KUZIBEZA KURA ZA MAONI NI KUJIDANGANYA

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2005.

KUZIBEZA KURA ZA MAONI NI KUJIDANGANYA

Kura za maoni ni kitu kinachofanyika sehemu nyingi duniani. Zinafanyika kura za maoni kuhusu mambo mbali mbali, yawe ya kidini, kisiasa, au sanaa, michezo nk. Mara nyingi kura za maoni hazikosei Mbinu zinazotumika kupiga kura za maoni hazina mwanya wa kutembeza bahasha. Watu wanapiga simu, wanatuma ujumbe kwenye simu za mkononi na kutuma barua pepe. Hawa ni watu wa aina mbali mbali na wenye maonjo tofauti. Labda kitu kigumu kukifanyia kura za maoni bila kukosea ni uchaguzi wa Baba Mtakatifu. Wanajaribu, kuendesha kura za maoni, lakini mara zote hawafanikiwi. Kwa vile uchaguzi huu unaongozwa na “roho mtakatifu” kura za maoni ni lazima zigonge ukuta. Baba Mtakatifu, anachaguliwa kwa siri kubwa na kwa mtindo usiojulikana kwa mtu yeyote isipokuwa Makadinali wanaokuwa wamejifungia bila ya kuwa na mawasiliano yoyote na ulimwengu mwingine zaidi ya chumba chao wakimsubiri “roho Mtakatifu”. Lakini kwa vitu kama siasa ambazo zinaongozwa na demokrasia, vimezungukwa na vyombo vya habari na kila kitu kinaendeshwa kwa uwazi. Ni vigumu kura za maoni kufanya makosa.

Hivi majuzi BBC, iliongoza kura za maoni juu ya watanzania watano waliokuwa wamejitokeza kwa wakati huo kugombea urais wa taifa letu kupitia chama cha Mapinduzi. Waliopigiwa kura za maoni ni Babu, Mwandosya, Kikwete, Sumaye na Salim. Kikwete, aliibuka wa kwanza kwa kujizolea kura nyingi. Kabla ya hapo zilishafanyika kura nyingine za maoni kama tatu, ambazo nazo Kikwete, aliibuka mshindi. Na baada ya kura za maoni za BBC, ilifuata nyingine iliyofanyika kule Arusha. Pia na hii Kikwete aliibuka mshindi.

Hawa wote watano wanafahamika vizuri. Wamepikwa na kupitia mikononi mwa Baba wa Taifa. Ukimtoa Sumaye, aliyepanda chati kwenye serikali ya awamu ya tatu, kwa sababu ambazo Mungu, peke yake ndiye anajua, wengine wote wameandaliwa na Mwalimu. Hata kama Mwalimu, angekuwa hai leo angepatwa na kigugumizi kwa Salim na Kikwete. Angekuwa na kibarua kumpitisha Salim, kwa kuwashawishi watu wa Visiwani kumkubali. Kazi iliyomshinda 1985, ingemshinda pia mwaka huu. Salim, anakubalika bara kuliko anavyokubalika Visiwani! Nabii, hakubaliki nyumbani! Kura za maoni zinaonyesha Salim, akimfukuza Kikwete, kwa mbali kidogo. Mwalimu, asingekuwa na kigugumizi kwa Babu. Msimamo wake unajulikana. Angerudisha kadi! Kura za maoni zimeonyesha hivyo! Hata angefanya nini ni lazima aandamwe na zimwi la Mwalimu. Mwandosya na Sumaye, wangepata karipio kali kutoka kwa Mwalimu na kushauriwa wagombee ubunge. Ushauri kama alioupata Mrema, akaukataa. Kura za maoni zimeonyesha hivyo.

Wagombea wameongezeka na kufikia zaidi ya kumi. Labda namba hii itaongezeka maana Mangula, anataka kuutunisha mfuko. Kila mgombea kutoa milioni si mchezo. Hata wakiendelea hadi ishirini, ikiletwa kura ya maoni ni lazima Kikwete, atakuwa wa kwanza. Hao wanaokuja, hawatoki mwezini. Ni watanzania tunaowajua. Mungu, akipenda na Makamu wa Rais, akachukua fomu, Kikwete, atakuwa mbele! Hali inaonyesha hivyo. Inaweza kupuuzwa ikatumika mizengwe na nguvu za dola “chama” lakini ukweli utabaki pale pale na kawaida ukweli unauma na kuchoma!

Mheshimiwa Mapuri na vigogo wengine wa CCM, wamesikika wakizibeza kura za maoni. Wanasema hazina ukweli wowote na wala CCM, haiwezi kumchagua mtu kwa kufuata kura za maoni. Siku za nyumba Mwenyekiti wa CCM, alionya kwamba CCM, haiwezi kumchagua mgombea wake wa urais kwa kushinikizwa na vyombo vya habari.

Wagombea wa CCM, hawatoki mwezini. Ni watu wanaoishi kwenye jamii yetu. Tunawafahamu. Hivyo CCM, haiwezi kukwepa ushawishi wa wananchi. Hakuna ushahidi wa kutosha kuonyesha kwamba Halmashauri kuu, inawafahamu vizuri sana wagombea kuwazidi watanzania wengine. Na kama CCM, inamtafuta mtu wa kuliongoza taifa, haiwezi kukwepa maonjo na mapenzi ya watu wote wanachama wa CCM na wale wasiokuwa wanachama. Kama mtu ni fisadi, anajulikana kwa kula rushwa, anajulikana kwa kufuja ovyo pesa za serikali, anajulikana kwa kiburi chake na majigambo, anajulikana kwa kutotumikia bali kutumikiwa, anajulikana kwa kutolipenda taifa lake na kulithamini, anajulikana kwa kukaribisha miradi hewa na kushiriki kuiuza nchi, anatibiwa nje ya nchi, kila kitu chake kinanunuliwa nje ya nchi na watoto wake wanasomea nje ya nchi, halmashauri kuu haiwezi kuibadilisha hali yake. Mtu akishazidi miaka 55 ni vigumu kumbadilisha. Samaki hukunjwa angali mbichi, msemo wa Kiswahili!

Kama kura za maoni zingekuwa zinamtaja Lipumba, Mbowe, Mbatia, Mrema, Mtikila, Cheyo nk, kwamba hawa ndio wanafaa kuchaguliwa kuwania urais kupitia chama cha Mapinduzi, vigogo wa chama hicho wangekuwa na haki zote za kubeza kura hizo za maoni. Ingawa hawa niliowataja wana uwezo mkubwa wa kuliongoza taifa letu, lakini kwa vile ni wa vyama vya upinzani, CCM, ina haki ya kuwabeza. Sasa anayetajwa ni Kikwete. Huyu ni mwanachama wa CCM, tena wa ngazi ya juu. Si leo tu, hata mwaka 1995 chupu chupu akichukue kiti cha urais. Maneno ya vijiweni, eti mizengwe ilifanyika. Huyu si mtu wa kuchezea. Kikwete, si “Matonya”! Anakijua chama na chama kinamjua! Amekulia kwenye chama na siasa. Ni mtumishi wa serikali kwa muda mrefu. Amekuwa waziri wa mambo ya nchi za nje kwa kipindi cha miaka Kumi, amekuwa waziri wa Nishati na Madini na kushika nyazifa nyingine mbali mbali katika chama na serikali.

Kuna habari za vijiweni zinasema Kikwete, anawanunua watu wa kumpigia kura za maoni, kwamba anavinunua vyombo vyote vya habari, kwamba anamnunua kila mtu anayemwandika vizuri Kwamba mtu akimwandika vibaya, gazeti lote linanunuliwa na kuchomwa! Huyu Kikwete, ana pesa gani hizo? Mbona hatuzioni? Amezificha shimo gani?

Kama nilivyosema hapo juu, hawa wagombea hawatoki mbinguni. Tunaishi nao. Kikwete, anapendwa kwa vile amejionyesha kuwa ni mtu wa watu. Anachanganyika na watu wote wa kila aina na kila rika, jambo linalochukuliwa kama “Uhuni” .Hana makuu, Hatujamsikia akisema kwamba anaweza kuonana na Rais, wakati wowote anaoutaka, kama alivyosema mheshimiwa Fulani kwamba Ofisi yake na ya Rais zimetazamana, hivyo ni mtu wa maana sana. Kikwete, hana kashifa za wizi wa mali ya umma. Ameonyesha moyo wa kizalendo katika utendaji wake. Anashutumiwa kwa “Ufuska”. Lakini viongozi wote wanaomzunguka ni nani wa kumnyoshea kidole? Hili ni tatizo ambalo karibu ni la watu walio wengi. Ni tatizo linalohitaji mfumo wa kuyashughulikia maisha ya kiroho. Ni tatizo linalowakumba hata viongozi wetu wa dini. Wale tunaowaita watoto wa mitaani, wanatokana na tatizo hili. Hivyo huu ni mradi wetu sote. Ni lazima kukaa chini kama taifa na kutafuta mbinu za kupambana na tatizo hili. Mbinu za kufundisha mahusiano, au tuseme uhusiano kati ya mtu na mtu. Na wala hiki si kikwazo cha kumzuia mtu kuwa kiongozi wa taifa. Kama wengine wameongoza na mambo yakaenda vizuri wakati wana unyonge kama wa Kikwete, kwa upande wa mabibi, ni kwa nini Kikwete, asiweze?

Wanazusha kwamba Kikwete, ana Ukimwi. Kwa kuogopa maneno ya watu, yeye alikimbia hospitali kupima afya yake na kutangaza kwamba yeye ni safi. Ningekuwa yeye nisingefanya hivyo. Hata kama ni kweli, hii si sababu tosha ya kumzuia mtu kugombea urais. Kama ni Ukimwi, atakuwa hakuupata leo. Mbona alikuwa akizifanya kazi zake vizuri? Wenye virusi vya Ukimwi wana haki sawa na Mtanzania yeyote yule, wana haki ya kushiriki kila kitu hata uongozi wa juu katika Taifa letu.

Wanazusha kwamba Kikwete, hakununua nyumba ya Serikali, hivyo akipata nafasi ya kuwa rais, atazirudisha nyumba za serikali. Kwamba Kikwete, hakujenga mahekalu, hivyo atawahoji wale wote wenye mahekalu wakati hawana kipato cha kuwawezesha kuyajenga. Kwamba watoto wa Kikwete, wanasoma hapa ndani ya nchi na wengine wako Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam, hivyo akiwa Rais, atawahoji wale wanaosema Elimu ya Tanzania ni nzuri wakati wao watoto wao wanasoma nje ya nchi.

Wanazusha kwamba Kikwete, ni mkorofi. Ndani ya CCM, hakuna wa “kumfunda”. Eti yeye alikuwa ana “Fundwa” na Marehemu Mwalimu Nyerere. Hivyo akichaguliwa kuwa rais, atawapatia matatizo wazee wa chama na labda kusababisha chama kisiendelee kushika utamu.

Wanazusha kwamba Kikwete, amezungukwa na wahuni. Hivyo akichaguliwa Taifa letu litaongozwa na wahuni. Ukiangalia hoja hii kwa makini, wale wanaopachikwa jina la wahuni, ni vijana. Mbona tunawashuhudia wazee wahuni kuliko vijana?

Wanazusha kwamba Kikwete, hafuati muda. Je, ni yeye peke yake? Ni nani anafuata muda hapa Tanzania? Huu ni ugonjwa wa kila Mtanzania, Ni ugonjwa wa kutafutiwa dawa . Ni lazima sote kama taifa kutafuta na kubuni mfumo wa kutufanya kufuata muda na kufanya kazi masaa yaliyopangwa. Hii si kasoro ya Kikwete, peke yake. Hata hivyo hatujasikia kwamba hilo ni kikwazo kwa utendaji wake. Akiwa na wasaidizi wazuri, wasiokuwa na unafiki, atafuata muda tu! Si tunaambiwa rais ni kama mfungwa, anafuata maelekezo ya wasaidizi wake!

Mimi ninashangaa sana. CCM, wangekuwa wanajivuna kwa hizi kura za maoni. Anaposifiwa Kikwete, inasifiwa CCM. Kura za maoni zinaonyesha kwamba akisimamishwa Kikwete, CCM, itakuwa na kazi ndio ya kumpigia debe na kumuuza kwa wananchi. Kule kuendelea kuzibeza kura za maoni na ule woga kwamba kuna watu watakikimbia chama wasipoteuliwa kugombea urais, zinaonyesha wazi kwamba vigogo wa chama hawako upande wa Kikwete.
Tunabaki kujiuliza, kama CCM, wanabeza kura za maoni, wao wanamtaka nani huyo ambaye havutii hisia za watu? Maana kama anavutia ni lazima ataonekana kwa kila mtu. Kama anavutia ni lazima atapa kura za maoni. Atatoka wapi kama si miongoni mwa wale wale tunaowajua na kuishi nao? Atatoka wapi kama si wale wanaopitapita huku na kule wakisambaza bahasha miongoni mwa wajumbe wa mkutano mkuu?

Si lengo la makala hii kumpigia debe Kikwete. Wala hanifahamu mimi kwa sura. Hizo pesa zake sijakutana nazo. Mimi kama Mtanzania na mzalendo wa kweli, nina lengo la kuwakumbusha vigogo wa CCM, kwamba sauti ya watu ni sauti ya Mungu. Mheshimiwa Sumaye, alisema kwamba Rais wa Tanzania, atachaguliwa na Mungu. Na Mheshimiwa Magufuli, akarudia kauli hiyo, mara kwa mara vigogo wa CCM, wamekuwa wakirudia kauli hiyo kwamba Rais wa Tanzania, atachaguliwa na Mungu. Ni Mungu, gani anayeongelewa asiyepitia kwa watu wake? Kwa upande wa CCM, Mungu amesema kupitia kwa watu kwamba mtu mwenye sifa ni Kikwete. Hiyo ndiyo sauti ya Mungu. Si maoni yangu,. Bali ni maoni ya watu waliopiga kura za maoni. CCM, inaweza kuamua kuziba masikio, lakini ukweli utabaki palepale!

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment