yao, na wala siyo kutenganisha mambo hayo mawili.
Si lengo langu kuijadili makala hii ninayoitaja na kujadili taasisi hii ya Opus Dei ambayo kwa Kiswahili ina maana ya “Kazi ya Mungu”, na wala sina mpango wa kumjadili Ruth Kelly na jinsi waigeleza walivyomtilia mashaka kuwa ni mwanachama wa taasisi ya siri ya Kanisa katoliki. Mimi nimelenga kwenye riwaya ya Dan Brown ya The Da Vinci Code. Ukweli ni kwamba ni makala hii ninayoiongelea iliyonisukuma kukitafuta kitabu cha Dan Brown kwa udi na uvumba. Bila kuisoma makala hii labda hadi leo nisingekuwa na habari juu ya riwaya ya Don Brown. Mwezi wa tatu mwaka huu nilipokuwa Dar-es-Salaam nilimkuta rafiki yangu akikisoma kitabu hiki. Alishindwa kunipatia nami nikisome kwa vile na yeye alikuwa amekiazima kwa rafiki mwingine. Baadaye na mimi nimefanikiwa kupata nakala yangu, nimemaliza kuisoma leo hii! Baada ya kukisoma nimegundua kwamba kitabu hiki kinapatikana pia kwenye mtandao: www.thedavincicode.com!
Kitabu hiki ni riwaya, ni hadithi ya kubuni, lakini inaongelea vitu vya uhakika na ukweli. Mfano vikundi viwili vya siri katika Kanisa katoliki vinavyoongelewa katika riwaya hii vipo na wala si vya kubuni: The Priory of Sion, ni kikundi cha siri kilichoanzishwa mwaka wa 1099. Kuna ushahidi wa kutosha kwamba watu maarufu kama Sir Isaac Newton, Botticelli, Victor Hugo na Leonardo da Vinci walikuwa wanachama wa kikundi hiki. Dan Brown, anaelezea vizuri muundo wa The Priory of Sion, kiasi kwamba mtu aliyejifunza historia ya kanisa, atakubaliana nami kwamba mtu huyu amefanya utafiti wa kina na wala si kazi ya kubuni tu.
Opus Dei,(Kazi ya Mungu), ni taasisi iliyoanzishwa mwaka 1928 na Padri wa Kihispanishi, Jose-Maria Escriva de Balaguer. Kuna ushahidi wa kutosha kwamba watu mashuhuri na wenye utata ni wanachama wa Opus Dei, kwa mfano iligunduliwa kwamba mawaziri na wakuu wengine waandamizi katika serikali ya Jenerali Franco,(anayejua huyu alikuwa ni kiongozi wa namna gani ni laima aweke alama ya kuuliza kwa kikundi hiki cha Opus Dei) aliyekuwa kiongozi wa Hispania, walikuwa wanachama waaminifu wa kikundi cha Opus Dei. Miaka mitatu iliyopita, iligunduliwa kuwa Robert Hanssen, kachero wa Shirika la Upelelezi wa Jinai la Marekani (FBI) aliyeuzia siri za marekani kwa Urusi, alikuwa anahusiana na Opus Dei. Dan Brown, anaielezea vizuri Opus Dei, kiasi cha kutilia shaka kwamba labda na yeye alikuwa au ni mwanachama.
Hivyo ingawa The Da Vinci Code, ni riwaya inaelekea imefanyiwa utafiti wa kina na imebeba ukweli mwingi wa kihistoria. Ukweli huu ni lazima utagusa imani ya wale waliokuwa katika giza kwa muda mrefu. Wale waliokuwa wanaamini kinyume cha Thomas, kugusa, kutafiti, kuhoji na kujadiliana. Na kwa upande wa Afrika, au niseme kabisa kwa upande wa Tanzania, kitabu hiki ni changamoto kubwa, na kimekuja wakati mbaya kabisa. Zamani ingetosha kukusanya vitabu kama hivi na kuvichoma moto au kuvipiga marufuku. Leo hii haiwezekani, maana hata ukikichoma moto kitabu bado watu watakikuta kwenye mtandao na kukisoma. Watahoji na kutaka wapatiwe majibu ya kitaalamu yenye kufanyiwa utafiti.
