KUONYA TU HAITOSHI!

MAKALA HII ILICHAPISHWA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2005

KUONYA TU HAITOSHI!

Kanisa katoliki limewaonya wagombea wanaotoa pesa wakati wa uchaguzi. Limewataka waumini wake kutowachagua wagombea uongozi wanaowashawishi wapiga kura kwa kumwaga pesa. Onyo hili lilitolewa na Rais wa Baraza la Maaskofu katoliki Tanzania (TEC), Askofu Severin NiweMugizi, tarehe 20 mwezi huu katika kanisa Kuu la Kristo wa Msalaba, wakati wa Ibada aya Misa ya kumsimika Askofu mpya wa Jimbo la Dodoma, Mhashama Yuda Thadeus Rwa,ichi.

Askofu Severin, alisema kuwa yeye na maaskofu wenzake wanasikia kuwa wapo baadhi ya wagombea wanaotaka uongozi ambao wanapita katika maeneo mbalimbali na kumwaga pesa ambazo hazijulikani zilikotoka. Aliwataka wananchi kuwakataa viongozi wa namna hiyo, kwani watawawezesha kushiba kwa siku moja na kuwasahau baada ya uchaguzi. Aliwataka Watanzania kuacha tamaa ya fedha ili kuliepusha taifa na mauti. " Tamaa mbele mauti nyuma" alisisitiza.

Ni jambo zuri na muhimu kwa maaskofu wetu kutoa maonyo juu ya mambo mbali mbali katika jamii yetu na hasa wakati huu tunapoelekea uchaguzi mkuu. Maaskofu ni manabii. Ni kazi yao kusema bila woga, bila kulenga kumfurahisha mtu yeyote, lengo lao ni kuifurahisha jamii nzima, ni haki ya jamii nzima, ni uzima wa jamii nzima. Wao ni sauti ya Mungu, katika maisha yetu ya kila siku, sauti isiyo pendelea wala kubagua, sauti isiyopotosha wala kupumbaza, sauti ya ukweli haki, wema na huruma!

Jambo la kuwakumbusha maaskofu wetu, na hili ni la kuwakumbusha kwa unyenyekevu, nikiwa nimepiga magoti tena bila kustahili! maana ni nani mwenye uwezo wa kuwakumbusha maaskofu wetu kitu chochote kile? Wao ni mwanzo na mwisho, Alfa na Omega! Ninapenda kuwakumbusha kwamba KUONYA tu haitoshi! Si lengo la makala hii kupunguza "Ualfa na Uomega" wa maaskofu wetu. Lakini alama za nyakati zinalazimisha jambo hili! Ni lazima waonyeshe kwa matendo kwamba wanaichukia rushwa, kwamba wanachukia hongo na wanauchukia umasikini wakati wa uchaguzi. Ni lazima wawe na mifumo ya kuwazuia watu kutenda dhambi. Rushwa ni dhambi kama zilivyo dhambi nyinginezo. Mwanadamu ni mwanadamu, anabaki hivyo hadi kifo, ni lazima akumbushwe na kusaidiwa kwa karibu. Kwa maneno mengine, wanadamu wanahitaji mifumo ya kusaidiana wao kwa wao ili kuishinda dhambi!

Mtu mchokozi, asiyekuwa na imani, asiyetambua "Ualfa na Uomega" wa maaskofu, mtu asiyekuwa na heshima na utovu wa nidhamu, anaweza kuuliza swali: Mheshimiwa Askofu Severin, anaposema: " Mimi na wenzangu tunasikia kuwa wapo baadhi ya wagombea wanaotaka uongozi ambao wanapita katika maeneo mbalimbali na kumwaga pesa ambazo hazijulikani zilikotoka", Je, maaskofu wanajua pesa zinazomwagwa makanisani zinatoka wapi? Tunasikia vigogo wa serikali na wafanyabiashara wachache wanaomiliki uchumi wa nchi hii wanatoa sadaka, zawadi na misaada kanisani. Ni pesa nyingi kiasi cha kutia shaka kwa Mtanzania wa kawaida. Pesa hizi zinatoka wapi? Viongozi wa serikali mishahara yao inajulikana. Mbona maaskofu wasishangazwe na hilo? Kwanini washangae anapolengwa mlalahoi? Hongo wakati wa uchaguzi mkuu inawalenga walalahoi, ni wakati wao wa kuvuna na kuneemeka, japo kwa si chache! Ni wakati wa kuonja tone la matunda ya uhuru wa nchi yao!

Kuna watu wanasema zafanana. Pesa zote zinafanana! Zile za wizi na zile za halali. Zile za kununua kura na zile za kutoa sadaka, zaka na zawadi kanisani. Zote zafanana! Kama ni kuzikataa, basi zikataliwe zote! Na kama ni kuzikubali basi zikubaliwe zote. Kama zinapokelewa za sadaka na zaka, kwa nini zisipokelewe za kura. Wanaozitoa ni wale wale. Wanakozichota ni kule kule! Hii tu peke yake inatosha kuonyesha jinsi kuonya tu, kusivyotosha. Watu hawawezi kuelewa. Utabaki utata. Au watu watajifanya kuelewa kwa kusema: Ya Kaizari mpe Kaizari na ya Mungu mpe Mungu. Kwa msingi huu hatuwezi kujenga taifa lenye haki na usawa, taifa linalompendeza Mwenyezi Mungu.

Kama nilivyotaja hapo juu rushwa na hongo ni dhambi kama dhambi nyingine. Hivyo kwa mfumo wa kanisa katoliki, hizi ni miongoni mwa dhambi zinazowekwa kwenye meza ya kitubio. Hivyo mapadri na maaskofu wa kanisa katoliki wanafahamu zinakotoka pesa za rushwa na hongo. Hata hizi za uchaguzi wanafahamu zinatoka wapi. Baadhi ya hawa wanaotoa pesa za kununua kura ni Wakatoliki. Siku ya siku ni lazima waungame dhambi hii ya mauti! Kwa kiapo chao cha sakramenti ya kitubio, mapadri na maaskofu wanakatazwa kutumia kitubio kama ushahidi. Hivyo kutoa onyo juu ya kitu wanachokifahamu chanzo chake ni sawa na mchezo wa kuuigiza. Kwa maneno mengine wanaendeleza mifumo ambayo mtu anaweza kuiita " Adui wa Umma".

Na kwa upande mwingine ni kwenda kinyume na mafundisho ya Yesu Kristu anaposema:
" Basi, msiwaogope watu hao. Hakuna cho chote kilichofunikwa ambacho hakitafunuliwa, wala kilichofichwa ambacho hakitafichuliwa. Ninalowaambieni ninyi katika giza, lisemeni katika mwanga; na jambo mlilosikia likinong’onezwa, litangazeni kwa sauti kuu."(Matayo 10:26-27).
Ni maadili mazuri kutunza siri za kitubio, lakini kwa upande mwingine, kitubio ni "Adui wa Umma". Adui anajulikana, anatunzwa na kulindwa! Mbaya zaidi hakuna mfumo wa kumshughulikia adui huyu. Anaendelea na madhambi yake, kwa vile ana Mbuyu wake!

Wakati wanatoa onyo kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka huu ni bora maaskofu wetu wakatafakari maneno haya kwa kina:
" Ninyi ni kama chumvi kwa dunia! Lakini chumvi ikipoteza ladha yake itakolezwa na kitu gani? Haifai kitu tena, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu. Ninyi ni mwanga wa ulimwengu! Mji ukijengwa juu ya mlima hauwezi kufichika. Wala watu hawawashi taa na kuifunika kwa chungu, ila huiweka juu ya kinara ili iwaangazie wote waliomo nyumbani. Vivyo hivyo, ni lazima mwanga wenu uangaze mbele ya watu , ili wayaone matendo yenu mema, wamtukuze baba yenu aliye mbingu." (Matayo 5:13-16).

Kama maaskofu wetu bado wanapiga kelele ya rushwa, hongo na kununua kura, maana yake ni kwamba chumvi imepoteza ladha yake! Tunaishi kwenye giza na taa imefunikwa kwa chungu. Uko wapi mwanga wa maaskofu wetu? Uko wapi mji wetu uliojengwa juu ya mlima?

Tafiti mbalimbali zinaonyesha kwamba Watanzania wengi ni maskini, hasa wale wanaoishi vijijini. Mmoja kati ya Watanzania watano hawapati chakula cha kutosha, na mmoja kati ya Watanzania watatu wanashindwa kukidhi mahitaji ya msingi. Mabadiliko ya kiuchumi ya miaka ya 90 yamewatajirisha wachache, bila kupunguza umasikini wa walio wengi. Utajiri umo mikononi mwa chache.

Tanzania imekuwa miongoni mwa mataifa yaliyopata misaada mingi ya kifedha na kitaalamu kutoka kwa wafadhili, lakini matunda yake ni madogo sana. Nchi imejaa miradi ambayo haikukamilishwa.

Sera ya kuwa na soko la pamoja inatekelezwa kupitia Muungano wa Forodha wa Afrika Mashariki na kufuatiwa na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC). Uchumi wa Tanzania unakuwa huria, na nchi inafurika bidhaa kutoka nje, na kuwa kitovu cha uwekezaji na ajira kwa wageni. Kwa vile Watanzania wengi hawana ujuzi unaohitajika, wengi watashindwa kunufaika na fursa zitakazojitokeza. Faida yote ya uwekezaji itapelekwa bila kizuizi. Bidhaa zetu za kilimo zitakosa soko kutokana na uzalishaji na ushindikaji duni.
Huko wapi mwanga wa Maaskofu wetu katika mambo haya? Iko wapi ladha ya chumvi? Ni watanzania wachache tu walio katika sekta rasmi inayobebeshwa mzigo mzito wa kodi nyingi na sheria ngumu. Hivyo, wengi wetu tunajipatia riziki kwa kubangaiza tukitumia ujanja wetu kuzalisha na kuuza kinachowezekana, hiyo ndiyo " Bongo land".

Ongezeko kubwa la watu linachangia uharibifu mkubwa wa mazingira. Watu wanatafuta mkaa kupikia, ardhi kulimia na maji kumwagilia, hivyo kuchochea mifarakano zaidi. Watu wanaendelea kumiminika mijini kwa matumaini ya kujipatia maendeleo. Soko huria linawanufaisha wenye mitaji na ujuzi na kuwaacha hoi makabwela. Vijana wanabaki kufukuzia ajira chache zilizopo. Umasikini unakithiri na pengo kati ya matajiri na maskini linaongezeka. Wimbi la ujambazi linatanda, hasa katika miji mikubwa ya Dar-es-Salaam Mwanza na Arusha.

Kuonya tu haitoshi. Maaskofu wetu watoe mwanga kwa mambo mengi yanayolikabili taifa letu, mfano: Idadi ya watu inayoongezeka kwa kasi na umuhimu wa kukidhi mahitaji yao, mvua zisizotabirika na umuhimu wa kuwa na mbinu mpya za kilimo ili kulisha taifa letu, mzigo mzito kutokana na magonjwa yanayoibuka,( UKIMWI unatishia kuliangamiza taifa letu, Maaskofu wetu wamekalia kuonya, na kusema acha hili acha lile, bila kuingia kwenye kiini cha tatizo lenyewe) utandawazi na soko huria, ukweli kwamba wengi wetu hatuna ujuzi unaohitajika katika mfumo wa ushindani mkali duniani.

Mtu wa kijijini ambaye kwa mwaka mzima hawezi kutengeneza shilingi 50,000, ambaye anadaiwa karo ya shule, pesa za matibabu, mchango wa kijiji, mchango wa kujenga shule, sadaka na zaka za kanisa, atakataa vipi kupokea 100,000 za kumpitisha mgombea. Kwa nini amchague asiyekuwa na kitu kama yeye, kama kuna uwezekano wa kufaidika na mwenye pesa? Hata hivyo tunawachagua kufanya nini"? Tuliwachagua 1995, tukawachagua tena 2000, walifanya nini? Si kula tu? Na sasa wanataka tuwachague tena 2005, watafanya miujiza ipi? Atajiuliza mtu wa kijijini. Ni bora achuke hizo pesa amalize shida yake ya wakati huo huo. Maana hata asipowapatia kura, watapita tu! Si ni bora kupata faida hata kama ni ya siku moja? Heri kupata kuliko kukosa!

Askofu hawezi kununuliwa wakati wa kupiga kura. Ana shida gani? Ana chakula cha kutosha, ana nyumba nzuri, anapata matibabu, ana usafiri, ana pesa nje na ndani ya nchi, anatunza jamaa zake. Magumu ya maisha wanayoyaonja watanzania walio wengi, yeye yanapitia mkono wake wa kushoto! Siku anazoishi hapa tanzania kwa mwaka ni chache ukilinganisha na zile anazokuwa nje ya nchi. Hivyo si haki kwa maaskofu wetu kutoa onyo la kutopokea pesa za uchaguzi wakati hawana mfumo wa kuwasaidia watu kuinua kipato chao na wakati wao wanaishi zaidi nje ya nchi!

Tatizo lililo mbele yetu ni kubwa zaidi ya kununua kura, zaidi ya kubadilisha uongozi. Ni swala la kujiuliza sisi watanzania ni nani? Kwa nini tuko hivi? Tunatoka wapi na tunakwenda wapi? Je, jamii yetu imejengeka katika mtandao na mahusiano yanayosimamia haki na kutimiza majukumu yetu kwa familia, koo, taifa, na imani zetu, tukiwa kazini, shuleni na katika shughuli zetu nyingine za kulijenga taifa letu?

Kuyajibu maswali haya ni lazima mtu awe na mfumo Haya ni maswali yanayojibiwa katika maisha ya siku kwa siku. Maisha yenye mpangilio, maisha yenye malengo. Ni maswali ambayo kila mtu anaweza kuyajibu peke yake, lakini ili yawe a maana ni lazima yaonyeshe uwajibikaji wa mtu kwa mtu, jirani kwa jirani, familia kwa familia. Maaskofu wetu wana nafasi ya pekee kuliwezesha hili. Lakini giza limetanda na chumvi haina ladha tena.

Tunapolekelekea uchaguzi mkuu mwaka huu, tunahitaji matendo zaidi ya maonyo, tunawahitaji watu wa kujitoa muhanga kuipandisha taa juu ya kinara ili iwaangazie wote waliomo nyumbani, wote wanaoishi Tanzania! Tunawahitaji wa kujenga mji wetu mtukufu juu ya mlima Kilimanjaro!

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment