TUTAFIKA?

MAKALA HII ILCHAPISHWA KWENYE GAZETI LA RAI 2005

TUTAFIKA?

Sina hakika kama ni Tutafika? Au Tutafika! Tarehe 15 hadi 17 mwezi wa pili mwaka huu nilialikwa na shirika la Kivulini, kushiriki warsha ya kuwajengea uwezo wa kukusanya, kuchambua na kusambaza habari wanaharakati wa shirika lao. Kwa wale ambao ni mara yao ya kwanza kusikia shirika la Kivulini. Yafuatayo ni maelezo mafupi: Kivulini ni shirika lisilo la kiserikali la kutetea haki za wanawake lenye makao yake makuu jiji Mwanza linalokutanisha watu wa jinsia zote kujadili, kutafakari na kutafuta suluhisho la ukatili majumbani.

Baada ya kushiriki warsha hiyo ya Kivulini, nilizawadiwa kitabu. Mimi na wewe tumezoea warsha za kuvuna, warsha za kujaza mifuko. Kivulini, ni tofauti kidogo, badala ya kujaza mifuko, wanaujaza ubongo! Wanatoa zawadi za vitabu, vipeperushi na mabango. Nilipowatembelea mara ya kwanza mwaka jana walinizawadia "t-shirt " yenye maneno " Tokomeza ukatili dhidi ya wanawake majumbani". Si lengo la makala hii kuzungumzia Kivulini na zawadi zao, ingawa si jambo baya kuziongelea maana ni zawadi zinazofikirisha na kuchochea mabadiliko katika jamii yetu na hasa kutokomeza ukatili majumbani.

Lengo langu ni kujadili zawadi yangu ya kitabu. Kitabu nilichopewa na Kivulini, kinaiitwa Tutafika Hatima Ya Taifa Letu Tanzania. Kitabu hiki ni matokeo ya Mradi wa Tutafika Tanzania, uliowajumuisha Watanzania vijana wenye fani mbalimbali, katika mijadala iliyohusu hatima ya taifa. Mradi huu ulijumuisha michango ya Watanzania kutoka sehemu za mijini na vijijini. Kitabu hiki kimechapishwa na SID Tanzania Chapter kwa kushirikiana na Hakielimu.

SID "Society for International Development"( Shirika la Kimataifa la Maendeleo) ni mtadao wa kimataifa wa watu na taasisi zisizo za kiserikali lililoanzishwa mwa 1957 kwa lengo la kukuza haki katika jamii na kuhamasisha ushiriki mkubwa wa watu Kwa kupitia miradi mbalimbali SID inaimarisha uwezo wa pamoja, kuwezesha mazungumzo na kubadilishana uzoefu na maarifa miongoni mwa washiriki wake. SID inajaribu kukabili masuala ya maendeleo kwa mtizamo unaozingatia uwiano wa ki-sekta, hivyo inakazania malengo ya muda mrefu kwa nia ya kuleta mabadiliko katika mifumo ya jamii na taasisi.

HakiElimu ni shirika la hiari linalolenga kufikia usawa, ubora, haki na demokrasia katika elimu na jamii. Inafanya hivyo kwa kuwezesha jamii kubadili shule na mfumo wa uundaji wa sera; kuimarisha ubunifu wa mijadala ya umma; kufanya utafiti na utetezi yakinifu na wenye kuchambua na kupanua nafasi kwa wananchi kushiriki katika utawala.

Si lengo la makala hii kuyapigia debe mashirika ya SID na HakiElimu, ingawa pia si dhambi kuyasifia mashirika yanayochochea mabadiliko chanya katika jamii yetu. Lengo la makala hii ni kujadili kitabu cha Tutafika?, Tutafika! Zawadi iliyoujaza ubongo wangu kutoka Kivulini!

Kitabu hiki kilitolewa 2003, nimekisoma 2005! Wewe umekisoma lini au utakisoma lini? Kuna msemo kwamba watanzania hatuna utamaduni wa kusoma. Hii ni kweli? Au tatizo ni kutojua tusome nini na kwa wakati upi? Labda na mimi kama si Kivulini, ningekisoma kitabu hiki baada ya uchaguzi wa mwaka huu au nisingekisoma kabisa. Lakini pia inawezekana ningekipata na kukiweka vunguni mwa kitanda bila kukisoma. Ni majarida mangapi tunapata lakini hatusomi, ni magazeti mangapi tunanunua na kuishia kusoma udaku na kuziacha makala za kufikirisha? Umekisoma, hukukisoma, ninaomba ukitafute na kukisoma tena ili tutafakari kwa pamoja.

Kwa ufupi kitabu hiki kinasema hivi:
" Tanzania ni taifa kubwa lenye wingi wa maajabu. Kati ya maajabu yake ni hali ya utulivu na amani ukizingatia tofauti za wakazi wake wapatao milioni 34;zaidi ya makabila 123, asili mbalimbali, na waumini wa dini tofauti. Tanzania inakabiliwa na mitihani migumu ya kiuchumi na kijamii. Tofauti na ilivyokuwa baada tu ya uhuru, Watanzania wengi tunaonekana kukata tamaa. Tunaishi katika hali ya wasiwasi, hofu na mashaka.

"Tukikabiliwa na matatizo kede kede, tunapaswa kujiuliza maswali muhimu: Sisi watanzania ni nani? na Tunakwenda wapi? Mnamo mwaka 2001 vijana wa Kitanzania wapatao 40 walikaa chini na kutafakari kwa kina maswali haya.

" Mradi wa Tutafika Tanzania unaibua mjadala mbalimbali kuhusu changamoto zitakazolikabili taifa katika miaka ijayo kwa kupitia visa vitatu. Kisa cha Yale Yale kinaelezea taifa lilikokwama, lisilo na unafuu au mabadiliko yoyote. Kisa cha Mibaka Uchumi kinaelezea taifa lililoporwa na watu wachache kwa manufaa yao. Kisa cha Amka Kumekucha kinaelezea taifa linaloimarishwa na nguvu ya mitandao ya kijamii, utundu na utayari wa wananchi kuwajibika.

" Hatuwezi kutabiri hali ya baadaye, ila tunaweza kuitafakari. Visa hivi vitatu vinaelezea mambo yanayoweza kutokea Tanzania ndani ya kipindi cha miaka 30. Utaiandaaje familia yako, shirika lako, kijiji chako, mji wako na taifa lako kukabiliana na hali hizi? Ijulikane wazi kwamba, hali ya baadaye ya taifa letu inategemea maamuzi tunayoyafanya leo. Hatima ya Tanzania imo mikononi mwetu".(Kutoka kwenye Kitabu cha Tutafika Tanzania).

Hivyo kwa kifupi kitabu kinaongelea visa vitatu: Yale Yale, Mibaka Uchumi na Amka Kumekucha. Sitaigia kwa undani kujadili visa hivi vitatu hadi pale na wewe utakapokuwa umekipata kitabu hiki na kukisoma! Kitu ambacho siwezi kukwepa kujadili leo hii ni yale maswali mawili yanayojitokeza kwenye kitabu hiki: Sisi Watanzania ni nani na Tunakwenda wapi? Mimi ningebadilisha kidogo maswali haya hivi: Sisi Watanzania ni nani ,Tuko wapi na Tunatoka wapi?

Ili kutetea hoja yangu nitatumia michoro miwili iliyo kwenye kitabu chenyewe. Mchoro wa kwanza uko kwenye juu ya jarida la kitabu na wa pili uko ukurasa wa kumi na tatu. Mchoro wa kwanza unawaonyesha wananchi wakiyajongea masanduku matatu ya kupiga kura au kutoa maoni? Masanduku haya yana majina ya Yale Yale, Mibaka Uchumi na Amka Kumekucha.

Ningekuwa mchoraji, ningebadilisha kidogo mchoro huu. Ningeacha karibu kila kitu kilivyo, labda daladala ya kuwaonyeshwa wananchi wakiyajongea masanduku ya kupiga kura au maoni, ningewaonyesha wakipiga hatua kurudi nyuma kinyume kinyume. Masanduku yakiwa mbele yao, nao wakirudi nyuma na kuendelea na safari kinyume nyume Huo ndio ukweli wa historia Mbele ndiyo nyuma na nyuma ndiyo mbele! Yale tunayoyajua yako mbele ya macho yetu. Yale tusiyoyajua na ambayo hatuwezi kuyajua yako nyuma yetu. Tukiyafahamu vizuri yale yaliyo mbele ya macho yetu, tukiyatafakari na kuyachambua vizuri tunaweza kupiga hatua kwa kujiamini kuelekea kule tusikokujua. Waandishi wa kitabu hiki wanasema hivi:
" Hatuwezi kutabiri hali ya baadaye, ila tunaweza kuitafakari".
Mimi ninasema ndiyo na hapana. Ndiyo kwa kukubali kwamba hatuwezi kutabiri hali ya baadaye, na hapana kwa sababu hatuwezi kuitafakari hali ya baadaye pia! Hatuwezi kutafakari kitu kisichokuwepo. Tunaweza kutafakari hali ya sasa na hali iliyopita. Sasa hivi hali yetu ni ya Yale Yale, Mibaka Uchumi na Amka Kumekucha. Je, jana tulikuwa na nini? Bila kufahamu vizuri, kutafakari, kupima vizuri ya jana na leo ni vigumu kupiga hatua. Ndiyo maana mimi ninapendekeza maswali ya Sisi Watanzania ni nani? Tuko wapi na Tunatoka wapi? Ni sasa na jana, na wala si Kesho! Sasa hivi tunajua, na jana tunajua, kesho ni kitu kingine.

Leo, jana na kesho, ni vitu vinavyotuchanganya tunapoangalia mtiririko wa maisha yetu katika jamii. Hata waandishi wa kitabu hiki wamejichanganya vizuri kwenye ukurasa wa kumi na sita:
" Pamoja na kuelemewa na matatizo, hatuagalii tumetoka wapi. Tumejisahaulisha machungu ya enzi ya utumwa, na tunahusisha matatizo yetu mengi na kipindi cha ukoloni. Hatuonyeshi kushughulishwa na hali ya baadaye. Hatuna mbele wala nyuma. Matarajio tuliyokuwa nayo baada ya uhuru yamefifia katika hali ya kukata tamaa."

Kwanini hatuna mbele wala nyuma, kwa nini tunasahau utumwa na kwa nini matarajio ya uhuru yamefifia? Ni kwa vile hatutilii maanani ya jana na ya leo. Tunakazania kuingia kwenye ndoto za kesho. Ni watanzania wangapi wanaifahamu vizuri hali ya Yale Yale. Ni wangapi wanafahamu vizuri kwamba ingawa uchumi unaonyesha unakua, lakini matunda yote yanabaki mijini, kwamba maduka makubwa ya kisasa yanaongezeka kukidhi mahitaji ya tabaka la juu, kwamba hakuna atakayenunua nyanya zako na kuacha za Afrika Kusini zenye bei nafuu na ubora wa hali ya juu.

Mibaka Uchumi, tunaielewa halii. Tunakubaliana kwamba hali hii ni mabaya na haiwezi kutusaidia kupiga hatua. Tunajua jinsi viongozi wa Taifa letu wanavyowajali Mibaka Uchumi na kuwasahau kabisa wananchi wa kawaida wale tuliozoea kuwaita walalahoi? Jinsi Wanasiasa wanavyowategemea Mibaka Uchumi kuwapatia pesa za kuendesha kampeni wakati wa uchaguzi? Na kwamba Mibaka nao wanadai upendeleo katika biashara na mikataba minono inayotoka serikalini. Tunajua hali hii inavyodhoofisha uhusiano katika ya wananchi na viongozi wao na kwamba wananchi pia wanawageukia Mibaka ili kujipatia chochote? Hii ni hali ngumu ambayo haiwezi kumruhusu mtu kupita hatua kwenda popote, iwe mbele wala nyuma!

Mchoro wa pili katika kitabu hiki ninaoutumia kutetea hoja yangu ni ule wa mtu amekalia stuli ya dhahabu na bado anaomba. Mchoro huu uko kwenye ukurasa wa kumi na tatu. Ningekuwa ni mimi mwandishi wa kitabu hiki, mchoro huu ulitosha kuelezea kila kitu. Tunakalia dhahabu, mafuta na utajiri mwingi wa nchi hii, lakini bado tunaomba. Bado tunajiita taifa masikini. Haya ndiyo ya kutafakari. Si ya kesho, hapana! ya leo na ya jana. Ni kwa nini tumekalia dhahabu na bado tunaomba? Tatizo ni nini? Hili si tatizo la kesho, ni tatizo la sasa hivi. Kama tunaweza kujibu swali hili, kama tunaweza kurekebisha ujinga huu wa kukalia stuli ya dhahabu na kuendelea kuomba, kesho itakuja inataka isitake.

Kufika ama kutofika kunategemea kwa kiasi kikubwa hali ya leo na ya jana. Juhudi kubwa iwekwe katika kuwachochea watu kuweka bidii kuitafakari hali ya leo na ya jana. Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kama ilivyo HakeElimu, Kivulini,SID nk, yaongeze bidii katika kuchochea jambo hili. Badala ya kuijaza mifuko ya watu wanaokwenda kwenye semina, mikutano na warsha, wawapatie watu chakula cha ubongo, vitabu, vipeperushi na mabango, vitu vitakavyochochea tafakuri. Na tafakuri hizi uwe mjadala wa kitaifa. Uwe mradi wetu wa pamoja. Kila mtu ashirikishwe mahali atakapokuwa, vijijini, mijini, kazini, kwenye nyumba za ibada, ijadiliwe wakati unaofaa na usiofaa. Umuhimu wa kuijua na kuitafakari hali ya sasa na ile ya jana, hautupatii nafasi ya kukaa na kutulia, nafasi kuendelea kukali stuli ya dhahabu, ni wakati wa Amka kumekucha. Ni jukumu letu kuamshana sisi kwa sisi. Tukisubiri wengine watuamshe, watasita, maana ukimwamsha aliyelala utalala mwenyewe. Na hali hii ya utandawazi na utandawizi hakuna anayetaka kulala. Ni ujanja na mbinu za kuwaibia wale waliolala. Kila Mtanzania aliyeamka achuke jukumu la kumwamsha ndugu yake Mtanzania aliyelala usingizi wa pono! Amka Kumekucha! Tutafakari pamoja, tujifunze pamoja na tutembee pamoja, Tutafika!

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment