MAKALA HII ILICHAPWA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2005
NI KWELI RAIS HUCHAGULIWA NA MUNGU, LAKINI.........!
Hoja ya Mheshimiwa Magufuli, aliyoitoa jana mjini Dodoma, wakati akiongea na vyombo vya habari kwamba rais huchaguliwa na Mungu, na kwamba rais wa Tanzania amekwisha chaguliwa na Mungu, ni ukweli mtupu. Sidhani kuna mtu wa kupingana naye kwa hilo. Watanzania ni wacha Mungu. Namba kubwa ni waumini wa dini zetu za kigeni na waliobaki wanamwabudu Mungu wa dini zao za jadi. Magufuli, alikuwa akikanusha uvumi kwamba na yeye kama walivyo wana CCM wengine, anataka kuwania urais katika uchaguzi mkuu mwaka huu.
Katika dini zote tunafundishwa kwamba Mungu, alishapanga yote na anajua yaliyopo sasa na yale yanayokuja kesho. Yeye hutoa na kutwaa. Ndiye ajuaye saa na wakati wa kila jambo. Binadamu hupanga na Mungu, hupangua. Haya ni mafundisho yaliyo kwenye dini zote.
Hivyo si lengo la makala hii kupingana na Mheshimiwa Magufuli, mjinga anaweza kupingana naye. Nisingependa kujiweka kwenye kapu la wajinga, hata hivyo ni mjinga gani ana ubavu wa kukubali kwamba yeye ni mjinga? Mjinga akikubali ujinga wake anakuwa si mjinga tena. Mjinga ni yule asiyetambua kwamba yeye ni mjinga! Ni watu wachache waliojaliwa neema ya kukubali hali zao. Mlevi, kukubali kwamba ni mlevi anakuwa hajalewa, aliyelewa sawa sawa atakwambia, Pombe umeninywesha wewe? Mwizi, kukubali kwamba yeye ni mwizi ni kazi, atakwambia, Ninasingiziwa! Hali ni mbaya hadi kufikia hatua ya kuficha magonjwa. Mtu atakwambia anaumwa kichwa, mgongo au tumbo, kumbe anasumbuliwa na magonjwa ya zinaa. Magonjwa haya yanatibika, lakini kwa kuendekeza tabia hii ya kutokubali hali halisi kuna watu wanapoteza maisha yao kwa njia hii. Madaktari wanatibu kichwa, kumbe mtu anaoza sehemu zake za siri. UKIMWI, umeenea kwa njia hii, watu wanaficha, inabaki kusema shinikizo la damu, ugonjwa wa muda mrefu, homa nk. Ipo mifano mingi ya kuonyesha jinsi mwanadamu asivyopenda kukubali hali halisi. Kwa upande wa sisi wa Afrika, au niseme sisi watanzania, hali ni mbaya zaidi. Wenzetu katika nchi zilizoendelea, wamekwisha jijengea tabia ya kukubali hali halisi.
Mimi si mjinga! Isichukuliwe kwamba ninakataa kukubali hali halisi. Ningekuwa mjinga, ningekubali ujinga wangu, ili nitolewe kwenye kundi la wajinga. Sipingani na Magufuli! Lengo la makala hii nikutaka kuuliza swali: Mheshimiwa Magufuli, kama rais wetu amekwishachaguliwa na Mungu, kazi yetu sisi watanzania ni nini? Tukae tu na kubweteka? Kwa nini tuwepo kama hatuwezi kusaidiana na Mwenyezi Mungu, kujichagulia rais anayetufaa? Alituumba tu kama mapambo?
Ingawa watanzania ni Wachamungu, ninashindwa kuamini kama wanaweza kuikumbatia mantiki ya mheshimiwa Magufuli. Mantiki aliyoitumia ni sawa na kusema: Mungu alishapanga tutakufa, hivyo basi tusile, tusitibiwe na kujishughulisha na chochote. Ya nini kula kama kesho tutakufa? Ya nini kutibiwa kama kesho tutakufa? Ya nini kufanya kazi kama kila kitu tutakiacha kesho? Ya nini kumpenda jirani yangu kama uhusiano wetu utaisha kesho? Ya nini kuoa na kutengeneza familia kama maisha yanaisha kesho? Haya ni mawazo ya kiwendawazimu!
Kabla ya kuendelea, kuna jambo la kujikumbusha: Mungu, aliyetuchagulia Rais wetu wa awamu ya nne,( maana kufuatana na maoni ya Magufuli, mtu huyu amekwisha chaguliwa na yupo ametulia!) ni yule yule aliyekuwa amemchagua Idd Amin wa Uganda. Tunafundishwa kwamba Mungu, ni mmoja. Hivyo alivyotuchagulia sisi ndivyo anavyowachagulia na watu wengine katika nchi zao. Kufuatana na historia ni kwamba Mungu, huyu alikuwa akimtokea Idd Amin, na kumwelekeza kutekeleza mambo mbali mbali kama kuwafukuza Wahindi na mambo mengine mabaya dhidi ya ubinadamu. Amin, aliweza kuitawala Uganda, zaidi ya miaka minane! Alifanya mema na mabaya. Kwa macho yetu sisi wanadamu, maana hakuna mwenye ujuzi wa kipimo cha Mwenyezi Mungu, mabaya ya Idd Amin yalizidi mema yake. Aliwachinja watu ovyo kufikia hatua ya kuua hata mke wake na mtoto wake, hakufuata katiba wala sheria, hakuheshimu haki za binadamu, watu waliishi kwa woga na wasiwasi. Wachunguzi wa mambo ya kisiasa wanasema Obote, rais wa kwanza wa Uganda, ambaye naye alikuwa amechaguliwa na Mungu, aliua watu wengi zaidi ya Idd Amin.
Hakuna shaka kwamba Mungu, ndiye aliyekuwa amemchagua Mobutu. Kama bado tunazingatia mantiki ya kwamba Mungu, hupanga na kujua yote, yaliyopo na yasiyokuwepo. Tunayajua mabaya ambayo Mobutu, aliwafanyia watu wake. Alipora mali yote na kuuza uhuru wa nchi yake! Hadi leo hii DRC, haijatulia kufuatana na mbegu mbovu iliyopandwa na mtu wa Mungu, marehemu Mobutu.
Kwa mantiki ile ile tunaweza kusema kwamba hata na Hitler wa Ujerumani, alikuwa amechaguliwa na Mungu, kuwaongoza watu wake. Hitler, alifanya mazuri na mabaya. Ila ubaya ulichomoza zaidi ya uzuri. Mauaji ya Wayahudi milioni sita, ni dhambi ambayo haitasahaulika hapa duniani na kule mbinguni.
Baada ya kujikumbusha hayo machache tuendelee na hoja yetu . Mheshimiwa Magufuli, anawashangaa wale wanaokwenda Jangwani. Kwa maoni yake wanapoteza muda wao, maana rais amekwishachaguliwa na Mwenyezi Mungu Kwenda Jangwani na kufanya maandamano si msaada wa lolote!
Mtu mwingine anaweza kuuliza na kushangaa kama anavyoshangaa Magufuli:Ya nini basi mkutano mkuu wa CCM, kukutana Dodoma? Ya nini kutumia pesa za walalahoi wa Tanzania, kuendesha mkutano ambao hauna kazi yoyote? Maana kama rais amekwishachaguliwa na Mwenyezi Mungu, kani ni kumtangaza. Jambo hili halihitaji pesa wala kura! Ya nini kujiandikisha kupiga kura? Ya nini kupiga kura?
Kama Rais, amechaguliwa na Mungu, wabunge na madiwani nao wamechaguliwa na Mungu! Itakuwa dhambi kubwa kutumia pesa ambazo zingesaidia kufanya mambo mengine kuendesha uchaguzi ambao umekwisha malizika. Pesa za uchaguzi zijenge mashule, mahospitali, zisambaze maji na umeme vijijini na kujenga barabara.
Magufuli ni mbunge wa CCM, ni waziri wa CCM na ni kada wa CCM. Anajua jinsi CCM, ilivyo na pesa, anajua jinsi CCM, ilivyoshikilia dola. Anajua vyema kwamba hakuna linaloshindikana mbele ya pesa. Anajua jinsi dola ilivyo na nguvu. Sauti ya pesa ni sauti ya Mungu na sauti ya dola ni sauti ya Mungu. Haya ni tofauti na msemo ule wa "Sauti ya watu ni sauti ya Mungu!"
Kama sauti ya CCM, ni sauti ya watu, CCM basi ni sauti ya Mungu! Magufuli, anataka tuamini hivyo. Kwanini basi CCM, itumie pesa nyingi katika kampeni. Kwanini viongozi wa CCM, wanakimbia huku na huko nchi nzima wakitafuta kuungwa mkono? Kwa nini tusikie vitisho kwamba mkuu wa wilaya atakayeachia jimbo la uchaguzi kuchukuliwa na wapinzani atakuwa amejifuta kazi? Kwanini CCM, isikae tu na kuusubiri ushindi? Kama watu wanaipenda wasiwasi ni wa nini? Chema chajiuza na kibaya chajitembeza Mbona namba ya wanaCCM ni chache ukilinganisha na idada ya watanzania wote?
Magufuli, hatofautiani na Mheshimiwa Mwapachu. Kama wabunge wa CCM, wamepitisha muswada wa mabadiliko ya 14 ya Katiba ya jamuhuri ya Muungano ya Tanzania, ni sawa na kusema: Roma imesema na shauri limefungwa! Kwa maoni ya Mheshimiwa Mwapachu, wabunge wa upinzani ni wachache na hawana nguvu za kuukwamisha muswada. Hata hivyo wabunge wa CCM, wamechaguliwa na wananchi, kama si kuchaguliwa na Mungu!