Nimesikia kwenye redio kwamba kijana mwingine amejitokeza kule Dar, na kusema naye alilawitiwa na padri, yule aliyekamatwa akilawiti kesi bado iko mahakamani na watu bado wamechanganyikiwa kutokana na tukio hilo, kule Mwanza, padri mwingine alilivamia bweni la wasichana na kufanya fujo usiku, nyumba ndogo zinaongezeka kwa kasi kiasi watu wanaanza kuhoji sheria ya kanisa ya ndoa ya mke mmoja mme mmoja, UKIMWI unayaweka mafundisho ya kanisa njia panda na kuzua maswali mengi, umasikini unawalazimisha watu waanze kusita kuupokea wito wa kuzaa na kuujaza ulimwengu, wanafikiria kufuata njia ya uzazi wa mpango, maaskofu wanapigana,(Tumeshuhudia ya KKT) dini zinageuka kuwa biashara, Askofu wa dhehebu Fulani alikuwa matatani kule Arusha na mwingine aliwekwa ndani Dar, baada ya kugundua alighushi hundi – ni kipindi cha utata na changamoto kubwa.
Riwaya kama ya Dan Brown ya The Da Vinci Code, inawachochea watu kuanza kuchokonoa na kuhoji mambo mengi yenye utata. Maaskofu wetu na wanateolojia wamejiandaa vipi kukabiliana na changamoto kama hii ya The Da Vinci Code? Huu si wakati wa kuzuia kitu bila maelezo. Huu ni wakati wa kufanya utafiti, kujadiliana na kuelimishana. Ni wakati wa kujenga imani yenye mizizi katika jamii, imani inayotokana na watu wenyewe, kwa kuzingatia historia yao, mila zao na jinsi Mungu Mwenyewe anavyojifunua kwa watu wake aliowaumba na kuwapatia uwezo wenye mapungufu!
Mfano katika riwaya hii Dan Brown, anaelezea ukweli wa historia kwamba Injili nne tulizonazo kwenye Agano jipya zilipitishwa kwa kura kwenye mkutano wa Nicaea wa 325 AD ulioitishwa na kusimamiwa na Mfalme Constantine, ambaye alikuwa mpagani na aliendelea kuwa mpagani hadi mwisho wa maisha yake alipobatizwa akiwa mgonjwa kiasi cha kutokuwa na uwezo wa kukataa ubatizo. Yeye aliona faida ya kuutumia Ukristu kuupanua utawala wake. Aliutumia Ukristu kama chombo cha kumzidishia madaraka na nguvu ya kuzitawala himaya zake, hakuutumia Ukristu kuijenga imani yake na kuishi utu wema.
Injili zilikuwa nane, zilitupwa nne na kukubaliwa nne tu ambazo hazikuonyesha wazi uhusiano wa karibu sana kati ya Yesu na Maria Magdalena. Kati ya Injili zilizotupwa ni Injili ya Philip na ile aliyoiandika Maria Magdalena mwenyewe. Waliopata bahati ya kuzisoma injili hizi( Dan Brown, ni mmoja wao) zilizotupwa na hasa ile ya Philipo na Maria Magdalena, wanakili wasiwasi, mashaka na chuki iliyokuwepo kati ya mitume wengine wanaume na Maria Magdalena, walilalamika wazi kwamba Yesu, alimpenda Maria Magdalena zaidi kuliko alivyowapenda mitume wengine, Mtakatifu Petro, ndiye alilalamika sana juu ya upendo wa Yesu, kwa Maria Magdalena. Hata na zile Injili zilizobaki kama ile ya John, jambo hili linajitokeza ingawa kufuatana na mabadiliko yaliyofanywa na Mkutano wa Nicaea, tunayasoma kwa mtazamo mwingine, lakini ukweli unabaki kwamba aliyekuwa akilalamikiwa ni Maria Magdalena, maana hakuna popote katika Injili tulizonazo inapoonyeshwa wazi kwamba Yesu, alikuwa na uhusiano wa karibu na mtume wa kiume zaidi ya mitume wengine. Soma mistari hii kwa macho ya Dan Brown, uone ukweli uliofichwa na Mkutano Nicaea:
“ Hapo Petro akageuka, akamwona yule mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda, anafuata.(Huyu ndiye ambaye wakati wa chakula cha jioni, alikaa karibu sana na Yesu na kumwuliza: Bwana, ni nani atakayekusaliti?) Yesu akamjibu Petro, ‘Kama nataka abaki mpaka nitakapokuja, yakuhusu nini? Wewe nifuate mimi’. ( Yohana 21:20-22).
Kufuatana na Injili ya Philipo na Maria Magdalena, ni kwamba Petro, hakuamini na kukubali kwamba Yesu, angeliliacha kanisa lake mikononi mwa mwanamke na kuwaacha wanaume. Hivyo Constantine, kwa kuita mkutano wa Nicaea na kuusimika mfumo dume katika kanisa, iliendana na mapenzi ya Mtakatifu Petro.
Mbali na kuingiza mfumo dume katika kanisa, Constantine, aliingiza mambo mengine mengine mengi ya kiupagani. Mfano siku ya Jumapili, ilikuwa ni siku ya kipagani ya kuliabudu Jua. Leo hii ndiyo siku inayoheshimika sana katika dini ya Kikristu! Yako mengine mengi anayoyataja Dan Brown, ambayo hayana kitu wala uhusiano na Yesu wa Nazareti, bali ni upagani aliouingiza Constantine.
Kanisa Katoliki linaulinda mfumo dume kwa gharama yoyote ile. Linakataa kuwaparisha wanawake na kuwanyima nafasi ya aina yoyote ile ya kuchomoza na kusifika. Jinsi alivyofunikwa Maria Magdalena na kusahaulika ndivyo kanisa linavyotaka wanawake wote wafunikwe na kusahaulika! Hili linaweza kuelezea vizuri magomvi ya Kanisa Katoliki la Tanzania na Padri Nkwera, anayemtanguliza sana Mama Maria kuliko kitu kingine. Padre Nkwera, anamsikiliza na kumheshimu Mama Maria, kuliko anavyomsikiliza na kumheshimu Askofu wake! Hili halikubaliki katika mfumo dume!
Katika riwaya yake Dan Brown, anaelezea ukweli mwingine wa kihistoria usiokuwa na upinzani kwamba ni mkutano huo huo wa Nicaea, ulioamua juu ya Umungu wa Kristu. Kwamba Kristu, ni mwana wa Mugu, ni kitu kilichopigiwa kura na Maaskofu katika Mkutano Nicaea wakiongozwa na Constantine!
Kikundi cha The Priory of Sion, kinatunza siri ya Maria Magdalena. Kikundi hiki kinaamini kwamba Yesu Kristu, aliliacha kanisa mikononi mwa mwanamke na wala si kwa Petero. Kuna ushahidi wa kutosha kwamba kikundi hiki bado kinatunza masalia ya mwili wa Maria Magdalena na mzao wake. Kuna imani kwamba kuna watu wenye uhusiano wa damu na Yesu kwa kupitia kwa Maria Magdalena! Kikundi hiki kinailinda siri hii kwa gharama yote yote ile. Kanisa katoliki limekuwa likiitafuta siri hii kwa udi na uvumba ili kuhakikisha limeifuta kabisa na kuwa salama. Riwaya ya Dan Brown, inaelezea mapambano kati ya Kanisa Katoliki na kikundi kinachoitunza siri ya Maria Magdalena. Haya ni mapambano ya watu walio tayari kufanya mauaji kwa kulilinda kanisa, wanamwaga damu, wanafanya mambo mabaya na baadaye wanapiga magoti na kusali. Wanajitesa kwa kujipiga mijeledi, kufunga chakula na kujifunga minyororo. Watu hawa wanaamini kwamba wanafanya Kazi ya Mungu “Opus Dei”!
Riwaya Dan Brown ina mambo mengi yanayoligusa kanisa Katoliki na yanaweza kuliyumbisha kama Maaskofu wetu na wanateolojia wetu wakikaa kimya na kuipuuzia riwaya hii. Inawezekana kabisa Maaskofu wetu hawajaisoma riwaya hii – na inawezekana kabisa wakaipiga vita kwa kusikia tu kwamba ni riwaya ya hatari! Ole wao wasipoisoma na kuifanyia kazi!
Sina maana ya kusema kwamba kila kilichoandikwa kwenye riwaya hii ni ukweli, lakini pia sina nguvu za kupinga yale yaliyofanyiwa utafiti wa kina na kuonyesha dalili za kushabiiana na yale ambayo watu watu wengine wamekuwa wakihoji mfano kutowaparisha wanawake na kupotea kwa Maria Magdalena katika historia ya kanisa. Itakuwa je mtu aliyekuwa karibu hivyo na Yesu Kristu, afutike na
kusahaulika kiasi hicho?
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment