MAKALA HII ILICHAPWA KWENYE GAZETI LA HEKO LA MAREHEMU BEN MTOBWA (mungu amlaze mahali pema peponi) 2005.
ASKOFU TUTU ANA HAKI YA KUTOA MAONI.
Hivi majuzi Mheshimiwa Askofu Methodius Kilaini, wa Jimbo Kuu la Dar-es-Salaam, alimshambulia Askofu Tutu, kwa maoni yake kwamba Papa Benedict, hafai kuliongoza kanisa katoliki katika karne ya 21. Kilaini, anasema uzee wa Tutu na msimamo wake wa kuunga mkono ndoa za mashoga ndio vinamsukuma kumponda Papa mpya.
Tumkumbushe Kilaini, kwamba, labda ni bahati mbaya Papa Benedict wa 16, alijulikana sana kabla ya kuwa Papa. Dunia nzima iliufahamu msimamo wake wa kutopenda mabadiliko. Ndio maana watu wameanza kumshambulia mapema hivi. Pia, Askofu Kilaini, akumbuke kwamba, Askofu Tutu, ana uhuru wa kutoa maoni yake. Huu ni uhuru alionao kila mwanadamu, na jinsi Mungu, alivyotuumba kila mtu ana maoni yake na si lazima maoni yote kufanana. Askofu Tutu hapendi kufuata mkumbo. Hapendi kuunga mkono kwa vile watu wengine wanaunga mkono. Tunamfahamu Askofu Tutu kama mtu mwenye msimamo. Alipinga ubaguzi wa rangi bila kuteteleka. Ameongoza tume ya mapatano ya Afrika ya kusini bila kuteteleka. Heshima anayopewa dunia nzima ni kwa sababu ya msimamo wake usioyumba. Tunaamini yale aliyoyapitia Tutu, Kilaini hawezi kuyagusa hata kwa kidole chake!
Kinachomsukuma Tutu, si uzee. Ni kwamba Tutu si mnafiki. Anasema yale yaliyo moyoni mwake. Hasemi kumfurahisha mtu au kuogopa kupoteza nafasi yake kama walivyo maaskofu wa kanisa katoliki na Kilaini, akiwemo. Unafiki unakwamisha mambo mengi. Unarudisha maendeleo nyuma na kukwamisha kila fikra mpya, na wakati mwingine zinakuwa fikra zenye manufaa makubwa katika jamii. Maaskofu wengi wa kanisa katoliki, wanaficha misimamo yao na kukubali kila kitu kutoka Roma, kwa kuogopa kupoteza nafasi zao za uaskofu au kunyimwa misaada.
Dunia yote sasa hivi inaongelea usawa wa kijinsia. Watu wanahoji ni kwa nini wanawake wasipate upadri katika kanisa katoliki. Kama wanawake wanaweza kuwa madaktari, maprofesa, madreva, wabunge, mawaziri nk., watashindwa nini kusoma theolojia na kupanda daraja la ukasisi. Haya ni maswali ya watu wengi wa karne hii. Haya si ya Tutu, peke yake. Yameongelewa katika makanisa mengine, na wanawake wameparishwa na kupata upadri (uchungaji). Papa Benedict wa 16, aliyekuwa kiranja wa kulinda imani ya kanisa katoliki, hawezi kuruhusu kitu kama hicho kutokea, si kuruhusu tu, hata mjadala hauna nafasi. Hivyo Tutu ana haki kusema huyu si Papa wa karne hii. Karne hii ni ya majadiliano na ushirikishwaji, ni karne ya uwazi na ukweli!
Dunia nzima inajua kwamba Papa huyu ndiye aliyenyamazisha Theolojia ya ukombozi. Sasa hivi watu wanaohitaji ukombozi ni wengi. Masikini wamejaa ulimwengu wa tatu. Wanyonge wamejaa ulimwengu wa tatu. Lengo la Theolojia ya ukombozi ni kuwatetea masikini na wanaonewa, ni kuifanya imani ya Kikristu iwe na maana kwa watu wenye hali ya chini. Tunaambiwa katika Biblia, kwamba Kristu, alikuja kuwakomboa wanyonge. Yeye mwenyewe alizaliwa katika umasikini. Theolojia ya ukombozi inalenga watu hawa maskini na wanyonge wawe na matumaini na kumwangalia Kristu kama mkombozi wao. Kule Latin Amerika, ilikoanzia Theolojia hii kuna unyanyaswaji wa hali ya juu. Na mbaya zaidi ni kwamba hata kanisa linakuwa upande wa wanyanyasaji. Hivyo Mtu kama Askofu Tutu, kiongozi wa dini katika ulimwengu wa tatu, kiongozi aliyepigana na ubaguzi wa rangi na kusimama upande wa wanyonge, hawezi kumpenda mtu anayepinga theolojia ya Ukombozi. Ana haki kusema kwamba Papa Benedict wa 16 si wa kuliongoza kanisa katika karne hii tuliyomo.
Papa Benedict wa 16, mwenyewe amekiri kwamba hata kwenye Conclave, haja ya kutaka mabadiliko ilijitokeza kwa nguvu. Ingawa hatakubali mabadiliko, lakini anajua kwamba kuna haja ya mabadiliko. Siku za nyuma yeye mwenyewe alikuwa akidai mabadiliko. Alifundisha theolojia ya kimapinduzi. Wanafunzi wake ni miongoni mwa wanateolojia wanaodai mabadiliko katika kanisa katoliki. Labda aliyemteua kuwa Kadinali, alikuwa na lengo la kumziba mdomo. Na kweli baada ya kuchaguliwa kuwa Kadinali na kuhamishiwa Roma, kuwa kiranja wa kulinda mafundisho ya imani ya kanisa katoliki, alianza kuwanyamazisha wanafunzi wake na wanateolojia wenzake. Na hivi sasa amepanda ngazi na kuwa Kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki dunia, ndio atawafyeka wote wenye mwelekeo wa theolojia ya mabadiliko na ya ukombozi.
Afrika kusini ni kati ya nchi zilizoshambuliwa sana na UKIMWI. Kuwazuia watu wasitumie Kondomu, ni sawa na kuwatakia watu kifo. Papa Benedict wa 16, hawezi kuruhusu matumizi ya kondomu. Huyu hawezi kupatana na Tutu. Yeye anaangalia uhai wa watu na Papa Benedict wa 16 anaangalia kutunza imani. Tutu, anaangalia hali halisi ya sasa hivi, anaangalia jinsi UKIMWI unavyoenea kwa kasi ya kutisha. Kwake yeye ili mtu awe na imani ni lazima awe na uhai kwanza. Hivyo ana haki kusema kwamba Papa huyu si wa karne hii.
Ndoa za mashoga ni kitu kilicho kwenye jamii sasa hivi. Si kitu cha kupuuzia wala kukemea tu. Hiki si kitu cha watu wawili au watatu. Ni kitu cha mamilioni ya watu. Tena utafiti uliofanyika hivi karibuni na shirika la kujitegemea la Amerika, ni kwamba wale mashoga wanaojitangaza ni robo ya mashoga tulionao katika dunia hii. Hivyo tatizo ni kubwa zaidi ya tunavyojua. Inasemekana kwamba hata na wale wanaoupinga ushoga kwa nguvu zao zote, kumbe nao ni mashoga. Mungu, atakuwa na kazi kubwa wakati wa hukumu!
Dawa si kukemea na kulaani. Dawa si kutukana na kuwalaumu mashoga. Hii haisaidii. Dawa ni kutafiti na kutafuta chimbuko la kitu hiki na kutafuta namna ya kuwasaidia wale walio na tatizo hili kama kweli ni tatizo. Panahitajika namna Fulani ya kuongea na mashoga, kuwasikiliza na kuwasaidia kimawazo. Wengine wanakuwa wamekatishwa tamaa katika ndoa zao za kawaida. Wanagundua kwamba wenzi wao wa ndoa hawawapendi, bali wanakuwa wanataka mali, watoto na heshima ya kuolewa. Upendo wa kweli unakosekana. Kwa maana hiyo utakuta mashoga wengine hawakutani kimwili bali ni kuwa na mtu wa karibu wa kushiriki naye maisha. Yako mengi ambayo bila kuwakaribia mashoga hayataeleweka milele. Tutabaki kuwalaani, na wenyewe wataendelea na mambo yao.
Anachosema Askofu Kilaini, ni kweli. Ushoga si jambo la kawaida. Hakuna anayebisha kwa hili. Lakini ukweli ni kwamba jambo hili lipo. Kama lipo tufanye nini? Kuna baadhi ya nchi zimeanza kuzitambua ndoa za mashoga. Kwa vile siku hizi dunia ni kijiji kimoja, hili litasambaa kwa kasi na sisi litatufikia. Tufanye nini? Ni lazima watu wote wanaojali kufanya kazi kwa pamoja bila kulaumiana wala kutukanana ili kupambana na tatizo hili la mashoga.
Nimekuwa nikimsikia Askofu Kilaini kwenye Redio na luninga. Daima anachanganyikiwa anapojadili mambo ya kijamii na imani. Mfano juzi kwenye kipindi cha wiki hii cha BBC, alisema kwamba kwenye ndoa, akijitokeza mmojawapo ana virusi na mwingine hana, basi dawa ni kuacha tendo la ngono! Wenye ndoa wasitumie kondomu, bali waache tendo. Yeye mwenyewe anajua kwamba kitu hicho hakiwezekani. Yeye mwenyewe, Mungu anisamehe, anaweza? Ni wangapi wanaweza? Kwanini tutake kuwabebesha watu msalaba ambao sisi wenyewe hatuwezi kuubeba? Je kuwaambia wenye ndoa wasifanye tendo la ngono kwa vile mmoja wao ana virusi, si kuruhusu uasherati? Huyu mzima atawezaje kuvumilia bila kutimiza ukamilifu wa mwanadamu?
Kuhusu kuwaparisha wanawake, Askofu Kilaini, anasema kwamba Yesu, hakuwaweka mapadri wa kike. Je, ni wapi katika Agano jipya, panapoonyesha kwamba Yesu, aliwaweka mapadri wanaume? Anaweza kutaja mstari unaosema hivyo? Yesu, alikuwa na wafuasi, lakini hakuwa na mapadri kama tunavyowafahamu leo hii. Wafuasi hawa ni kila yule aliyepokea neno la Mungu na kulishika. Wafuasi hawa walikuwa wanaume na wanawake. Maria Magdalena, alikuwa karibu na Yesu, kuliko mfuasi mwingine yeyote yule. Ufufuko, ambo ndio msingi wa imani ya Kikristu, ulishuhudiwa na Maria Magdalena. Yesu, alijionyesha kwanza kwa mtu aliyemwamini kuwa na imani zaidi ya wengine. Kwani, kwa nini Yesu, akujitokeza kwa Petro, kwanza?
Luka, anatwambia kwamba wanawake ndo walimtunza Yesu na wafuasi wake. Wanawake, ndo walikuwa na pesa na nyumba. Wanaume walikuwa wavuvi, hawakuwa na kitu. Kama ni kulisimika na kuliongoza kanisa la kwanza, ni wanawake waliofanya kazi hiyo. Mtakatifu Paulo, anawataja wanawake hawa, anawaita watumishi, mitume na wafuasi.
Kawanza kuna hoja nzito kwamba Yesu, hakuanzisha kanisa. Alichofanya ni kuhubiri na kuwataka watu wamugeukie Mungu. Kanisa,kama kanisa tunavyoliona sasa hivi na sheria nyingi zilizolizunguka ni maendeleo ya baadaye. Hasa baada ya kanisa kukutana na falsafa ya Kigriki na kuingiliwa na watu wenye uchu wa madaraka kama Costantine. Ni wakati huu ambao hata na orodha ya mitume ilipunguzwa na kubakiza ya wanaume peke yao. Injili zinazotaja mchango wa wanawake katika kanisa zilifutiliwa mbali. Hata na zile jumuiya za mwanzo hazikuwa na mfumo tunaouona sasa hivi.Kanisa limepitia historia chafu hadi kufikia hapa tulipo.
Kama Askofu Kilaini, ni mkweli, basi aanzishe mijadala ya kina kuhusu maswala mbali mbali ya dini katika jamii yetu. Na hii iende sambamba na kuwaruhusu walei kujifunza Teolojia. Kila kitu kinachotajwa katika jamii, kinaweza kujadiliwa. Karne hii ya utandawazi na maendeleo ya teknolojia ni vigumu kuendeleza ile hali ya kuwaacha watu kwenye giza.
Mfano mzuri ni Mazishi ya Papa Yohana wa pili na kuchaguliwa na kusimikwa kwa Papa Benedict wa 16, kila kitu kilikuwa kwenye TV. Ni kinyume kabisa na mwaka 1978 wakati wa kifo cha Paulo wa sita, kuchaguliwa kwa Yohana Paulo wa kwanza, kifo chake na kuchaguliwa kwa Yohana Paulo wa pili. Dunia ya tatu ni wachache walioshuhudia matukio hayo. Sasa hivi watu wanaona mambo, wanahoji, wanauliza na wanataka kupata majibu. Mfano watu wanauliza, mbona Roma kumejaa wazungu watupu? Kanisa hili ni letu kweli? Mbona makadinali weusi ni wachache? Kama Roma ni makao makuu ya kanisa Katoliki, mbona weusi hatuwaoni huko? Hakuna weusi wanaofanya kazi Roma? Mbona hatukuona kaburi la Baba Mtakatifu? Anazikwa au anakaushwa na kuwekwa kanisani? Ni lazima Papa awe mzungu? Mbona hatoki Asia, Amerika au Afrika? Maswali hayo yote yanahitaji majibu. Huwezi kuyajibu kwa mkato kama anavyofanya Mheshimiwa sana Askofu Kilaini.
Hivyo Askofu Kilaini, asimlaumu Askofu Tutu.Ajue kwamba sasa hivi tunaishi kwenye ulimwengu ulio wazi zaidi. Changamoto zilizo mbele yetu zinahitaji majibu. Tukiendelea kuzifunika, zitafika mahali zilipuke.
Na,
Padri Privatus Karugendo
0 comments:
Post a Comment