Nchi inayoongozwa na Mungu, hata maoni ya mtu mmoja yanaheshimiwa. Kila mtu anasikilizwa. Wabunge wa upinzani ni wachache, lakini nyumba yao kuna watu wengi. Mtu msomi kama Mwapachu, ni lazima ajue kwamba CCM, kuwa na wabunge wengi, haina maana inasimamia watanzania wote. Tanzania ina watu zaidi milioni 35. CCM, haina wanachama zaidi ya milioni 4, na watu waliokuwa wakijitokeza kupiga kura siku za nyuma si zaidi ya milioni 10. Ukitoa namba ya watoto wadogo, utajikuta zaidi ya watu milioni 15, hawana upande na hawana mtu wa kuwakilisha maoni yao bungeni. Na hatuwezi kusema kwamba kwa vile hawana upande wanaiunga mkono CCM.
Hata hivyo muswada wa mabadiliko ya 14 ya katiba umekuja katika kipindi kibaya. Kila mbunge wa CCM, angetaka kurudi Bungeni. Kuonyesha msimamamo wa kupinga maamuzi ya serikali, ni kujitengenezea kitanzi. Ni nani katika vikao vya CCM, atakubali kupitisha jina la mbunge anayepinga maamuzi ya serikali yake? Hivyo wabunge wengi wa CCM, wanakufa na tai shingoni na kuficha makucha yao: Mtaka cha uvunguni ni sharti kuinama, japo kwa muda mfupi!
Nina swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Magufuli: Ana uhakika gani kwamba sisi tuliopo sasa hivi na mheshimiwa mteule wetu kutoka kwa Mungu, tutakuwa bado hai ifikapo Oktoba mwaka huu? Sisi ni bora kuliko binadamu wenzetu waliokumbwa na Tsunami? Kati ya hao waliopoteza maisha katika tufani hilo la Tsunami, hawakuwemo marais, wabunge na madiwani watarajiwa katika nchi zao? Uhakika kwamba rais amechaguliwa na Mungu, na kama sikosei anamfahamu, anaupata wapi? Ya kesho anayajua wapi? Ya leo anayajua na ya jana anayajua, lakini ya kesho ni kazi ya Mungu! Yeye anajenga barabara, ni kazi nzuri na watu wanampongeza. Wengine wanapitisha mikataba mibovu, watu wanalalamika. Rushwa inaendelea kuota mizizi. Utandawazi unatumeza! Haya ndiyo tunayoyajua sisi na Magufuli, akiwemo. Kwamba tunamjua rais wa Oktoba mwaka huu, ni uongo mtupu. Hata kama ni kutumia pesa na dola, hakuna anayeweza kusema kwa uhakika.
Huyo Mungu anayewachagua marais wema na wabaya ndiye aliyetuumba na kutupatia akili na utashi na uwezo wa kutambua mema na mabaya. Ndiye aliyetupatia uwezo wa kuwazuia ndege kujenga viota juu ya vichwa vyetu na kutunyima uwezo wa kuwazuia ndege hao kuruka juu ya vichwa vyetu.
Tanzania tuna mfumo wa siasa ya vyama vingi. Hatuna uwezo wa kuvizuia vyama kufanya kazi zake, lakini tuna uwezo wa kuzuia vyama kujenga viota juu ya vichwa vyetu. Ndio maana watu wanajadili ni rais gani wa kuitawala nchi yetu, ni chama gani cha kulitawala taifa letu. Kila Mtanzania ana uwezo huu, ndio maana wengine wanakwenda Jangwani, wengine Dodoma na wengine wanasubiri kununuliwa. Zote hizo ni harakati za kuwazuia ndege wasitengeneze viota juu ya vichwa vyetu.
Kelele zinatosha kumfukuza ndege. Lakini kuna ndege wakaidi ambao kuwafukuza ni lazima utengeneze vinyago vya kuwatishia. Kelele na vinyago vikishindikana, basi kwa vile Mungu, ametuumba na utashi na akili na nguvu, basi ndege hufukuzwa kwa kupigwa! Hali ikifikia hapo, ndoto za akina Magufuli, huyeyuka! Majigambo yote hugeuka majuto. Mifano ipo, anayeitaka, anikumbushe baada ya uchaguzi, Mungu, akiniruhusu kuwepo!
Maoni yangu ni kwamba tusikatishwe tamaa na akina Magufuli. Kama kweli sauti ya watu ni sauti ya Mungu. Tuamini kwamba Mungu, atawatumia watanzania wote kumchagua rais. Na rais huyo atakuwa Mtanzania. Hakuna anayemfahamu kwa sasa hadi pale tutakapomaliza kupiga kura na atakapoingia Ikulu. Uchaguzi wa rais ni mambo ya kesho! Sasa hivi tuangalie yale yaliyo mbele yetu. Tuangalie yale tunayoyajua: rushwa, maadili bora, kupambana na umasikini, kupambana na UKIMWI, kuwatunza watoto yatima na wa mitaani, kuongeza juhudi katika kuzalisha mali, uwajibikaji na kujenga moyo wa uzalendo.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment