MAKALA HII ILICHAPISHWA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2005
MIAKA KUMI YA BEIJING
Tarehe 8 za mwezi huu wa tatu tunasherehekea siku ya Wanawake duniani. Sherehe za mwaka huu ni za pekee maana ni miaka kumi baada ya Ulingo wa Beijing. Ni wakati mzuri wa kupima mafanikio katika maeneo ya kipaumbele kama yalivyobainishwa na Ulingo wa Beijing: Je hapa Tanzania tumefanikiwa kuwawezesha wanawake kiuchumi na kuwasaidia kuondoa umasikini? Tumeweza kuwapatia wanawake haki na kuwaongezea uwezo wa kisheria? Je elimu kwa wanawake imeongezeka na wamepata ajira? Je wanawake wanashirikishwa katika maamuzi mbalimbali katika jamii yetu? Je wanawake wanashirikishwa katika kuchangia maendeleo na kutunza mazingira? Je afya ya wanawake imeboreshwa? Uzazi wa mpango umezingatiwa? Je tumefanikiwa kuondoa ukatili dhidi ya wanawake? na je mtoto wa kike amepewa kipaumbele?
Mbona bado tunashuhudia ukatili majumbani? Mbona vitendo vya ubakaji na udhalilishaji wa mwanamke bado vinashika kasi hapa Tanzania? Mbona akina mama wanabebeshwa mimba bila mpangilio? Akina mama wanakufa wakati wa kujifungua? Tunashuhudia ndoa za wake wengi na si ndoa za wanaume wengi? Manyanyaso kwenye ndoa yanamwangukia mwanamke na lawama za uzinzi ni za changudoa kana kwamba tendo la uzinzi ni la jinsia moja! Miaka kumi ya Ulingo wa Beijing, imebadilisha mtizamo wa watanzania kuhusu maswala ya kijinsia? Maswali haya ni muhimu wakati tunasherehekea. Isiwe kuimba, kunywa na kula, bali kutafakari na kupiga hatua!
Wanawake wenyewe wamejikomboa kiasi gani? Ni wangapi wanaithamini michango ya wanawake wenzao katika jamii? Ni wangapi wanaweza kumchagua kiongozi mwanamke katika jamii yetu na kumwacha kiongozi mwanaume? Ni wangapi wanaamini kwamba wanawake wanaweza kufanya mambo mengi sawa na wanaume?
Mkutano wa Beijing, ulitanguliwa na mikutano miwili mikubwa juu ya wanawake. Mkutano wa kwanza ni ule uliofanyika Mexico mwaka 1975 ambao ulitangaza Muongo wa Kimataifa wa Wanawake (International Decade for Women). Mkutano wa pili ni ule uliofanyika Nairobi mwaka 1985, ambao ulibainisha Mikakati ya Nairobi kuhusu Usawa, Amani na Maendeleo( Nairobi Strategies on Equity, Peace and Development). Mikutano hii miwili ndiyo iliyoweka misingi ya Mkutano wa Dunia wa Wanawake uliofanya mwaka 1995 huko Beijing, China.
Ili kuweka misingi mizuri ya kutekeleza maeneo ya kipaumbele Serikali yetu iliibua maeneo manne ya kipaumbele. Maeneo hayo ni:
- Kuwapatia wanawake haki na kuwaongezea uwezo kisheria;
- Kuwawezesha wanawake kushiriki katika ngazi za maamuzi;
- Kuimarisha wanawake kiuchumi na kuondoa umasikini;
- Kuwapatia wanawake elimu, mafunzo na ajira.
Ni kiasi gani serikali yetu imefanikiwa kuboresha, kuhamasisha na kushughulikia maeneo hayo yaliyopewa kipaumbele ni kazi ya kila Mtanzania kupima. Ni kiasi gani wanawake wamepatiwa haki na kuongezewa uwezo wa kisheria, ni kiasi gani wanawake wameshirikishwa katika ngazi ya maamuzi, ni kiasi gani wanawake wameongozewa nguvu za uchumi na kuufukuza umaskini, na kiasi gani elimu na ajira vimeongezeka upande wa wanawake. Hapa tunahitaji takwimu na si blabla.
Mambo ambayo yanaonekana wazi ni kwamba bado wanaume wanashikilia madaraka makubwa. Katika kipindi hiki cha miaka kumi, hatukuweza kumpata rais mwanamke, makamu wa rais mwanamke, waziri mkuu mwanamke au spika wa Bunge mwanamke. Tofauti na Getruda Mongela, mbunge wa AU. Tunao wanawake wengi wenye uwezo mkubwa. Nikianza kutaja majina, makala hii itakuwa majina matupu. Hawa wote wamefunikwa na mfumo dume! Vyama vyote vya siasa hapa nchi bado vinaongozwa na wanaume! Chama cha kina mama kilichokuwa kinaongozwa na Profesa Anna Tibaijuka, kiliponukia harufu ya siasa kilinyanyaswa na kutupwa shimoni! Sasa hivi Profesa Anna, ni miongoni mwa watu mashuhuri duniani, si wa kupuuzwa, labda kwa yule mwenye ulemavu wa akili!
Ukatili majumbani umeendelea kwa mtindo mmoja na wanaume wameendelea kuwa vichwa na viongozi wa familia. Mfumo dume unaendelea kushika hatamu na utamu katika taifa letu.
Jambo ambalo limejitokeza ni kwamba Ulingo wa Beijing haukuwafikia watanzania katika mfumo wa ushirikishwaji. Lilibaki fumbo na "Slogan" miongoni mwa watu wa hali ya juu, wasomi, viongozi na watu wa mijini. Kwa vijijini ni wimbo kama nyimbo nyinginezo za uhuru, maendeleo, demokrasia, utandawazi na utandawizi, soko huria na uwekezaji Nyimbo zinazoongozwa na watu walioshiba na wenye afya nzuri, nyimbo za kupumbaza na kudumaza akili ya watu wenye njaa na afya za ovyo! Mashirika mengi yameanzishwa kwa jina la kuwatetea wanawake. Mikutano, warsha na semina nyingi zimeendeshwa ndani na nje ya nchi kwa jina la kutetea haki za wanawake. Wale wanaojiita wanaharakati, wanaendesha magari mazuri na kuishi kwenye nyumba za kifahari Pesa nyingi zimetolewa kwa jina la kutetea haki za wanawake. Lakini mwanamke wa kijijini na wanawake wa majumbani waishio mijini, wamebaki katika giza nene kuhusiana na haki zao.
Inawezekana kuna mashirika yanayowashughulikia wanawake wa vijijini na wa majumbani. Ninasema inawezekana, maana hatuyasikii na kama yanasikika, yatakuwa yanatumiwa kama chambo cha pesa! Lakini pia kuna tatizo la mchango wa akina mama kutoandikwa na vyombo vya habari! Mfano mzuri ni shirika la Kivulini, ingawa halisikiki sana hapa Tanzania, kama yanavyosikika mashirika mengine yanayotajwa kwenye vyombo vya habari kila kukicha, Kivulini ni shirika lililoonyesha mfano wa pekee katika kutetea haki za wanawake.
Je, msomaji wa makala hii, umewahi kulisikia shirika la Kivulini? Kivulini ni shirika lisilo la kiserikali la kutetea haki za wanawake lenye makao yake makuu jijini Mwanza linalokutanisha watu wa jinsia zote kujadili, kutafakari na kutafuta suluhisho la ukatili majumbani.
Neno Kivulini linalotambulisha shirika hili linatokana na neno kivuli, kwa maana ya chini ya mti au paa ambako watu hukutana na kujadiliana kwa amani juu ya matatizo yao katika jamii. Ndoto za kivulini ni kujenga jamii salama isiyokuwa na ukatili ambayo haki za wanawake zinathaminiwa na kuheshimiwa.
Si kivuli cha maneno, ni kivuli kweli. Ukifika Jijini Mwanza, maeneo ya Mlango mmoja (Langolango),utakikuta kivuli hicho kinachowakusanya watoto, vijana, wazee wake kwa waume, kama si majadiliano juu ya usuluhishi katika familia, watakuwa wanajadili mbinu za kutumia kutokomeza ukeketaji, kupambana na ukatili majumbani, kuomba msaada wa kisheria juu ya mirathi, midahalo juu ya vyanzo vya ongezeko la ukatili katika jamii, kujengewa uwezo juu ya ukusanyaji, uchambuzi na usambazaji wa habari.
Ingawa jiji la Mwanza lina mashirika mengi yasiyokuwa ya kiserikali, Kivulini ni shirika pekee lilioanzishwa na wanawake na linalishughulikia kuzuia ukatili majumbani. Pia ni shirika pekee lenye mfumo wa kushirikiana na makundi mbalimbali katika jamii kama viongozi wa mitaa, vijiji, dini, vikundi vya kijamii na wanaharakati wa kujitolea.
Shirika la kivulini linachukua jukumu la kujenga uwezo wa kuelewa madhara ya ukatili unaotendeka majumbani miongoni mwa makundi mbali mbali na kuyaachia makundi hayo kubuni mbinu za kukomesha ukatili majumbani. Wawezeshaji wa Kivulini, hawachagui wala kupendekeza mbinu yoyote. Kazi yao ni kuelekeza ,kushauri, kuchochea kuhamasisha na kupandikiza mbegu ya ujuzi na utaalam katika mfumo mzima. Maamuzi ya nini kifanyike yanabaki mikononi mwa walengwa!
Jambo jingine la pekee katika shirika hili, ni kwamba wanawaachia uhuru wanajamii kuchagua ni kitu gani wangependa kujifunza kuhusiana na sheria za mirathi, ndoa, jinsia, stadi za maisha, ushauri nasaha, uchumi nk., wakichagua jambo la kujifunza, kivulini inashughulika kumtafuta mtaalamu. Mfano, wanajamii wanaleta maombi juu ya mdahalo wanaoutaka na njia wanayoitaka kuitumia, kama ni kwa njia ya filamu, ziara za kimafunzo, uchoraji, muziki msaada wa kisheria hasa pale wanawake wanapodhalilishwa. Ikilazimu, wanasheria wao wanakwenda kutoa msaada wa kisheria mahakamani au kutoa ushauri.
Kinachovutia Kivulini na kuleta matumaini ni kwamba wakati mashirika mengi yanakuwa na malengo ya kuhudumia maeneo makubwa, jambo linalozorotesha mafanikio, Kivulini inahudumia maneno machache katika wilaya mbili za Jiji la Mwanza, wilaya za Ilemela na Nyamagana, katika kata za Mirongo,Mbugani,Pamba,Nyakato,Buswelu,Mahina,Isamilo na Ilemela. Hii inawasaidia kuwafikia watu na kuwahudumia kwa karibu. Pia inakuwa rahisi kuunda vikundi vya majadiliano na ushirikishwaji. Kwa njia hii wameweza kupambana na changamoto kubwa ya mtazamo wa dini katika suala zima la kuleta uwiano kati ya wanaume na wanawake, mitizamo ya kimila na desturi, jinsi ya mazoea ya mwanamke na mwanamme ambapo katika baadhi ya maeneo mwanamke anaonekana ni sawa kunyanyaswa na changamoto ya wanandoa kutokuwa wazi juu ya kipato chao na wanakitumiaje. Changamoto hizi wamekutana nazo na kuzitafutia ufumbuzi kwa vile wanahudumia maeneo machache wanashirikisha walengwa, wanatengeneza jukwaa la majadiliano, wanasikiliza zaidi kuliko kusikilizwa.
Ili Ulingo wa Beijing, ufanikiwe, ni bora kuiga mfano wa Kivulini. Wimbo wa haki za wanawake, uingizwe katika matendo, utofautishwe na nyimbo nyingine tulizozizoea za uhuru, maendeleo, utandawazi, uwekezaji na demokrasia. Wananchi, na hasa wale wa vijijini waelimishwe juu ya haki za binadamu. Washirikishwe wote, wajadiliane na kukubaliana.
Serikali na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yaunde mazingira ambayo yatawasaidia watu kuanza kutafakari. Watu wenyewe waone hitaji la kukomesha ukatili dhidi ya wanawake, waone hitaji la kumsomesha mtoto wa kike, waone hitaji la kumshirikisha mwanamke katika maamuzi.
Kuna njia nyingi za kufanya haya. Badala ya kuonyesha video za miziki na vita, watu waonyeshwe video zinazoonyesha mambo ya jinsia, zinazoonyesha ukatili majumbani. Watu waonyeshwe video za wanawake viongozi, madakrati, maprofesa nk.
Michezo ya kuigiza, nyimbo na usanii vinaweza kuchochea mageuzi katika mtizamo. Hivyo serikali isambaze umeme vijijini, ili vyombo vya habari kama luninga na redio viweze kutoa huduma vijijini. Haki wa wanawake lisiwe ni jambo peke linalojitegemea, liingizwe katika mchakato mzima wa maisha ya siku kwa siku. Uwe ni mradi pamoja!
Mfano kati ya progmu sita za kivulini, ni ile ya Utetezi na Ushawishi, ambayo hushughulika na kushawishi mabadiliko ya miundo, sheria na kanuni zinazopingana na mikataba ya kimataifa ya Haki za Mwanamke, hasa haki ya kulindwa kisheria kuanzia katika ngazi ya kaya hadi taifa. Kimsingi progamu hiyo inawalenga watoa maamuzi katika ngazi ya mtaa, kata, wilaya, mkoa hadi taifa. Katika ngazi ya mtaa, programu hiyo hufanya kazi na viongozi wa jamii na dini ambao ni wa kwanza kuombwa msaada kwa vitendo vya ukatili unaotokea majumbani. Ndio maana programu hiyo huendesha midahalo. Katika ngazi ya taifa, programu hii imejikita katika jitihada za kushawishi sera na maboresho yake kwa kupitia mitandao kama GECHENET,TEN/MET,NGO Policy Forum na TANGO.
Miaka kumi ya Ulingo wa Beijing, ituelekeze kwenye matendo. Tuache maneno, unafiki na udanganyifu katika swala zima la kutetea haki za wanawake. Mungu azibariki sherehe zetu za siku ya mwanamke duniani na kuwabariki wanawake mama zetu na dada zetu wapendwa.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment