Uwazi na Ukweli

Makala hii ilitoka kwenye gazeti la RAI 2004

Sunday, July 04, 2004

RAI

UWAZI NA UKWELI MASHAKANI


Ni imani yangu kwamba watanzania wote tumemwombea na tunaendelea kumwombea Mheshimiwa rais Benjamin William Mkapa, Mungu amponye na kumrudishia afya yake ili aendelee kuliongoza Taifa letu hadi uchaguzi ujao, Atakapo kabidhi na kurithisha uongozi wa taifa letu kwa Mtanzania mwingine, Na kuendelea kushauri na kuishuhudia Tanzania ya kesho.

Ni jambo la kuleta matumaini kuona pamoja na ugonjwa, na kuzingatia ushauri wa madaktari, Rais, apumzike kwa muda wa kutosha. Bado kiongozi wetu anajitahidi kutimiza ahadi yake ya kulihutubia taifa kila mwisho wa mwezi.

Katika hotuba yake ya tarehe 30.6.2004, amegusia mambo ambayo yameuweka Uwazi na Ukweli mashakani. Kwa Kiswahili cha siku hizi tungesema: Uwazi na Ukweli, umewekwa kiti moto. Wataalamu wa lugha wangekwenda mbali na kuanza kuchunguza maana ya maneno haya mawili: Uwazi na Ukweli. Kamusi ya Kiswahili sanifu inaelezea neno Uwazi, kuwa ni; hali ya kutokuwa na kitu ndani, kwa maneno mengine, utupu. Linavyotumika katika siasa za Tanzania, lina maana ya kutokuwa na usiri, kuweka mambo yote wazi, kutokuwa na chuki, kinyongo na hasa kwa maana ya ndani kabisa, ni kuongoza kwa kuzingatia sheria za nchi. Na, neno Ukweli, ni pana sana. Lakini Kamusi ya Kiswahili sanifu inalielezea hivi: Uhakikisho wa jambo kama lilivyo; lakini. Kinyume cha maneno haya mawili ni: Giza na Uongo!

Katika hotuba yake Mheshimiwa Rais Benjamin William Mkapa, alimsifia sana Mheshimiwa Cheyo:

“ Lakini natambua na kuheshimu pia ukomavu wa kisiasa aliouonyesha mgombea wa UDP, Mhe John Momose Cheyo. Ninampongeza kwa uungwana wake katika kushindwa. Kwa hakika amethibitisha methali yetu ya Kiswahili, Asiyekubali kushindwa si mshindani. Na mimi naongeza kauli yangu: Asiyekubali kushindwa, si muungwana. Namshukuru Mhe.Cheyo kwa kuimarisha msingi wa ushindani wa kiungwana kwenye siasa za nchi yetu”

Tukitaka kuwa waaminifu kwa maneno haya ya Uwazi na Ukweli. Tutakubaliana kwamba baadhi ya viongozi wa vya upinzani hapa nchini ni waungwana kama Cheyo. Na ndio maana amani imeendelea kudumu! Kweli! Ni waungwana kuliko viongozi wengi wa CCM!

Ushauri wa bure ni kwamba uungwana huu usielekezwe upande mmoja. Sitaki kuamini kwamba Mheshimiwa Rais Benjamin William Mkapa, hana habari juu ya yale yanayotendeka katika nchi na hasa yale yanayotendwa na wanachama wa CCM:

Juzi diwani wa CCM wa kata ya Rwamishenye, Bukoba, aliandaa kikundi cha “Majambazi” kuuchambulia msafara wa mwenyekiti wa CUF kitaifa Mheshimiwa Lipumba. Je, huo ni uungwana? “ Asiyekubali kushindwa si muungwana”, anayehitaji msemo huu ni nani? Vurugu zinazojitokeza mjini Bukoba, zinatokana na CUF kushinda kiti cha Ubunge cha Bukoba mjini. Mpaka leo hii CCM, haijakubali kushindwa!!

Nimemsikia na kumwona kwenye luninga Mheshimiwa Mbunge wa Moshi vijijini kupitia chama cha TLP Thomas Ngawaiya, akilalamika Bungeni, kwamba Serikali inafahamu “wahuni” waliomvamia na kumpiga. Huo, ni Ungwana?

Kule Karatu, wamepata misaada yenye thamani ya mamilioni ya pesa kutoka Ujerumani, kupitia chama cha CHADEMA. Wakati wa makabidhiano ya msaada huo kati ya wahisani na viongozi wa Wilaya ya Karatu, viongozi wa serikali inayoongozwa na CCM, hawakuonekana! Walisusia, kwa vile msaada huo ulikuwa umepitia CHADEMA. Msuguano wa kila mara kati ya viongozi wa serikali na viongozi wa chama cha CHADEMA, wilayani Karatu, hauonyeshi ukomavu wa kisiasa na uungwana kwa upande wa CCM. Mpaka leo hii CCM, haijakubali kushindwa kwake kule Karatu!

Ingawa kila chama kina malengo ya kushinda. Nguvu na pesa zinazotumiwa na chama cha CCM katika uchaguzi mdogo, hazionyeshi ukomavu wa kisiasa na uungwana. Tuliona yaliyotokea Hamugembe,Bukoba, wakati wa uchaguzi mdogo wa udiwani, tumeyaona ya Bariadi. Pesa zimemwagwa na nguvu za dola zimetumika; tuiachie historia kuhukumu! Uwazi na Ukweli, maana yake ni chama kimoja kuwa na madiwani wote na wabunge wote? Kama ni hivyo maana wa vyama vingi vya siasa ni ipi? Demokrasia, ni kuhakikisha chama kimoja kinatawala? Kama hivyo ndivyo ilivyo basi ukweli ni kwamba Uwazi na Ukweli umeingia mashakani.

Mheshimiwa Rais anasema hivi; “ Kwanza, ukweli ni kuwa kila chama kinatafuta ushindi. Hakuna chama kinachoingia kwenye uchaguzi kutafuta kushindwa. Kwa vyama ambavyo bado havijulikani sana, kama vile ambavyo ndiyo kwanza vimeandikishwa, au vipo mbioni kuandikishwa, au vipo mbioni kuandikishwa, uchaguzi ni fursa ya kujitangaza ili vijulikane. Vinatafuta kujulikana kwa kuvisindikiza vile ambavyo tayari vimejijenga na vinaamini vinaweza kushinda! Uwazi na Ukweli. Vitajulikana kwa kuandaa nakutangaza ilani ya Uchaguzi, na sifa za wagombea wake”

Haya ni maneno matamu tu yenye unafiki ndani yake. Vyama vinavyoruhusiwa kujitangaza ni vile vyenye mwelekeo wa CCM, au vilivyopandikizwa na CCM. Vyama ambavyo wanachama wake wakimaliza kazi wanarudi nyumbani na kupokelewa kwa shangwe na vifijo. Mifano ni mingi! Vyama vinavyoonyesha sera za kuiyumbisha CCM, vinazikwa haraka. Mfano wa chama cha HAMASA, chama cha vijana, kilifutwa bila sababu za msingi. Kama Ofisi ya msajili wa vyama ingekuwa chini ya Bunge au chini ya chombo ambacho hakiendeshwi kwa nguvu zote na chama tawala, HAMASA, isingefutwa. Giza na Uongo!

Ipo mifano ya wafanyabiashara waliohama CCM, na kujiunga na vyama vya upinzani. Biashara zao zilivurugwa. Walilazimika kurudi CCM, ili mambo yao na biashara zao ziende vizuri. Je, huo ni uungwana?

Tumewasikia baadhi ya viongozi wa juu katika CCM wakisema, Ukitaka mambo yako yaende sawa, jiunge na CCM; ukitaka ukipate cha mtemakuni jiunge na upinzani. Huo ni Ungwana na ukomavu wa kisiasa?

Ninapenda nikubaliane na Mheshimiwa Rais Mkapa, anaposema: “ Tatu, ukweli ni kuwa, katika nchi zote ninazojua habari zake, chama kinachoshinda, na hata vyama vinavyoshindwa, huwashukuru waliovichangia kwa namna mbalimbali. Nchini Uingereza wanaweza kupewa kazi, ua heshima, tuzo na nishani mbalimbali. Wanavyozitumia ni jambo jingine.”
Ni kweli, maana kama mtu amefanya kazi ni lazima apate tuzo. Tukiangalia Uingereza, wale wanaopewa kazi kama tuzo kwa kukisaidia chama tawala, ni watu wenye sifa na kisomo cha kazi wanazopewa. Ni watu wenye uzalendo na upeo. Ni watu wanaoiandaa Uingereza, ya jana leo na kesho. Nina imani Waingereza wanaweza kuandamana wakijua kwamba kuna mtu amepewa kazi kama tuzo wakati mtu huyo hajui kusoma wala kuandika au hana ujuzi wa kazi aliyopewa. Binafsi na wala si kuambiwa, nimeshuhudia wenyeviti wa vijiji kupitia chama cha CCM, wasiojua kusoma wala kuandika. Tuna makatibu tarafa, wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa ambao kisomo chao na uelewa wao ni mdogo kiasi cha kukwamisha mipango ya maendeleo. Rushwa, tunayoiimba kila siku kiasi kikubwa inaendeshwa na viongozi wa serikali, inayoongozwa na CCM!

Uko wapi uzalendo wa viongozi wa serikali waliopitisha mradi wa IPTL? Ni ukweli kwamba bila IPTL, tungekuwa na matatizo makubwa ya umeme kama anavyotetea mheshimiwa Waziri mkuu. Mradi wa gas ya Songosongo, ulianza kabla ya IPTL, ulipigwa vita na wale wenye sababu zao. Leo Uwazi na Ukweli, tunaelezewa kwamba IPTL, ni mkombozi! Mkombozi wa nchi au mkombo wa matumbo ya watu wachache?

Mheshimiwa Rais anaipongeza Bajeti 2004/05 na kuwashukuru waheshimiwa wabunge kwa kuipitisha kwa kishindo. Wanaichambua kweli, tena wengine kwa maneno makali, lakini mwishoni kama mchezo wa kuigiza wanaunga mkono asilimia miamoja! Giza na Uongo! Kwa mtu anayeishi mjini na kwa viongozi wa Serikali, hii ni bajeti nzuri. Kwa sisi tunaoishi vijijini, kwa mtu ambaye hana uwezo wa kununua chumvi, sukari, nguo, dawa; kwa mtu ambaye hana huduma ya maji, hospitali, shule, umeme na huduma nyingine muhimu, bajeti hii ni kama nyingine zote ambazo zimemtelekeza mkulima kwa miaka mingi. Kama kuna dhambi kubwa inayofanyika katika taifa letu ni kuwatelekeza wananchi wanaoishi vijijini. Watu bado w anaishi kwenye umasikini unaonuka! Heshima na thamani ya watu wa vijijini inaonekana tu wakati wa uchaguzi. Hali ya maisha katika vijiji vyetu inapingana kwa kiasi kikubwa na hali ya maisha katika miji yetu mikubwa, Watu wa vijijini wakipatiwa uhuru wa kuchagua kati ya Uwazi na Ukweli, Giza na Uongo; watachagua Uongo na Giza!

Mheshimiwa Rais, alimalizia hotuba yake kwa kuhimiza na kuelezea umuhimu wa maonyesho ya biashara. Alihimiza watanzania kupenda bidhaa zetu na kushughulikia ukomavu wa soko la ndani: “ Soko la ndani ndio mhimili mkuu wa uchumi wa taifa lolote, na ndio mwanzo wa ushiriki wetu katika uchumi wa kisasa na wa autandawzi” na kwamba “…….Ukarimu huanzia nyumbani; na ujenzi wa uchumi wa kisasa lazima uanzie nyumbani kwetu Tanzania”.

Swali si kupenda bidhaa zetu na kukuza soko la ndani. Swali ni je kuna maandalizi gani? Serikali inafanya mipango gani ili bidhaa hizi ziwafikie watu kule vijijini na ziwafikie kwa bei nafuu. Mfano wananchi wanaoishi kwenye mipaka ya Uganda,Rwanda,Burundi, wanapendelea kununua bidhaa za nchi hizi kwa sababu zinawafikia na zinakuwa na bei ya nafuu. Jambo linaloshangaza hata na mafuta ya taa, ambayo husafirishwa kutoka Dar hadi nchi hizi za jirani, bei yake ni nafuu kuliko hapa Tanzania. Kwa mtu ambaye uchumi wake ni wa chini na kipato chake ni sawa na hakuna, ni lazima atakimbilia kule ambako bidhaa zinanunuliwa kwa bei nafuu.

Kwa watu wa mkoa wa Kagera, soko la ndizi la ndani, linaweza kupandisha hali ya uchumi. Sasa hivi ndizi zinaivia tu shambani. Kule Kibare, Karagwe, kuna mkulima mwenye uwezo kuvuna ndizi 100 kwa siku. Kwa vile hakuna soko, au kwa maneno mengine hakuna uwezo wa kulifikia soko, ndizi zinaharibika tu! Wakati ndizi inanunuliwa shilingi 100, kule Karagwe,Dar, mkungu wa ndizi unaenda hadi sh. 10,000! Ukikusanya mashangingi yote ya serikali yaliyosambaa hadi wilayani, thamani yake inaweza kununua ndege mbili za mizigo ambazo zingekuwa zinasaidia kusambaza bidhaa zetu na mazao yetu nchi nzima. Lakini kupanga ni kuchagua, Alisema Mwali Nyerere. Yananunuliwa mashangingi! Uwazi na Ukweli!

Rais, anasema: “ Kwa sababu hiyo, nawahimiza wakazi wa jiji la Dar-es-Salaam na Watanzania wote wenye uwezo kwa ujumla, waende kutembelea maonyesho hayo ili wajionee hatua tunayopiga kwenye uzalishaji, huduma na biashara. Na wale wenye umri mkubwa kidogo wawe wa kweli, walinganishe kwa makini tulikotoka na tulipo leo”

Ni kweli kuna maendeleo ya uzalishaji. Lakini, hakuna pesa! Ina maana gani kuviangalia vitu bila kuwa na uwezo wa kuvinunua! Watanzania wengi wangependa kufika Dar, na kujionea wenyewe maonyesho ya biashara, lakini walio wengi hawana uwezo wa kusafiri. Labda Rais, wetu hana habari kwamba kuna watanzania ambao hawajawahi kufika hata kwenye makao makuu ya wilaya zao. Si kwamba hawataki, hawana uwezo. Watu hawana uwezo wa kujenga nyumba bora na za kisasa, hawana uwezo wa kununua godoro, mashuka, blanketi na vitu vingine vya muhimu kuweza kuyafanya washindwe kuwa na viatu na vitu vingine muhimu kwa kuustiri mwili: Watu wanaishi kwenye umaskini unaonuka. Watu walio wengi hapa Tanzania, wamezungukwa na Giza na Uongo. Katika hali kama hii ni lazima tuseme na kukubaliana kwamba Uwazi na Ukweli unaingia mashakani!

Na,
Padre Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment