SALA ZA KISIASA!

MAKALA HII ILICHAPISHWA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2005.

JE, NI VYAMA VYOTE VITAOMBEWA SALA NA VIONGOZI WA DINI ZA KIKRISTU?

Kuomba ni jambo jema na kila mja analazimika kuomba kwa muumba wake. Hata na majambazi wana sala yao wanayoiomba kabla ya kwenda kuvamia na kufanya mauaji. Wanajeshi wanaokwenda vitani wakijua vita ni kutoa uhai na kuharibu mali, wanaomba pia kwa muumba wao kabla ya kuanza vita. Machangudoa na Malaya wanaokwenda kinyume na maadili nao wana sala yao kabla ya kuanza kazi zao za kuuza miili yao na kawaida hawa ni kati ya watu wanaotoa sadaka kubwa kule makanisani!

Siku chache kabla ya mikutano ya chama cha mapinduzi ya kumtafuta mgombea wa urais, viongozi wa dini za Kikristu, walikutana Jangwani, Dar-es-Salaam kuiombea mikutano hiyo ya CCM. Sala hiyo ilikuwa na lengo la kuomba Mungu, awasaidie wanaCCM, kumchagua kiongozi bora, na si bora kwa CCM tu bali bora kwa Taifa zima la Tanzania. Kwa maneno mengine ilikuwa sala ya kuomba apatikane rais bora wa Tanzania, kutoka CCM!

Kusali na kuomba ni kitu cha kawaida. Tunachokihoji hapa si kusali wala kukiombea chama, tunachokihoji ni kule kukiombea chama kimoja wakati nchi yetu ina vyama vingi vya siasa. Tunachokihoji ni viongozi wa dini wenye dhamana ya kuwaongoza waumini wenye maoni tofauti, vyama tofauti, makabila tofauti, kuwalazimisha waumini wao kukipenda chama kimoja cha siasa. Tunachokihoji ni viongozi wa dini za Kikristu kutumia jukwaa la sala na kuligeuza jukwaa la siasa na kampeni! Tunachokihoji ni hii ndoa ya siasa na dini, na hasa dini moja, katika nchi yenye dini nyingi, kufunga ndoa na chama kimoja cha siasa, wakati nchi ina vyama vingi vya siasa. Hiki ndicho tunachokihoji. Huu ndio wasiwasi wetu mkubwa!

“Mnaposali, msifanye kama wanafiki. Wao hupenda kusimama na kusali katika masinagogi, na katika pembe za njia ili watu wawaone. Kweli nawambieni, hao wamekwisha pata tuzo lao. Lakini wewe unaposali, ingia chumbani mwako, na ukisha funga mlango, Sali kwa Baba yako asiyeonekana. Naye Baba yako aonaye yaliyofichika atakutuza. Mnaposali, msipayuke maneno kama watu wasiomjua Mungu. Wao hudhani kwamba Mungu atawasikiliza ati kwa sababu ya maneno mengi, Msiwe kama wao. Baba yenu anajua mnayoyahitaji hata kabla ya kumwomba” (Matayo 6:5-8).

Sala ya Jangwani, ilikuwa kinyume na maelekezo ya Bwana Yesu, kuhusu kusali na kuomba. Badala ya kusali makanisani kwao kwa maficho, viongozi hawa walikusanyana kwenye viwanja vya Jangwani! Ilikuwa sala ya maneno mengi na kupayuka sawa na sala ya watu wasiomjua Mungu. Je, Baba yetu aliye Mbinguni, hajui kwamba tunamhitaji Kiongozi bora? Awe wa CHADEMA, TLP, CUF au CCM?

Jambo la pili ni kwamba sala yenyewe ilivyoendeshwa ni kana kwamba viongozi hawa na waumini wao waliokusanyika kuomba walikuwa wakiomba Mungu, awapatie rais bora kutoka CCM! Hii ilijionyesha wazi kwenye maombi yaliyotolewa na kila Askofu kutoka madhehebu mbalimbali. Sala ya Askofu Kilaini, ilikuwa ya wazi kuliko za wengine. Alisali akielekeza moja kwa moja kwa CCM. Hata kama kwa uchambuzi wake, kwa vile yeye ni msomi na mtu mwenye akili nyingi, ameshatabiri ushindi wa CCM, si busara yeye kama kiongozi wa dini kuonyesha hilo wazi wazi. Nchi ambayo inaongozwa kwa demokrasia ya vyama vingi kiongozi wa nchi huchaguliwa kwa kura ya siri na wala si kwa sala na uchambuzi wa mtu binafsi!

Ingekuwa sala ya kuombea uchaguzi mkuu, au sala ya kuviombea vyama vyote vichague wagombea bora, hakuna ambaye angehoji. Sasa ni lazima tuhoji. Hizi dalili za dini moja kuunga mkono chama kimoja cha siasa ni hatari sana. Ni ugonjwa unaohitaji dawa ya haraka, vinginevyo utalitafuna taifa letu kama mdudu asiyeonekana! Sala za namna hii ni lazima zilaaniwe na kila Mtanzania anayelitakia mema taifa letu!

Rwanda, kabla ya vita vya maangamizi vya 1994, maaskofu wa Kanisa katoliki, walikuwa wakiunga mkono chama tawala. Wengine walikuwa kwenye Kamati kuu na halmashauri kuu ya chama hicho. Matokeo yake sote tunayajua. Maaskofu wanne, waliuawa na jeshi la RPF. Mapadre na watawa walishiriki katika mauaji. Kwa vile chama tawala walichokuwa wakikiunga mkono kilikuwa hatarini kuondoka madarakani, ilibidi wakitetee kwa nguvu zote.

Ukishaunga mkono kitu wazi wazi, na hasa chama cha kisiasa, inakuwa vigumu kuweka mipaka. Inakuwa vigumu kujipangia ushiriki hadi wapi. Unakuwa mkereketwa, mfurukutwa na ngangali. Mtu akikigusa chama hicho anakuwa amekugusa na wewe. Mtu akikipinga chama hicho anakuwa amekupinga na wewe.

CUF, walifanya uchaguzi wao. Hatukusikia viongozi wa dini za Kikristu wakikusanya waumini kuombea uchaguzi wa CUF. Je, viongozi hawa wataitisha sala kuombea uchaguzi wa CHADEMA, NCCR-Mageuzi, UDP na vyama vingine? Ili hii iwe jadi yetu kwamba vyama vya siasa vinapowachagua viongozi wa kuwania kiti cha urais, sala za waumini mbali mbali zinafanyika kwenye majukwaa ya wazi kama lile la Jangwani?

Tujuavyo, si waumini wote wa dini za Kikristu ni wapenzi wa CCM. Baadhi wanaipenda CCM, na baadhi wanavipenda vyama vingine. Kitendo cha viongozi wao kuonyesha wazi wazi kwamba wanakipenda chama Fulani – yaani chama cha CCM, ni kuleta mgawanyiko katika dini zao. Mgawanyiko huu hauwezi kuishia kwenye dini zao tu, ni lazima usambae nchi nzima. Hakuna machafuko mabaya kama ya kidini. Mara nyingi kwenye machafuko ya kidini watu hawatumii akili zao bali huongozwa na imani. Hii ni hatari zaidi. Mtu akianza kutetea hoja zake kwa kutumia imani ya dini, anakuwa kipofu. Anakuwa hana tena uwezo wa kutambua ukweli na uongo. Anaweza kubeba bomu la kujimaliza yeye na maadui zake. Tunayasikia haya yakitokea katika nchi mbali mbali. Si kwamba yalianza ghafla, yalianza pole pole kama yanavyoanza hapa kwetu kwa hizi sala zisizokuwa na mpangilio wala vision ya mbali.

Tunajua jinsi serikali ya CCM, inavyoyasaidia mashirika ya kidini. Tunajua misamaha ya ushuru inayotolewa kwa mashirika ya dini, Tunajua jinsi serikali ya CCM, inavyotoa uhuru mwingi kwa viongozi wa dini. Wanapata heshima kama VIP, na kupendelewa kwa mambo mengi. Lakini kwa vile wao ni viongozi wa watu wote wa Tanzania, si busara kuonyesha mapenzi yao wazi kwa chama kimoja. Ni nani amewaambia kwamba CUF, ikiingia madarakani, au CHADEMA, TLP, NCCR-Mageuzi na vingine, upendeleo wanaoupata kutoka serikalini utasitishwa?

Ni bora viongozi hawa wafanye kazi yao. Wafundishe neno la Mungu. Wachochee maadili bora katika jamii. Mambo ya siasa wawachie wanasiasa. Muumini ambaye amefundishwa maadili mema ni lazima atakuwa mwanasiasa bora. Kwa vile hatuna wanasiasa bora, maana yake ni kwamba viongozi wetu wa dini hawajafanya kazi yao vizuri.

Tunawaomba sana viongozi wetu wa dini za Kikristu, swala la siasa, wasilifanye ni agenda ya kidini. Kama wanakipenda chama cha mapinduzi, wakipende moyoni mwao, wasianzishe ushawishi wa wazi unaoweza kuzua balaa kubwa katika taifa letu.

Na
Padri Privatus Karugendo.

SASA NURU YA CCM INAANGAZA!

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2005

SASA NURU YA CCM INAANGAZA!

Rejea makala yangu iliyopita yenye kichwa cha habari: “ Kama nimesema uongo, nuru ya CCM, na iangaze”. Kwenye makala hiyo nilitoa nukuu ya Bwana Yesu, ambayo ningeomba niirudie kwa vile bado hatujafika mwisho wa safari:

“Ninyi ni kama chumvi ya dunia. Lakini chumvi ikipoteza ladha yake, itakolezwa na kitu gani? Haifai kitu tena, ila hutupwa nje na kukanyagwa na watu. Ninyi ni mwanga wa ulimwengu! Mji uliojengwa juu ya mlima hauwezi kufichika. Wala watu hawawashi taa na kuifunika kwa chungu, ila huiweka juu ya kinara ili iwaangazie wote aliomo nyumbani. Vyivyo hivyo, ni lazima mwanga wenu uangaze mbele ya watu, ili wayaone matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni” ( Matayo 5:14-16).

Niliandika makala hiyo kabla ya CCM kufanya uchaguzi wa mgombea wao wa urais kupitia chama hicho. Uchaguzi umefanyika! Wasi wasi wa watu kwamba Chama kitasambaratika, kwamba wanachama ambao kipenzi chao hatapitishwa watakimbia na kujiunga na vyama vingine, kwamba CCM itafanya makosa wakati kumchagua mgombea wake, kwa sasa utabiri wa Baba Taifa, kwamba upinzani wa kweli utatokea CCM, unaelekea kutimia, haikutokea! Kwa mshangao ya wengi mambo yamekwenda shwari. Hata hivyo watu wenye busara na hekima, watu wenye uchungu na taifa letu walitegemea yatokee yale yaliyotokea Chimwanga.

Ingawa mzee wa Dodoma, mwenye umri wa miaka 100, ambaye kama sikosei ni kati ya waasisi wa Chama cha CCM, hakufurahishwa na hotuba ya Rais Mkapa, pale iliposisitiza umuhimu wa vijana. Mzee huyu alikuwa na maoni kwamba ni lazima wazee watangulizwe. Hata hivyo wazee wanatangulizwa, maana bila ushauri wa wazee kama vile Mzee Kawawa, Mzee Mwinyi, Mzee Ngobale na Mzee Malecela, yaliyotokea Chimwanga, yasingetokea kamwe!

Kumbe chumvi bado ni chumvi na mwanga haujafifia, taa imetundikwa juu ya mlima wa Kilimanjaro! Chumvi na mwanga, ni Hekima, Busara na fikra pevu! Kamati kuu ya CCM, halmashauri kuu ya CCM na Mkutano mkuu wa CCM, wametuonyesha kwamba wao bado ni chumvi na hakuna haja ya kuwatupa barabarani ili wakanyagwe na wapita njia!

Hivyo basi ushauri wa kila anayelitakia mema Taifa letu ni kwamba hekima, busara na fikra petu, visiishie kwa uchaguzi wa Jakaya Kikwete. Safari bado ni ndefu sana. Bado kuna uchaguzi mkuu utakaoshirikisha vyama vyote vya siasa. Kuna wagombea wengine wa urais kupitia vyama vingine. Kuna uchaguzi wa wabunge na madiwani. Rushwa isitumike, vitisho visitumike, dola isitumike kukipendelea chama tawala. Chema chajiuza na kibaya chajitembeza. Kama CCM bado ni chumvi na ni mwanga watu wataichagua bila kutumia polisi na kumwaga damu.

Ina maana gani kutumia pesa kununua kura, kutumia vitisho na ubabe na baadaye kujigamba kwamba ni ushindi wa kimbunga? Ushindi wa kweli ni kushinda kwa mvuto, ni kushinda kwa kukubalika, ni kushinda kwa kuwa na sera inayotekelezeka, ni kushinda kwa kuwa na vision, ni kushinda kwa kutaka kutumikia na wala si kutumikiwa!

Hekima, busara na fikra pevu, iliyojionyesha Chimwaga, ijionyeshe kule Zanzibar. Ni upumbavu kuamini kwamba kule Zanzibar, hali ni shwari. Mvuto uonekane kule Zanzibar, kukubalika kuonekane kule Zanzibar, sera, vision na utumishi vionekane kule zanzibar.

Inawezekana Mheshimiwa Mkapa, ana mpango wake mzuri kuhusu Zanzibar, ambao ni siri yake, maana hata uchaguzi wa mgombea wa kiti cha urais kupitia CCM, ilikuwa ni siri kubwa aliyoitunza moyoni mwake. Kama ni hivyo, hicho ndio tunachokiomba. Tunaomba amani, utulivu na haki kule Zanzibar. Hakuna mtu anayetaka kuona vurugu na umwagaji wa damu.

Kabla ya uchaguzi wa Kikwete, yalisemwa mengi juu ya Rais Mkapa. Kuna waliosema kwamba Mkapa, alikuwa na mtu wake ambaye si Kikwete. Wakati wanachama wa CCM wanaendelea kujitokeza kuchukua fomu za kugombea, namba ilipofikia kumi, kuna waliosema kwamba chaguo la Mkapa, alikuwa hajachukua Fomu. Siku za kuchukua fomu zilipokwisha. Wakasema chaguo la Mkapa ni Mheshimiwa Sumaye. Wengine wakasema chaguo lake ni Balozi Dk Salim. Kuna waliovumisha kwamba chaguo lake ni Balozi Chokala. Wengine wakasema ni Mheshimiwa Kigoda na wengine wakasema chaguo lake ni Profesa Mwandosya. Hatukusikia kwamba chaguo la Mkapa ni Kikwete! Kumbe yeye alikuwa na lake moyoni!

Hotuba ya Mheshimiwa Rais Mkapa, wakati wa kufungua mkutano mkuu iliyokuwa imejaa busara, hekima na fikra pevu ilikuwa inamlenga Kikwete!

Rais Mkapa, alisisitiza achaguliwe Kijana. Tukifuata umri wa wagombea, aliyekuwa kijana ni Kikwete. Ingawa hapa Tanzania mtu mwenye umri wa miaka 55 huwezi kumwita kijana maana wastani wa kuishi kwa Mtanzania ni miaka 45! Lakini walivyokuwa Kikwete, ndio alikuwa kijana.

Rais Mkapa, alisisitiza achaguliwe mtu anayekubalika visiwani na Bara. Kutokana na kura za maoni, ambazo ni hakika Rais Mkapa, hakuweza kuzipuuzia, mtu aliyonyesha kukubalika ni Kikwete.
Rais Mkapa, alishauri achaguliwe mtu anayekifahamu chama cha CCM na aliyekulia kwenye chama hicho. Aliyekuwa na sifa hizo si mwingine bali Kikwete!

Ukiichambua hotuba yake yote ni kama yalikuwa maelekezo kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM, kumchagua Kikwete. Hakuna shaka kwamba Mheshimiwa Mkapa, aliitoa hotuba hiyo bila shinikizo la mtu au kikundi cha watu. Ni hotuba aliyoitoa kwa uhuru wake akiwa anasukumwa na hekima, busara na fikra petu, lakini hasa kwa kutanguliza uhai wa chama chake cha CCM na uhai wa Taifa letu la Tanzania.

Ili nuru ya CCM iangaze, ili CCM iendelee kuwa chumvi ya Taifa letu la Tanzania, hekima, busara na fikra pevu iliyomwongoza Rais Mkapa, kule Chimwaga, iendelee kumwongoza kipindi chote cha uchaguzi mkuu. Watanzania tupige kura zetu kwa haki na amani. Vyama vyote vya siasa vipate haki sawa. Wagombea wa CCM na wa vyama vingine vya siasa wapendekezwe na kuchaguliwa kufuatana na sifa zao, si kwa kupendelea au kutumia pesa. Madiwani na wabunge na wagombea wa urais wa vyama vyote wawe na sifa zinazofananafanana na za Mheshimiwa Kikwete. Wawe vijana, watu wanaokubalika, watu wanaovifahamu vyama vyao na wazalendo wa kweli.
Chimwaga ni mfano wa pili unaoonyesha kwamba busara na hekima imeanza kulitawala taifa letu. Mfano wa kwanza ni jitihada za busara zilizotumika kuvishawishi vyama vya upinzani kusitisha maandamano wakati wa mkutano wa amani ya maziwa makuu uliofanyika mjini Dar-es-Salaam. Mifano hii miwili inatofautiana na jinsi tulivyokuwa tumezoea kule nyuma wakati ubabe, na nguvu za dola vilikuwa vikitumika bila busara na hekima na wakati mwingine bila hata sababu za msingi.

Kama anavyosema Mheshimiwa Kikwete, sasa hivi ni wakati wa kuanza na ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya. Sote tulenge kuijenga Tanzania yenye maendeleo ,haki, amani na utulivu. Nuru ya Tanzania iendelee kuangaza!

Na,
Padri Privatus Karugendo.

HEKIMA NA UCHAGUZI

MAKALA HII ILICHAPISHWA KATIKA GAZETI LA RAI 2005.

HEKIMA HII ITAENDELEA HADI UCHAGUZI MKUU?

Hapana shaka kwamba vikao vya CCM vilivyomalizika tarehe 4.5.2005, kule Dodoma viliongozwa na hekima, busara na fikra pevu. Watu wengi walitegemea CCM, isambaratike! Hili halikutokea! Wengine walitegemea fujo kwenye vikao hivyo, hata na wanaCCM wenyewe walikuwa na wasiwasi huo hadi Mheshimiwa Mapuri, akatangaza kwenye vyombo vya habari kwamba wamejizatiti ndani ya chama na kwa kutumia vyombo vya dola kukabiliana na fujo zitakazojitokeza. Fujo hizo hazikujitokeza! Hadi leo hii ninapoandika makala hii, fujo hizo hazijajitokeza popote. Tunachokisikia ni sherehe na maandamano ya kumpongeza Kikwete, mgombea mwenza na Rais Karume.

Habari kutoka Mwanza, zilizotolewa na gazeti dada la Mtanzania zinasema: “Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa wamewasili Mwanza na kupata mapokezi ya kihistoria kutokana na kuchaguliwa kwa Jakaya Kikwete kuwania nafasi ya urais kupitia chama hicho….. Baada ya kupokewa, wajumbe hao walivishwa mashada ya maua kama ishara ya ushujaa kutokana na uamuzi wao wa kumpigia kura Kikwete ambayo inaaminika kwamba huo ulikuwa ndiyo msimamo wa wakazi wa Kanda ya Ziwa….Baadhi ya watu walisikika wakisema kwa kupaaza sauti kwamba ole wao kama wajumbe hao wangeliwasaliti kwa kuwaletea mgombea asiyekuwa chaguo lao”(Mtanzania, Jumamosi, Mei 7,2005).

Msimamo wa Rais Mkapa, haukujulikana kabla ya hotuba yake ya kuufungua mkutano mkuu. Hakuonyesha kuwa na upande wowote. Ni imani yangu na imani ya watu wengi kwamba hotuba aliyoitoa Rais Mkapa, wakati wa kufungua mkutano mkuu, aliitoa kwa uhuru bila ya shinikizo lolote lile kutoka kwenye kundi la watu na kwenye nafsi ya moyo wake. Chaguo la mtu aliyemtaka alilitunza moyoni mwake. Mtu msiri sana huyu! Ilikuwa siri kubwa ambayo watu wengi hawakuifahamu. Wasi wasi ulitanda ndani na nje ya chama cha CCM, kwamba rais, akimuunga mkono mtu asiyekubalika, basi chama kingemeguka. Wengine wakaanza kusema kwamba utabiri wa Mwalimu Nyerere, kwamba upinzani wa kweli utatoka CCM, ulikuwa unaelekea kutimia. Usiri wa Rais Mkapa juu ya mgombea anayemtaka ulisaidia sana. Hizi ni kati ya sifa anazojizolea anapoelekea mwishoni mwa utawala wake. Hekima, busara na fikra pevu alizozionyesha kwa kumtumza moyoni mwake mtu anayependa arithi kiti chake kwa tiketi ya CCM, bila kukigawa chama ,zichipuke na kukua hadi uchaguzi mkuu.

Hatukusikia fujo kwenye kikao cha Kamati Kuu ya CCM kule Dodoma, mbali na uvumi kwamba Mzee Malecela, alihoji hapa na pale kuhusu jina lake kutupwa au kuombwa aendelee kuwa tingatinga! Labda hii ni siri za chama! Lakini kwa vile kamati kuu iliweza kuwateua watu watano kati ya kumi na mmoja waliokuwa wameomba kugombea kiti cha urais na kuwapendekeza kwenye mkutano wa Halmashauri kuu bila kelele zozote, tunalazimika kuamini kwamba mambo yalikuwa shwari kwenye kamati kuu. Halmashauri kuu iliwachagua watatu kati ya watano kwa kura tulizotangaziwa. Hatukuzikia malalamiko yoyote. Mkutano mkuu ulirushwa kwenye luninga. Tulijionea wenyewe jinsi utulivu, demokrasia, hekima, busara na fikra pevu vilivyoutawala ukumbi wa Chimwaga.

Hali ya Chimwaga, iliwachagaza wageni kutoka nje ya Tanzania. Mfano Katibu mkuu wa chama kinachotawala kule DRC, alishangaa sana kuona kiongozi aliyemadarakani, Rais Mkapa, anaendelea “kuwachunga” (Kuwatunza) viongozi waliomtangulia. Alishangaa kuuona Mzee Mwinyi, bado anapewa nafasi na heshima kwenye chama na bado “anachungwa” vizuri na Rais Mkapa. Dr. Salimin, naye bado anapewa heshima na “kuchungwa” vizuri na Rais Mkapa. Hata Mama Maria Nyerere, naye “anachungwa” vizuri. Ili aweze kuelezea vizuri ukomavu wa kisiasa wa Tanzania, kule kwao DRC, Katibu huyo kutoka DRC, aliomba ruhusa ya Rais Mkapa, ili “akamate picha” (kupiga picha) na Mama Maria Nyerere, awaonyeshe kule kwao kwamba hata na Mke wa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, bado anapata heshima ndani ya chama cha CCM na kwenye taifa zima.

CCM, imeonyesha ukomavu wa kisiasa na demokrasia ya juu si hapa tu bali hadi nchi jirani na za mbali. Pamoja na pongezi hizi zote, wasi wasi ni je, hekima, busara, demokrasia na fikra pevu vilivyojitokeza kule Dodoma, vitaendelea hadi uchaguzi mkuu? Tutegemee kuwa na uchaguzi wa haki, huru na amani? Uchaguzi usiokuwa na vitisho, rushwa, upendeleo, ukabila na udini? Uchaguzi usiokuwa na udanganyifu – kura zipigwe, zihesabiwe bila kupinda? Kwa vile CCM, ndicho Chama tawala, ndicho chama chenye dola na ndicho kinachosimamia uchaguzi mkuu, kitatuvusha salama kwa kuzingatia ukomavu wa kisiasa uliojionyesha Chimwaga na kushuhudiwa na dunia nzima? Majigambo haya ya kushinda kwa kimbunga na tufani la tsunami yana busara na hekima ndani yake?

Majigambo haya yakitamkwa na watu wenye uelewa mkubwa na waliokomaa kisiasa, wazalendo na wenye vision, hayana shida. Lakini yakidondoka mikononi, masikioni na akilini mwa washabiki na wapiga debe wa CCM, bila ya kuchujwa itakuwa tsunami ya kweli ndani na nje ya chama!

Tunaweza kulijadili hili kwa pande zote mbili. Ndani ya chama cha mapinduzi na nje ya chama hicho. Tukianzia ndani ya chama: Hotuba ya Mheshimiwa Rais Mkapa, yenye hekima na busara, wakati wa kufungua mkutano mkuu, iliweka bayana kauli mbiu: Ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya! Hakusita kusema wazi kwamba asilimia kubwa ya wapiga kura ni vijana. Hivyo, ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya ni lazima isukumwe na vijana! Hotuba hii ilimaliza kimya na usiri wa Rais Mkapa, juu ya mtu amtakaye kuichukua nafasi yake ndani ya chama cha mapinduzi.

Je, kigezo hiki cha vijana kitachukua mkondo wake hata kwa kuwasimamisha wabunge na madiwani? Wabunge wakongwe kama Mheshimiwa Sr George Kahama, watakubali kuwa tingatinga kama alivyokubali kufanya Mheshimiwa Mzee Malecela? Watakubali kukaa pembeni na kuwashauri vijana wa CCM?

Je, upepo huu wa vijana kushika hatamu utakiacha salama chama cha mapinduzi? Je vijana na wazee watashirikiana kumsaidia Kikwete na kuisaidia Tanzania? Au sasa ndio siri zote za CCM zitafumuka, kashfa za uongo na za kweli kusambaa kwenye magazeti na kuwa silaha kubwa ya vyama vingine vya siasa kwa lengo si kuimaliza CCM, bali kuwakwamisha vijana na kuleta vurugu katika taifa zima!

Mzee wa Dodoma, mwenye umri wa miaka 100, ambaye ni kati ya waasisi wa CCM, hakuipenda hotuba yote ya Rais Mkapa, ya kufungua Mkutano mkuu. Alipohojiwa na TVT, mzee huyu alisema Rais, alikosea kuwatanguliza vijana. Ni imani yangu na wale wote wanaojali kwamba mzee huyu alikuwa anaongea kutoka moyoni na bila unafiki wowote. Alisema ni lazima wazee watangulie na vijana wafuate nyuma. Wakati anahojiwa matokeo ya uchaguzi yalikuwa hayajatangazwa. Nina mashaka makubwa kama mzee huyu alifurahishwa na uchaguzi wa Kikwete! Inawezekana mzee huyu anawakilisha maoni ya wazee wengi wa nchi yetu ambao ni hazina kubwa. Inawezekana pia mzee huyu anayawakilisha maoni ya wale walioichukulia hotuba ya Mheshimiwa Mkapa, kuwa usaliti mkubwa kwa wazee wa chama wasiopenda mabadiliko na wanafikiri Chama Cha Mapinduzi, ni mali yao! Inawezekana pia kwamba mzee huyu ni sauti ya wale wanafiki ambao hawakupokea uchaguzi wa Kikwete, kwa furaha na wanaendeleza mapambano ya chini kwa chini!

Alichosema mzee wa Dodoma, ni ukweli. Ni lazima wazee wawe mbele. Ndiyo maana CCM, iliwaweka mbele Mzee Mwinyi, Mzee Kawawa, Mzee Kingunge, Mzee Dr Salmin na Mzee Malecela. Bila wazee hawa CCM, ingesambaratika! Kuwa mbele haina maana ya kushika madaraka na kufanya kazi za siku kwa siku. Kuwa mbele ni kushika taa na kuonyesha njia. Kuwa mbele ni kutoa ushauri wa kizalendo, ni kuamsha fikra pevu, ni kuambukiza hekima na busara!

Tukibaki ndani ya chama. Je demokrasia iliyojionyesha pale Chimwaga, itatumika wakati wa kuwapendekeza wabunge na madiwani? Rushwa, upendeleo, ukabila, udini vitathibitiwa? Uongozi wa CCM kwenye ngazi ya Kata, Wilaya na Mkoa, utaweza kuisimamia demokrasia ya kweli? Watu wasiokuwa na pesa, lakini wana vipaji, wana ari mpya, kashi mpya na nguvu mpya, wataweza kupenyeza?

Upande wa pili, nje ya chama cha Mapinduzi. Rais Mkapa, amejijengea jina kwa kuongoza vikao vya CCM, kwa amani na utulivu bila Mwalimu. Je, sifa hii ataibeba hadi mwisho? Atahakikisha vyama vyote vya siasa vinapata nafasi sawa ya kujitangaza na kuwashawishi wapiga kura? Maana kama demokrasia imekomaa ndani ya CCM, ni lazima ikomae ndani ya nchi nzima. Rais wa nchi, si rais wa chama, bali ni rais wa nchi nzima. Sifa zake ni lazima ziliambukize taifa zima!

Zanzibar, si shwari. Upinzani uliochipuka na kufifia dhidi ya Rais Karume, ni fukuto. Hatuwezi kujituliza kwamba Chimwaga, imetibu na kupoza fukuto. CUF, inaongeza nguvu na nia ya kutorudi nyuma! Bila busara na hekima, kuna hatari ya kushuhudia zaidi ya yale yaliyotokea 2001.
Kama nilivyosema hapo juu, watu walitegemea CCM, isambaratike mwaka huu, walitegemea fujo kwenye mkutano wa Chimwaga, lakini hekima, busara na fikra pevu vimekuwa kinga. Sasa hivi kuna watu wanasubiri Tanzania, isambaratike wakati wa uchaguzi mkuu, wanasubiri fujo na umwagaji damu. Mzigo mkubwa vinatupiwa vyama vya upinzani hasa chama cha CUF, kwa upande wa Visiwani. Si kweli kwamba vyama vya upinzani havipendi amani. Si kweli kwamba vyama vya upinzani vinatamani kumwaga damu. Tatizo ni ukomavu wa kisiasa kwa pande zote mbili. Hakuna wa kumlaumu mwingine! Hekima, busara na fikra pevu isiponyauka na kukauka, ikiendelea kuota kwa afya, wenye nia mbaya watashangaa sana kuiona Tanzania, ikipeta!

Mfano mzuri ni uchaguzi wa Kikwete, ingawa vyama vya upinzani vinajipanga kupambana naye vilivyo, vinamkubali na kuipongeza CCM kwa chaguo hilo. Baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wamesikika wakisema kwamba CCM, ingemchagua mtu mwingine, kinyume na Kikwete, basi upinzani ungeichukua nchi kilaini!

Wazee wetu wa CCM, wazee wetu wa vyama vya siasa kama mzee Mtei, Makani, Mapalala na wengine, wazee wetu wa dini, wazee wetu wasiokuwa na vyama wala dini wakishikamana , wakawa mbele ya vijana wakashika taa na kuonyesha njia, Tanzania, itapeta na kuendelea kuwa kisiwa cha amani. Kinyume na hapo ni hatari kubwa. Wakati huu wa kuelekea uchaguzi ni wa kuomba kwa nguvu zote. Tuombe sote, na kushikamana kwa moyo wa kizalendo, tulijenge taifa letu kwa ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya!

Na,
Padri Privatus Karugendo.

TUMWOGOPE MUNGU

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA RAI 2005

TUMWOGOPE MUNGU KWA MATENDO YETU YOTE, KILA SIKU NA KILA WAKATI!

Wakati tunapoelekea kwenye kipindi cha uchaguzi mkuu na hasa juma hili CCM inapomteua mgombea wake wa kiti cha urais, viongozi wetu wa dini wameanza zao, wameanza kujifanya wanayafumba macho yao na ya kwetu, wanataka tuamini kwamba wao ni wachambuzi wazuri wa mambo ya kisiasa, wanataka tuamini kwamba wao wanawachukia viongozi wabovu, viongozi wasiolipenda taifa letu, viongozi wanaotupokonya uhuru wetu na kuipora nchi yetu.

Wanaogombea tunawajua, hawakuzaliwa leo, wengi wao wametumikia serikali zote zilizopita. Karibia hao hao ndio wanataka kugombea tena! Kama ni kuwatilia mashaka, viongozi wetu wa dini wamechelewa! Wanatukumbusha kumwongopa Mungu, wakati wa uchaguzi. Maana yake ni nini? Kwamba watu wasikubali kununuliwa na kumchagua mtu asiyelifaa taifa letu, kwamba watu wachague kwa uhuru bila ya shinikizo wala vitisho, kwamba watu wafanye uchaguzi wakizingatia amani na utulivu wa taifa letu, kwamba watu wakifanya mchezo mchafu wakati wa uchaguzi wakumbuke Kwamba Mungu, anawaona na anaweza kuwaadhibu!

Viongozi wetu wa dini wanayaona haya vizuri leo, kuliko walivyokuwa wakiyaona jana! Ni nani anajua labda keshokutwa watayaona haya vizuri zaidi ya wanavyoyaona leo! Ikiingia madarakani serikali inayowakumbatia viongozi wa dini wote bila kujali mwenye hoja, mwenye uwezo wa kuona mbali, mwenye mchango wa maana katika jamii au mzalendo, serikali itakayo zaiachia dini zifanye zinavyotaka bila kuhoji kitu chochote, hatutasikia kelele, ushauri wala maonyo!

Ujumbe huu wa viongozi wetu wa dini kwamba tumwogope Mungu wakati wa uchaguzi ni wa muhimu na unakuja kwa wakati wake. Tofauti ni kwamba tusimwogope Mungu, wakati wa uchaguzi na katika siasa tu, tumwogope Mungu, kwa matendo yetu yote, kila siku na kila wakati.
Tumwogope Mungu, kwa matendo yetu mabaya, Tuongope kuwatendea ndugu zetu yale tusiyopenda kutendewa na sisi.
Tumwogope Mungu, tunapopokea sadaka na zaka nzito nzito kutoka mikononi mwa wanasiasa, bila kuuliza wala kuhoji. Tumwogope Mungu, tunapowakumbatia wanasiasa wenye sifa za ufisadi na kuwaalika kuendesha harambee za kujenga misikiti na makanisa. Tumwogope Mungu, tunaposamehewa kutoa ushuru na badala ya kuwahudumia wanyonge na masikini, tunajitenga na jamii na kuishi maisha kifahari. Tumwogope Mungu, tunapokula na kusaza, wakati wengine wanakufa kwa njaa. Tumwogope Mungu, tunapoziingilia familia na kuzisambaratisha. Tumwogope Mungu, tunapozaa watoto na kuwatelekeza kwenye mitaa ya miji. Tumwogope Mungu, pale tunaposhughulikia afya zetu kwenye mahospitali mazuri na kuwaacha wanyonge kufa kwa magonjwa yanayotibika. Tumwoge Mungu, tunapojikinga na ugonjwa wa UKIMWI na kuendelea kuwapumbaza watu kwamba kutumia kondomu ni dhambi. Orodha ni ndefu! Ni lazima kumwogopa Mungu, kwa matendo yetu yote mabaya.

Kwa viongozi wetu wa dini za Kikristu, ujumbe huu unaweza kuwasaidia kutafakari zaidi:
“……. Nendeni katika moto wa milele aliyotayarishiwa Shetani na malaika wake. Maana nilikuwa na njaa nanyi hamkunipa chakula; nilikuwa na kiu hamkunipa maji; Nilikuwa mgeni hamkunikaribisha; nilikuwa mgonjwa na mfungwa nanyi hamkuja kunitazama…… Nawaambieni kweli, kila mlipokataa kumtendea mambo haya mmojawapo wa hawa wadogo, mlikataa kunitendea mimi” ( Matayo 25: 41- 46).

Yesu, aliongelea mambo yanayotendeka kila siku katika jamii, mambo ambayo yanawatenga watu na Mungu wao. Hivyo orodha hii inaweza kurefushwa: “Mlinibagua kufuatana na rangi yangu ya mwili, kabila langu na dini yangu, mlininyanyasa, hamkunisikiliza, hamkunionea huruma nilipolala mitaani, hamkunipatia ushauri mzuri mme wangu alipoanza kutembea nje ya ndoa na kuambukizwa na virusi vya UKIMWI, mlinizuia kutumia kondomu, sasa na mimi nimeambukizwa, watoto wetu watabaki yatima, hamkunisaidia kuwalea na kuwatunza watoto mlionishauri nizae bila mpango, mlinibagua, mlinibaka, mlinitomasa na kuninyanyasa kijinsia.. nk”.

Orodha ni ndefu. Hoja ni kwamba ni lazima kumwogopa Mungu, kwa matendo yetu yote mabaya. Tusisubiri wakati wa uchaguzi na kwenye siasa!
Mfano: Yule anayewafukuza Wanawaombi Kanisani, ni lazima amwogope Mungu. Yale anayowafanyia wanawaombi, anakuwa anamfanyia Mungu. Jinsi watu walivyo na uhuru wa kumchagua kiongozi wao wa kisiasa, ndivyo walivyo na uhuru wa kumwabudu Mungu wao jinsi wanavyotaka. Uhuru ni uhuru, uwe ni wa kisiasa au wa kidini. Kuusukuma uhuru kwa upande wa siasa na kuunyamazisha kwa upande wa dini, ni dhambi na huku si kumwogopa Mungu! Tunashauriwa kuondoa kwanza vibanzi kwenye macho yetu kabla ya kuangalia yale yaliyo kwenye macho ya wengine!
- Yule anayewanyanyasa wanawake na kuwanyima nafasi ya uongozi katika kanisa na nafasi ya kufanya maamuzi muhimu katika jamii kama vile ndoa na familia, kuzaa watoto wengi au kuzaa kwa mpango, kutoa mimba au kulinda uhai kwa kupoteza uhai ( mfano mwanamke mwenye matatizo kwenye kizazi, ambaye kama angetoa mimba, angeponyesha maisha yake), kuhusu malezi nk., ni lazima amwogope Mungu, maana kuwabagua na kuwanyanyasa wanawake ni Kumbagua Mungu Mwenyewe. Tunafundishwa kwamba sote tumeumwa kwa mfano wa Mungu, na kwamba binadamu wote ni sawa. Bahati nzuri Katiba yetu inakubaliana na kitu hiki.

- Yule anayewabagua walei na kuwaweka katika nafasi ya kusikiliza na kupokea kila kitu bila kushiriki maamuzi yote, ni lazima amwogope Mungu, maana kuwabagua walei, ni kumbagua Mungu mwenyewe.
- Yule anayewabagua watu wa dini nyingine, ni lazima amwogope Mungu, maana sisi sote ni watoto wa Mungu. Ukweli unaotuzunguka sasa hivi ni kwamba Waislamu wanajiona wana haki zaidi ya wengine, Wakristu pia wanajiona wana haki zaidi ya wengine. Wakristu wanagawanyika katika madhehebu ambayo kila dhehebu linajiona kuwa na haki zaidi ya mengine. Dini zinakuwa kikwazo cha ushirikiano, udugu kama vile ndoa nk, wakati mwingine hata viongozi wa serikali wanachaguliwa si kwa sifa bali kwa kufuata dini zao.
- Yule asiyependa majadiliano, ushauri, ushirikishwaji, ni lazima amwogope Mungu, maana Wakristu wanamwamini Mungu, wa ushirikiano, Mungu wa utatu: Mungu baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu. Hata dini nyingine zinamwamini Mungu, anayesikiliza, Mungu mwenye huruma , upendo na wema.
- Yule asiyekuwa upande wa wanyonge na wanaoonewa, ni lazima amwogope Mungu, maana mbali na hukumu inayotajwa na Matayo katika sura ya 25, mstari wa 31 na kuendelea, Yesu, alisisitiza sana kuwajali wanyonge, wanaoonewa na wafungwa:

““Roho wa Bwana yu pamoja nami, kwani ameniteua rasmi niwaletee maskini habari Njema. Amenituma niwatangazie wafungwa kwamba watapata uhuru, vipofu watapata kuona tena; amenituma niwakomboe wanaoonewa, na niutangaze mwaka ambao Mungu atawakomboa watu wake” ( Luka 4:18-19).

Habari njema inakuja kwa maskini, wafungwa na wanaoonewa, si kwa matajiri na wenye madaraka. Ili ujumbe huu uwe na maana, Yesu, mwenyewe alijitokeza miongoni mwa maskini na wanaoonewa. Alizaliwa katika umaskini na kukulia katika umaskini. Enzi zake kulikuwa na matajiri wenye majumba ya kifahari, lakini hakuyachagua! Aliishi na masikini. Mitume wake wote walikuwa ni watu maskini. Aliwaponya wagonjwa, waliwafufua wafu na kuwapatia uzima mpya, uzima tele. Wenye njaa aliwashibisha chakula cha mwili na roho, wenye kiu aliwapatia maji ya uzima. Alifanya miujiza mingi bure bila kudai ujira.

Ili ujumbe wa viongozi wetu wa dini na hasa Wakristu uwe na maana yoyote ile ni lazima wajiulize wamesimama upande gani? Kama zilivyokuwa enzi za Yesu, leo hii kuna matajiri na maskini, kuna majumba ya kifahari na kuna vibanda ambavyo ni sawa na zizi la ng’ombe aliko zaliwa Yesu. Viongozi wetu wa dini wanaishi kwenye majumba ya kifahari au wanaishi kwenye vibanda? Wanapanda daladala au magari ya kifahari? Je, wako upande wa maskini na wanaoonewa au upande wa matajiri na wenye madaraka. Je, wanaponya wagonjwa? Wenye njaa wanawapatia chakula? Wenye kiu wanawapatia maji ya kunywa? Je wanafanya miujiza bila ya kudai ujira?


Viongozi wetu wa dini na hasa Wakristu, wanapotukumbusha kumwogopa Mungu, wakati wa uchaguzi unaokuja, ni bora wao wakatafakari ujumbe wa Yesu kwanza. Je, wao wanamwogopa Mungu? Je wao wanashiriki kiasi gani kuchangia hali hii ya watu kuishi bila kumwogopa Mungu. Kwanini watu waamue kuuza haki yao ya kupiga kura? Kwanini watu waamue kumchagua kiongozi si kufuata sifa zake bali wafuate kabila, dini, pesa, pilau na kanga wanazozipata wakati wa kampeni? Je, viongozi wetu wa dini wanachangia kiasi gani katika kuujenga uchumi wetu?

Kama bado kuna dalili za watu kufanya mambo bila kumwogopa Mungu, katika jamii yetu, basi viongozi wetu wa dini hawajafanya kazi yao vizuri. Mafundisho yao yatakuwa yanapeperushwa na upepo, hayajikiti katika jamii! Kutukumbusha ni jambo zuri, lakini pia kutengeneza mifumo ya kubadilisha hali hii mbaya ni jambo muhimu zaidi.

Mungu, ametuumba ili tusaidiane na kukumbushana wajibu zetu. Mtu, akisimama peke yake anaanguka haraka Bahati mbaya hatuna mfumo mzuri wa kukutana na kusaidiana. Watu wanaokutana kanisani au msikitini ni wengi kiasi ni vigumu mtu kumkaribia jirani yake na kumsaidia. Tungekuwa na mpango wa familia chache kukutana, kusali pamoja, kujadiliana na kusaidiana kimawazo, kihali na mali, ungekuwa msaada mkubwa. Haya ndio viongozi wetu wa dini wangekuwa wakiyafanyia kazi.
Jumuiya za mwanzo za Wakristu zilikuwa na mfumo huu na ulizisaidia sana jumuia hizi kuishi kwa kufuata mpango wa Mungu. Mfumo huu ukifufuliwa unaweza kusaidia hata leo hii! Ni kazi ya viongozi kugeukia wajibu zao kuliko kuwanyoshea kidole wanasiasa!

Bahati mbaya Kanisa Katoliki, lilitupilia mbali mfumo wa demokrasia tunaousikia kwenye jumuia za mwanzo na kukumbatia uchaguzi unaoongozwa na nguvu za Roho Mtakatifu, anayepitia kwa watu wachache sana. Kwa misingi hii, ushauri wa Kanisa Katoliki kwa demokrasia ya watu wengi, demokrasia inayomtaka kila mwananchi kupiga kura, si wa kuzingatiwa. Maaskofu wanachaguliwa kwa kura ya siri inayoongozwa na Roho Mtakatifu. Makadinali wanachaguliwa kwa kura ya siri inayoongozwa na Roho Mtakatifu, hawa watashauri nini kwenye uchaguzi wa wazi, wa watu wote, wa vyama vingi vya siasa, uliojaa heka heka, rushwa, upendeleo, kupakana matope, kujinadi nk.?

Ile demokrasia tunayoisikia kwenye makanisa ya mwanzo, ikirudi, kanisa litakuwa katika hali nzuri ya kuwashauri viongozi wa nchi na wananchi wanaoamini katika kuwachagua viongozi kwa kura ya demokrasia, vinginevyo kwa vile viongozi wetu wa dini ni wananchi kama wananchi wengine, ni bora wakashiriki kupiga kura kimyakimya bila kupaaza sauti zao ambazo zinageuka kuwa mwiba katika nguzo zao wenyewe! Viongozi wetu wa dini watufundishe kumwogopa Mungu kwa matendo yetu yote mabaya, mambo ya siasa wawaachie wanasiasa na wale wanaoamini katika demokrasia!

Na,
Padri Privatus Karugendo.

WATANZANIA NA CHAMA KIMOJA CHA SIASA

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA HEKO LA MAREHEMU BEN MTOBWA ( Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi) 2005

WATANZANIA WANAPENDA SIASA YA CHAMA KIMOJA!

Kura za maoni zilizofanyika wakati Tanzania, inajiandaa kuipokea siasa ya vyama vingi vya siasa, zilionyesha kwamba asilimia 20 ya watanzania walitaka siasa ya vyama vingi na asilimia 80, walitaka siasa ya chama kimoja. Watanzania walijua nguvu za Chama Cha Mapinduzi, walijua uchu wa madaraka waliokuwa nao viongozi wa Chama Cha Mapinduzi, waliujua unafiki wa Chama Cha Mapinduzi, walijua CCM ina wenyewe, na hao wenyewe ndo walikuwa na nguvu ya pesa na kuyashikilia madaraka, walijua jinsi upinzani wa kweli ulikuwa bado haujazaliwa, walijua jinsi wale wote waliojiita wapinzani walikuwa wamenyimwa nafasi ya kula ndani ya chama cha mapinduzi. Kwa kuyapima yote hayo, waliona ni bora kubaki na utawala wa chama kimoja, maana haikuwa na maana kuudanganya ulimwengu kwamba tunafuata siasa ya vyama vingi na huku ukweli ni chama kimoja tu ndicho kinachoshika utamu wote.

Kwa sababu ya shinikizo la jumuiya ya kimataifa, utandawazi na sera za dunia hii zinazoukumbatia ubepari na unyama zaidi ya utu na haki, Tanzania ililazimika kupinga maoni ya watu wengi na kukubali kuanzisha siasa ya vyama vingi iliyoungwa mkono na asilimia kidogo ya wananchi. Lakini hata mjinga na mwendawazimu anajua jinsi Tanzania, inavyoendeleza siasa ya chama kimoja cha siasa! Chama ni CCM tu, vyama vingine vinakisindikiza chama cha mapinduzi.


Uchaguzi wa kwanza uliofanyika 1995, ulikuwa wa moto moto kweli. Baadhi ya watu waliokuwa wamechoka na ukiritimba wa chama kimoja walikihama chama cha Mapinduzi na kujiunga na vyama vya upinzani. Wengi wa watu hawa ni kati ya ile asilimia 20, iliyokuwa ikiunga mkono siasa ya vyama vingi. Watu kama Mrema, walivuma na kuleta matumaini kwamba ,hatimaye Tanzania, inaweza kutawaliwa na chama kingeni, ingawa watu walikuwa walewale, maana Mrema, alikuwa amekimbia CCM, baada ya jina lake kutupwa kapuni wakati wa kutafuta kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi kuwania nafasi ya urais. Nguvu za Chama Cha Mapinduzi za kutumia mbinu mbali mbali na pesa, zilimsambaratisha Mrema hadi kesho akikubali kurudi CCM!

Chama Cha Mapinduzi, ambacho ndicho kilikuwa kikishikilia hatamu ya dola wakati wa uanzishwaji wa siasa za vyama vingi, kilikubali shingo upande kuvipokea vyama vingine katika ulingo wa siasa. Wakati CCM, ikitumia vyombo vya dola katika kampeni, vyama vingine vya siasa viliachwa hivyo hivyo kujishughulikia kwa kila kitu. CCM, iliweza kuzunguka kila kona ya nchi kwa kutumia ndege na magari ya serikali. Kwa maneno mengine vyama havikupata haki sawa. Tume ya uchaguzi iliendelea kuwa na bado iko mikononi mwa serikali inayoongozwa na CCM. Watendaji wa tume hiyo walichaguliwa na bado wanachaguliwa na rais wa nchi, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM. Katika hali kama hii ni vigumu kuitegemea tume ya uchaguzi kuvitendea haki vyama vyote vya siasa. Kama CCM, ilikuwa na lengo la kuanzisha siasa ya vyama vingi, basi ingependekeza tume huru ya uchaguzi.

Wale wote waliokihama chama hicho na kujiunga na vyama vya upinzani walishughulikiwa ipasavyo. Mheshimiwa Philip Mangula, Katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, amefichua siri hiyo hivi majuzi wakati akiwaonya wanaCCM waliokuwa wakiomba nafasi ya urais wa Jamhuri ya Tanzania, kupitia chama hicho kwa uchaguzi wa Oktoba mwaka huu. Alisema kwamba ambao majina yao yatatupwa wasithubutu kuhamia vyama vingine, maana wakifanya hivyo watashughulikiwa ipasavyo.

CCM, ilijenga picha miongoni mwa wananchi, picha inayodumu hadi leo hii kwamba kujiunga na vyama vya upinzani ni sawa na uhaini ! Kampeni hii ilifanikiwa sana na kuwafanya watu wavipuuzie vyama vya upinzani. Ni maeneo machache katika nchi ambayo watu wamejikomboa kiasi cha kufahamu maana ya vyama vya upinzani. Mfano, Karatu, Kyerwa, Hai, Kigoma mjini, Bukoba mjini, Zanzibar, wanafahamu ni nini maana ya vyama vya upinzani. CCM, inatumia pesa na ushawishi wa juu katika maeneo ili kupanda mbegu ile ile iliyopandwa katika taifa zima. Mbegu ya kuvichukia vyama vya upinzani.

Uchaguzi mkuu wa pili wa vyama vingi uliofanyika 2000, ulishuhudia wimbi kubwa la watu waliokuwa wamekihama chama hicho cha mapinduzi mwaka 1995, wakirudi tena ndani ya chama hicho. Walio wengi hawakurudi kwa kutaka au kwa kukipenda chama. Walirudi kuyasalimisha maisha yao, kusalimisha shughuli zao na biashara zao kwa wale waliokuwa na biashara. Ni imani yangu kwamba uchaguzi wa mwaka huu, utashuhudia wimbi jingine kubwa la kutoka kwenye vyama vya upinzani na kurudi chama tawala.

Tegemeo la vyama vya upinzani lilikuwa kwamba CCM, ingemeguka mwaka huu. Lakini kwa bahati nzuri au mbaya, hekima na busara vimetawala ndani ya CCM, hakuna makosa yaliyofanyika. Hivyo chama hakikumeguka. Uchaguzi wa Kikwete, kama mgombea wa urais kwa tiketi ya CCM, kumetokea kama pigo kwa vyama vya upinzani.

Ni kweli kwamba CCM, si shwari. Lakini matatizo yaliyo ndani ya CCM, sasa hivi si yale ya kukifanya chama hicho kumeguma. Mzee Malecela, hakufurahi na watu wengi wanafikiri hakutendewa haki. Lakini Mzee, huyu hawezi kukifanya chama kimeguke. Hata hivyo chama kina njia nyingi za kumshughulikia kama kilivyowashughulikia wale wote waliokihama na kukimbilia vyama vya upinzani. Hoja nyingine ni kwamba Mzee Malecela, hakubaliki sana kwenye vyama vya upinzani na wala si kipenzi cha vijana ambao ndio wanaotaka mabadiliko. Hata angekihama chama au kujitoa kabisa kwenye siasa, CCM, haiwezi kuyumba kamwe!

Mtu mwingine, aliyetupwa jina lake na anaweza kule chokochoko kwenye Chama Cha Mapinduzi ni mheshimiwa Sumaye. Lakini pia naye chokochoko zake haziwezi kukifanya chama kimeguke. Sumaye, ni mtu mwenye bahati mbaya. Na huenda bahati hii mbaya ni ugonjwa wa kujitakia. Sumaye, hakubaliki ndani ya chama, hapendwi na wananchi hata na watoto wadogo wanajua yeye ni mlarushwa ni fisadi mkubwa. Akiamua kukimbia chama chake, atakuwa amejimaliza kabisa. Hakuna chama cha kumpokea na hakuna mwananchi wa kumpatia kura. Inawezekana akakivuruga chama kwa kiasi Fulani, maana kambi yake ilikuwa na nguvu ya pesa. Inawezekana pesa hizi zikaendelea kutumika kwa lengo la kuvuruga na kuhatarisha amani. Kwa vile anajulikana itakuwa kazi ya chama kumshughulikia na kumnyamazisha.

Dr.Salim, huyo hawezi kukihama chama. Huyu ana hasira zake binafsi na Mtukufu Rais Mkapa. Labda kama Rais, angekuwa mkweli, akamwambia kwamba yuko upande wa Kikwete, asingejisumbua kujiingiza kwenye kinyanganyiro. Hotuba ya mheshimiwa Mkapa wakati wa kufungua mkutano mkuu wa CCM, ilikuwa inamkanyaga Salim. Rais, alisisitiza achaguliwe kijana. Salim, ndio alikuwa mzee(63) kati ya wote, Mwandosya (57) na Kikwete(55). Hakuna aliyekuwa kijana kati yao kwa maana ya neno kijana, lakini kwa vigezo vya CCM, mwenye miaka 55 ndio alikuwa kijana! Rais, alisisitiza mtu aliyekulia CCM. Salim, ana historia ya Hizibu, hivyo kigezo hicho kilikuwa kinamtupa nje. Rais, alisisitiza mtu anayekubalika Bara na Visiwani. Salim, anakubalika bara, lakini visiwani ni sumu! Hivyo na kigezo hiki kilikuwa kinamtupa nje! Ilianza kujitokeza kwamba yeye alihusika moja kwa moja na mauaji ya Mzee Karume. Mkapa, kwa sababu zake mwenyewe aliamua kumtosa Salim! Hivyo ni wazi Mheshimiwa Dr.Salim, ana hasira kubwa. Hasira hizi haziwezi kukigusa chama wala nchi. Hasira hizi hazina msaada wowote kwa vyama vya upinzani.

Wengine ndani ya chama cha mapinduzi wenye hasira na hawana furaha ni vigogo wote waliokuwa wakimpigia debe Dr.Salim. Kufuatana na vyombo vya habari na habari zilizoandikwa na gazeti la Tanzania Daima, ni kwamba timu yote ya Nyerere Foundation, wakuu wa mawilaya, wakuu wa mikoa, baadhi ya mawaziri na baadhi ya wabunge, hawakufurahishwa na uteuzi wa Kikwete. Hivyo wana hasira. Lakini hasira hizi haziwezi kusababisha chama kimeguke, Hawa wote wanaweza kushughulikiwa na Chama! Hivyo CCM, haiwezi kumeguka mwaka huu na haitameguka hivi karibuni! Matumaini ya vyama vya upinzani yanaingia shimoni. Tena shimo lenye kina kirefu sana!

Badala ya watu kutoka CCM na kujiunga na vyama vya upinzani, tutashuhudia kinyume. Watu watahama vyama vya upinzani na kujiunga na CCM. Zoezi hili litaonekana wakati wa kuwatafuta wabunge na madiwani.

Mheshimiwa Kikwete, amesema CCM, itaendelea kutawala hadi miaka 100 ijayo! Huu ni ukweli. Hali inavyojionyesha. Si kazi rahisi kupambana na CCM, bila vyama vya siasa kukubali kuungana. Muungano huu wa vyama vya siasa ni ndoto. Mrema, anataka kusimama peke yake. CHADEMA, inasema vyama vingine vina unafiki na haviwezi kufanya muungano wa kweli. CUF, wanataka wasimame peke yako. NCCR-mageuzi nao pia wanataka wasimame peke yao. Kwa njia hii hata na vile viti vilivyokuwa vikishikiliwa na vyama vya upinzani bungeni vitapungua sana. Itafikia mahali vyama vingi itakuwa ni wimbo tu!

Ni nani wa kubeba lawama hizi? Hakika si watanzania. Maana asilimia 80 ya watanzania ilipendekeza siasa za chama kimoja. Lakini serikali ya CCM, ikakumbatia pendekezo la asilimia 20 kuanzisha siasa ya vyama vingi.

Lawama hizi zinaendelea upande wa serikali ya CCM, maana baada ya kukubali kwenda kinyume na matakwa ya watanzania, haikuwa na nia ya kuendeleza siasa za vyama vingi. Iliendelea kuvipiga vita na kuwanyanyasa na kuwashughulikia wapinzani huku ikiudanganya ulimwengu na jumuiya ya kimataifa kwamba inafuata siasa ya vyama vingi.

Watanzania walio wengi hawapendezwi na mwenendo wa Chama Cha Mapinduzi, lakini kila mtu anajua jinsi ukitaka mambo yako yanyooke ni lazima upeperushe bendera ya Chama Cha Mapinduzi. Wafanyabiashara walio wengi si wapenzi wa CCM, lakini kwa kutaka mambo yao yanyooke wanatoa michango kwenye chama cha mapinduzi na kupeperusha bendera ya chama cha mapinduzi.

Si kweli kwamba watanzania wanapenda siasa ya chama kimoja. Ukweli ni kwamba wanalazimishwa na hali ilivyo kukipenda Chama Cha Mapinduzi. Ni nani wa kuueleza ukweli huu kwenye jumuiya ya kimataifa? Bila ukweli huu kutoka nje, Tanzania, itabaki chini ya utawala wa chama kimoja na maendeleo yatakuwa ni ndoto. Ni vigumu nchi kuendelea bila kuwa na vyama vya upinzani vyenye nguvu kutoa changamoto kwa chama tawala. Ni kazi ya watanzania wote kushirikiana kujenga nguvu za upinzani vinginevyo tutabaki kuimba wimbo wa umasikini hadi mwisho wa dunia!

Na,
Padri Privatus Karugendo

KISWAHILI LUGHA YETU!

MAKALA HII ILICHAPWA KWENYE GAZETI LA RAI 2005

KISWAHILI LUGHA YETU!

“Hapana lugha damiri, ana yake kila mtu,
Mimi hasa nafikiri, tunachekwa na wenzetu,
Tumo katika ngururi, yakutupa lugha yetu,
Hima pakutane watu au tahasiri.

Lugha ngeni nakiri, zina manufaa kwetu,
Tujifunze kwa dhamira, tuseme kama upatu,
Walakini tufikiri ubora wa lugha yetu, Hima
Pakutane watu au tutahasiri.” (Shaaban Robert –
Lugha Yetu).



Wakati wa uhuru 1961, Watanganyika wengi walikuwa wanaweza kuzungumza na kukielewa Kiswahili. Hii ilitokana na sababu mbali mbali zilizosaidia kukieneza Kiswahili kutoka pwani hadi bara: Biashara na misafara ya watumwa kutoka Zanzibar hadi DRC, wavumbuzi na wamisionari, lakini hasa serikali ya Wajerumani iliyoshinikiza Kiswahili kutumika kwenye serikali za mitaa na kwenye shule za misingi. Lakini msukumo mkubwa wa kukiendeleza Kiswahili uliletwa na mwalimu Nyerere, alipokitangaza Kiswahili kama lugha ya taifa na kuanza kulihutubia bunge letu kwa lugha ya Kiswahili mnamo mwaka wa 1962. Siasa ya Ujamaa na kujitegemea iliyotangazwa mwaka 1967, iliharakisha matumizi ya Kiswahili maana viwanda, mashirika, mashamba na vijiji vya ujamaa vilivyoanzishwa chini ya mfumo huo viliwakutanisha watu mbalimbali kutoka makabila 120 ya Tanzania, na walilazimika kutumia Kiswahili ili kuwasiliana na kuelewana.
Mwaka wa 1968, Kiswahili kilianza kutumika kama lugha rasmi ya serikali. Elimu ya kujitegemea ilianzishwa mashuleni na Kiswahili kilianza kutumika kama lugha ya kufundishia kwenye shule za msingi.

Vitu vingine vilivyosaidia kukiendeleza Kiswahili ni kama vile kuanzishwa kwa wizara ya utamaduni, Tanzania Publishing house, kwa ajili ya kuchapisha vitabu(1966),BAKITA(1967), Kitivo cha Kiswahili kwenye Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam(1970),TAKILUKI –Zanzibar(1978),Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) (1986),mfuko wa utamaduni Tanzania(1998),Redio Tanzania, Sauti ya Zanzibar , na magazeti ya Kiswahili na shirika la UKUTA, lilioanza kwenye miaka ya 1958. Hivi ni baadhi ya vitu vilivyokisaidia Kiswahili kushika kasi kubwa nchini Tanzania kwenye miaka ya 60 na 70.Kufikia mwaka 1970, Kiswahili kilikuwa kimekubalika kiasi kikubwa kwa watanzania wote kuwa ni lugha ya taifa.

Pamoja na jitihada zote hizo nzuri za kukiendeleza Kiswahili, Tanzania ilishindwa kufanya mambo manne muhimu na ya msingi ambayo ni: 1. Kukisimika Kiswahili kama lugha ya taifa kisheria. Hadi leo hii hakuna sheria yoyote ya kukitaja Kiswahili kama lugha ya taifa. Hata katiba ya nchi iliyoandikwa kwa lugha ya Kiswahili, haitaji kwamba Kiswahili ni lugha ya taifa. Jambo hili limekikwamisha Kiswahili. Watu wanaweza kukipuuzia Kiswahili na kuendelea kutumia lugha nyingine wanavyotaka katika shughuli za serikali na mashuleni maana hakuna sheria inayowabana. Hii ndiyo sababu inayolidekeza bunge letu kuendeleza mijadala kichaa ya kutumia au kutotumia lugha yetu kufundishia. Hakuna anayeweza kufikishwa mbele ya sheria kwa kukataa kukitumia Kiswahili. Hili ni tatizo kubwa katika jitihada za kukikuza na kukiendeleza Kiswahili.

2.Kuchelewa kuzitafsiri sheria za nchi katika lugha ya Kiswahili. Ingawa baadhi ya kesi huendeshwa kwa lugha zote mbili, Kiingereza na Kiswahili, lakini sheria zote bado ziko kwenye Kiingereza na mara nyingi hukumu huandikwa kwa Kiingereza. Kwa vile sheria zinamgusa kila Mtanzania, hili lingekuwa jambo la kwanza kushughulikia na kwa njia hii Kiswahili kingepanuka haraka.
5. Kushindwa kupambana na ile hali ya kutojiamini kwamba Kiswahili hakiwezi kumudu sayansi ya teknolojia. Kama lugha nyingine zimeweza, kwa nini Kiswahili kishindwe?

4. Kuchelewa kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia elimu ya sekondari na vyuo vikuu. Mjadala mkali juu ya kutumia Kiingereza au Kiswahili kufundishia ulianza kufukuta kwenye miaka ya 1965-1980. Ripoti ya tume ya Makweta ya 1982, ilipendekeza kwamba Kiswahili kianze kutumika Kama lugha ya kufundishia kwenye sekondari kuanzia mwaka 1985. Lakini kabla mpango huo haujaanza kutekelezwa serikali ilitoa mwongozo kwamba Kiingereza kiendelee kutumika katika sekondari na vyuo. Tamko hili lilizua mjadala ambao unaendelea hadi leo hii. Rais William Benjamin Mkapa, alipoingia madarakani mnamo mwaka wa 1995, aliogopa kujifunga kwa tamko au ahadi yoyote juu ya majadiliano haya. Alipendekeza mjadala uendelee hadi kufikia muafaka! Bila nia ya kweli, bila kuthubutu, mjadala huu ni ndoto ambayo haitakaa iwe kweli siku moja!

Kuchelewa huku kuanza kukitumia Kiswahili katika elimu ya sekondari na vyuo kumekumbana na kuanguka kwa ukomunisti na kuzaliwa upya ubepari mtakatifu wenye jina la utandawazi. Kasumba mpya imeanza kujengeka, ukoloni mambo leo umeanza kuzagaa, na watu sasa wanakubali kwamba Kiswahili hakiwezi kumudu kasi ya mageuzi haya mapya ya utandawazi, soko huria na uwekezaji. Hivyo lugha za kigeni zinaonekana za maana zaidi! Zinaanza kutolewa sababu kwamba Kiswahili hakiwezi kumudu sayansi na teknolojia, hakina misamiati ya kutosha, hakina vitabu nk. Mambo mengi ya kimagharibi yameanza kuwa na mvuto, kuanzia kwenye magari hadi nguo. Vijana wa kizazi kipya wameanza kuimba nyimbo za Kiswahili wakiigizia zile za Ulaya na Amerika. Mtu aliyeendelea na kuwa wa kisasa ni yule anayevaa, chana nywele na kuongea kama mzungu!

Kama tulivyoona, jitihada zote hizi za kukiendeleza Kiswahili zilikuwa zinaanzia juu kuja chini. Zilikuwa ni jitihada za viongozi kama Mwalimu Nyerere na wengine. Ndiyo maana kwa kiasi Fulani zilifanikiwa na lugha ya Kiswahili ilikuwa ikipiga hatua ya kupendeza. Lakini hitaji la sasa, hitaji la kutumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia linatoka chini kwenda juu. Ni hitaji la kidemokrasia zaidi. Hitaji la watu wenyewe katika jamii wanaouona ukweli wa mambo kwamba bila lugha yetu tutamezwa. Inashangaza kuona nchi inayojitangaza kufuata demokrasia, hailioni hitaji hili! Kuna haja ya watu wa chini kuendelea kusukuma kwa nguvu hadi serikali ikubali kutunga sheria ya kukitangaza Kiswahili kama lugha ya taifa.

Pamoja na vikwazo nilivyovitaja vinavyochelewesha kuendelea kwa lugha ya Kiswahili hapa Tanzania, dalili za lugha hii kuendelea kukua na kuenea ni kubwa. Sababu za nyuma zilizokisaidia Kiswahili kusambaa ndani ya nchi na je bado ziko pale pale. Watu wanaendelea kuhama kutoka vijijini na kwenda mijini, huko wanakutana na watu wa makabila mbali mbali, hivyo lugha ya kuwaunganisha ni Kiswahili! Kuna ongezeko kubwa la magazeti ya Kiswahili, redio zinazotangaza kwa Kiswahili na luninga zinazorusha matangazo ya Kiswahili. Vyama vingi vya siasa vimeleta changamoto katika siasa, hivyo ni lazima wanasiasa kwenda vijijini kujitangaza na huko lugha inayotumika ni Kiswahili.

Kwa upande wa kimataifa, vita vya maziwa makuu vimekisaidia Kiswahili kuenea zaidi. Wakimbizi wa Rwanda, Burundi na DRC, waliokimbilia Tanzania, wamejifunza Kiswahili. Wanyarwanda waliokuwa hapa zaidi ya miaka 30 na kurudi Rwanda mwaka 1994, Kiswahili ni lugha yao ya kwanza! Kwa vile nchi za Rwanda na Burundi, zinaomba kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki, Kiswahili kilichoanzia kwenye makambi ya wakimbizi kitaendelezwa, kupanuliwa na kusambazwa kwenye kila kona ya nchi hizi. Lakini pia na wakimbizi wa Somalia, Ethiopia na Sudan, waliokuwa Kenya, wamejifunza Kiswahili pia. Marais wa Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi na DRC, wanaweza kuzungumza kwa pamoja kwa Kiswahili.
Kufuatana na takwimu za Profesa Mulokozi, watu milioni 15 wa DRC, wanaongea Kiswahili, Burundi ni milioni 2, Kenya ni milioni 20,Rwanda ni milioni 2,Tanzania ni milioni 32, Uganda ni milioni 8 na nchi nyingine zilizobaki ni milioni 21, jumla ni milioni 80, lakini Profesa Mulokozi, anasema dunia nzima inawezekana kuna watu milioni 100 wanaoongea Kiswahili!

Kiswahili kinafundishwa kama lugha kwenye zaidi ya vyuo vikuu 100(Mulokozi) dunia nzima. Idadi hii ni bila kuhesabu vyuo vya Amerika vya Waamerika weusi wanaokifundisha Kiswahili kama lugha yao ya pili! Kwa kifupi ni kwamba Kiswahili ni kati ya lugha zinazofundishwa kwa wingi duniani.

Kiswahili kinatangazwa kwenye zaidi ya redio na luninga 100 duniani. Zaidi ya kumi ziko Tanzania na Kenya. Nchi nyingine za Kiafrika zinazotangaza kwa Kiswahili ni: DRC, Burundi, Rwanda, Mlisiri, Iran, Sudan, Uganda, Afrika ya Kusini. Nchi nyingine kama Uingereza (BBC), Germany (Deutsche Welle), Amerika (Voice of America).

Vitabu vya lugha mbali mbali vimetafsiriwa kwa Kiswahili. Wakati wa Ukomunisti, vitabu vya Kichina, Kikorea na kirusi vilitafsiriwa sana. Siku hizi vinatafsiriwa vya kimagharibi. Lakini pia waandishi wa Kiafrika, wanaoandika kwa Kiingereza na Kifaransa vinatafsiriwa. Mfano Barua ndefu kama hii kilichotafsiriwa kutoka kwenye Kifaransa na Mkuki na Nyota Publishers.

Sasa hivi zinatengenezwa programu za computer za Kiswahili. Hizi ni dalili za wazi kwamba Kiswahili kinaendelea kwa kasi.

Kiswahili, sasa kinakubalika kwenye mikutano ya kimataifa. AU, baada ya changamoto ya Rais mstaafu wa Msumbiji, Chisano, Kiswahili kimeanza kutumika. Miaka michache ijayo mikutano yote itakipokea Kiswahili. Watahitajika watu wa wakutafsiri Kiswahili kwenye mikutano hiyo ya kimataifa. Watahitajika watu wanaokifahamu Kiswahili vizuri na lugha nyingine za kimataifa vizuri. Kwa vile sisi tunaipuuzia lugha yetu ya Kiswahili ambayo ndiyo ingetusaidia kuzifahamu vizuri lugha za kimataifa kama Kiingereza na Kifaransa, tutashtukia nafasi zote za ukalimani wa Kiswahili zinachukuliwa na Wanyarwanda, Warundi, Wakenya, Waganda na watu kutoka Afrika ya Kusini!

Inaweza kuonekana kama matani, lakini jinsi hali inavyo kwenda, tunaweza kujikuta watanzania tunakwenda nchi za nje au za jirani kama Rwanda, Burundi au Kenya, kujifunza Kiswahili! Tumeshindwa kufundisha elimu ya sekondari kwa Kiswahili, watakaotutangulia kufanya hivyo, watatufundisha! Hii itatudhalilisha na kushusha kiburi chetu ambacho tumekuwa nacho siku zote kwamba Tanzania ni mama wa Kiswahili!

Kazi iliyombele yetu, kazi ambayo ni ya kila Mtanzania, ni kuishinikiza serikali kutunga sheria ya kukitangaza Kiswahili kama lugha ya taifa. Shinikizo hili liendelee hadi Kiswahili iwe lugha ya kufundishia elimu ya sekondari na vyuo vikuu. Shinikizo hili liendelee hadi serikali ifanye mpango maalum wa kuwaandaa walimu wa lugha. Vijana wenye vipaji vya lugha, wafundishwe Kiswahili vizuri, maana mtu anayekifahamu Kiswahili vizuri ndiye anayeweza kujifunza kwa haraka lugha za kigeni na kuzifundisha kwa Waswahili, vijana hawa wakihitimu mafunzo ya Kiswahili, watumwe nchi za nje kujifunza lugha za kigeni, kama Kiingereza, Kifaransa, Kijapani, Kichina nk., wakirudi wafundishe lugha hizi kwenye sekondari na vyuo. Hii ndiyo njia peke yake ya kukiendeleza Kiswahili kwa kasi inayokubalika na kuendelea kuilinda Tanzania, kuwa mama wa lugha ya Kiswahili!

Na,
Padri Privatus Karugendo.

PADRI KULAWITI

MAKALA ILITOKA KATIKA GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2005.


TUNAJIFUNZA NINI KUTOKANA NA TENDO LA PADRI LA KULAWITI?

Wachambuzi wa mambo ya kanisa, hapa Tanzania, wanajua fika jinsi Askofu Kilaini, anavyojitahidi kulitetea kanisa hata pale ambapo mambo ni wazi kiasi cha kueleweka hata kwa mtoto mdogo. Kwa mfano Askofu Kilaini, anapinga matumizi ya KONDOMU, kwa kusisitiza kwamba, mtu anayeugua ugonjwa wa kisukari ni lazima kuacha kutumia sukari, mwenye matatizo ya ugonjwa wa miguu, ni lazima kuacha kula nyama ya mbuzi, hivyo na mgonjwa mwenye virusi vya UKIMWI, ni lazima kuacha tendo la ngono!

Mungu, kwa kutaka kuonyesha ukweli, Padri wa kanisa katoliki, amefanya kitendo cha kulawiti katika Diocese iliyo chini ya uongozi wa Askofu Kilaini, Jimbo Kuu la Dar-es-Salaam. Hili ni pigo kubwa na ni fundisho. Ni wazi kama kawaida yake Askofu Kilaini, atajitahidi kupuuzia tukio hili, lakini nguvu zake za kuufunika ukweli zimepungua! Sasa ni wazi kwa watanzania wote kwamba kuwanajisi watoto si tatizo la Wazungu peke yao, kama alivyokuwa akidai Askofu Kilani, ni tatizo la kibinadamu. Ndoa za mashoga si tatizo la kanisa la Agilikana peke yake, ni tatizo la dunia nzima. Pia tukio hili la padri kulawiti, limekuwa fundisho kwa Askofu Kilaini, kwamba kuachana na tendo la ngono si rahisi hivyo kama yeye anavyofikiri na kufundisha. Kama padri wake amefikia hatua ya kufanya ngono kinyume cha maumbile, itakuwaje kwa watu ambao ngono ni sehemu ya maisha yao, ni kitulizo, ni furaha, ni ubinadamu na ni msingi wa uhusiano kati ya mtu na mtu?

Watanzania wamemzoea Askofu Kilaini, Kashifa ikilikumba Kanisa Katoliki, wanafahamu majibu yake hata kabla hajaongea. Sasa hivi karibu kila mtu , Mkristu na asiyekuwa Mkristu, hata na mtoto mdogo, anajua atakavyosema juu ya Padri aliyelawiti: Kwamba hilo ni tatizo la mtu mmoja na wala si tatizo la kanisa zima! Kanisa haliwezi kufanya makosa! Au kwamba makosa ya kanisa ndio yanalifanya kuendelea kuwepo hadi leo hii!

Tumemsikia Askofu Kilaini, akisema kwamba Padri aliyelawiti, amesimamishwa kutoa huduma za kiroho na kuendesha ibada. Kwa maneno mengine amepata adhabu na kuwajibishwa. Lakini adhabu hii haimsaidii padri huyu, haimsaidii kijana aliyelawitiwa, haisaidii familia ya padri na kijana zilizoumbuliwa na kuathiriwa na tukio hili la aibu na wala adhabu hii haiwasaidii waumini waliokwazwa na kitendo hiki. Padri anahitaji msaada wa kiroho na wala si adhabu. Kijana aliyelawitiwa anahitaji pia msaada wa kiroho na kiakili ili kumrudisha katika hali ya kawaida. Familia za pande zote mbili zinahitaji msaada wa kiroho, kiakili na kiimani. Waumini wote na wale wote walioguswa na tukio hili kwa namna moja ama nyingine ni lazima washirikishwe katika mchakato wote wa kutibu makovu ya aibu hii ili kurudisha imani na utulivu wa kiroho katika jamii yetu.

Hatuwezi kusema tabia hii ya padri huyu aliyemlawiti mtoto, imenyesha kama mvua. Tunasikia uhusiano wake na huyo kijana ni wa miaka mitatu. Tunaamini padri alikuwa akiungama dhambi hii kwa mapadri wenzake. Swali ni je mapadri hawa walimsaidia vipi au walikuwa wanafanya kazi ya kusafisha dhambi na kumpatia baraka kuendelea na tabia yake ya kulawiti. Walikuwa wanafanya kazi ya kumruhusu padri afumbue mdomo wake na kusema yaliyo moyoni mwake wakati wao wanaifumba midomo yao na kuzifunga roho zao?

Binafsi siwezi kumlaumu padri huyu. Ametenda kosa lenye heri. Ametusaidia kugundua udhaifu ulio katika jamii yetu. Ametusaidia kutambua madhara ya upweke katika jamii na katika kanisa. La msingi ni je tumejifunza nini na tufanye nini ili tukio kama hili lisitokee tena. Tunafanya nini kumsaidia padri wetu na kijana aliyelawitiwa. Hili lililomkuta padri linaweza kumtokea kila mtu – hakuna shujaa wa kuweka kifua mbele kwamba hawezi kuguswa na hili lililompata padri wetu. Kama si kulawiti, mtu atafumaniwa, atanyanyasa watumishi wa kike, atakuwa na kibustani au kuiingilia ndoa za watu.

Badala ya kumsimamisha kazi, kumlaani na kumtupa kwenye shimo la wenye dhambi, padri wetu, ni bora tuanze kutafakari kwa kina juu ya Uhusiano wa mtu na mtu. Jambo hili linachukuliwa kijuu juu tu na wala hakuna jitihada za pekee zinazofanyika kulifundisha na kuliishi kwa pamoja kama jamii.

Uhusiano wa mtu na mtu unaanzia wapi na kukomea wapi? Je, unaweza kuhusiana na mtu kiakili bila kuhusiana naye kiroho? Je, unaweza kuhusiana na mtu kikazi bila kuhusiana naye kiakili na kiroho na bila kugusa hisia zozote mwilini mwako? Je, unaweza kuhusiana na mtu kimichezo bila kuhusiana naye kiakili, kiroho na bila kuamsha hisia zozote za kimwili? Je, unaweza kujifunua wazi kwa mtu, ukamweleza furaha yako, matatizo yako, matumaini yako na siri nyingine za moyo wako, bila kuguswa au kuamsha hisia za aina yoyote ile mwilini mwako? Je mipaka ya uhusiano ni ipi? Inawekwa na nani na inalindwa na nani? Na ni kwa nini kuwepo mipaka katika uhusiano? Je, mtu binafsi anaweza kujiwekea mipaka ya uhusiano na kuilinda au ni lazima asaidiwe na jamii inayomzunguka?

Tuchukue mfano wa padri wetu aliyeanguka kwenye tendo la kulawiti. Je uhusiano wake na huyo kijana ulianza ukiwa hivyo tangia siku walipokutana siku ya kwanza? Au walianza polepole, kwa kuhusiana kikazi, kimichezo kiakili na kiroho na hatimaye kimwili? Je, haiwezekani kwamba upweke wa padri ndio ulimsukuma kushindwa kuweka mpaka wa uhusiano kati yake na huyo kijana?

Au tukiangalia upande wa ndoa. Kile kinachoitwa uaminifu katika ndoa, ni hali ya wanandoa kujenga mipaka ya uhusiano kati yao na watu wengine wanaowazunguka. Maana mtu akiolewa au kuoa, anaendelea kuhusiana na watu wengine katika jamii inayomzunguka. Atakuwa na uhusiano na wafanyakazi wenzake, wanamichezo wenzake, wanakikundi wenzake, marafiki wenzake nk. Hoja ni je anaendelea kuhusiana nao kwa kiasi gani? Ugumu unaojitokeza hapa ni kuendeleza uhusiano bila mvuto, na kama mvuto ukitokea usiambatane na kitendo. Kwa maneno mengine ni kuendeleza uhusiano na watu wengine nje ya ndoa, bila kuvunja uaminifu wa ndoa.

Uhusiano wa mtu na mtu kiakili, kiroho, kikazi, kichama, kiurafiki nk. bila kuvunja uaminifu, bila kushirikisha sehemu zote za mwili, mikono, miguu, midomo na nyeti nyingine ni kitu kigumu ambacho mtu binafsi hawezi kukimudu. Uhusiano wa mtu na mtu ni lazima ulindwe na jamii nzima. Wale wanaojaribu kufanya kitu hiki bila kuishirikisha jamii, wanakwama. Mfano ndoa zile ambazo wanandoa wanajifungia kwenye ndoa yao, bila ya kuwa na washauri, bila kuyaweka matatizo yao wazi mbele ya ndugu na jamaa wa karibu au mbele ya waumini wenzao, wanaingia matatani. Ndoa ambazo zinatawaliwa na upweke, zinaingia matatani!

Tutake tusitake, ni lazima mtu ahusiane na watu wengine. Na watu hawa hawana mwisho, kwa maana kusema, sasa hesabu aliyonayo mtu inamtosha. Mungu, anaendelea kuumba, na mwanadamu ana tabia ya kuhama kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine, na kila sehemu kuna watu wapya, wenye akili mpya, roho mpya na mvuto mpya, hivyo mahusiano na watu hayakomi hadi mtu anapoingia kaburini.

Matatizo yanayojitokeza katika jamii yetu ya watoto wa mitaani, ndoa kuvunjika, ukosefu wa uaminifu katika ndoa, nyumba ndogo, vibustani, changudoa, ushoga, usagaji, kulawiti, kutoa mimba, UKIWMI na matumizi ya kondomu, chimbuko lake ni Uhusiano wa mtu na mtu!

Msaada mkubwa ni kutengeneza mifumo ya kijamii inayoruhusu mijadala ya pamoja. Mijadala ambayo kila mtu anaweza kutoa mawazo yake, wasiwasi wake, udhaifu wake na mchango wake katika kuwasaidia wengine. Tunahitaji kutengeneza mifumo ya kuufukuza upweke mioyoni mwa watu, kuufukuza upweke kwenye ndoa, kwenye familia na kwenye jamii nzima. Bila kufanya hivyo tutamezwa na matatizo haya yanayojitokeza. Mwenye masikio na asikie!

Na,
Padri Privatus Karugendo

KISWAHILI NI LUGHA YA AFRIKA

MAKALA HII ILITOKA KAIKA GAZETI LA RAI 2005

KISWAHILI NI LUGHA YA AFRIKA

Kiswahili ni kati ya lugha nne za taifa la DRC. Rais wa DRC, Joseph Kabila, anaongea Kiswahili sanifu. Kwa vile rais wa nchi anaongea Kiswahili sanifu, hii itakuwa chachu ya kukiboresha Kiswahili cha DRC, na kukieneza kwenye nchi zinayoizunguka DRC, kwa upande wa kaskazini. Kiswahili ni lugha ya taifa la Tanzania, Uganda na Kenya. Ingawa Kiswahili, si lugha ya taifa la Rwanda na Burundi, lakini vita vya maziwa makuu vimekifanya Kiswahili kuzungumzwa karibu na watu wote wa Rwanda na Burundi. Mipango iko mbioni kukifundisha Kiswahili kwenye shule za msingi za Rwanda na Burundi. Msukumo huu unatokana na nchi hizi mbili kuomba kujiunga na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.

Kwenye miaka ya themanini, Kenya ilifanya jitihada nyingi kukiendeleza Kiswahili. Kiswahili lilifanywa somo la lazima kwenye shule za sekondari. Matokeo yake yameanza kujitokeza miongoni mwa kizazi kipya cha Kenya, kwa kuongea Kiswahili sanifu kuliko kile Kiswahili cha kizazi cha miaka ya nyuma. Pia ongezeko la vyuo vikuu nchini Kenya vimeongeza ufanisi wa Kiswahili, kila mwaka zaidi ya vijana 2000 wanaokifahamu vizuri Kiswahili wanahitimu vyuo vikuu. Hii itachangia kuwapata walimu wazuri wa kufundisha lugha ya Kiswahili na wataalamu wazuri wa lugha ya Kiswahili. Ingawa magazeti ya Kiswahili hayajaongezeka kwa kasi kubwa, lakini uchapishaji wa vitabu vya Kiswahili uko juu zaidi nchini Kenya kuliko Tanzania. Kenya inatoa vitabu vingi vya Kiswahili na usambazaji wake ni mzuri kuliko wa Tanzania. Pia Wakenya wanasoma vitabu kuzidi watanzania. Bidii ya Kenya, katika kukikuza Kiswahili itachangia kwa kiasi kikubwa kuieneza lugha hii katika nchi zinazopakana nayo upande wa kaskazini, kama vile Somalia, Sudan na Ethiopia. Tukizingatia kwamba wakimbizi wengi kutoka katika nchi hizi wamekuwa wakiishi nchini Kenya. Hizi ni dalili za kukipanua Kiswahili kuwa lugha ya Afrika nzima!

Tofauti na Tanzania, ambapo Kiswahili, karibu kinatumika kila sehemu katika jamii, Kenya Kiswahili kinatumika kama lugha ya siasa, dini na wasomi. Ingawa hii inaonyesha picha hasi ya kukiendeleza Kiswahili katika jamii nzima ya Wakenya, lakini pia kwa njia hii Kiswahili kinaweza kuongeza kasi ya kuongea lugha ya kisayansi na kiteknolojia na kujikita katika utandawazi kwa haraka zaidi ya Tanzania.

Kwenye miaka ya Sabini, Iddi Amin, alikitangaza Kiswahili kuwa lugha ya taifa ya Uganda. Lakini waganda na hasa “Baganda” hawakukipokea Kiswahili kwa vile wanaipenda sana lugha yao ya “Luganda”. Sababu nyingine ni kwamba wanajeshi wa Iddi Amin, walitumia Kiswahili kama lugha ya jeshi. Matendo maovu ya jeshi la Iddi Amin na mauaji yaliyofanywa na jeshi hilo, yalikipaka matope Kiswahili na kuwafanya watu wa Uganda, kukichukie. Pia waganda walimchukulia mtu anayeongea Kiswahili kuwa ni “Mswahili” mjanja mjanja na mtu asiyeaminika. Lakini pia waganda wengine walikihusisha Kiswahili na Uislamu, maana Waislamu walikitumia kama lugha ya dini kwa kukichanganya Kiswahili na Kiarabu, au kutafsiri Kiarabu katika kistahili. Kwa nchi kama Uganda, ambayo imepitia migongano na michafuko mikubwa ya kidini, kujifunza Kiswahili ilikuwa ni sawa na kuamsha vita kati ya Wakristu na Waislamu.

Jeshi la Museveni, na Museveni mwenyewe walitumia Kiswahili. Hadi leo hii Kiswahili ni lugha ya jeshi la Uganda. Hii haikuwavutia waganda waliokuwa wamechoka na utawala wa kijeshi. Hivyo Kiswahili ilibaki ni lugha ya jeshi na biashara ya magendo kati ya Uganda, Tanzania na Kenya.

Kwa sababu ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, ambayo waganda wanaiona ina faida kubwa kuliko hasara, wameanza kuwa na hamu ya kujifunza Kiswahili. Serikali ya Uganda imepitisha kwamba kuanzia mwaka kesho Kiswahili litakuwa somo la lazima katika shule za msingi na sekondari. Huu utakuwa ni msaada mkubwa wa kukikuza Kiswahili na kukipatia picha ya kuwa lugha ya Afrika ya Mashariki na hatimaye Afrika nzima.

Kwenye makala iliyopita nilielezea jinsi Tanzania, ilivyofanikiwa kukisambaza Kiswahili nchi nzima na kuifanya lugha hii kuwa ya taifa ingawa haikutangazwa kisheria. Hivyo sirudii haya kwenye makala hii. Labda kutaja tu hapa kwamba Mwalimu Nyerere, kukubali Dar-es-Salaam, kuwa kitovu cha mapambano ya uhuru wa nchi za kusini mwa Afrika, kulisaidia kukisambaza Kiswahili katika nchi hizo za Kusini mwa Afrika.

Mpango wa IPP Media Group wa kuanzisha gazeti la Kiswahili liitwalo Afrika ya Mashariki, utakuwa mchango mkubwa katika kukifanya Kiswahili lugha pana inayoweza kukubalika Afrika nzima. Huu unaweza kuwa uwanja wa kuzua malumbano na majadiliano ya kuelekea kukikomaza Kiswahili kama enzi zile washairi wa Afrika ya Mashariki walivyokuwa wakijibizana na kulumbana katika uwanja wa ushairi. Bado kuna ushahidi wa kutosha jinsi mashairi yalivyosaidia kukikuza Kiswahili.

Vita vya ukombozi kusini mwa Afrika, vimekifanya Kiswahili isiwe lugha ngeni katika nchi za Zimbabwe, Namibia, Angola, Msumbiji na Afrika ya kusini. Lakini pia wakimbizi wa Sudan, Somalia na Ethiopia, walioishi Kenya na Uganda wamesaidia kukisambaza Kiswahili hadi kwenye nchi zao. Wafanyabiashara wa Kisomali ambao hufanya kazi ya kusafirisha mizigo kwenye magari ya mizigo kwenye maeneo yote ya Afrika ya Mashariki, Kati na kusini wamekuwa mabalozi wa kuisambaza lugha ya Kiswahili.

Ingawa kuna lugha zingine za Afrika zinazozungumzwa na watu wengi kama Kihausa. Kiswahili kinachomoza zaidi kwa sababu si lugha inayofungamana na kabila au taifa Fulani. Mfano ni tofauti na Kihausa. Ingawa Kihausa kinazungumzwa na watu wengi wa Afrika ya Magharibi, kinafungamana na kabila kubwa la Wahausa ambalo limekuwa kwenye migogoro na mapigano na makabila mengine kwa muda wa miaka mingi. Lengo lolote la kutaka kukifanya Kihausa kuwa lugha ya Afrika nzima, ni lazima litaamsha chuki miongoni mwa makabila makubwa ya Afrika magharibi ambayo nayo yangependa lugha zao zichukue nafasi ya kwanza.

Profesa Mulokozi, kwenye mada yake: “Kiswahili as a National and International Language” Anaelezea kisa alichosimuliwa na Kanyama Chiume, pale Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam, mwaka 2002; kwamba mwaka 1959, wapigania uhuru wa Afrika walikuwa na mkutano ulioitishwa na Sekou Toure, katika mji wa Conakry, Guinea, ili kupanga harakati za kudai uhuru. Mkutano huu ulihudhuriwa na watu kutoka nchi zilizokuwa zikiongea Kiingereza na Kifaransa. Tatizo kubwa lililojitokeza katika mkutano huo ni lugha ya kutumia. Wajumbe walikaa wakitafakari zaidi ya masaa mawili juu ya lugha ya kutumia katika mkutano huo ili wote waweze kusikilizana na kuchangia hoja. Waliotoka kwenye nchi zilizokuwa zikiongea Kiingereza hawakufahamu Kifaransa na wale waliotoka kwenye nchi zilizokuwa zikiongea Kifaransa hakukifahamu Kiingereza. Huu ulikuwa mtindo wa wakoloni, wakutaka kufundisha lugha zaidi ya lugha yao. Baada ya muda mrefu wa kutafakari namna ya kuendesha kikao hicho kigumu, Kanyama Chiume, ndiye aliyeokoa jahazi. Alipendekeza: Kwa vile yeye alifahamu Kiswahili na Kiingereza, na Patrice Lumumba, alifahamu Kiswahili na Kifaransa, mkutano ungeweza kuendelea kwa wajumbe waliokuwa wakitumia Kiingereza, kuongea kwa Kiingereza na Kanyama Chiume, kutafsiri yote kwa Kiswahili ili Patrice Lumumba, aweze kutafsiri Kiswahili kwa Kifaransa. Vilevile na wale wa upande wa Kifaransa waliongea kwa Kifaransa na Patrice Lumumba, alitafsiri kila kitu kwa Kiswahili ili Kanyama Chiume, aweze kutafsiri kwa Kiingereza.

Kufuatana na maelezo ya Kanyama Chiume, mkutano huo uliendelea kwa ufanisi mkubwa ingawa ulikuwa wa kuchosha. Lakini wajumbe walielewana vizuri kwa msaada wa Lumumba na Kanyama Chiume waliokuwa wakikifahamu Kiswahili. Ndiyo kusema Kiswahili kiliwaunganisha Waafrika katika mkutano huo. Na kama nilivyosema hapo juu, ni kwamba Kiswahili ni tofauti na Kihausa au lugha nyingine maana si lugha ya Kabila Fulani au taifa Fulani. Mfano katika mkutano huu wa Conakry wa mwaka 1959, Patrice Lumumba alitokea Congo na Kanyama Chiume, alitokea Malawi! Kiswahili, haikuwa lugha ya kabila la Lumumba na wala haikuwa lugha ya kabila la Kanyama Chiume. Tunaweza kusema Kiswahili ilijitokeza kama lugha ya Waafrika katika mkutano huo. Huu ulikuwa ni mwanzo mzuri, kama si uvivu na kutojali kwa watu wanaojiita chimbuko la Kiswahili, kama vile watanzania, leo hii Kiswahili, kingekuwa kimepiga hatua kubwa katika Bara zima la Afrika na duniani kote.

Mfano mwingine anautoa Profesa Mulokozi, ni ule wa mwanamapinduzi Che Guevara, wakati akiongoza harakati za mapambano ya vita vya msituni kuikomboa Congo, akiwa bega kwa bega na Laurent Kabila, alilazimika yeye na wapiganaji kutoka Cuba, kujifunza Kiswahili, hadi yeye Che Guevara, akabatizwa jina la Kiswahili la Tatu! Waligundua kwamba hii ndio lugha pekee iliyoweza kuwaunganisha Waafrika waliokuwa wakipigana msituni na kwamba adui aliyeongea Kiingereza na Kifaransa asingeweza kufuatilia nyendo zao katika mawasiliano. Che Guevara, ni mwanamapinduzi anaheshimika duniani kote na historia yake imejaa mvuto wa pekee na kati ya mvuto huu ni lugha ya Kiswahili!

Lakini kitu kinachokifanya Kiswahili kionekane kuwa ni Lugha ya Afrika, wale wanaoisukuma mbele si watu wa Afrika Mashariki na wala si watu wanaotoka kwenye nchi ambazo zinaaminika kuwa ni nchi za Kiswahili kama Tanzania na Kenya. Tumeona mfano wa Kanyama Chiume na Lumumba. Mfano mwingine ni wa Chisano kutoka Msumbiji kwenye nchi inayoongea Kireno, na lugha nyingine za Kiafrika ambazo ni kubwa pia, kuwa rais wa kwanza wa Afrika, kuhutubia Umoja wa nchi za Afrika, kwa lugha ya Kiswahili.

Mkutano wa viongozi na wataalam wa maziwa makuu uliofanyika Aprili 2002 kwa kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere, ulitoa mwito wa kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya mataifa ya maziwa makuu.

Katika miaka ya sitini Mwandishi Maarufu wa Nigeria Wole Soyinka , alitoa mwito wa kukitangaza Kiswahili kuwa ni lugha ya Afrika nzima. Nigeria, kuna lugha kubwa za Kiafrika, lakini Wole Soyinka, aliguswa na lugha ya Kiswahili! Baadhi ya vitabu vyake vimetafsiriwa katika lugha ya Kiswahili.

Mwito huu ulirudiwa tena na mwandishi mwingine wa Ghana, Ayi Kwei Armah, mnamo mwaka wa 1985, yeye alikiona Kiswahili kama lugha ambayo inaweza kuingiza maneno mengi kutoka kwenye lugha nyingine za Kiafrika na kukifanya Kiswahili kuwa tajiri kwa msamiati. Ayi Kwei Armah, aliishi na kufanya kazi Tanzania. Alifundisha kwenye Chuo cha Walimu Chang’ombe. Kitabu chake “Te Beautiful Ones Are Not Yet Born” kimetafsiri katika Kiswahili: “Wema Hawajazaliwa”.

Kiswahili kilitumika kwenye mkutano mkuu wa UNESCO, Parish, Ufaransa. Hizi ni dalili kwamba Kiswahili kinatambulika kuwa ni lugha kubwa kutoka Afrika.

Mwanzoni mwa miaka ya themanini, UNESCO iliamua juzuu nane (8-volume) za historia ya Afrika zitafsiriwe kwenye lugha zaidi ya tatu za Kiafrika, Ukiondoa Kiarabu, lugha nyingine zilizopendekezwa ni Hausa,Fulfulde na Kiswahili. Juzuu za Kiswahili zimekamilika na kuchapishwa. Huu ni mchango mkubwa wa lugha ya Kiswahili katika historia ya Afrika. Kwa wale wanaofikiri kwamba Kiswahili si lugha ya kisomi, juzuu hizi ni changamoto kubwa kwao. Na huu ni ushahidi kwamba Kiswahili ni lugha ya Afrika.

Kwa vile utandawazi unatishia kuzimeza nchi za ulimwengu wa watu na hasa Afrika, kwa karibu kila kitu, ni vyema na Afrika itafute kitu cha kuuza kwenye utandawazi. Tukishindwa kuuza vitu vingine kama utamaduni, kazi za mikono na bongo zetu, basi tuuze lugha zetu na hasa zile zinazoelekea kukubalika Ulimwengu mzima kama vile Kiswahili.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

SILAHA 100 ZA KIONGOZI

UHAKIKI WA KITABU: SILAHA 100 ZA KIONGOZI; KATI YA HIZO UNAZO NGAPI?

1. REKODI ZA KIBIBLIOGRAFIA

Jina la Kitabu kinachohakikiwa hapa ni: Silaha 100 za Kiongozi; Kati ya hizo unazo ngapi na kimetungwa na Pius B. Ngeze. Mchapishaji wa kitabu hiki ni Kampuni ya Tanzania Educational Publishers Ltd (TEPU) ya mjini Bukoba, Mkoani Kagera na amekipatia namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 978-9987-07-005-3. kimechapishwa mwaka huu wa 2008 kikiwa na kurasa 64.Bei ya kitabu hiki ni shilingi 4,000 za Kitanzania. Na anayekihakiki sasa hvi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo.

11. UTANGULIZI

Kitabu hiki cha Silaha 100 za Kiongozi, ni kati ya vitabu vitano vilivyozinduliwa na Kampuni ya Tanzania Educatinal Publishers Ltd, Mjini Bukoba hivi karibuni. Vitabu vingine ni: Ushuhuda wa Muujiza wa 11 Mei 2007, siku ambayo Mzee Pius Ngeze na viongozi wengine wa Chama na Serikali walinusurika kifo baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria kwenda Ukerewe ulipo zama katika ziwa Victoria. Vitabu vingine ni Wanyonge Wasinyongwe – kikiwa na utetezi wa biashara ya matumizi ya pikipiki na baiskeli; Mwanzo na Mwisho wa Uongozi na Maisha ya Alhaji Abubakari Rajabu Galiatano. Vitabu vyote hivyo vitafanyiwa uhakiki kwenye safu hii.

Tunaweza kusema kwamba kitabu hiki kinazo sura 100! Maana kila silaha ya kiongozi inayotajwa ni kama sura inayojitegemea. Katika aya zifuatazo nitatoa muhtasari na tathmini yake, lakini baada ya kudokeza mazingira yanayokitangulia kitabu hiki.

III. MAZINGIRA YANAYOKIZUNGUKA KITABU.

Tarehe 10/9/2007, Mzee Pius Ngeze, aliamua kung’atuka Uenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Kagera. Lakini pia hakukubali kushika wadhifa wowote katika Serikali inayoongozwa na rafiki yake wa karibu Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete. Aliamua kuachana na siasa na kuacha utumishi serikalini. Uamuzi huo uliwashangaza baadhi, maana Wazee wenye umri wake bado wanang’ang’ania kwenye utumishi Serikalini. Hawataki kustaafu! Lakini walio wengi waliupongeza uamuzi wa mzee Pius Ngeze. Maana wazee ni lazima waarithishe vijana uongozi.

Katika kitabu chake cha Silaha za Kiongozi, silaha ya 89 ni Andaa Viongozi wa Kesho: “ Viongozi wa sasa, na wewe ukiwamo, ni wa kupita tu. Si wa kudumu. Hakuna mwandamu yeyote ambaye ni wa kudumu hapa duniani. Kiongozi yeyote anaweza kuondoka uongozini wakati wowote kutokana na kifo, kujiuzuru, kufutwa uteuzi wake, kumalizika kwa kipindi cha uongozi, kutochanguliwa na kufukuzwa uongozi kutokana na kupungukiwa na sifa za kuendelea kuwa kiongozi. Kutokana na sababu hizi, kiongozi bora ni yule anayeandaa aua anayechangia maadalizi ya viongozi wa baaadaye,viongozi wa kesho. Usiandae mtu mmoja au wawili,Andaa watu wengi kwa kila aina ya nafasi. Lengo ni kuwa na benki yenye akiba ya watu wengi wanofaa kuongoza watu. Kiongozi asiyeandaa viongozi wa baadaye hafai, ni mbinafsi, ni mchoyo na ni mwoga. Si jasiri. Viongozi bora huandaliwa. Nchi yetu inahitaji viongozi walioandaliwa vizuri kushika madaraka. Shiriki kufanya kazi hiyo”. (uk 51-52)

Mawazo kama haya anayaendeleza kwenye Silaha ya 96, inayosema hivi: “ Using’ang’anie uongozi kwa kipindi Kirefu”. Anafanuua zaidi kwa kusema: “ Uongozi ni mtamu. Una heshima na marupurupu mengi. Ukishapewa uongozi,umepewa nafasi ya kuonekana, kujulikana, kusifiwa kukalia kiti cha mbele n.k. Kadiri unavyokaa katika uongozi kwa kipindi kirefu, ndivyo mambo yanavyozidi kukunogea. Lakini, ukikaa kwenye uongozi wa aina moja kwa kipindi kirefu umuhimu na umaarufu wako unapungua sana. Huna jipya. Huna mawazo mapya. Unawazoea sana watu na wao wanakuchoka……..Ushauri wangu ni, ‘Using’ang’anie uongozi kwa kipindi kirefu’. Kipindi kimoja au viwili havitoshi? Fikiria mwenyewe na amua kipindi cha kukaa uongozini”. (uk 56-57)

Mzee Pius Ngeze, ana uzoefu wa zaidi ya miaka 35 kama kiongozi wa familia yake, miaka zaidi ya 38 akiwa kiongozi kazini na miaka 33 akiwa kiongozi wa siasa nchini. Amewahi kugombea uongozi na kushinda mara sita, pia amewahi kugombea na kushindwa mara mbili. Hivyo anajua raha na faraja ya kushinda, pia, anajua masikitiko na uchungu wa kushindwa. Kwa sababu hii, ametengeneza silaha hizi za kiongozi kutokana na uzoefu alionao katika uongozi.

Mzee Pius Ngeze, ni mwandishi wa vitabu wa siku nyingi. Lakini kwa vile ameamua kutumia muda wake wa kustaafu kuendelea kuandika na kuielimisha jamii, ni ushuhuda kwamba huyu alikuwa kiongozi wa kweli.

IV. MUHTASARI WA KITABU.

Silaha 100 za Kiongozi, ni silaha za aina ya pekee na ni maalumu. Hizi ni tofauti kabisa na silaha tulizozoea kuziona au kuzisikia. Silaha hizi zimetegenezwa ili zimsaidie kiongozi kumlinda dhidi ya mashambulizi kutoka kwa “maadui” wake. Silaha zinazozungumziwa katika kitabu si zana wala vifaa, bali ni matendo, tabia na mienendo ya kiongozi. Hizi ni silaha kubwa na nzito zaidi kuliko bunduki, bastola, rungu, mishale, mikuki, mabomu na kadhalika.

Katika kitabu hiki, neno Kiongozi, linajumulisha viongozi wa familia, siasa, serikali, dini, kazi, ushirika, taasisi za serikali asasi zisizo za serikali, asasi za serikali, mashirika ya umma, makampuni na wengine. Viongozi hawa wote wanapigwa vita vya kila namna, kwa hivyo ili waendelee kuongoza wanahitajii kuwa na silaha za kujilinda. Vita hivi vinatoka kwa viongozi wenzao kwa watu wanaowaongoza na hata watu wasiowaongoza. Vita vipo na vya kweli. Asipopigana kwa kutumia silaha hizi ataangamia.

Wanachi nao (watu wasio viongozi) wanahitaji kujua silahai hizi ambazo zimetengenezwa kwa ajili ya viongozi wao. Wakizijua watakuwa wameeelewa mambo ya kutegemea kutoka kwa viongozi wao.

Silaha zote kuanzia ile ya kwanza ambayo ni Jitambue, hadi ya mwisho ya 100 ambayo ni: Usiwe mwoga na uwe na moyo mgunu, ni muhimu sana kwa kingozi.

Hata hivyo kuna ambazo zinagusa sana kama ile ya 43: Usiwe mtu wa kulipa Kisasi. Baadhi ya viongozi wanapenda kulipa kisasi, na jambo hili lina kwamisha maendeleo: “ Kisasi ni nia au kusudio la kulipiza ubaya aliofanyiwa mtu. Hupashwi kulipa kisasi. Ukifanya hivyo wewe si kiongozi. Kuudhiwa, kukosewa, kudharauliwa, kutukanwa, kusingiziwa, kuandikwa vibaya magazetini n.k. ni mambo ya kawaida kwa kiongozi….” (27-28).

Nikizitaja zote, nitamaliza utamu wa kitabu chenyewe. Kinunue upate uhondo na kuelimika. Lakini hii hapa ni muhimu na siwezi kuacha kuitaja:-

Silaha ya 23: Uwe Mbunifu, Mwanamikakati, Manaharakati na mwenye mawazo mapya, pamoja na mambo mengine inasema hvi: “ Kiongozi lazima uwe mbunifu mwenye mikakati, mwanaharakti na mwenye mawazo mapya. Haiwezekani wewe ukawa ni wa kutekeleza mikakati, mbinu na mawazo ya w atu wengine tu. Ya kwako yako wapi? Je, utakumbukwa kwa lipi? Utasifiwa kwa lipi? Utalaumiwa kwa lipi?.........”( Uk 17)

V. THAMINI YA KITABU

Baada ya kuona muthasari huu sasa tufanye tathmini ya kazi hii aliyofanya Mzee Pius Ngeze.

Awali ya yote lazima nisema kwamba kwa kuangalia hadhira anayoikusudia, kitabu hiki kinasisimua sana kutokana na mtindo alioutumia wa kutaja kila silaha ya kiongozi na kuielezea. Kila kiongozi atajipima na kuona kati ya silaha hizi 100 za uongozi yeye anazo ngapi? Inawezekana mwingine akaongezea ya 101! Kuzipunguza ni vigumu, maana mwandishi amechimba kweli.

Pili, ni wazi kamba mwandishi amefanikiwa kutimiza lengo lake, yaani kuzitaja zilaha zote 100 kuzitolea maelezo kwa kuzingatia uzoefu wake mwenyewe na uzoefu wa viongozi mbali mbali. Kila kiongozi atakayekisoma kitabu hiki atajipima na kujichambua.

Tatu, mwandishi amefanikiwa kukifanya kitabu chake kiwe cha kuaminika kwa kutoa mfano wake yeye mwenyewe wa kuamua kuacha uongozi ili na vijana waweze kuendeleza uongozi. Alikuwa bado anapendwa, kama angeombea angechaguliwa. Rafiki yake Mheshimiwa Rais Jakaya Kiketwe, angeweza kumpatia kazi hata ya kuwa Mkuu wa Mkoa Lakini aliamua kustaafu ili apate nafasi ya kuandika na kuielimisha jamii.

Nne, Mwandishi wa kitabu hiki ambaye ndiye Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Tanzania Educational Publishers Ltd, alifanya jambo la maana kukizindua kitabu hiki na vingine kwa halfa iliyohudhuriwa na viongozi wa madhehebu ya dini mbali mbali, serikali na chama cha CCM, waandishi wa habari na wasomaji wa vitabu wa rika zote wakiwemo pia wanafunzi kutoka baadhi ya shule za sekondari zilizomo katika Mkoa wa kagera. Kwa njia hii anatangaza vitabu na kuwashawishi watu kupenda kusoma vitabu ili kujipatia maarifa.

Hata hivyo, mwandishi na wengine wenye nia ya kusambaza usomaji wa vitabu hadi vijijini bado wana changamoto kubwa. Vitabu havifiki vijijini, lakini hata vikifika huko, maisha ni magumu. Mtu ataamua kununua mafuta ya taa, sukari na chumvi badala ya kununua kitabu. Lazima Serikali ifanye mpango maalum wa kusambaza vitabu vijiji.

VI. HITIMISHO.

Kwa kuhitimisha basi, kwa upande mmoja ,nawashauri viongozi wote wakitafute kitabu hiki na kukinunua. Kitawasaidia sana katika kazi zao za kila siku. Busara, hekima na uzoefu ulio kwenye kitabu hiki utawasaidia kuwa viongozi bora na kuleta maendeleo katika taifa letu.

Lakini kwa upande mweingie namwomba mwandishi wa kitabu hiki kufanya jambo moja zaidi la kufanya ushawishi miongoni mwa viongozi wa serikali, viongozi wa dini, viongozi wa mashirika na wafanyabiashara, kuanzisha vituo vya kusoma vitabu vijijini na kuviiimarisha. Kwa njia ya kusoma vitabu, tunaweza kusamba elimu nchi nzima na kwa njia hii kuharakisha maendeleo ya taifa letu la Tanzania.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

MWANZO NA MWISHO WA UONGOZI WA KISIASA

UHAKIKI WA KITABU: MWANZO NA MWISHO WA UONGOZI WA KISIASA.

1. REKODI ZA KIBIBLIOGRAFIA

Jina la kitabu kinachohakikiwa hapa ni Mwanzo na Mwisho wa Uongozi wa Kisiasa na kimetungwa na Mzee Pius B. Ngeze. Mchapishaji wa kitabu hiki ni TANZANIA EDUCATIONAL PUBLISHERS LTD (TEPU) na amekipa namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 978-9987-07-010-7. Kimechapwa mwaka huu wa 2008 kikiwa na kurasa 46. Na anayekihakiki sasa katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo.

II. UTANGULIZI.

Kitabu hiki Mwanzo na Mwisho wa Uongozi wa Kisiasa ni kati ya vitabu vitano vilivyozinduliwa na Kampuni ya Tanzania Educatinal Publishers Ltd, Mjini Bukoba hivi karibuni. Vitabu vingine ni Silaha 100 za Kiongozi , Wanyonge Wasinyongwe , Ushuhuda wa Muujiza wa 11 Mei 2007 na Maisha ya Alhaji Abubakari Rajabu Galiatano ambavyo tiyari nimevifanyia uhakiki .Vitabu hivi vinapatikana kwenye duka la TEPU na Upendo Nyumba ya Kulala wageni, Bukoba mjini. Dar-es-salaam, vitabu hivi vinapatikana Duka la TEPU lililopo makutano ya Mitaa ya John Rupia na Uhuru, Kariakoo.

Mwanzo na Mwisho wa Uongozi wa Kisiasa ni kitabu chenye hotuba tatu za mmoja wa wanasiasa wakongwe nchini. Naye ni ndugu Pius B. Ngeze aliyeongoza Chama Cha Mapinduzi katika Mkoa wa Kagera akiwa Mwenyekiti wa mkoa huo kwa miaka 25. Zimo pia makala za mahojiano na maoni ya magazeti kadhaa nchini. Hivyo kitabu hiki kinazo sura 8 na picha za Mwandishi na za matukio mbali mbali katika uongozi wake wa Kisiasa. Katika aya zifuatazo nitatoa muhtasari na tathmini yake.

III. MUHTASARI WA KITABU.

Hotuba ya kwanza ni ile ya kuwashukuru wajumbe waliomchagua kwa mara ya kwanza Septembe 21, 1977.
Inaonyesha jinsi alivyoanza safari yake ya uongozi akizingatia “Ushirikishwaji” wimbo ambao leo hii unaimbwa na kila mmoja na ndilo hitaji la wakati tuliomo:

“Kazi ya Uenyekiti wa Mkoa, hasa Mkoa huu wa Ziwa Magharibi,ni nzito na ngumu. Kwa sababu hiyo, nahitaji kuanzia sasa hivi ushirikiano wenu na viongozi wengine wa Chama, Serikalini, Mashirika ya Umma, Madhehebu ya Dini na wananchi wote kwa ujumla” (Uk 4).

Hotuba ya pili ni ya kuaga Uenyekiti huo Oktoba 18,1997 na ya tatu ni ya Kuaga na Kung’atuka Uenyekiti wa Mkoa Septembe 10 2007 baada ya kuwa amerejea uongozini mwaka 2002.

Sura ya tatu ni habari iliyoandikwa kwenye gazeti la Rumuli, Februari, 2007: Ngeze Atangaza Kustaafu Uongozi.

Sura ya nne ni habari iliyoandikwa kwenye gazeti la Mtanzania,20 Machi, 2007: Ngeze Ang’atuka CCM.

Sura ya tano, ni habari iliyoandikwa kwenye gazeti la RAI, Aprili 5-11,2007: Ngeze Aionya CCM na Fedha za Shetani: “ Mkongwe katika siasa za nchi yetu na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi mkoani Kagera, Pius Ngeze, amevionya vyama vya siasa nchini kuachana na mtindo wa kuombaomba fedha badala yake vibuni miradi yake kwani katika ombaomba vinaweza kupokea fedha za shetani…” (uk 22).

Sura ya sita ni Mahojiano ya Pius Ngeze na Bw. Elia Mbonea, Mwandishi wa Habari, Gazeti la Rai, Aprili 5-11-2007: Ngeze, akisema “ Ninataka kupumzika, ni safari ndefu..” (Uk 25).

Sura ya saba ni maoni ya Mhariri, Gazeti la Mtanzania, 5-11 Aprili, 2007: “Wengine wanasubiri Nini Kung’atuka?”: “….Tunachukua fursa hii kuwapongeza Ngeze na Ndejembi, kwa uamuzi wao wa busara. Uamuzi wa kung’atuka kwa hiari, unawajengea heshima kubwa mbele ya umma. Daima wataendelea kuheshimiwa, na kwa hakika ushauri wao utapokelewa na kutekelezwa na wale waliowaacha madarakani. Raha ya kung’atuka kwa hiari tumeiona kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, pale alipoamua kuacha urais, na baadaye uenyekiti wa CCM..” (Uk 31).

IV. TATHMINI YA KITABU.

Kama tulivyoona kwenye vitabu vilivyotangulia, Mwandishi amefanikiwa sana kuweka uzoefu wake wa uongozi kwenye maandishi. Huu ni msaada mkubwa kwa kizazi cha leo na vizazi vijavyo.

Mwandishi amefanikiwa pia kutufundisha kwamba “ Kilichoandikwa, kimeandikwa”. Kumbukumbu itabaki. Watakuja kusoma na kujifunza.

Lakini pia, mwandishi anatufundisha juu ya hitaji la kujenga utamaduni wa kung’atuka. Kwamba wazee warithishe vijana. Wazee wengi wamekuwa na tabia ya kutotaka kuongodoka madarakani, hadi wengine wanaondolewa kwa aibu ya kukataliwa kwa kura.

Lakini, pia fundisho jingine ni kujenga utamaduni wa kusoma vitabu kwa kuandika vitabu. Daima tunasema watanzania hawana utamaduni wa kusoma. Watasoma nini kama hatuandiki vitabu? Badala ya kusoma mambo ya nje, tunaweza pia kusoma ya hapa nyumbani, kama vile kusoma maisha Ya Ngeze, Mzee Alhaji Abubakari Rajabu Galiatano na wengine wengi.

V. HITIMISHO.

Kwa kuhitimisha, napenda kuendelea kuwashawishi watanzania kukitafuta kitabu hiki na kukisoma. Na msisitizo ninauweka kwa viongozi na wale wanaotaka kuwa viongozi. Kitabu hiki kitawasaidia sana.

Kwa upande mwingine, ningemshauri Mwandishi, kuandika zaidi juu ya Mchango wa wanawake katika uongozi wa Taifa letu na pia mchango wa wanawake katika uongozi wake. Kwenye orodha ya mwandishi ya watu karibia 30 waliomlea kisiasa, anatajwa mwanamke mmoja! Mama Kandika Kitu! Nina mashaka na hili. Nafikiri wako wanawake wengi lakini hawatajwi! Tukizingatia kwamba mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Kagera, aliyepokea kijiti kutoka kwa Pius Ngeze, ni mwanamke, ni lazima mchango wao si haba!

Lakini pia kuna Wanawake Mashuhuri katika Mkoa wa Kagera na taifa kwa ujumla ambao mchango wao katika uongozi na maendeleo ya taifa letu umesahaulika. Kuna akina mama walioujenga Mji wa Bukoba, kuna akina mama waliowasomesha baadhi ya wasomi wa Bukoba, kuna akina mama waliowazaa na kuwaleea watu mashuhuri wa Kagera. Hawa noa kuna umuhimu wa kuandika historia ya maisha yao. Kwa vile Tanzania Educational Publishers LTD, ina mpango wa kuandika Maisha ya watu mashuhuri wa Mkoa wa Kagera, watakumbuka na wanawake pia.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

MWANDISHI ELIESHI LEMA

MWANDISHI ELIESHI LEMA.

Nimekuwa nikifanya uhakiki wa vitabu mbali mbali vya mwandishi Elieshi Lema. Mama huyu amejitokeza kuwa mwandisi mzuri wa vitabu vya watoto na watu wazima. Vitabu vyake ambavyo nimefanyia uhakiki hadi sasa hivi ni Parched Earth, Freshi na Maisha, kitabu cha kwanza hadi cha nne, Mkate Mtamu, Mwendo na Wanawake wa TANU. Wale waliofanikiwa kusoma uhakiki wangu, waliweza kutambua mchango wa mama huyu katika jamii yetu. Ubunifu wake wa kuandika hadithi za watoto kwa lengo la kufikisha ujumbe mzito kwa watoto ni jambo la kusifia.

Uchambuzi wangu na uchambuzi unaofanywa na watu wengine juu ya vitabu vya Elieshi Lema, au vitabu vya waandishi wengine unatoa mwanga wa kitabu, lakini wakati mwingine inakuwa vigumu kugusa kikamikilifu alicholenga kuandika mwandishi. Mara nyingi mahojiano na mwandishi wa kitabu yanasaidia kuongeza mwanga.

Mnamo mwaka 2000, Elieshi Lema, alifanya mahojiano na Mwalimu wa Kiswahili Irmi Hanak, kutoka Vienna Austria, juu ya vitabu vyake viwili: Safari ya Prospa na Mwendo. Mahojiano yalifanyika kwa lugha ya Kiswahili na kiingereza na baadaye kutafsiriwa kwa Kijerumani na Mwalimu Irmi Hanak.

Nilishafanya uhakiki wa Mwendo, kwenye safu hii ya Kisima cha Ujuzi. Na siku za hivi karibuni nitafanya uhakiki wa Safari ya Prospa. Kwa faida ya wasomaji nieleze kwa kifupi juu ya vitabu hivi viwili: “Safari ya Prospa” ni hadithi ya mtoto wa miaka kumi hivi anayeondoka
nyumbani ili kumtafuta mpwa wake Merisho aliyepotea. Anasafiri mpaka
Dar-es-Salaam akiwa peke yake. Anapata msaada kutoka kwa watoto mitaani,
hasa kwa msichana Sara anayemkuta njiani. Mwishoni wanafaulu kumpata
Merisho na kumrudisha kwa mama yake.

“Mwendo” ni hadithi ya msichana wa miaka kumi na minne. Felisia anaondolewa
shuleni na wazazi wake ili achezwe kufuatana na mila ya Kimakonde.
Walimu wa Felisia wanashindwa kufahamu. Felisia mwenyewe anahofu, kwa
vile alisikia hadithi ya kutisha ya wasichana waliotahiriwa.
Lakini Shangazi Helena Margareta ambaye ni mtu bila woga anaondoa wasiwasi
wake na kumsindikiza katika njia yake. Anaeleza wazi kwamba ni mila
yenye faida tu inayofaa kufuatwa na kuendelezwa. “Sitakubali kamwe mwili
wangu uguswe na mtu ye yote bila ya idhini yangu” ni ujumbe wake muhimu
kwa Felisia.
Mwishoni Helena Margareta anawakabili walimu wa shule wanaokataa Felisia
arudi darasani baada ya kutofika shuleni kwa miezi kadhaa.

Sasa tumsikilize Elieshi, mwenyewe anavyosema juu ya vitabu vyake. Nimeaandika habari hii kwa kusaidiwa na Internet na maongezi na Elieshi mwenyewe:
Swali: Irimi Hanak: Kitu gani ni muhimu zaidi katika kuandika vitabu kwa watoto au vijana?

Jibu: Elieshi Lema: Kuandika hadithi kwa watoto – kitu kimoja ambacho ni
muhimu sana – lazima uwapende watoto, na ukishawapenda, unawatazama na
ukiwatazama, unajaribu kuwaelewa ni kwa nini wanafanya hivi, ni nini
kinachowafurahisha, nini kinachowasikitisha, kwa hiyo unaweza ukajiingiza
katika nafsi yao na wewe mwenyewe ukawa mtoto.
Kwa hiyo ndivyo hivyo unaweza kuandika kitabu cha watoto, wakaonekana
kweli watoto walio ndani, na wahusika wako ukawachora kama watoto, na
siyo kama mtu mzima anayezungumza kuhusu watoto.

Swali: : Irimi Hanak: Kabla ya kuandika kitabu cha Safari ya Prospa, ulifanya utafiti mrefu. Ulichunguza nini hasa katika utafiti huo?

Jibu: Elieshi Lema: Vyote viwili nimefanya utafiti, “Mwendo” ndiyo nimefanya utafiti wa muda
mrefu zaidi. Utafiti wa “Safari ya Prospa” ulikuwa rahisi. Kwa sababu
nilitaka kufahamu anapitia wapi, na pale anapopitia, wana utamaduni wa
namna gani. Kwa sababu „Safari ya Prospa“, mtoto anatazama sana jamii,
anasikiliza, anauliza ni kwa nini. Kwa hiyo jamii inatathminiwa na mtoto.
Kwa hiyo ni lazima ufanye utafiti, ili ujue hiyo jamii ikoje, na mtoto
anapoona vitu vya namna hii, anafikiria nini, kwa mfano askari anauliza
maswali, anasema “Haya nitakwenda kufanya utafiti”, askari anachukua muda
wake.

Yeye mtoto (Prospa) anaona “A-a, mtoto amepotea, huyu atachukua muda
mrefu kiasi gani, mpaka apate mtoto.“ Kwa askari, kuna urasimu. Hatafanya
utafiti kwamba mtoto amepotea, huku aliko anaweza akaumia, sijui .. Aa,
urasimu, lazima njia fulani zifuatwe. Kwa hiyo unafanya utafiti wa vitu vyote
hivyo, halafu unajua ile jamii ikoje, na huyo mtoto anapokuja, anaitazama ile
jamii na kuitathmini, anatazama vitu gani. Huu ndiyo ulikuwa utafiti wa
“Safari ya Prospa”. Na kwa vile walifika mpaka Zanzibar, ilibidi nijue
Zanzibar ikoje, na watu wakoje, na ni vitu gani muhimu kwao, na hivyo mtoto
akienda, ataona vitu vya namna gani.

Swali: : Irimi Hanak: mimi kama msomaji nafikiri ule mtazamo wa mtoto ndiyo muhimu sana, unasema nini juu ya hili?
Jibu: Elieshi Lema: Ni muhimu kwa sababu mara nyingi, hatuna subira kwa watoto, hatuna subira
kabisa, tunasema “We mtoto acha utundu” Hatujajua, hatujamwuliza ni kwa
nini unafanya hivi. Au “Nieleza unajisikiaje.” No. Tunaingia tu, tunahukumu,
tunatoa ama ni adhabu au ni sifa au ni nini. Sasa watoto wanatuonaje,
wanatazama hiyo jamii, wanaona “Nyie watu wa ajabu kweli”
Nilitaka mtoto apotee, yule mtoto anapopotea, Prospa, kila anapopita,
anatathmini, anauliza, anafanya uamuzi, na kwa hiyo ule uamuzi
unamwendesha. Halafu Prospa anakutana na Sara. Sasa unajua mambo ya
jinsia pale, yanajitokeza yenyewe tu kwa mitazamo yao wenyewe, kwa
mitazamo yao wenyewe watoto. Na siyo kusema - Prospa hana uamuzi kamili
juu ya Sara kama mtoto wa kike... Lakini anauliza maswali ambayo Sara
anamjibu, na wakati wenzake wanapokuja kumwambia “Aa msichana hawezi
kufanya chochote, msichana yule atasema tu”, Prospa anasema “ Hata, no,
mimi sana namwamini, hawezi kusema“, unaona, ameshafanya utathmini
wake mwenyewe, kwa kutembea na Sara, na kumwona anavyofanya vitu,
anavyofanya uamuzi. Si kwamba ni rahisi, wanagombana wakati mwingine,
na Sara anamshinda kabisa, na „agh huyu mbona siwezi kumshika, siwezi
kumcontain“.

Huyu ni mtoto. Mtoto akifanya vitu, isiwe ni mimi mtu mzima nizungumze
kwa niaba ya mtoto. Mtoto anaonaje jamii, na kwa hiyo tafsiri yake ya jamii
inakuwaje? Mtoto anaonaje jinsia, na kwa hiyo tafsiri yake ya jinsia
inakuwaje? Na ni pande zote mbili, wa msichana na mvulana. Na kwa hiyo
kwa kusema kwamba watoto wenyewe hawajengi mawazo mabovu kuhusu
jinsia. Ni jamii ya watu wazima inayowafanya watoto wajenge yale mawazo
mabovu kuhusu jinsia. Siyo watoto wenyewe. Watoto wenyewe wana
heshima. Wanajiona kama watoto. Halafu jamii, watu wazima inapoleta yale
mawazo yao, mtoto wa kike ni hivi, mtoto wa kiume ni hivi, wanaanza kujua
“aha sehemu yangu ni hiyo, na sehemu yako ni hiyo”. Na kwa hiyo yale
mawazo tofauti, na ni watu wazima wanaosema hivi, wanaojua watu wazima
ni sahihi, kwa hiyo wanachukua yale mawazo.

Swali: : Irimi Hanak: Kwanini uliamua kuandika kuhusu mada ngumu kama ile ya watoto mitaani?

Jibu: Elieshi Lema: Kwanza ilikuwa rahisi zaidi kwa sababu hiyo ilikuwa tu sehemu ya kitabu,
siyo kitabu kizima. Mimi nilijiambia baada ya kutoa “Safari ya Prospa”, nilitaka
kwenda kumfuata Sara mitaani, kwa sababu Sara alibaki. Kwa sababu
Sara alikuwa mtoto wa mitaani. Na kila siku nasema nikipata nafasi, lazima
nirudi kwa Sara, ili nimchukue Sara pale kama mtoto wa mitaani. Lakini nahitaji
utafiti mrefu, mkubwa, kwa hiyo kidogo hiyo nafasi imekuwa bado sijaipata.
Lakini hapo sasa, ingekuwa niyachukue na mambo yale ya ukatili wa
wenyewe kwa wenyewe, ukatili wa watu wazima kwa watoto wa mitaani, na
shida wanayoipata, an wao wenyewe wanatazamaje.
Nisipofanya utafiti, itakuwa ni mawazo ya mtu mzima nayaweka kwa watoto.
Na yanaweza yapata mengine yakawa ukweli, na mengine yasiyo kweli. Na
hutaki kuandika kitu bila kujua ni kwa nini unaandika.

Kwanza, watoto wa mitaani, ni kitu kipya Tanzania. Na tulikuwa tunashangaza
kila mtu. Watoto wa mitaani walikuwa hawapo miaka kadhaa iliyopita. Na
ilipokuja sasa ikawa phenomenon. Watu wakawa eh – “watoto wa mitaani, ni
watoto wabaya, piga, ni wezi nyiye”. Halafu unafanya urafiki na watoto wa
mitaani, unaanza kujua kwamba kweli siyo wezi, siyo watoto wasio na heshima,
ni watoto wenye shida. Na kwa hiyo watoto hapa wanapokuja, kwanza
wanapokutana (na Sara na Prospa) wanavunja chupa wanasema “Wewe unakaa
kwenye ile kundi” ni kwamba kwanza wanahitaji uongozi ili waweze
kuishi mitaani. Wakajua kwamba hawa siyo watoto wa mitaani. Wakamwambia
usilale ovyoovyo utaumia, ni kama wamekuwa wazazi sasa kwa wale
watoto. Na wakawachukua, wakawaambia wewe uende huku na wewe uende
huku, kwa sababu wanaishi tofauti, na wakapata familia mpya, wakaishi nao.
Wakaongozwa, jinsi ya kuishi, unaenda wapi unapata chakula, unaishi vipi,
unsafisha magari unafanya hivi unafanya hivi, wakaishi. Na mimi nilifanya
makusudi kwamba kwa sababu ya kuelewa maisha ya mitaani na maisha ya
shida, yana tena ile tathmini ya jamii, inatoka vizuri sana hapo, na wanatathmini
jamii vizuri kabisa, na ukiangalia wamekuwa na stadi za kuishi, ambazo
zinazidi hata za watu wazima, kwa sababu wanapokutana na yule mjomba,
mjomba hana stadi za kuishi. Anaishi vizuri, ana gari nzuri anafanya biashara
nzuri, anaendesha gari na anaishi huku, mbali na dunia ya mtaani, hana stadi
za kuishi. Kwa hiyo anaposema ingia we peke yako, wanaingia wote, na wanajua
jinsi ya kuingia na jinsi ya kukaa, na jinsi watakavyofanya mambo. Na
ni katika hivyo mpaka wanakuja kugundua kwamba mtoto kweli amepotelea
wapi.

Swali: : Irimi Hanak: Kwa vipi ulipata kufahamu wa watu wanaoishi kama wahusika wako?

Jibu: Elieshi Lema: Kuna ule utafiti kwa vitendo. Unajua kama uko kwenye utafiti wa watoto
usiowajua. Kwa sababu mimi sijui, sijaishi, maisha ya mtoto mtaani, kwa
hiyo siwezi kuyajua, sasa njia wa kuyajua ni kufanya utafiti kwa vitendo na
kuyafuata. Unajua, anaishi wapi, unaenda, anakula nini, unajua, anafanya kitu
gani, kazi gani, na wakati mwingine unamwambia “We fanya, nioshe gari nikupe
pesa”, na kwa hiyo, wanakuwa rafiki na wanaanza kukuambia, “mimi
ninaishi mahali fulani, baba yangu alikuwa hivi, mama yangu alikuwa hivi”,
halafu unauliza maswali ilikuwaje, wanakuambia “mimi sipendi kukaa mitaani
basi, lakini nikienda nyumbani napigwa, kwa hiyo afadhali tuwe hapo.”
Baada ya kujua ndani kwao wanajisikiaje unaweza sasa ukafuatilia ukahisi,
ukajenga ile hisia na kusema ingekuwa mimi. Imenisaidia kuchora hawa wahusika
watoto wa mtaani kwa huo utafiti.

Swali: : Irimi Hanak: kitabu chako cha pili, “Mwendo” kinazungumzia jinsi ya wasichana wanavyokuwa watu wazima na pia tatizo la tohara kwa watoto wa kike. Kwa nini umechagua tena mada inayogusa matatizo tele ya jamii?

Jibu: Elieshi Lema: Kwa sababu hiyo ndiyo ilinigusa na tulikuwa tunaizungumzia sana hiyo, na
kwa muda mrefu. Watu wanazungumza female genital mutilation, halafu unaandika
makala kwenye gazeti, halafu watu wanafanya semina lakini hakuna
kinachotokea. Na kuna kitu kingine hapo - issue ya “Oh ni utamaduni wetu,
kufanya hivi na hivi” Kwa hivyo hicho kitu kikanigusa. Na mwaandishi kila
mara huandika vizuri wakati anapoandika kitu kilichomgusa yeye mwenyewe,
anasema “Ah, lazima niseme kitu hapo” Kweli ilikuwa ngumu, nilifanya utafiti
kwa miaka mitatu. Kwanza ilibidi nichague.

Nilichagua jamii ya Kimakonde kwanza, kwa sababu wao hawatahiri. Kwa
hiyo nilijua nitatumia hiyo jamii ambayo haitahiri kama kioo cha ile inayotahiri.
Hiyo ni moja. Halafu baada ya kuamua hivi, sasa ilibidi nifuatilie, wanapitia
katika rituals gani, wakati mtoto anapofika huo. Kwa hiyo ilibidi nifanye
utafiti. Mimi siyo Mmakonde. Ilibidi niwatafute Wamakonde, niwafahamu,
niwaeleze nilitaka kufanya nini, nizungumze na watu, waweze kuzungumza
na watu wengine ambao wanafanya vitu hivyo katika zile rituals, ili niweze
kuona zinafanywaje. Nikaongea na wanawake wa Kimakonde wengi, nikaenda
Mtwara, nikazungumza na wasichana, nikaenda Lindi, kwenye shina la
Wamakonde.
Kila nilipokuwa nikiandika “Mwendo” nilifika mahali nikajikuta aa siwezi
kuendelea kwa sababu sijui kwa hiyo nina haja, naenda tena kwenye utafiti,
kuulizia hiki kinakwendaje. Kwa hiyo kweli kilinipa shida, kile kitabu kimenipa
shida sana, lakini nafurahi kama kimetokea, kama wasomaji wakisoma,
wanaona kile kitu nilichotaka kusema kimetoka. Mwanamke Helena Margareta,
yule mama nampenda sana, kwa sababu ilibidi nimtumie yeye kuonyesha
kwamba kuna myth na kuna ukweli wa maisha, na kwamba rituals tunazitengeneza
wenyewe. Na kwamba tunaweza tukazibadilisha wenyewe. Kwa hiyo
ile kitu ya “Ni utamaduni wetu, kwa nini tusitahiri wasichana”, hiyo siyo valid,
kwa hiyo Helena Margareta – kwangu kumchora Helena Margareta ilikuwa
rahisi kwa sababu ni mtu mzima, anazungumza ninachojua mimi, lakini
wale wasichana na wale wavulana pia, wanavyopita na wanapokuwa na kuona
ulimwengu wa watu wazima - ngumu.

Swali: : Irimi Hanak: Uliwahi kuwakuta watu kama Helena Margareta?

Jibu: Elieshi Lema;
Hakuna mtu niliyekutana naye ambaye ni Helena Margareta. Hakuna kabisa.
Kwanza, watu unaoongea nao wanaamini kwamba hicho wanachofanya ni
sawasawa. Lakini Helena Margareta nilimpenda kwa sababu mimi niliweza
kutumia akili yangu ya mtu mzima zaidi katika kumchora. Umefahamu? Kwa
hiyo nilimpenda, alikuwa anasema vitu ambavyo mimi kama mtu mzima niliweza
kupenda.
Nimekuta mama Felisia, ni typical, hao nimewakuta, ambao walisema: “Aa,
mtoto wa kike lazima achezwe, asipochezwa tunamkataa”, hao wapo, hao nimekutana
nao.
Helena Margareta ni vipande, nimesikia, labda ni wanaume nusu, labda ni
wanawake nusu, labda ni robo kidogo tu sehemu fulani. Na Helena Margareta
amechorwa zaidi kwa kusikia mtoto wa kike mdogo aliyekuwa amechezwa,
alivyokua anazungumza.
Unajua unaweza ukasikiliza mtoto mdogo anavyozungumza ana mawazo safi
kabisa, hayaendani na tabia ya wale watoto wengine ambao unawachora. Kwa
hiyo unawaleta kwenye - nani - ya watu wazima. Ni kitu nimechora kutokana
na watu wengi, na mtazamo hasa ile ya Margareta anatokana na mtazamo wa
mwandishi. Nampenda kwa sababu ndiye ametoa ile changamoto, anakuja
kwa mwalimu anasema:
“Aa. Hiyo ni harakati. Na mimi nilipokuwa katika harakati ya ukombozi
Msumbiji, niliambiwa kwanza kabla ya hujabadilisha kitu lazima uamini, ili
ukibadilisha unabadilisha kitu ambacho unaamini kwamba kile kingine kitakachokuwa
ndicho”. Hasa huo ni mtazamo wangu ambao kwamba tukisema
tu: “Aa, hatutabadilisha kitu”. yatakuwa mabadiliko superficial.
Kwa hiyo nilimpenda Helena Margareta, alinipa hiyo fursa ya kusema unaotaka
wewe kama mwandishi useme. Alifungua dirisha, nikaweza kupata
mambo ya kuweza kumchora na kuwa hivyo alivyokuwa. Lakini kwa kweli
wanawake wengi ni kama mama yake Felisia.

Swali: : Irimi Hanak: Reception ya kitabu hiki ikoje, wasomaji watanzania wanaonaje?

Jibu: Elieshi Lema: Hivi vitabu vilinunuliwa na “Mradi wa Vitabu vya Watoto Tanzania” na vilisambazwa
shuleni. Kila mara naambiwa watoto wanakipenda. Kitabu hiki,
watoto wa kike waliamua wavulana hawatasoma. Vilikuwa vinafichwa, yaani
akishapata mmoja, hataki kukitoa, anasoma, anampa mwingine, anasoma,
anampa mwingine anasoma, anampa mwingine. Watoto wenyewe, ambao
ndiyo haswa niliwaandikia, walikipenda, wameona kwamba kuna kitu nimesema
ambacho nilitaka niseme. Mimi ndiyo hiyo ilinifurahisha kuliko vyote.
“Safari ya Prospa” vilevile. Safari ya Prospa inapendwa sana.
Shida moja hapa Tanzania ni uwezo wa kununua vitabu. Hiki kitabu tunakiuza
elfu mbili mia tano, ni ghali kwa jamii ya kawaida ya Tanzania. Kwa hiyo
kusambaza kwake kwa watoto wengi ni kwamba lazima kuwe na mpango
maluum ya kuvinunua na kuvisambaza. Hapo vitafikia watoto wengi zaidi.
Hiyo ni moja. Pili, usambazaji wa vitabu hapa ni mgumu, kwa sababu nchi hii
ni kubwa. Hatuna wasambazaji wa vitabu wenye uwezo wa kifedha na organisation
wa kuweza kusambaza vitabu mpaka huku vijijini. Na vikifika huku
vijijini, kama ni wasambazaji wa kuuza, havitanunuliwa, kwa sababu bei yake
ni juu, bei ya hiki kitabu itashindana na bei ya unga, bei ya sukari. Kwa hiyo
sitegemei mkulima aache kununua unga anunue “Mwendo“”
Ukiniuliza ni watu wangapi wanaonunua “Mwendo” mimi sijui.
Na hapa utamaduni huo wa “reading session” haupo. Tuseme tukimaliza
kutengeneza ofisi yetu, tutakuwa tukifanya readings kila mara. Lakini mara
nyingine hakuna mahali maalum ya kufanyia readings. Kwa hiyo lazima sisi
tuanzishe tukimaliza ofisi.

Watu wazima waliokisoma hiki kitabu, wamefurahi, wakarudi wakanunulia
watoto wao kama zawadi, nampa mwanangu zawadi, soma. Ilikuwa vizuri.
Halafu hiki kitabu, tulikilaunch kwenye telvisheni, kwa hiyo kilijulikana, kwa
mara moja kilijulikana sana. Lakini wengine waliuliza kwa nini, watu wengine
walioona kwenye televisheni walishangaa: “Aa, kwa nini ameandika, kwa
nini Mchagga aliandika kuhusu Wamakonde” kwa hiyo kwanza hawana utamaduni
wa vitabu, pili hawatazami maswala, wanatazama kwa nini Mchagga
aliandika kuhusu Wamakonde.”
Kwa hiyo matatizo ni mengi, kama tunataka kuanza utamaduni kama huu.

Swali: : Irimi Hanak: Ukiandika katika lugha ya Kiswahili, unawaandikia wasomaji gani?

Jibu: Elieshi Lema: Mwandishi wa Tanzania ambako Kiswahili kinaongeka, watu wanaongea
Kiswahili zaidi ya asilimia tisini na tisa, huna uchaguzi mkubwa sana, kama
unawaandikia Watanzania. Inakubidi kama una swala linalokuchokoza na ni
la jamii ya Watanzania na unataka kuwaandikia jamii ya Watanzania, lazima
unandike kwa Kiswahili. Kiingereza watu wengi hawaongei. Kwa hiyo hii
ilinibidi niandike kwa Kiswahili. Lakini pia nimeandika vitu vingine kwa
Kiingereza, na hata hivyo, nimeandika kwa Kiingereza nikijua kama kweli
ikibidi Watanzania wasome nitafsiri kwa Kiswahili.

Swali: : Irimi Hanak: Lakini kama ungeandika kwa kiingereza, watu wengi zaidi duniani wangeweza kusoma vitabu vyako. Na pengine ungeuza vitabu vingi zaidi.

Jibu: Elieshi Lema: Mimi nahusika kama mwandishi, jukuma langu la kwanza ni kuwaambia vijana
wanaokuwa kitu fulani, kwamba mnao uwezo ndani mwenu ya kuamua
kiasi fulani ya maisha yako yaende vipi. Hiyo ilikuwa ni lazima, ilinikera kwa
hiyo ilinibidi nijaribu kuambia. Na hao vijana wataelewa Kiswahili. Na walipata
ujumbe: Aa, kumbe naweza nikakataa. Naweza nikakataa mwili wangu
usiguswe na mtu mwingine. Yaani ni kitu muhimu mno, ilibidi niandike kwa
Kiswahili kwanza. Level ya pili ndiyo hiyo kama publisher. Wakaja kuniambia
“Unajua Elieshi, nitafsiri kitabu chako kwa Kiingereza”, nikasema ni sawa,
lakini kile kitu nilichotaka kusema ningekisema kwa lugha ya Kiswahili
tu. Kwa hiyo lazima niwe mwandishi kwanza, halafu niwe mchapishaji baadaye.
Hiyo nyingine ambayo niliandikia ambao ni ya watu wazima ni Kiingereza.
Kwa sababu maswala yanayohusu watu wazima yameshajadiliwa na yanajulikana,
yapo.

Hiki kitabu kipya ni riwaya pia, ni hadithi ya msichana aliyekulia kijijini. Anafanya
hivyo hivyo, anatathmini jamii pia. Na huyo ni msichana, amezaliwa
katika nyumba ya single mother, ach, kama kuna tathmini ya jamii ya patriarchy,
unafanywa hapo. Vyote vile vidogovidogo nilikuwa nilijaribu kuzungumzia
huku vidogo tu, huku ni mtoto, kwa hiyo huwezi kuzungumza mambo
makubwa (Anaonyesha kitabu cha “Mwendo”). Lakini hapa (anaonyesha kitabu
kipya), hapa kila kitu anatathmini, kila kitu anauliza maswali ni kwa nini
kiwe hivi, na kweli njia yangu ni hii. Kwa hiyo ambacho kinanikera ambacho
bado kinaendelea, labda kimepata culmination hapo. Kitabu hiki kitatokea
hivi karibuni. ( kitabu hiki kimeshaoka, na nimekifanyia uhakiki – ni kitabu chenye ujumbe mzito)
Hii nimeandika kwa Kiingereza inaweza ikasomwa na watu wengi zaidi. Lakini
pia ni ukweli wameshakuja watu kama wawili hivi, wanataka kutafsiri
“Safari ya Prospa” kwa Kiingereza. Hiki ndiyo kipya zaidi hawajaja watu wa
kutafsiri. Ila sidhani kama mimi ni mtafsiri, sitaweza kutafsiri mimi mwenyewe.
Nilipenda mtu mwingine atafsiri halafu nikione utafsiri ukoje. Mimi
ningepewa uchaguzi ni kipi kianze, naona hiki (“Mwendo”) kwanza kipate
tafsiri, kwa vile kinazungumza mambo makubwa, makubwa hata kwa kitabu
cha mtoto.
Unajua, pia sitaki ile cut-throat thing. Mtu kama akiona kuna maswala muhimu
akatafsiri, ndivyo ningependa. Hili ni swala muhimu na ni lazima tulishughulikie
katika mtazamo fulani. Hiyo sympathetic approach, bila hiyo inaweza
ikatokea ukasema “aa kaa huko, kwa nini unanijua, huwezi kunisemea
miye, kaa huko.” Sasa sisi tunasema kaa huku, wale wanasema “mm, una shida
gani” hakuna kitakachofanyika. Unajua hizo ni levels, kuna international
levels, kuna national levels, halafu unakuta level ya kabila kwa kabila, kwa
hiyo kila siku hatuwezi kusema “Mm, wewe mbaya, wewe ovyo, wewe akili
yako mbovu” hatuwezi kusema, lazima tuingie ndani, tufanye utafiti tujue,
wanaangaliaje hiki kitu, ni kwa nini wanafanya hivi vitu, maana yake ni nini.
Uzuri wa Helena Margareta, ameshaanalyze ritual na kusema: kuna maana
yake, kuna vizuri, kuna vibaya, vibaya, achana naye, vizuri enda navyo. Kwa
sababu ritual ni identity ya watu, huwezi kuifuta identity kwa kusema sipendi
hiyo ritual. Unaangalia hiyo ritual na unasema: Ni nini katika hiki kinachosaidia
hawa watu kukuwa, to grow, kwa sababu tunakuwa katika mazingira.

Swali: : Irimi Hanak: Tungeweza kusema kwamba kitabu cha Mwendo kina ajenda ya feminism?

Jibu: Elieshi Lema: Ni kweli. Definitely there is a lot of feminism in everything I write. Lakini
Feminism siyo kitu cha Ulaya. Jina la feminism ndiyo linalotoka Ulaya. Lakini
concept ni ya dunia nzima. Wanawake ni watu na wana mtazamo. Basi.
Wanawake wanaishi katika jamii ya wanawake na wanaume. Na wana
mtazamo wa maisha. Ambao ni tofauti na wa wanaume, kwa sababu wao ni
wanawake. Sasa hiyo ni feminism. Siyo lazima iwe na neno feminism, lakini
the essence ndiyo hiyo. Kwa hiyo mimi hata ukiniambia Western feminism
inasema nini, mimi bado sijui sana, najua kidogo tu.

Wengine wanafikiri feminism ni kitu kinachotoka Ulaya. Feminism iko hapa
hapa! Mahali popote anapoishi mwanamke katika jamii, na wanawake wengine
na wanaume, lazima kutakuwa na feminism. Kwa sababu ni mtazamo wao.
Ni ile kusema: sisi tunataka hivi, sisi tunaona hivi, iendelee hivi. Dunia yangu
naitazama hivi naitafsiri hivyo.
Lakini feminism – huwezi kuwa mwanamke katika jamii, uwe na mwamko,
usiwe feminist. Ni jina tu tunaliogopa. ... Mimi sijiiti feminist. Sina haja ya
kujiita feminist. Hata siku moja. Ninajiita tu mwanandishi ambaye anatazama
maswala ya wanawake, na ambaye anachunguza, kila siku naingia ndani,
nauliza maswala.
Irimi Hanak: Ningependa kukushukuru kwa mazungumzo yetu.

Jibu: Elieshi Lema: Nakushukuru pia kwa sababu mara nyingi waandishi wa Kiafrika hatupati
sympathi kutoka Ulaya, ile ya hata kujua wanazungumzia maswala gani, matatizo
yao ni nini, waandishi wanafikaje pale wanapofika. Kuwa mwandishi
wa Kiafrika, ni vigumu in the sense kwamba unafanya vitu vingi mno. Hatuna
ile starehe ya kuwa mwandishi peke yake. Unakuwa mwandishi, unakuwa
mama, unakuwa mchapishaji, unakuwa unafanya kazi na vikundi, unafanya
vitu vingi, kwa hivyo kufanya utafiti tu wa kitu hiki kinachukua miaka mitatu
ambayo mahali pengine ni miezi sita au even miezi mitatu kwa sababu inafanywa
tu. Kwa hiyo kweli na mimi nafurahi umechukua ile jukumu ya kupeleka
ujumbe wa mwandishi mdogo katika jamii yako.

Na,
Padri Privatus Karugendo.