FALSAFA NA UFUNUO WA MAARIFA

UHAKIKI HUU ULICHAPWA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA 2009

UHAKIKI WA KITABU: FALSAFA NA UFUNUO WA MAARIFA.

1. Rekodi za Kibibliografia

Jina la kitabu kinachohakikiwa hapa ni “ Falsafa na Ufunuo wa Maarifa” na kimetungwa na Dk. Adolf Mihanjo, ana shahada ya Licentiate na ya Udaktari wa falsafa katika falsafa (Doctor of Philosophy in philosophy) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Aquino Philippines, amefundisha vyuo mbali mbali duniani na sasa hivi ni mhadhiri wa falsafa katika chuo Kikuu cha Dar-es-salaam na mhadhiri mgeni katika Chuo Kikuu kishiriki cha falsafa cha Salvatorian Morogoro. Mchapishaji wa kitabu hiki ni SALVATORIANUM, na amekipatia namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 9987 645 16X. Kimechapishwa mwaka 2005 kikiwa na kurasa 220.Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo.

II. Utangulizi

Hiki ni kitabu cha pili cha aina yake kinachohusu somo na dhana ya falsafa kwa lugha ya kiswahili. Katika kitabu hiki Dacta Adolf Mihanjo anayachambua na kuyatafakari kwa makini mawazo na mipangilio ya hoja za wanafikara wakuu wa enzi za kati na usasa, kati yao wakiwa wanafikara wa kikristo, wa kiisalamu, wa kiyahudi na wa kisayansi, Wanafalsafa hao ni Augustino, Boethius, Pseudo Dionysius, Erigena, Anselm, Gauinilon, Avicenna, Averroes, Moses Maimonides, Thomas Aquino, John Duns Scotus, William wa Ockham, Johannes Eckhart, Erasmus, Luther, Machieavelli, Michel De Montaigne, Kepler, Galileo, Copernicus, Isaac Newton, Bacon na Thomas Hobbes.

Katika kitabu hiki, Dacta Mihanjo anaonyesha ni namna gani wanafikara hawa waliyatumia mawazo ya wanafalsafa wa awali hasa Plato na Aristole katika kujenga usanisi wa falsafa zao, falsafa ambazo zilitoa mihimili ya hoja za kimaadili, kisiasa, kidini na za kisheria. Aidha Dacta Mihanjo anaonyesha kuwa, mpangilio huarifiwa na itikadi ya kisiasa ambayo nayo hupata urejeo wa uarifiwa wake kutoka aina moja au nyingine ya falsafa.

Kitabu hiki kina sura Saba, tofauti na kitabu cha kwanza, kitabu hiki hakina maswali ya majadiliano, ila kina orodha ndefu ya vitabu vya rejeakuliko cha kwanza kitu kinachoonyesha kazi muhimu na ya makini aliyoifanya Dk Adolf Mihanjo. Kama ilivyo katika kitabu cha kwanza kitu kinachovutia zaidi katika kitabu hiki ni orodha ya maana ya baadhi ya maneno (Kiswahili- Kingerea na Kingereza-Kiswahili) anayotuwekea Dk Mihanjo mwishoni mwa kitabu. Ameonyesha jinsi Kiswahili kinavyoweza kumudu kupambana na kila aina ya elimu.

Kitabu hiki kimesheheni maneno mengi, ambayo wengi wetu tumezoea kuyatumia kwa kuchanganya kiingereza na kiswahili, kwa kufikiri kwamba hakuna kiswahili chake. Maneno kama: Necessary being- Uwepo lazima, Contigent being- Uwepo wezekano, Skeptics- Wakushuku, Emanation – utokeo nk. Katika aya zifuatazo nitatoa muhtasari na tathmini ya kitabu, lakini baada ya kudokeza mazingira yanayokizunguka kitabu hiki.

III. Mazingira yanayokizunguka kitabu hiki

Pengine cha kutia moyo zaidi ni kuwa, Dacta Mihanjo anaufunua ukweli wa kihistoria wa kukua kwa mawazo ulaya akionyesha kuwa, ni pale tu ambapo falsafa iliandikwa kwa lugha enyeji au lugha za watu husika ndipo mapinduzi makubwa ya kifikara na ya kijamii yalianza kuchukua kasi ya ajabu. Locke na Hume waliandika kwa kiingereza, Voltaire na Rousseau kwa kifaransa na Kanti kwa Kijerumani.

Kitabu hiki kinakuja wakati taifa letu liko katika majadiliano ya ni lugha gani itumike katika kufundishia.
Wapo wanosema, tutumie lugha ya kiingereza, na wapo wanasema tutumie kiswahili. Maswali kama, je, tunaweza kusema kuwa fikara na mawazo ya mtu au jamii yako katika lugha yake na kukomaa kwa fikara za mtu huenda sambamba na kukomaa kwa lugha yake na kwa hiyo kama wazo haliko wazi kwake, haliwezi kupata lugha iliyokuwa wazi? Yatapata majibu katika kitabu hiki. Na swali jingine, Kama je, kukomaa kwa fikara ni sharti muhimu la kukomaa kwa lugha? Litapata jibu katika kitabu hiki.

Kitabu hiki kinatoa mwanga kwamba tafsiri, elimu yetu, mawazo yetu na lugha yetu lazima vikue na kuendelea kukotana na maghamuzi yetu. Mawazo yaliyomo katika lugha za kigeni yatasaidia tu kukomaza maghamuzi yetu. Hivyo tafsiri ya maneno ya kisayansi na falsafa katika kiswahili itakuwa na maana tu kama itasaidia kukomaza maghamuzi yetu na kuleta maghamuzi mapya ambayo yatahitaji maelezo mapya.

Kwa umakini wa hali ya juu Dacta Mihanjo anaonyesha namna gani akili na upevu wa binadamu wa kuelewa mambo na uwezo wa kujenga hoja chini ya msingi ya nadharia maalum ulikuwa unakua kutoka hatua moja hadi nyingine.Aidha anaonyesha namna gani nadharia za kifalsafa zilikuwa zinazuka na kutoa maelekeo ya kijamii, kisiasa, kiuchumi na kimaadili katika vipindi na nyakati tofauti.

Hoja zinazotolewa hapa ni za kihistoria. Si kubahatisha wala kubishana kwa nia ya kubishana. Hoja zinazotumiwa hapa si za kukipendelea Kiswahili kwa manufaa ya watu Fulani kama mawazo ya watu wengine wanaopinga matumizi ya kiswahili. Hoja zinazotumika katika kitabu hiki si za kutaka kutengeneza soko la vitabu vya Kiswahili au kutaka kukiuza kitabu hiki, ni ukweli ambao kuupinga ni lazima kwanza kuikana historia!

Walengwa wa kitabu hiki ni Wanafunzi wa vyuo vikuu vya Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla, Walimu na vyuo vya ualimu, Wanafunzi wa Sekondari, viongozi wa wananchi na kila mtu mwenye hamu ya kukuza upeo wake wa kuuelewa dhana ziongazo ulimwengu ambamo yeye ni sehemu. Baada ya maelezo haya sasa tuone kitabu chenyewe kwa muthasari.

IV. Muhtasari wa Kitabu.

Sura ya kwanza inaangalia umuhimu wa Falsafa katika Tanzania ya leo kwa ujumla, falsafa na dhana ya usomi na kazi, dhana ya Kiswahili na Falsafa, Somo Kutoka kukua na kupanuka kwa Maarifa Ulaya, hisoria fupi ya Mapambano ya hoja, Mjadala Kuhusu Dhana ya Haki, Maadili na Sheria.

“ Hakuna kipindi ambacho Tanzania katika uhai wake inahitaji malezi ya kifalsafa kama katika kipindi hiki cha mpito wa kifikara. Kwa yule ambaye kwake maisha ni kula, kulala, kushiba, kunywa na pengine kuendesha gari lake zuri, anaiona Tanzania katika mtazamo wa kimaendeleo kwani anajitosheleza katika mahitaji yake anayofikiri ni muhimu. Kwake hali ya kushangaa haipo. Hashangai iwapo haya maendeleo yana uhimili wa kiasi gani na yanaacha utata upi. Hashangai iwapo kama hali iliyopo sasa hivi ndio inayotakiwa kuwepo. Na mbaya zaidi, hashangai juu ya nini kinapaswa kufanywa” (Uk. 11).

Katika sura hii Dacta Mihanjo, anaendelea kujenga hoja kwa kuelezea umuhimu wa falsafa katika maisha ya binadamu na kwa Mtanzania:
“ Mwanafalsafa mashuhuri Socrates anatuambia kuwa ‘ an unexamined life is not worthy living’ yaani maisha yasiyotafakariwa hayafai kuyaishi.Naye mwanafalsafa Jeremy Bentham anatuambia kuwa ‘ it is better to be a huma n being dissatisfied than being a pig satisfied’, yaani ni bora kuwa binadamu asiyetosheka kuliko kuwa nguruwe aliyetosheka.” (Uk wa 11).
Mihanjo, anaichambua Tanzania baada ya Uhuru, Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea na mabadiliko ya kisiasa yaliyoikumba dunia katika miaka ya 1980 hadi miaka ya 1990, yaliyoifanya falsafa na itikadi ya kijamaa kupoteza nguvu yake ya kimamlaka na hivyo kuyaacha maamuzi yetu ya kijamii, kisiasa, kiuchumi na hata kisheria bila ya uhimili maalum wa kifalsafa wa kuarifu ubora wa maamuzi yetu.

“ Ukosefu wa falsafa ya kijamaa, nguvu ya mamlaka ya kimapokeo na kifo cha Mwalimu Nyerere, vimeiacha Tanzania katika hali ya utupu ama wa kinadharia au kimamlaka ya mapokeo. Hii ina maana kuwa, Tanzania katika karne hii ya utandawazi inayoongozwa na falsafa ya kiliberali, imeachwa bila ya mihimili maalum yakifalsafa ua kinadharia ya kuongoza au kuarifu maamuzi yake ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Katika hali kama hii, uwezo wetu wa kufikiri kwa kina na wa kuyachambua mambo, ndio vitu pekee vilivyokabi vya kutaarifu ubora wa maamuzi yetu.”(Uk wa 12).

Katika sura hii, Mihanjo anagusia, dhana ya usomi na kazi katia taifa letu, na kupendekeza njia mbadala. Watu walisoma ili wapate kazi. Hali ya sasa hivi watu wanahitimu, lakini hawapati kazi! Hivyo, kufuatana na mawazo ya Mihanjo: “ Badala ya elimu ile inayolenga moja kwa moja soko la ajira, yahitajika kutolewa kwa elimu ambayo humuunda mtu ajiunde mwenyewe… haya mapana ya kifikara yanahitaji kwa kiasi kikubwa sana malezi ya kifalsafa”(Uk wa 15).

Kwa kusisitiza matumizi ya Kiswahili, mwandishi anatoa mfano wake mwenyewe, pale alipoanza kufundisha falsafa kwa lugha ya kiswahili na kugundua kwamba wanafunzi walielewa zaidi kuliko alipokuwa akitumia lugha ya kiingereza. Wazo la kuandika vitabu vya Falsafa kwa kiswahili lilisukumwa na maangamuzi yake ya kufundisha falsafa kwa kiswahili.

Katika sura hii mwandishi anaelezea kwa kifupi Historia fupi ya Mmapambno ya hoja na mjadala kuhusu dhana ya haki, Maadili na Sheria.

Sura ya pili, inashughulikia Falsafa ya Augustino.Historia yake na mawazo yake. Tathmini ya Augustino Juu ya Maarifa ya Binadamu, maelezo yake kuhusu ukushuku, maarifa na mahisio, maumbile na mahusio, nadharia ya uvuvishi. Sura hii, pia inaelezea msimamo wa Augustino juu ya Mungu, Ulimwengu Umbwa, Nadharia ya uumbaji- kutoka kusikokuwepo, Kanuni ya Uzalishaji, Falsafa ya Maadili nk.

“Falsafa ya Augustino iliibuka kama matokeo ya jitihada zake za kuushinda uovu wake. Swali la msingi lililokuwa linasumbua sana kichwa chake ni swala kuhusu chanzo cha uovu. Aliyaona na kuyatambua maovu na mapungufu makubwa katika maisha yake na kujiuliza kama hivyo ndivyo alipaswa kuishi”(Uk wa 33).

Shughuli za kifalsafa za Augustino, ziliibuka katika akili yake kama matokeo ya nia yake kubwa ya kujihusisha na hatma ya maisha yake. Hitaji la kujua hatma ya maisha yake ilitoa msukumo mkubwa katika kujihusisha kwake na mambo ya falsafa. Tatizo la msingi ambalo lilijenga muhimili au msingi wa safari yake ya utafiti wa ukweli lilikuwa ni swala la UOVU kama ni tatizo la kimaadili: “ Namna gani mtu anaweza kuuelezea uwepo wa maovu katika maisha ya binadamu? Wakushuku walikuwa wamesema kuwa Mungu ni muumbaji wa kila kitu na vile vile Mungu ni mwema Kama mungu ni mwema je inawezekanaje maovu kuibuka kutoka kwenye dunia ambayo Mungu aliiumba kama kamilifu?” (Uk wa 35).

Katika sura hii, bila kuchoka wala kukweka, Dacta Mihanjo, anaelezea falsafa yote ya Augustino.Mawazo ya Augustion, yanayoonekana kuwa magumu kwa lugha ya kiingereza, kama vile Mji wa Mungu, Upendo, na Historia, yanafafanuliwa vizuri kwa lugha ya kiswahili.

Sura ya tatu, inashughulikia Falsafa wakati wa kipindi cha Ugiza. Kipindi hiki ni kile cha kuanguka kwa himaya ya kirumi katika mwaka 476. Katika kipindi hiki watu hawakuongoza mawazo na matendo yao chini ya fikara pembuzi za kifalsafa. Kilikuwa ni kipindi cha ugiza wa fikara. Ilikuwa ni wale watu ambao walikuwa na fikara zisizofunuka na duni ambao walibomoa nguvu za kisiasa za Urumi, na ambao waliharibu taasisi za kiutamaduni au fikara za kifalsafa za Ulaya magharibi. Katika kipindi hicho, tabia ya usomaji na uundaji wa fikara pembuzi ulikuja kuwa karibu ufe au kutuama kabisa. Kwa sababu hiyo, maarifa yote ya kifalsafa na tabia ya uchambuzi wa mambo vilikuja kupotea kwa kipindi cha karne sita zilizofuata, Falsafa iliwekwa hai na wanafikara wa kikristo ambao walikuja kuwa kama chombo ambacho kazi za kifalsafa za akina Socrates, Plato, Aristotle na wanafalsafa wengine wa awali zilikuja kuwafikia watu wa magharibi.

Wanafalsafa wanaojadiliwa katika kipindi cha ugiza ni: Boethius, Dionysius Areopagite na John Scotus Erigena na mawazo ya mgawanyo wa maubile; maumbile ambayo Yameumbwa na ambayo hayajaumbwa, maumbile ambayo yamembwa na ambayo huumbwa, maumbile ambayo yameumbwa na ambayo hayaumbi na maumbile ambayo hayaumbi wala hayajaumbwa.

“Nadharia ya Erigena ya mgawanyo wa maumbile, ilionyesha kwa kiwango kikubwa maarifa aliyokuwa nayo ya “ Neo-Platonism”. Lakini pamoja na ukweli huo, ilimfikisha vile vile kwenye hitimisho lisiloepukika la “Pantheism”= (Uwepo wa Mungu ndani ya kila kitu)” (Uk wa 81).

Sura ya Nne, Dacta Mihanjo, anajadili matamshi ya Awali kuhusu matatizo Makuu ya Kifikara na kifalsafa: Tatizo la uhusianishwi wa kitu kionwacho na wazo lijengwalo la uwepo wa mawazo jumla, Nadharia ya egemeo hodhi ya vitu ndani ya mawazo jumla, Nadharia ya Mawazo utupu, na Nadharia ya uhusisho.

“ Kipindi hiki kilikuwa ni kipindi ambacho kilitegemewa kuamsha moyo wa usomi na utaaluma chini ya Charlemagne.Tumaini hili lilitokana na changamoto iliyotokana na kuonekana kwa makala ya Erigena, makala ambayo iliandikwa kwa ufundi na ustadi wa hali ya juu na ambao ulionyesha mpangilio safi wa kifikara kuanzia kigezo kikuu hadi mahitimisho” (Uk wa 83).

Sura hii pia inajadili uthibitisho wa uishi wa Mungu, hizi ni hoja za kiontolojia za Anselm.Hoja za Anselm zinatajwa na kukanushwa na Gaunilon.Anselm, anajibu ukanusho wa Gaunilon. Hitimisho la sura hii ni uchambuzi wa imani na fikara katika falsafa za waarabu na wa yahudi.Wanafalsafa wa Kiarabu wanaojadiliwa ni Avicena na Averroes. Na Mwanafalsafa wa kiyahudi anayejadiliwa ni Mosess Mamonides.

Sura ya Tano, inajadili kilele cha Falsafa ya enzi za kati: Muundo wa “Scholastic” wa Thomas Aquino.Haya ni mafanikio ya Thomas Aquino 1225-1274 ya kuweka pamoja usanisi usiotikisika, maang’amuzi yaliyokuwemo kwenye kazi za kiwango cha juu sana ya kifalsafa ya wagiriki, warumi na teolojia ya Kikristo. Thomas Aquino, aliipatia Falsafa sura ya Ukristo.Anakumbukwa kwa kuuibatiza Falsafa.

“Thomas Aquino, aliacha kumbukumbu kubwa sana. Aliacha maandiko ambayo yamepata umamlaka mkubwa sana. Kazi zake zinawaacha watu wengi kwenye mshagao wa kustaajabia hasa pale tunapokumbuka kuwa kazi zote alizoziandika ambazo ni kubwa ajabu alizifanya kwa kipindi cha miaka ishirini. Baadhi ya kazi zake muhimu zilikuwa ni uhakiki wa kazi nyingi za Aristole, ujenzi wa hoja zenye umakini mkubwa dhidi ya makosa ya falsafa ya kigiriki na Averroes, kazi za awali zenye upevu mkali wa kiakili zilizohusu kiini kiarifu (essence) na uwepo au uishi (existence), tasnifu (makala=treatise) kuhusu mada ya siasa na utawala kwa watawala (political rulers) na kazi nyingine nyingi za thamani ya hali ya juu. Hata hivyo kuna kazi kubwa mbili ambazo zinamfanya Thomas Aquino aonekane mtu wa pekee katika ulimwengu wa kisomi na kitaaluma nazo ni “Summa Contra Gentiles” na “Summa Theologica” (Ukr 116-117)

Sura hii inaongelea pia Chuo Kikuu cha Paris.Chuo hiki kiliibuka kutokana na zile shule zilizokuwa zinaitwa shule za kanisa. Chuo kikuu cha Paris kiliibuka kutoka shule ya kanisa katoliki ya Notre Dame.Sheria na taratibu za uendeshaji wa chuo kikuu hiki cha Paris ziliidhinishwa na mwakilishi wa Papa mwaka 1225.

Kwa vile Thomas Aquino, aliingiza Ukristu katika Falsafa, sura hii inaongelea Falsafa na Teolojia, Falsafa na Fikara mantiki, Uthibitisho wa uwepo wa Mungu, Maarifa ya Maumbile ya Mungu, Uumbaji, Uovu kama ukosefu wa kile kilichotakiwa kuwepo, Maadili na sheria za maumbile, uhusiano wa sheria za maumbile na ujumla wa dhana ya sheria na serikali kadri ya Aquino na mwisho ni maoni ya upinzani dhidi ya Aquino.Hapa tunaagalia Nadharia ya uhiari, umaneno tu na uaimanisho.

Sura ya Sita, Dacta Mihanjo, anajadili kipindi kipya cha usasa: Falsafa na Uibukaji wa Ulimwengu wa Sayansi. Kipindi hiki kinajulikana kama uvuvumko (Renaissance). Wanafalsafa wanaojadiliwa katika kipindi hiki ni Erasmus, Luther, Machiavelli (1469-1527), Michel de Montaigne (1533-1592). Hapa yanachomoza mawazo ya Luther, kuhusu Serikali na utawala, pia karama ya Kiongozi Kulingana na Machiavelli.

“ Roho ya falsafa ya enzi ya kati, ilikuwa tofauti na hii ya awali kuhusu uwanja wa falsafa katika maana kuwa, pointi yake ya kuanzia ilikuwa tayari imeshapangwa na nadharia ya teolojia ya kikristo. Na cha zaidi, mandhari ya utamaduni wote wa kifikara yalikuwa yameathiriwa na nguvu za kimamlaka za kifikara za kikanisa (katoliki) kiasi kwamba nadharia za kimaadili, kisiasa, taasisi za kijamii kama vile famili na kazi, sanaa na fasihi, na sehemu kubwa ya sayansi, vyote vilikuwa vina chapa ya teolojia.” (Uk wa 162).

Sura ya Saba na ya mwisho inajadili maendeleo ya Falsafa katika Kipindi cha Sayansi. Hapa tunakutana na wanafalsafa Mawakili wa Mbinu za Kisayansi, nao ni Bacon na Hobbes. Francis Bacon, anafafanua mbinu kama Ufunguo wa Maarifa. Dacta Mihanjo, anaelezea maisha na kazi za wanafalsa hawa wa kipindi cha sayansi. Anaeleza jinsi utaratibu wa uchunguzaji na udhanifu wa kimahesabu ulikuja kuwa kama ndio hali bainifu yasayansi ya usasa. Kwamba huu muundo mpya wa mawazo ya kisayansi uliathiri kwa kiasi kikubwa fikara za kifalsafa kwa namna kuu mbili, kwanza udhanifu kuwa mfanyiko tendani msingi wa maumbile ni wa kuonekana au ni wa kutazamika kwa mahisio na kwa maelezo ya kihesabu. Anaendelea kuelezea kwamba Matokeo ya pili ya fikara za kisayansi kwa falsafa ilikuwa ni ukadirio mpya wa mahali pa binadamu katika dunia. Wanafrikara wa enzi za kati walifikiri kuwa walikuwa wamemweka binadamu kwenye kilele cha uumbaji wakimweka duniani kama mahali pake, mahali ambapo palikuwa ni katikati ya ulimwengu. Mawazo hayo yalivunjwa vunjwa katika kipindi cha uvuvumko.

“Katika sura zilizotangulia tumeona kuwa, Augustino na Aquino wanaeleza kuwa ili matendo ya binadamu yawe huru ni lazima yaibuke kutoka kwenye utashi huru.Kinyume na mwono huo wa Augustino pamoja na Aquino ambao wote walijenga miono hiyo kutoka falsafa za Plato na Aristole, wanafalsafa wa sayansi ya usasa wanayaona matendo ya binadamu kama ni matokeo ya msukumo wa kimakanika wa vitu, ambapo binadamu hana la kufanya isipokuwa kukubali ulazima tabia yake kulanda na msukumo wa vitu kama unavyotokea katika hali inayotokea…..Kwa msingi huo, utashi wa kuchagua ndio unaopaswa kuthibiti tabia ya matukio na siyo matukio kuthibi tabia ya binadamu….Kama huo ndio ukweli wenyewe, inakuwa vigumu kuyaelezea mahangaiko yetu ya maisha ya kutafuta maisha bora siku hadi siku” (Uk wa 183-184).

V. Thathmini ya Kitabu.

Baada ya kuona muhtasari wa kitabu, sasa tufanye tathmini ya kazi hii aliyoifanya Dk.Mihanjo. Awali ya yote lazima niseme kwamba, kwa kuangalia hadhira anayoikusudia, kitabu hiki kinasisimua sana na uchochea mapenzi ya Falsafa. Kinatoa mwanga na matumaini ya matumizi ya lugha yetu ya kiswahili. Kama ilivyosemwa kwenye utangulizi, kitabu hiki kinafunua ukweli wa kihistoria wa kukua kwa mawazo ulaya ukionyesha kuwa, ni pale tu ambapo falsafa iliandikwa kwa lugha enyeji au lugha za watu husika ndipo mapinduzi makubwa ya kifikara na ya kijamii yalianza kuchukua kasi ya ajabu.Locke na Hume waliandika kwa kiingereza, Voltaire na Rousseau kwa kifaransa na Kanti kwa Kijerumani.

Pili, Hiki ni kitabu cha pili cha Dacta Mihanjo, kuandikwa kwa kiswahili juu ya falsafa. Pongezi nyingi zimwendee Dk.Mihanjo, kwa kufungua uwanja wa falsafa katika lugha ya kiswahili. Kwa vile hadi leo hii ameandika vitabu viwili vya falsafa kwa lugha ya kiswahili amefanya mchango mkubwa ambao unaungana na jitahda nyingine za TUKI, BAKITA na wataalamu wengine wa kiswahili ndani na nje ya Tanzania, kukikuza na kukiendeleza kiswahili ili kiweze kubeba mawazo ya dunia ya leo ya utandawazi.

Tatu, Dk.Mihanjo, amejitofautisha na wasomi wengi wataifa letu, ambao wengi wao wanasoma kwa kukariri tu bila kuwa na aina fulani ya ubunifu, shahada zao zinabaki kuwa za majigambo. Kuyaweka mawazo ya falsafa na hasa falsafa ya kigiriki iliyopitia lugha za kigeni kwenye lugha ya kiswahili ni kazi kubwa na yenye kuhitaji ubunifu wa hali ya juu. Wasomi wetu wangeiga mfano wa Dacta Mihanjo,taifa letu lingepiga hatua kubwa kuelekea maendeleo.

Nne, Mwandishi amefanikiwa kukifanya kitabu chake kiwe cha kuaminika kwa kunukuu mistari kutoka katika vitabu vya wanafalsfa mbali mbali na kutumia vitabu vya rejea. Mfano kutumia vitabu vya Plato, Aristotle, Boethius, Erasmus, Luther, Augustine, Thomas Aquino na wengine na kujitahidi kufanya tafsiri ya mawazo yao katika lugha kiswahili, kunaongeza uzito katika kitabu chake.


Tano, orodha ya maneno ya Kiingereza- Kiswahili,na Kiswahili –Kiingereza, aliyoiweka mwishoni mwa kitabu kama alivyofanya kwenye kitabu chake cha kwanza ni ishara kubwa ya uwezo wa mwandishi. Ameonyesha ubunifu katika kuunda baadhi ya maneno ya Kiswahili ambayo hayakuwepo katika lugha ya kawaida. Maneno haya ni mchango mkubwa, ni changamoto ya pekee kwa wasomi wa kitanzania kwamba kiswahili kinamudu Elimu zote!

VI. Hitimisho

Kwa kuhitimisha basi, ningependa kuwashauri watanzania kukisoma kitabu hiki, Falsafa na ufunuo wa Maarifa.Mimi binafsi nilijifunza falsafa mnamo mwaka wa 1975 na 1976, lakini nilipokisoma kitabu cha Dk.Mihanjo, kwa lugha ya kiswahili, nimepata mwanga mpya. Mambo mengi yameonekana kuwa mapya! Ni imani yangu kwamba na kwale waliosoma falsafa kwa kiingereza siku za nyuma, watafaidika sana na kupata mwanga mpya wakiisoma kwa lugha ya kiswahili. Kwa wale wanaoaanza kujifunza falsafa, vitabu vya Dacta Mihanjo, ni msaada mkubwa na kichocheo cha kumfanya mtu apende kuzama katika fikara.

Pia, ningependa kuendelea kupendekeza kama nilivyofanya katika kitabu cha kwanza kwamba kwa vile Dk, Mihanjo, amefungua uwanja, basi somo la falsafa liwe la lazima kwa shule za msingi, sekondari hadi vyuo vikuu. Ukweli ni kwamba, hakuna nchi yoyote duniani iliyoendelea bila ya watu wake kuzama katika fikara na kujifunza mambo mengi juu ya msingi wa falsafa.

Je, kutumia Kiswahili katika falsafa, kutaleta mabadiliko ya haraka katika hali ya kufikiri na kuchangia hatua kubwa ya maendenleo katika taifa letu? Jibu la swali hili tutalipata tukiingia uwanjani! Liwezekanalo leo lisingoje hadi kesho. Wakati ni huu, vitabu viwili vya falsafa katika kiswahili viko mbele yetu. Kazi ni yetu!
Na,
Padri Privatus Karugendo.

2 comments:

dickson kawovela said...

NAKUPONGEZA SANA PADRI KARUGENDO HASA KWA KUSISITZA WATU WASOME ZAIDI FALSAFA KWA LUGHA YA KISWAHILI HII ITAPANUA FIKRA MIONGONI MWA WANAJAMII WASOMI WA TANZANIA NA AFRIKA MASHARIKI KWA UJUMLA HONGERA SANA

LABORA PHARMACEUTICALS said...

Nawezaje kukipata kitabu hicho tafadhali?

Post a Comment