UHAKIKI HUU ULICHAPWA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA
UHAKIKI WA KITABU: “PARCHED EARTH”
1. Rekodi za Kibikiogarafia
Jina la kitabu kinachohakikiwa hapa ni “Parched Earth” na kimetungwa na Elieshi Lema. Mchapishaji wa kitabu hiki ni E&D Limited na amekipa namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN) 9987-622-22-4.Kimechapishwa mwaka 2001 kikiwa na kurasa 224. Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo.
II. Utangulizi
Hii ni hadithi ya kubuni .Mwandishi wa hadithi hii Mama Elieshi Lema, ni mwandishi mahiri .Siku chache zilizopita, nilifanya uhakiki wa vitabu vyake vya watoto. Vitabu vya Freshi na Maisha, vinaonyesha ubunifu wa Mama huyu wa kufikisha ujumbe mzito kwa watoto. “Parched Earth”, ni ushuhuda mwingine wa mwandishi kwamba ana mbinu si za kufikisha ujumbe kwa watoto peke yao bali na kwa wakubwa pia!
Hadithi yake inachokoza mawazo, inamfanya mtu kutafakari na kujiuliza maswali mengi juu ya maisha yake na juu ya uhusiano wake na jamii inayomzunguka. Hadithi yenyewe ina sura 19. Katika aya zifuatazo nitatoa muhtasari na tathmini yake, lakini baada ya kudokeza mazingira yanayokizunguka kitabu hiki.
III. Mazingira yanayokizunguka kitabu
Kitabu hiki kimeandikwa kwa lugha ya Kiingereza, kitu kinachoongeza mvuto wa kitabu na hadithi yenyewe. Ukweli ni kwamba mpaka sasa hapa Tanzania tuna vitabu vichache vya hadithi za Kingereza vilioandikwa na watanzania wenyewe. Inavutia kuona Mtanzania, anavyoweza kuandika hadithi inayohusu maisha ya Kitanzania kwa Kingereza. Huu ni mchango mkubwa katika kukuza na kuendeleza lugha hii ya kingeni ambayo ni lugha ya kimataifa na inaongoza katika kijiji cha Utandawazi. Na wala huku si kupiga vita Kiswahili, bali ni kuiendeleza lugha hii katika jamii ya Kitanzania .Mwandishi wa riwaya hii ya Kingereza, ameandika riwaya nyingi kwa lugha ya Kiswahili. Jambo la msingi ni kuzipatia nafasi lugha zote na hasa lugha kuu, mfano lugha ya taifa na lugha za kimataifa kama kingereza Mfano, mimi nimeisoma riwaya hii kwa Kingereza, lakini sasa ninafanya uhakiki wake kwa Kiswahili. Hata mtu ambaye hafahamu Kingereza, kwa kusoma uhakiki huu, anaweza kupata ujumbe wa riwaya hiyo – ingawa ingekuwa bora zaidi mtu kuisoma riwaya yenyewe kwa lugha iliyoandikwa.
Kitabu hiki kinatumika kwenye masomo Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam. Lakini kwa maoni yangu ni bora kabisa kingetumika hata sekondari maana riwaya hii imesheheni yale yasiyofundishwa popote, imesheheni yale ambayo kwa kawaida kila mtu anaachiwa kuongelea apendavyo. Wale wanaofanikiwa kuongelea vizuri, wanafanikiwa kuvuka – wenye bahati mbaya wanazama au wanaendelea kuogelea bila kufikia mwisho.
Bahati mbaya wale wanaoogelea hadi mwisho, hawako tayari kuelezea uzoefu wao na kutoa mbinu walizozitumia kufanikiwa. Walio wengi inakuwa ni kujaribu hili na kuacha lile, ni mchezo wa pata potea. Haitoshi kumwambia mtoto asizini, haitoshi kuwazuia vijana kufanya mapenzi, bila kuwapatia mwongozo na uzoefu wa kupambana na nafsi zao, bila mwongozo wa maisha ya kiroho ya kuweza kuweka kando mvuto wa kimwili na kuangalia ndani ya nafsi ya mtu, heshima ya mtu, furaha ya mtu, mema na mabaya ya mtu. Maana uzuri wa mtu si umbo lake, bali ni yale ya ndani yanayomfanya kuwa mtu, ni matendo yake yanayomtofautisha na wanyama wengine.
Kijana anayekua, anayesoma sekondari au chuo, hawezi kufahamu ukweli huu bila mwongozo, bila kuelekezwa. Ukweli ni kwamba hadi leo hii hapa Tanzania hatuna mwongozo wa vijana kuhusiana na mahusiano ya mtu na mtu, na hasa watu wa jinsia tofauti. Ni lazima kijana apate uzoefu kwa wale walioupitia ujana, ni lazima apate uzoefu kwa wale waliovutiwa na maumbile ya nje wakaishia kuzama badala ya kuongelea na kuvuka. Ni lazima apate uzoefu kwa wale waliovutiwa na maumbile ya nje, lakini wakaenda zaidi ya hapo na kuyatafuta yale ya ndani, na walipoyapata wakayavumilia na kuyapenda sambamba na maumbile ya nje.
