Wanawake wana uwezo mkubwa

Makala hii ilichapwa kwenye gazeti la Rai, mwaka 2004.

Saturday, August 21, 2004


WAMAWAKE WANA UWEZO MKUBWA

Wakati kila Mtanzania anajiuliza ni nani atamrithi Rais Mkapa, kuna mapendekezo yanayojitokeza kwamba sasa ni zamu ya akinamama kuliongoza taifa letu la Tanzania. Wengine wanakwenda mbali hadi kutaja majina ya akinamama hawa. Bahati mbaya wengi wa akina mama hawa wanaotajwa umri umewatupa mkono, wawili watu umri wao ni mdogo na kisomo chao kinaruhusu! Mawazo haya ni mazuri na ya msingi. Wanawake wana uwezo mkubwa; si kweli kwamba kuna mambo wanayoyaweza wanaume tu na wanawake hawayawezi. Tumeshuhudia mengi yanayoonyesha kwamba wanawake wana uwezo sawa na ule wa wanaume. Tofauti ni kwamba wanadamu tunazidiana katika nyanja mbali na kwamba uelewa unaziadiana kutoka mtu hadi mwingine:

Hakuna haja ya kutaja kwamba wanawake madaktari wanaongezeka kila kukicha, wasichana wanajiunga kwenye fani ya uinjinia na kwamba tunao wanawake mainjinia, uhasibu na fani nyingine ambazo zilifikiriwa kuwa fani za wanaume tu huko siku za nyumba. Uamuzi wa hivi majuzi wa KKT Dayosisi ya Kaskazini Magharibi (Bukoba) kuwabariki wachungaji wanawake, limekuwa pigo kwa “Wahaya” walioamini kwamba huduma za kiuchungaji ni kazi ya wanaume tu! Kwa vile KKT, ina ushawishi mkubwa mkoani Kagera na nchi nzima kwa ujumla, uamuzi huu wa kuwabariki wanawake limekuwa pigo kubwa kwa kanisa Katoliki, hasa kwa upande wa jimbo katoliki la Bukoba na Rulenge, ambao kanisa lao linaamini kazi ya uchungaji(upadre) ni ya wanaume tu. Mwanamke mchungaji wa Bukoba, atafungua ukurasa mpya kwa wale waliokuwa wakiamini kwamba kuna kazi zilizotengwa kwaajili ya wanaume peke yao.

Tanzania ina historia ndefu ya akina mama kushiriki katika mapambano ya kuleta uhuru na kuchangia maendeleo ya taifa. Majina ni mengi ya akina Bibi Titi, Sofia Kawawa, Lucy Lameck nk. Hata leo hii akina mama walio kwenye uongozi kama mawaziri wanatoa mchango mkubwa katika kulijenga taifa letu na kuchochea kasi ya maendeleo, hawatajwi kwenye kashifa za Rushwa, hatujawasikia wakishutumiwa kujilimbikizia mali, kupora au ubabe wa kugombania madaraka. Wanafanya kazi kwa kujiamini. Wana uwezo mkubwa wa kujieleza. Wanaweza kuzungumza Kiswahili kizuri, tofauti na wanaume wanaoongea kwa kuchanganya Kiswahili na Kiingereza. Wanawake hawa, ambao sote tunawajua kwa majina, wakiamua kuongea Kiswahili, ni Kiswahili tena Kiswahili fasaha. Wakiongea kingereza, ni kingereza safi!

Mkoani Kagera, kuna mchango mkubwa uliotolewa na akinamama ambao sasa hivi wengi wao ni wazee sana na wengine wamekufa. Akinamama hawa ni wale waliojiingiza katika biashara ya kuuza miili yao. Biashara inayojulikana kwa jina la “Umalaya”; walisafiri hadi Mombasa, Nairobi Kisumu, Mwanza, Dar-es-Salaam na miji mingine ya Afrika mashariki iliyokuwa ikifikika kwa usafiri wa meli na train. Pesa walizokuwa wakizipata huko walinunua vitu kama vinanda, vyerehani, baiskeli nk., na kuvileta Mkoani Kagera, pia walitumia pesa hizo kununua mashamba, kujenga nyumba na kusomesha watoto.

Mji wa Bukoba, una mtaa unaoitwa Uswahilini. Hii ni kati ya mitaa iliyokuwa imeendelea na kuwa na nyumba bora kwenye miaka ya 1950-1960, nyumba hizi ambazo zimedumu hadi leo hii zilijengwa na akina mama walioitumia miili yao si kwa manufaa yao tu bali kwa manufaa ya kuiendeleza jamii.

Wasomi wa kwanza wa mkoa wa Kagera, walisaidiwa na Kanisa, lakini ipo idadi kubwa iliyosomeshwa kwa msaada wa pesa za akina mama hawa walioiuza miili yao. Ni wazi tendo la “Umalaya” ni la aibu; si rahisi mtu kuungama wazi kwamba alisomeshwa na pesa kutokana na biashara hiyo. Ukweli unabaki palepale kwamba biashara hii ilichangia kiasi fulani maendeleo ya mkoa wa Kagera, katika nyanja mbalimbali.

Tusi, kwamba Wahaya wana jadi ya “Umalaya” si la haki. Mnamo mwaka wa 1910 Mjerumani Hermann Rehse, aliandika kitabu, akielezea kwamba “umalaya” lilikuwa ni jambo jipya mkoani Kagera. Mwandishi mwingine anayejulikana kwa jina moja la Bwana Swantz, anakubaliana na Hermann Rehse, kwamba “umalaya” ulianza kushika kasi mkoani Kagera, mnamo mwaka wa 1920.

Zipo sababu nyingi zilizopelekea biashara ya Umalaya kushika kasi mkoani Kagera. Baada ya Wajerumani na Waganda, kuingiza biashara hii mkoani Kagera, ilishika kasi: Magonjwa ya zinaa yalisababisha ugumba, na kama ilivyo kawaida, wanawake ndio walinyoshewa kidole, wale ambao hawakufanikiwa kupata watoto walifukuzwa kwenye ndoa na kulazimika kuishi kwa kujitegemea. Kwa vile wanawake walikuwa hawaruhusiwi kumiliki kitu kwa wakati huo, njia pekee ya kujitegemea ilikuwa ni kuuza miili yao.

-Wakati huo ndio Ukristu ulikuwa unaiingia na ilisisitiza ndoa ya mme moja mke mmoja. Wanaume waliokubali kubatizwa waliwafukuza wake zao wengine na kubaki na mke mmoja wa ndoa. Hawa wengine hawakuwa na njia ya kujitengea zaidi ya kusafiri na kufanya biashara ya kuuza miili yao.

Mpaka leo hii sote tunaamini kwamba UKIMWI, uliingia Tanzania kutokea Uganda. Wanaolaumiwa kwa kuuleta ugonjwa huu na kuueneza Tanzania, ni wafanyabiashara na wanajeshi waliopigana vita ya kumwondoa nduli Idi Amin. Pia ugonjwa wa zinaa uliingia Tanzania, kutokea Uganda. Mfalme Kabaka Mwanga(1880) wa Buganda, mwenye vituko vingi aliamini kwamba zinaa ni ugonjwa wa heshima na utukufu. Wanaume wote walipaswa kuwa nao. Kwa mtazamo huo ugonjwa huo ulienea kwa kasi. Wahaya waliokwenda kufanya kazi kwenye mashamba ya pamba kule Uganda, ndio waliubeba na kuuleta Bukoba. Mpaka leo hii kuna msemo kwamba wale waliokwenda kutafuta pesa Uganda, walileta pesa, maendeleo, magonjwa ya zinaa na dini za kigeni: Ukristu na Uislamu!

Ingawa akina mama waliouza miili yao, walionekana kuwa adui wa jamii kwa kusambaza magonjwa ya zinaa na kusambaza jina baya la wanawake wa Bukoba – jina la Umalaya, hatuwezi kukwepa mchango wao mkubwa na mzuri katika jamii. Chama cha TANU, kilipata michango ya pesa kutokana na kipato cha akinamama hawa. Watoto au jamaa wa mama hawa, waliosoma kwa pesa zilitokana na biashara ya umalaya, walikuwa mstari mbele katika kupigania UHURU wa nchi hii.

Ninakumbuka kuandika makala yenye kichwa cha habari “Ukombozi wa mwanamke, adui ni mwanamke mwenyewe”. Pamoja na ukweli kwamba wanawake wana uwezo mkubwa na wanaweza kutoa mchango mkubwa katika kuliendeleza taifa letu, bado kuna mawazo potofu kwamba mwanamke hawezi kitu. Bahati mbaya mawazo haya kwa kiasi kikubwa yamo kwenye vichwa vya wanawake wenyewe!

Ikitokea mwanamke akafungua biashara ya hoteli au mgahawa, atapenda kuajili mpishi mwanaume na wahudumu wanaume. Ukiuliza. Jibu linakuwa, Wanaume wanapika vizuri na kuhudumia vizuri, ukiwaajili wasichana watakuharibia kazi yako!

Kwa kawaida kuna mafundi wa nguo za kike, wanaume na wanawake. Idadi kubwa ya akinamama na wasichana wanapenda nguo zao kushonwa na mafundi wa kiume. Ukiuliza. Jibu linakuwa, Wanaume wanajua kushona na kubuni mitindo mizuri zaidi ya wanawake!

Utakuta mmiliki wa Salon ya nywele ni mwanamke. Lakini walioajiliwa kutengeneza nywele, kupaka rangi kwenye kucha, kulembesha uso ni mwanamme. Ukiuuliza, Jibu, Wanaume, wanasuka vizuri, wanapaka rangi vizuri na ujuzi wao wa kurembesha uso wa mwanamke ni wa hali ya juu kuliko wanawake. Siku hizi salon, ambazo hazina wanaume hazina wateja! Ni kweli wanaume wana ujuzi wa kutengeneza nywele kuliko akinamama? Ni kweli wanaume wana ujuzi wa kupaka rangi na kurembesha uso kuliko akina mama? Na je, haya ni mambo ambayo akinamama hawawezi kuyamudu?

Mvulana akiendesha gari, linaonekana ni jambo la kawaida na hakuna anayekuwa na wasiwasi kwamba huenda gari hilo si la kwake. Akiendesha msichana, utawasikia wasichana wenziwe wakiteta ,Huyu naye na kuringa, kwanza gari si lake, ni la mshikaji ni mali ya “buzi”!

Nimeshuhudia akinamama kumkimbilia Daktari Bingwa wa magonjwa ya akinamama mwanamme ,kuliko mwanamke mwenzao mwenye ujuzi uleule, kwa madai kwamba Daktari wa kiume, ana uwezo mkubwa, ana “mkono mzuri” na ana huruma kuliko Daktari wa kike! Haya yanasemwa na akinamama bila kulazimishwa, bila vitisho na bila unyanyaswaji wa aina yoyote ile, ni wazi ni matokeo ya kupumbazwa; ni ugonjwa unaohitaji tiba. Ni ugonjwa mkubwa kuliko tunavyoweza kufikiri na kujidanganya.

Sasa hivi, kwa sababu zinazotofautiana, watumishi wa ndani ni wavulana, kuliko wasichana! Kuna malalamiko kwamba hata wanaharakati wa kutetea haki za wanawake, wanawatesa, wanawanyanyasa na kuwadhalilisha wasichana wanaofanya kazi majumbani Umekuwepo pia ukweli wa wasichana wa ndani kupindua, kuingilia ndoa za waajili wao. Yote haya yamejikita katika hali nzima ya mwanamke kutojiamini na kutojithamini.

Hata zile ajila ambazo kwa kiasi fulani zingekuwa za akinamama na akina dada, bado zinachukuliwa na wanaume na kuwalazimisha wasichana kuishia kwenye “Uchangudoa”. Sitaki kuliongea hili kwa sasa, lakini kuna ukweli kwamba hata “Changudoa” wanatumia pesa zao kutunza watoto, kujenga nyumba, kusaidia ndugu na jamaa, sifa ile ile ya akinamama kuitumia miili yao si kwa manufaa yao tu bali kwa kuchangia kuliendeleza taifa letu.

Tuna akinamama wengi wenye uwezo wa kutawala nchi hii. Anayewakataa ni nani? Ni wanawake wenyewe. Jinsi wanavyowakatalia kufanya kazi kwenye mahoteli, salon na kususia ufundi wao wa kutengeneza nguo za kike ndivyo watasema, Mwanamke, ataongoza nini? Wanaume ndio wanafaa kuongoza. Ukiuliza, Mbona wanaume hawa wametuletea matatizo makubwa? Wanagombania madaraka, wanaleta vita, damu inamwagika, angalia yaliyotokea Zanzibar, angalia yanayotokea kila siku, rushwa, uporaji, nchi inauuzwa. Jibu, litakuwa, Mwanamme ni mwanamme hata kama ni lofa!

Si kwa kuambiwa. Nilimsikia mwenyewe akisema kwamba, Ukubwa ni ofisini, nikiingia nyumbani kwangu mimi ni mama wa ndani, ninapika na kumtunza mme wangu, na mme wangu ndio kiongozi na mtawala wa nyumba yetu, machachari yote haya mnayoyaona yanabaki nje ya mlango wa nyumba yetu. Huyu ni mama mwenye cheo cha juu katika serikali yetu, ni kati ya wale wanaotajwa kufaa kuliongoza taifa letu! Nywele zake zinatengenezwa na mvulana au msichana? Siri yake!

Mwingine ni rafiki yangu ambaye yuko mstari wa mbele kutetea haki za akinamama. Tunawaita wanaharakati Sikuamini macho yangu aliponiadikia akilalamika, Ninatamani ningezaliwa mwanaume ili niwe padri, ninaipenda sana haki hii, na ninawaonea wivu mapadri, ni bahati mbaya nilizaliwa mwanamke!

Kama mwanaharakati wa kutetea haki za wanawake anaona ni bahati mbaya kuzaliwa mwanamke, je akinamama wa kawaida, ambao hawakufanikiwa kusoma, wanawake wa kule vijijini watasema nini? Watawezaje kuwa na mawazo ya kumchagua mwanamke diwani, mwanamke mbunge na mwanamke rais? Kazi kubwa ni ile ya kumfanya mwanamke kujiamini na kujithamini, kuwaamini na kuwathamini wanawake wenzake. Jinsi jamii nzima ilivyoshiriki kuwapumbaza wanawake, ndio ilivyo kazi ya jamii nzima kushiriki katika kuwapatia akinamama mwanga mpya wa kujiamini na kujithamini.

Na, Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment