BURIANI BABA MTAKATIFU YOHANA PAULO WA PILI

MAKALA HII ILICHWAPWA KWENYE GAZETI LA RAI 2005

BURIANI BABA MTAKATIFU YOHANA PAULO WA PILI.

Kanisa katoliki limempoteza kiongozi wake. Huu ni msiba mkubwa wa dunia nzima. Tarehe ya kifo chake anaijua Roho Mtakatifu peke yake. Ingawa vyombo vya habari vilitangaza kifo chake mwishoni mwa mwezi wa tatu. Historia itakayoandikwa ni kwamba ameiaga dunia mwanzoni mwa mwezi wa nne tarehe mbili. Utata huu wa amekufa lini si wa msingi sasa hivi, utata huu una chimbuko lake katika historia ya kanisa wakati ambapo wahuni wangeweza kumteka nyara Baba Mtakatifu na kutangaza kifo chake, na kumteua Papa Mwingine wakati aliyemtangulia akiwa bado hai, ndio maana sheria ya kanisa inasisitiza awepo mtu rasmi anayetambuliwa na kanisa wa kukitangaza kifo cha papa, jambo la muhimu sasa hivi ni kwamba tumempoteza kiongozi wa kanisa katoliki, kipenzi cha watu, mchapakazi, kiongozi aliyeuthamini, kuulinda na kuutetea uhai.

Papa Yohana Paulo wa Pili, ni miongoni mwa mapapa wachache waliokikalia kiti cha mtakatifu Petro, kwa kipindi kirefu. Ameifunga miaka 25 kitu ambacho si cha kawaida katika kanisa katoliki na hasa kwa miaka ya hivi karibuni. Huyu ni Papa aliyevunja ukiritimba wa Waitaliano kuliongoza kanisa katoliki kwa zaidi ya miaka 450.Alikuwa Papa msomi na mwenye vipaji vingi, aliweza kuongea lugha mbalimbali kama Kiingereza, Kijerumani, Kifaransa, Kiitaliano, lugha yake ya Kipolish, alipoitembelea Tanzania, mwaka wa 1990, alijitahidi kuongoza ibada ya misa kwa lugha ya Kiswahili! Ni Papa wa kwanza kuitembelea dunia nzima akiwatia moyo wa imani ndugu zake Wakatoliki na kuchochea roho ya upendo amani, haki, kuvumiliana na kusameheana miongoni mwa watu wote wa dunia hii. Ni Papa aliyependwa na watu wote wa madhehebu mbali mbali na dini zote. Pia ni Papa aliyeishi kwa misukosuko na kuikabili kwa moyo wa kishujaa na kusamehe. Alipigwa risasi, akaponea chupuchupu, alifanyiwa upasuaji mkubwa kwenye tumbo lake ili kuondolewa risasi na alilazwa siku kadhaa hospitalini. Alitishiwa kuchomwa kwa kisu akaponyeshwa na msaidizi wake wa karibu. Alitishiwa kuuawa mara kwa mara na kuonywa asitembelee baadhi ya nchi, lakini yeye alilazimisha na kuendelea na ziara zake. Alikumbwa na maradhi ya mara kwa mara, lakini aliendelea na kazi zake kama kawadia. Hata alipoishiwa nguvu za kuweza kutembea, bado aliendelea na shughuli zake na ziara katika nchi mbali mbali. Ni papa kwanza kuingia msikitini na kwenye hekalu la Wayahudi. Itakumbukwa kwamba ni Papa aliyependa michezo kiasi cha kushuhudia mchezo wa mpira wa miguu. Hakuwa mtu wa kawaida. Ni Papa wa kwanza kuwatangaza watakatifu wengi, orodha ni ndefu! Hakuna shaka kwamba alikuwa mtu wa Mungu, aliyefanya kazi zake kwa uaminifu, upendo na kwa nguvu zake zote.

Amekuwa Papa, aliyefundisha, onya na kushauri waumini wake, mapadri, maaskofu na watu wote wa dunia hii. Amefundisha wakati unaofaa na wakati usiofaa. Hakuogopa kufundisha yale aliyokuwa akiyaamini wakati akijua kuna wapinzani wa mawazo yake. Bahati mbaya mafundisho yake mengi yalikuwa hayatekelezwi. Yalibaki tu kwenye maandishi – na wakati mwingine hayakuwafikia walengwa, hata hivyo historia itamtaja miongoni mwa watu waliotimiza wajibu wao, miongoni mwa walimu na manabii. Tarehe 11 march 2005, akiwa amelazwa kwenye hospitali ya Gemelli mjini Roma, alikutana na maaskofu wa Tanzania. Hotuba yake kwa maaskofu wetu ni miongoni mwa hotuba zake za mwisho na ni wasia wa kujivunia. Katika hotuba hii aliongelea mambo matatu muhimu:
- Kuzijali Familia,
- Kuwajali Mapadre,
- Ushirikiano wa kanisa na serikali katika kuyashughulikia maswala ya kijamii ya kupambana na umasikini na kuleta haki. Kanisa na serikali kushirikiana katika maswala ya elimu ili kuwawezesha masikini kusaidiana na kuwasaidia wengine. Kanisa Katoliki kuonyesha ushirikiano na dini nyingine hasa Waislamu na hasa kule Zanzibar. Kanisa Katoliki kuendelea kushirikiana na serikali kudumisha amani katika nchi za maziwa makuu na Afrika ya Mashariki, kuendeleza moyo wa kuwapokea wakimbizi na kuwahudumia.

Vipengele vyote vitatu vilikuwa na kitu kilichokuwa kikichomoza kama changamoto kwa maaskofu wa Tanzania. Utekelezaji wake ndio hakuna ajuaye. Kama nilivyosema hapo juu ni kwamba Baba Mtakatifu Yohana Paulo, amefundisha mengi na kutoa ushauri mwingi, lakini utekelezaji wake umebaki kuwa kitendawili.

Kitu kilichochomoza kwenye kipengele cha kuzijali familia, ni pale Baba Mtakatifu alipowashauri Maaskofu Wa Tanzania, kulijenga Kanisa kama Familia ya Mungu. Tujuavyo Familia ya Mungu, inakusanya kila mtu, wenye dhambi, wema, wenye vilema na kila yule asumbukaye. Familia ya Mungu, imejaa uvumilivu kusamehe na kuchukuliana. Kwa kanisa Katoliki la Tanzania, lisilokuwa na uvumilivu, lisilovumilia maoni tofauti na karama mbali mbali, lenye historia ya kuwatenga watu na kuwafukuza makanisani, ujumbe wa Baba Matakatifu, ulikuwa changamoto kubwa. Je, utafinyiwa kazi? Ni swali la kujiuliza wakati wa kipindi hiki cha maombolezo. Haina maana ya kulia na kusikitika kwa kumpoteza Baba Mtakatifu wakati tukiupiga mgongo wasia wake.

Kipengele cha kuwajali Mapadri. Baba Mtakatifu, aliwakumbusha Maaskofu wa Tanzania, kwamba Askofu ni Baba wa mapadri, ni ndugu(kaka) wa mapadri ni rafiki wa mapadri. Na kwamba kazi kubwa ya Maaskofu ni kuendelea kuchochea na kuamsha hamasa ndani ya mioyo ya mapadri wao ili wakazane na juhudi zao za kuutafuta ufalme wa Mungu. Baba Mtakatifu waliwakumbusha Maaskofu wa Tanzania, jukumu lao jingine la kuwatia moyo mapadri wao ili wadumishe vipaji vyao na si kuwakatisha tamaa, kuwanyanyasa na kuwatekeleza. Changamoto kubwa katika kipengele hiki ni jukumu la maaskofu la kuwatunza na kuwasaidia mapadri katika matatizo yao ya kimwili na kiroho. Je, hili litafanyiwa kazi? Ni swali la kujiuliza wakati wa kipindi hiki cha maombolezo. Haina maana ya kulia na kusikitika kumpoteza Baba Mtakatifu, wakati tukiupiga mgongo wasia wake. Padri Desderius Kashangaki, mzee wa miaka 94, aliyetelekezwa na Kanisa Katoliki la Bukoba na Rulenge, ataguswa na ujumbe huu wa Marehemu Baba Mtakatifu?

Hotuba ya Baba Mtakatifu kwa Maaskofu wa Tanzania, ni wasia tosha. Kama ukifanyiwa kazi, kanisa katoliki la Tanzania, litapiga hatua mpya katika milenia hii tuliyomo. Lakini kama nilivyotaja hapo juu ni kwamba maneno mazuri ya Baba Mtakatifu, yalikuwa yakipendeza wakati akiyasema. Akishayasema, yalikuwa yanabaki kwenye karatasi. Ni waumini wangapi wa Tanzania, wameisoma hotuba hii ninayoitaja kwenye makala hii?



Pamoja na jitihada zake zote za kueneza Amani, haki, Upendo, Wema na Huruma duniani kote ameliacha Kanisa katoliki jinsi alivyolikuta. Kitu pekee alichokifanyia mabadiliko yasiyokuwa ya kawaida ni baraza la makadinali. Amehakikisha amewachagua makadinali wengi wa nchi mbali mbali kiasi kwamba hakuna nchi mmoja itayathubutu tena kuhodhi kiti cha Mtakatifu Petro. Kwa kuwachagua makadinali ambao si Waitaliano, ameufyeka ukiritimba wa kumchagua Papa Mwitaliano, kila mara. Ikitokea akachagulia, atakuwa amechomoza kwa sifa zinazotosha bila kumtegemea Roho Mtakatifu mwenye upendeleo na ubaguzi. Hii pia ni sifa ya pekee ya Papa Yohana Paulo wa Pili.

Kama mapapa wote waliomtangulia, Baba Mtakatifu Yohana Paulo wa Pili, ameshindwa kuleta mabadiliko katika mambo muhimu yanayoliyumbisha kanisa hili: Useja wa kanisa katoliki, Uongozi wa kanisa katoliki, Upadre wa kanisa katoliki, Matumizi ya kondomu na swala zima la uzazi wa mpango, Utoaji mimba, Theolojia ya Ukombozi na Uteuzi wa Baba Mtakatifu.

Useja wa Kanisa Katoliki, ni mfumo unaohitaji mabadiliko makubwa. Katika kipindi cha utawala wa Baba Mtakatifu Yohana Paulo wa Pili, mapadre wengi wameacha wito huu na kuishi maisha ya ndoa. Hapa Tanzania, useja umechangia kuongeza idadi ya watoto wa mitaani, umevuruga ndoa za watu, umechangia kuendeleza unyanyasaji wa wanawake wanaolazimika kuwapenda na kuzaa na mapadri kwa kujificha na wakati mwingine kutelekezwa wao na watoto wao. Katika nchi zilioendelea kama Amerika, useja umesababisha madhara makubwa kwa mapadri na jamii nzima. Baadhi ya mapadri wameugua magonjwa ya akili, ulevi wa kupindukia na kujiingiza kwenye matendo yasiyofaa kama ushoga na kuwanajisi watoto wadogo wa kike na kiume. Matendo haya yamepunguza imani ya waumini na wengine kuamua kulikimbia kanisa katoliki.

Uongozi wa Kanisa Katoliki, nao pia unahitaji mabadiliko makubwa. Asilimia 99 ya waumini wote wa kanisa katoliki duniani inaongozwa na kikundi cha watu wasiozidi asilimia moja. Kikundi cha waseja. Maaskofu ambao ni wanaume na ni waseja wanachaguliwa kwa mtindo wa kizamani usiowashirikisha watu wengi. Ingawa amekuwa akisingiziwa Roho Mtakatifu, kuwapitisha maaskofu, kuna ushahidi unaoonyesha mchezo mchafu unaozunguka zoezi zima la kuwatafuta maaskofu hasa kwenye nchi za ulimwengu wa tatu.

Upadri wa kanisa katoliki pia unahitaji mabadiliko makubwa. Hadi leo hii hakuna wanawake wanaoruhusiwa kuwa mapadri. Milenia, hii inayozingatia haki na usawa wa jinsia zote, haiwezi kuendelea kuuvumilia mfumo huu wa kibaguzi wa kuwapendelea wanaume, peke yao kushika huduma za kanisa.

Swala la matumizi ya kondomu na uzazi wa mpango, ni la kujadiliwa na waumini wote. Mabadiliko yanayohitajika ni kwamba, swala hili ni la msingi kwa watu wa ndoa na familia. Waseja kuliingilia hili na kulitungia sheria ni kukiuka haki za binadamu. Wenye ndoa washirikishwe kulijadili. Ukimwi ni tishio kubwa kwa maisha ya wanadamu na hasa katika nchi zetu za Afrika. Tukizembea kizazi kitafutika! Tunasikia kwamba Baba Mtakatifu, aliutetea sana uhai. Kuutetea uhai ni kuulinda. Na kuulinda uhai katika janga hili la Ukimwi, ni kinga. Kondomu, ni aina ya kinga inayoaminika kwa asilimia kubwa. Hivyo yeyote anayetetea uhai, ni lazima kuhimiza matumizi ya Kondomu. Hili pia linahitaji mabadiliko makubwa.

Lakini kitu cha muhimu ambacho Baba Mtakatifu ameshindwa kufanyia mabadiliko ni jinsi ya kumteua baba Mtakatifu. Ingawa amejitahidi kuondoa ukiritimba wa Waitaliano, lakini kuendeleza mfumo unaoruhusu “Roho Mtakatifu wa Upendeleo”, “Roho Mtakatifu wa Ubaguzi” ni dosari kubwa. Makadinali ambao ndio wanapendelewa na Roho Mtakatifu kumchagua baba Mtakatifu, ni wanaume, wanaume wasiokuwa na ndoa wala familia, ni wazee na ni watu wanaoishi maisha bora ya kifahari. Uchaguzi huu unakuwa hauna uwakilishi wa kutosha. Hakuna uwakilishi wa vijana katika zoezi zima, hakuna uwakilishi wa wanawake na wenye familia. Hakuna uwakilishi wa wanyonge, wanaonyanyaswa na kupuuzwa.

Baba Mtakatifu, ni kiongozi wa watu wote, kiongozi wa matajiri na masikini, kiongozi wa wazee na vijana, kiongozi wa wanawake na wenye familia. Hivyo uchaguzi wake ni lazima uwe na ushawishi na uwakilishi wa makundi yote hayo niliyoyataja. Baba Mtakatifu, kiongozi wa zaidi ya Wakatoliki bilioni moja kote duniani, anachaguliwa na makadinali wasiozidi miatatu! Idadi kamili ni miamoja ishirini Uwiano wa wapi? Tanzania, tunawakilishwa na Kadinali Pengo. Kwa maisha yake anavyoishi pale Dar-es-Salaam, anayafahamu maisha ya walalahoi, wanyonge, wasiokuwa na sauti. Anafahamu maana ya njaa? Ukosefu wa huduma muhimu kama matibabu, maji, umeme na usafiri? Anafahamu matatizo yaliyo kwenye ndoa? Anayafahamu matatizo ya vijana? Anayajua matakwa ya wanawake wa Kitanzania? Anaweza kuwa mwakilishi wa kweli wa Mtanzania anayeishi kwa kumwamini Mwenyezi Mungu? Kama msaidizi wake, Askofu Kilaini, anaufananisha Ukimwi na magonjwa mengine kama kisukari, Kadinali, atakuwa katika hali ya kumwakilisha Mkatoliki wa Kitanzania kumchagua Baba Mtakatifu, atakayekuwa kiongozi wa sauti zisizosikika? Kiongozi wa watu wanaohitaji mwanga wa milenia mpya? Watu wanaotaka kuishi maisha ya heshima na thamani. Atachangia kumchagua Papa wa kutetea uhai, haki, wanyonge, masikini, usawa na utukufu wa ubinadamu?

Kwanini roho mtakatifu wa kumchagua Baba Mtakatifu, asipitie kwa vijana, wanawake na wenye familia? Kwanini roho huyu asipitie kwenye maisha ya watu wanyonge, wanaoonewa masikini na wanaopuuzwa?

Mbona Roho wa Bwana, alimpitisha “Mwana wa Mungu” katika tumbo la Mwanamke? Kwenye familia? Kwenye utoto na Mwana huyu akafa akiwa kijana wa miaka 33 tu? Mbona Mwana wa Mungu, alizaliwa katika umasikini unaonuka kwenye zizi la Ng’ombe? Mbona hakuzaliwa na Makuhani na matajiri wa enzi zile kwenye nyumba za kifahari?

Mbona Roho Mtakatifu wa kanisa la mwanzo alikuwa akiwashukia waumini wote na wala si kundi dogo la wateule?:
“ Siku ya Pentekoste ilipofika, waamini wote walikuwa wamekusanyika pamoja. Ghafula, sauti ikasikika kutoka angani; sauti iliyokuwa kama ya upepo mkali, ikaijaza ile nyumba yote walimokuwa wamekaa. Kisha, vikatokea vitu vilivyoonekana kama ndimi za moto, vikagawanyika na kutua juu ya kila mmoja wao. Wote wakajazwa na Roho Mtakatifu, wakaanza kusema lugha mbalimbali kadiri Roho alivyowawezesha” ( Matendo 2:1-4).

Buriani Baba Mtakatifu Yohana Paulo wa Pili. Tutakukumbuka kwa mengi na hasa kitendawili ulichotuachia cha mrithi wako. Ukimya wako juu ya mabadiliko muhimu hauwezi kulisaidia kanisa katoliki. Kasi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia, kasi ya mifumo ya demokrasia, majadiliano na ushirikishwaji, tunayoishuhudia haiwezi kumwachia mrithi wako kukwepa kushuhudia mpasuko mwingine katika kanisa katoliki kama ule wa Martin Luther! Mungu, akulaze pema peponi. Amina.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment