MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA HEKO LA MAREHEMU BEN MTOBWA ( Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi) 2005
WATANZANIA WANAPENDA SIASA YA CHAMA KIMOJA!
Kura za maoni zilizofanyika wakati Tanzania, inajiandaa kuipokea siasa ya vyama vingi vya siasa, zilionyesha kwamba asilimia 20 ya watanzania walitaka siasa ya vyama vingi na asilimia 80, walitaka siasa ya chama kimoja. Watanzania walijua nguvu za Chama Cha Mapinduzi, walijua uchu wa madaraka waliokuwa nao viongozi wa Chama Cha Mapinduzi, waliujua unafiki wa Chama Cha Mapinduzi, walijua CCM ina wenyewe, na hao wenyewe ndo walikuwa na nguvu ya pesa na kuyashikilia madaraka, walijua jinsi upinzani wa kweli ulikuwa bado haujazaliwa, walijua jinsi wale wote waliojiita wapinzani walikuwa wamenyimwa nafasi ya kula ndani ya chama cha mapinduzi. Kwa kuyapima yote hayo, waliona ni bora kubaki na utawala wa chama kimoja, maana haikuwa na maana kuudanganya ulimwengu kwamba tunafuata siasa ya vyama vingi na huku ukweli ni chama kimoja tu ndicho kinachoshika utamu wote.
Kwa sababu ya shinikizo la jumuiya ya kimataifa, utandawazi na sera za dunia hii zinazoukumbatia ubepari na unyama zaidi ya utu na haki, Tanzania ililazimika kupinga maoni ya watu wengi na kukubali kuanzisha siasa ya vyama vingi iliyoungwa mkono na asilimia kidogo ya wananchi. Lakini hata mjinga na mwendawazimu anajua jinsi Tanzania, inavyoendeleza siasa ya chama kimoja cha siasa! Chama ni CCM tu, vyama vingine vinakisindikiza chama cha mapinduzi.
Uchaguzi wa kwanza uliofanyika 1995, ulikuwa wa moto moto kweli. Baadhi ya watu waliokuwa wamechoka na ukiritimba wa chama kimoja walikihama chama cha Mapinduzi na kujiunga na vyama vya upinzani. Wengi wa watu hawa ni kati ya ile asilimia 20, iliyokuwa ikiunga mkono siasa ya vyama vingi. Watu kama Mrema, walivuma na kuleta matumaini kwamba ,hatimaye Tanzania, inaweza kutawaliwa na chama kingeni, ingawa watu walikuwa walewale, maana Mrema, alikuwa amekimbia CCM, baada ya jina lake kutupwa kapuni wakati wa kutafuta kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi kuwania nafasi ya urais. Nguvu za Chama Cha Mapinduzi za kutumia mbinu mbali mbali na pesa, zilimsambaratisha Mrema hadi kesho akikubali kurudi CCM!
Chama Cha Mapinduzi, ambacho ndicho kilikuwa kikishikilia hatamu ya dola wakati wa uanzishwaji wa siasa za vyama vingi, kilikubali shingo upande kuvipokea vyama vingine katika ulingo wa siasa. Wakati CCM, ikitumia vyombo vya dola katika kampeni, vyama vingine vya siasa viliachwa hivyo hivyo kujishughulikia kwa kila kitu. CCM, iliweza kuzunguka kila kona ya nchi kwa kutumia ndege na magari ya serikali. Kwa maneno mengine vyama havikupata haki sawa. Tume ya uchaguzi iliendelea kuwa na bado iko mikononi mwa serikali inayoongozwa na CCM. Watendaji wa tume hiyo walichaguliwa na bado wanachaguliwa na rais wa nchi, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM. Katika hali kama hii ni vigumu kuitegemea tume ya uchaguzi kuvitendea haki vyama vyote vya siasa. Kama CCM, ilikuwa na lengo la kuanzisha siasa ya vyama vingi, basi ingependekeza tume huru ya uchaguzi.
Wale wote waliokihama chama hicho na kujiunga na vyama vya upinzani walishughulikiwa ipasavyo. Mheshimiwa Philip Mangula, Katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, amefichua siri hiyo hivi majuzi wakati akiwaonya wanaCCM waliokuwa wakiomba nafasi ya urais wa Jamhuri ya Tanzania, kupitia chama hicho kwa uchaguzi wa Oktoba mwaka huu. Alisema kwamba ambao majina yao yatatupwa wasithubutu kuhamia vyama vingine, maana wakifanya hivyo watashughulikiwa ipasavyo.
CCM, ilijenga picha miongoni mwa wananchi, picha inayodumu hadi leo hii kwamba kujiunga na vyama vya upinzani ni sawa na uhaini ! Kampeni hii ilifanikiwa sana na kuwafanya watu wavipuuzie vyama vya upinzani. Ni maeneo machache katika nchi ambayo watu wamejikomboa kiasi cha kufahamu maana ya vyama vya upinzani. Mfano, Karatu, Kyerwa, Hai, Kigoma mjini, Bukoba mjini, Zanzibar, wanafahamu ni nini maana ya vyama vya upinzani. CCM, inatumia pesa na ushawishi wa juu katika maeneo ili kupanda mbegu ile ile iliyopandwa katika taifa zima. Mbegu ya kuvichukia vyama vya upinzani.
Uchaguzi mkuu wa pili wa vyama vingi uliofanyika 2000, ulishuhudia wimbi kubwa la watu waliokuwa wamekihama chama hicho cha mapinduzi mwaka 1995, wakirudi tena ndani ya chama hicho. Walio wengi hawakurudi kwa kutaka au kwa kukipenda chama. Walirudi kuyasalimisha maisha yao, kusalimisha shughuli zao na biashara zao kwa wale waliokuwa na biashara. Ni imani yangu kwamba uchaguzi wa mwaka huu, utashuhudia wimbi jingine kubwa la kutoka kwenye vyama vya upinzani na kurudi chama tawala.
Tegemeo la vyama vya upinzani lilikuwa kwamba CCM, ingemeguka mwaka huu. Lakini kwa bahati nzuri au mbaya, hekima na busara vimetawala ndani ya CCM, hakuna makosa yaliyofanyika. Hivyo chama hakikumeguka. Uchaguzi wa Kikwete, kama mgombea wa urais kwa tiketi ya CCM, kumetokea kama pigo kwa vyama vya upinzani.
Ni kweli kwamba CCM, si shwari. Lakini matatizo yaliyo ndani ya CCM, sasa hivi si yale ya kukifanya chama hicho kumeguma. Mzee Malecela, hakufurahi na watu wengi wanafikiri hakutendewa haki. Lakini Mzee, huyu hawezi kukifanya chama kimeguke. Hata hivyo chama kina njia nyingi za kumshughulikia kama kilivyowashughulikia wale wote waliokihama na kukimbilia vyama vya upinzani. Hoja nyingine ni kwamba Mzee Malecela, hakubaliki sana kwenye vyama vya upinzani na wala si kipenzi cha vijana ambao ndio wanaotaka mabadiliko. Hata angekihama chama au kujitoa kabisa kwenye siasa, CCM, haiwezi kuyumba kamwe!
Mtu mwingine, aliyetupwa jina lake na anaweza kule chokochoko kwenye Chama Cha Mapinduzi ni mheshimiwa Sumaye. Lakini pia naye chokochoko zake haziwezi kukifanya chama kimeguke. Sumaye, ni mtu mwenye bahati mbaya. Na huenda bahati hii mbaya ni ugonjwa wa kujitakia. Sumaye, hakubaliki ndani ya chama, hapendwi na wananchi hata na watoto wadogo wanajua yeye ni mlarushwa ni fisadi mkubwa. Akiamua kukimbia chama chake, atakuwa amejimaliza kabisa. Hakuna chama cha kumpokea na hakuna mwananchi wa kumpatia kura. Inawezekana akakivuruga chama kwa kiasi Fulani, maana kambi yake ilikuwa na nguvu ya pesa. Inawezekana pesa hizi zikaendelea kutumika kwa lengo la kuvuruga na kuhatarisha amani. Kwa vile anajulikana itakuwa kazi ya chama kumshughulikia na kumnyamazisha.
Dr.Salim, huyo hawezi kukihama chama. Huyu ana hasira zake binafsi na Mtukufu Rais Mkapa. Labda kama Rais, angekuwa mkweli, akamwambia kwamba yuko upande wa Kikwete, asingejisumbua kujiingiza kwenye kinyanganyiro. Hotuba ya mheshimiwa Mkapa wakati wa kufungua mkutano mkuu wa CCM, ilikuwa inamkanyaga Salim. Rais, alisisitiza achaguliwe kijana. Salim, ndio alikuwa mzee(63) kati ya wote, Mwandosya (57) na Kikwete(55). Hakuna aliyekuwa kijana kati yao kwa maana ya neno kijana, lakini kwa vigezo vya CCM, mwenye miaka 55 ndio alikuwa kijana! Rais, alisisitiza mtu aliyekulia CCM. Salim, ana historia ya Hizibu, hivyo kigezo hicho kilikuwa kinamtupa nje. Rais, alisisitiza mtu anayekubalika Bara na Visiwani. Salim, anakubalika bara, lakini visiwani ni sumu! Hivyo na kigezo hiki kilikuwa kinamtupa nje! Ilianza kujitokeza kwamba yeye alihusika moja kwa moja na mauaji ya Mzee Karume. Mkapa, kwa sababu zake mwenyewe aliamua kumtosa Salim! Hivyo ni wazi Mheshimiwa Dr.Salim, ana hasira kubwa. Hasira hizi haziwezi kukigusa chama wala nchi. Hasira hizi hazina msaada wowote kwa vyama vya upinzani.