Riwaya ya “Parched Earth” inavunja tabia hii ya uchoyo wa mafanikio. Kwa upande mwingine inavunja tabia ya kuyafunika matatizo na kujenga utamaduni wa unafiki. Baada ya maelezo haya sasa tuone kitabu chenyewe kwa muhtasari.
IV. Muhtasari wa Kitabu.
Riwaya hii inaelezea maisha ya msichana Doreen Seko, aliyelelewa kijijini, akapata elimu na kufanikiwa kuwa mwalimu. Doreen, kama walivyo watanzania wengi, anakumbana na changamoto ya mfumo dume na mahusiano ya kimapenzi. Safari ya kimapenzi kuanzia utotoni, utu uzima na hatimaye kumpata mchumba aliyefunga naye ndoa na matatizo yaliyojitokeza kwenye ndoa hadi akawa na mpenzi mwingine nje ya ndoa, ni somo zuri sana kwa vijana wanaoachiwa kuongelea bila mwongozo katika mahusiano ya kimapenzi.
Doreen, alifunga ndoa na Martin, na walipendana kweli. Lakini kwa vile Doreen, alizaa mtoto msichana na kuchelewa kumzalia Martin, mtoto mvulana, mapenzi yao yalipungua. Mchezo uliokuwa jukwaani haukuwa na mvuto tena kwa Martin! Pazia jingine likafunguliwa kwa Doreen na Martin. Wakati Doreen, alitamani kumpata mtu wa kumpenda, kumkubali na kumjali, mtu aliyeugusa moyo wake, Martin, alitamani kumpata mtu mwenye mvuto, lakini pia wa kumzalia mtoto wa kiume! Doreen, alianza kuonja uchungu wa kuwa kwenye ndoa na Martin, akatafuta mpenzi mwingine nje ya ndoa. Au kwa maneno mengine, mtu wa kumzalia mtoto wa kiume, si mapenzi bali ni kutafuta kitu kwa mtu! Uchungu au upweke wa Doreen, ukazaa uhusiano nje ya ndoa kati yake na mwanamme mwingine aitwaye Joseph. Huyu Joseph, ingawa alikuwa tajiri, aliachwa na mke wake, kwa sababu alishindwa kutambua kwamba alichokihitaji mke wake si mali bali upendo wa kweli.
Somo kubwa katika riwaya ya Parched Earth, ni uhusiano wa Joseph na Doreen. Joseph ndoa yake imevunjika, baada ya mke wake kukimbia. Na Doreen, ana matatizo kwa vile mme wake anapenda nje ya ndoa. Watu hawa wawili wanakutana si kwa kuvutwa na maumbile ya nje. Shida zinawaunganisha. Wanapendana na kufundishana mambo mbali mbali. Mfano Joseph, anamfundisha Doreen, uchoraji. Kwa njia hii wanapata nafasi ya kukaa pamoja na kuongea mambo yaliyo rohoni, wanafunuliana mioyo yao, kwa pamoja wanashirikiana kuufukuza upweke kwenye mioyo yao. Pazia linapofunguliwa, wanatambua kwamba wanaweza kuhusiana, kupendana na kusaidiana bila hata ya kufanya tendo la ndoa! Wanagundua kwamba mvuto wa maumbile ya nje si wa muhimu sana. Ukweli kwamba Doreen, aliweza kumpata mtu wa kumsikiliza na kushirikiana naye yale yaliyo moyoni mwake, ulibadilisha maisha yake. Ukweli huu ulimpatia nguvu za kumvumilia mme wake aliyekuwa anapenda mwanamke mwingine nje ya ndoa. Pia uvumilivu wa Doreen, unayabadilisha maisha ya Martin!
Ujumbe wa Mama Elieshi Lema, katika riwaya hii, kama nilivyoelewa mimi ni kwamba uhusiano wa mtu na mtu, na hasa uhusiano wa mwanamke na mwanamme, si jambo la kuachiwa hivi hivi kila mtu akafanya apendavyo. Ni swala la kiroho linalohitaji mfumo wa kijamii. Si mfumo dume, unaowafanya wanawake kuwa vyombo vya kuzaa watoto wa kiume au kufanya kazi za kumfurahisha mwanaume, bali mfumo unaohimiza uhusiano unaolenga kuunganisha nyoyo za watu zaidi ya kuunganisha miili ya watu!
Mfumo ambao unaweza kusaidia kuwafundisha vijana wetu juu ya uhusiano, juu ya kupenda na kupendwa, juu ya kuoa na kuolewa na juu ya kujenga familia zilizo bora. Vijana wakisoma “Parched Earth”, wakapata nafasi ya kujadiliana na kubadilishana mawazo na kusikiliza uzoefu wa wazee waliowatangulia, inaweza kusaidia kutoa mwanga katika maisha yao.
Mfano, vijana wakiyaangalia maisha ya Doreen, wakalinganisha na maisha yao ya sasa. Wanaweza kugundua uongo ulio katika upendo wa kuvutiwa na mwili, upendo ambao mara nyingi unadumu kwa muda mfupi.
V. Tathmini ya Kitabu.
Baada ya kuona muhtasari huu sasa tufanye tathmini ya kazi hii aliyoifanya Mama Elieshi Lema. Awali ya yote lazima niseme kwamba , kwa kuangalia hadhira anayoikusudia, kitabu hiki kinasisimua sana na kutoa mafundisho katika jamii yetu na hasa kuhusu uhusiano wa mtu na mtu. Au kuwa wazi kabisa, tuseme, uhusiano wa mwanamke na mwanamme.
Changamoto anayoitoa Mama Elieshi Lema, katika riwaya hii ni swali la kawaida: je, Mwanamme anahitaji nini kutoka kwa mwanamke na mwanamke anahitaji nini kutoka mwanamme. Na je ni mazingira gani yanaweza kumfanya mwanamke atambue anachohitaji mwanamme, na ni mazingira gani yanaweza kumfanya mwanamme atambue anachohitaji mwanamke.
Inawezekana hili ni swali la kawaida. Lakini tukiingia kwa undani hili linaweza kuwa swali kubwa ambalo halina jibu katika maisha yetu ya kawaida. Tuna mifano mingi ambapo wa kinamama wanaachwa na mabwana zao kwa vile hawakuzaa watoto wa kiume. Je, hicho ndicho wanaume wakitakacho kwa wanawake? Wapo pia akina mama wanaoachwa kwa vile hawakuzaa. Je wakitakacho wanaume ni watoto tu? Upendo wa mahusiano ni watoto?
Katika riwaya, upendo wa Doreen na Martin, unapungua pale Doreen, anaposhindwa kumzalia Martin, mtoto wa kiume. Inawezekana Martin, alimpenda Doreen, kwa lengo la kumzalia mtoto mvulana? Je, mtoto mvulana ndio angejenga uhusiano wa kweli, uhusiano wa kudumu kati ya Doreen na Martin? Jinsi riwaya inavyokwenda, si mali, kabila wala elimu vinavyosababisha uhusiano mbaya kati ya Doreen na Martin. Doreen ni wa Moshi na Martin ni wa Mbeya, lakini tofauti ya mila na desturi si kikwazo, bali ni pale Doreen anaposhindwa kuzaa mtoto mvulana, kana kwamba tatizo hilo ni la mwanamke peke yake!
Joseph naye ni mtu mwenye pesa nyingi na mali, lakini aliachwa na mke wake. Mwandishi, anaonyesha jinsi Joseph, alivyokuwa akitoa zawadi nyingi kwa mke wake. Lakini mwanamke, hakupenda mali, alipenda kitu kingine, alipokipata nje ya ndoa, alikimbia na kuziacha mali zote nyuma yake!
Kwa vyovyote tunataka tusitake, hali ilivyo sasa hivi ni lazima tuwe na vitabu kama hiki cha “Parched Earth”, ni lazima tukae na vijana wetu na kuwaelekeza jinsi ya kuogelea na kuvuka kwa salama. Ni lazima tutoe uzoefu wetu wa mahusiano, uwe uzoefu wa mafanikio au wa kushindwa, lakini ni lazima tutoe uzoefu wetu, ili pale tulipokosea sisi vijana wetu wasikosee. Pale tulipofanya vizuri vijana wetu watuige.
Mama Elieshi Lema, ameonyesha mfano mzuri wa kutuandikia riwaya ya “Parched Earth”. Ni bora kila mzazi angemnunulia mtoto wake kitabu hiki. Kama wazazi hawana nafasi ya kuongea na watoto wao, riwaya hii itaongea badala yao. Si lengo langu kukipigia debe kitabu hiki, bali ni kuupigia debe ujumbe mzito ulio katika riwaya hii iliyotukuka.
VI. Hitimisho
Kwa kuhitimisha basi, kwa upande mmoja, nawashauri watanzania kukisoma kitabu hiki ili waweze kujionea wenyewe uhondo uliomo ndani. Lakini kwa upande mwingine namwomba mwandishi wa kitabu hiki kufanya jambo moja la ziada, nalo ni kushirikiana na waandishi na wachapishaji wa vitabu na watu wengine wanaojali umuhimu wa vitabu katika jamii, kubuni mbinu za kuwashawishi watanzania kujenga utamaduni wa kujisomea. Bila mbinu hizi, uandishi wa vitabu na ujumbe wake utakuwa sawa na kupigia ngoma kwenye maji!
Na,
Padri Privatus Karugendo.
5 comments:
Yap Siku ya kwanza kuisoma hii novel nilikubali E. Lema is a real Radical Feminist
Nop. She is not a radical feminist. She is a liberal feminist.
Nop. She is not a radical feminist. She is a liberal feminist.
Feminism flow in women blood
For sure when i have been started reading this novel I fail to understand the intention of our honourable mother E . Lema but for sure she deserve a normal award 💪💪💪
Post a Comment