Wengine ndani ya chama cha mapinduzi wenye hasira na hawana furaha ni vigogo wote waliokuwa wakimpigia debe Dr.Salim. Kufuatana na vyombo vya habari na habari zilizoandikwa na gazeti la Tanzania Daima, ni kwamba timu yote ya Nyerere Foundation, wakuu wa mawilaya, wakuu wa mikoa, baadhi ya mawaziri na baadhi ya wabunge, hawakufurahishwa na uteuzi wa Kikwete. Hivyo wana hasira. Lakini hasira hizi haziwezi kusababisha chama kimeguke, Hawa wote wanaweza kushughulikiwa na Chama! Hivyo CCM, haiwezi kumeguka mwaka huu na haitameguka hivi karibuni! Matumaini ya vyama vya upinzani yanaingia shimoni. Tena shimo lenye kina kirefu sana!
Badala ya watu kutoka CCM na kujiunga na vyama vya upinzani, tutashuhudia kinyume. Watu watahama vyama vya upinzani na kujiunga na CCM. Zoezi hili litaonekana wakati wa kuwatafuta wabunge na madiwani.
Mheshimiwa Kikwete, amesema CCM, itaendelea kutawala hadi miaka 100 ijayo! Huu ni ukweli. Hali inavyojionyesha. Si kazi rahisi kupambana na CCM, bila vyama vya siasa kukubali kuungana. Muungano huu wa vyama vya siasa ni ndoto. Mrema, anataka kusimama peke yake. CHADEMA, inasema vyama vingine vina unafiki na haviwezi kufanya muungano wa kweli. CUF, wanataka wasimame peke yako. NCCR-mageuzi nao pia wanataka wasimame peke yao. Kwa njia hii hata na vile viti vilivyokuwa vikishikiliwa na vyama vya upinzani bungeni vitapungua sana. Itafikia mahali vyama vingi itakuwa ni wimbo tu!
Ni nani wa kubeba lawama hizi? Hakika si watanzania. Maana asilimia 80 ya watanzania ilipendekeza siasa za chama kimoja. Lakini serikali ya CCM, ikakumbatia pendekezo la asilimia 20 kuanzisha siasa ya vyama vingi.
Lawama hizi zinaendelea upande wa serikali ya CCM, maana baada ya kukubali kwenda kinyume na matakwa ya watanzania, haikuwa na nia ya kuendeleza siasa za vyama vingi. Iliendelea kuvipiga vita na kuwanyanyasa na kuwashughulikia wapinzani huku ikiudanganya ulimwengu na jumuiya ya kimataifa kwamba inafuata siasa ya vyama vingi.
Watanzania walio wengi hawapendezwi na mwenendo wa Chama Cha Mapinduzi, lakini kila mtu anajua jinsi ukitaka mambo yako yanyooke ni lazima upeperushe bendera ya Chama Cha Mapinduzi. Wafanyabiashara walio wengi si wapenzi wa CCM, lakini kwa kutaka mambo yao yanyooke wanatoa michango kwenye chama cha mapinduzi na kupeperusha bendera ya chama cha mapinduzi.
Si kweli kwamba watanzania wanapenda siasa ya chama kimoja. Ukweli ni kwamba wanalazimishwa na hali ilivyo kukipenda Chama Cha Mapinduzi. Ni nani wa kuueleza ukweli huu kwenye jumuiya ya kimataifa? Bila ukweli huu kutoka nje, Tanzania, itabaki chini ya utawala wa chama kimoja na maendeleo yatakuwa ni ndoto. Ni vigumu nchi kuendelea bila kuwa na vyama vya upinzani vyenye nguvu kutoa changamoto kwa chama tawala. Ni kazi ya watanzania wote kushirikiana kujenga nguvu za upinzani vinginevyo tutabaki kuimba wimbo wa umasikini hadi mwisho wa dunia!
Na,
Padri Privatus Karugendo
0 comments:
Post a Comment