MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZET LA RAI - 2004
USIONE SOO,SEMA NAYE!
Sikuyaamini masikio yangu niliposikia ikitangazwa kwenye vyombo vya habari kwamba tangazo la “Usione Soo, Sema Naye!” limepigwa marufuku hapa Tanzania. La kushangaza zaidi ni kwamba jambo hili lilijadiliwa na kupitishwa na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wabunge wetu, watetezi wetu na wawakilishi wetu! Inasikitisha na kukatisha tamaa. Naye Mzee Swallo, wa S.L.P.97, Njombe, ameandika kwenye barua za wasomaji:
“ Wengi wetu tulikuwa tunakerwa sana na matangazo hayo likiwamo lile la Usione Soo, Sema naye! Tangazo lile lilikuwa likiendelea kuchochea baadhi ya watu kusema naye ili kuelekea kwenye vitendo vibaya. Aibu ya kujifanya ya yule binti au mama hataki kumbe mwisho wake anakubali, ingeendelea kuwapatia ujasiri wale wavulana wenye aibu kusema na wasichana hata kama anakataa kwa sababu mwisho anakubali tu...” (RAI 580).
Anakubali kwa kusisitiza kutumia kondomu. Hili ni fundisho ambalo ni lazima litolewe. Waliobuni tangazo hili ni vijana. Wanajua tabia zao. Utakuwa ni upumbavu na kujidanganya wazazi kufikiri wanawafahamu vijana kuzidi wanavyojifahamu wao wenyewe. Vijana wanafahamu kwamba mwisho wa mwisho ni kukubali. Asiyekubali leo, atakubali kesho. Asipomkubali kijana mwenzake, atamkubali mheshimiwa mbunge, atamkubali kibosile au atamkubali kiongozi wa dini. Huu ndio ukweli wa maisha. Hivyo ajue siku atakapokubali ni kupima kwanza au kujikinga kwa kutumia kondomu. Inawezekana vipi tangazo lenye mafundisho muhimu kama hili liwe kero katika jamii yetu? Ni lazima kuna tatizo kubwa nyuma yake!
Naye Mheshimiwa Rais Benjamin William Mkapa, anasema kwamba wimbo wa Usione Soo, Sema Naye! Wa Ishi, unachekesha. Ingawa si lazima kwa vile unachekesha, haufai! Itakuwa ni kuidhalilisha falsafa, ikiwa rais wetu anafuata mtiririko potovu wa mawazo. Naye pia amekubali kwamba tangazo hili halifai na lipigwe marufuku. Inawezekana kweli tangazo hili linachekesha, ingawa mimi binafsi na baadhi ya wachambuzi wa mambo hatuoni linachekesha wapi. Hata kama linachekesha si kitu sana, maana katika nchi hii kuna mambo mengi ya kuchekesha. Watanzania walivyo waungwana hakuna anayeyakataa mambo hayo kwa vile yanachekesha: Mwaka 1995, tuliambiwa kwamba sifa ya msingi ya kuwania kiti cha urais kupitia chama cha mapinduzi ni mtu kuwa na digrii katika fani yoyote ile. Leo hii katika Ulimwengu wa ushindani na utandawazi, tunaambiwa kwamba digrii si kitu cha msingi tena. Watu walioweka vigezo hivyo bado wako hai- walipoweka kigezo cha digrii ilikuwa ni hatua ya kwenda mbele – itakuwaje watu wale wale wanaamua kupiga hatua ya kurudi nyuma? Inachekesha na inashangaza sana. Kichekesho ni kwamba kwa vile CCM, wameona kwamba digrii si kitu muhimu kwa rais wa nchi kupitia chama chao wanataka watanzania wote waamini hivyo kwa kuingiza jambo hili katika katiba ya nchi yetu.
Usicheke, ingawa inachekesha. Wahaya, wana msemo:
“ Huwezi kumcheka mama yako akiwa kichaa.”
Wazee wa miaka sabini hadi thamanini, walibatizwa Askari wa miavuli! Inachekesha? Au ni uongo? Yapo mambo mengi tu yanayochekesha. Hata na wale wazee wanaosinzia muda wote Bungeni, wanachekesha ati? Mbona taifa linaendelea kuwavumilia? Kama vijana wanawaelewa wazee na kuwavumilia – kwa nini wazee wasiwaelewe vijana na kuwavumilia? Vijana bado wanataka kuishi. Na kampeni yao ni ISHI. Ugonjwa wa UKIMWI, unawaletea wasiwasi na mashaka ya kuishi. Wametengeneza matangazo yao kwa lengo la kuwaelimisha vijana wenzao na jamii nzima juu ya kujikinga. Wanakatishwa tamaa kwa matangazo yao kupigwa marufuku. Huku ni kutojali na kulitakia mema taifa letu. Kuna hali ya kujifanya vipofu wa kutoliona tatizo na janga kubwa lililo mbele yetu. Yeyote asiyeonyesha kuyajali maisha ya vijana wetu ni adui wa taifa letu. litakuwa ni jambo la kushangaza vijana wakiendelea kuwapigia kura na kuwaingiza Bungeni, watu wasiolipendea mema taifa letu.
Tangazo hili la Usione Soo, Sema Naye! Limerushwa zaidi ya mwaka mzima. Uamuzi wa kulipiga marufuku leo umechelewa na ni wakuchekesha ati? Ndio maana baadhi ya wachambuzi wa mambo wanakuwa na wasiwasi kwamba amri ya kupiga marufuku tangazo hili itakuwa inalenga kitu, ama ni shinikizo la aina fulani. Ubaya wa tangazo hili hauonekani hadi mtu awe na mtizamo (unafiki) wa aina ya pekee! Kama ilivyo kawaida katika maisha; mwizi humtambua haraka mwizi mwenzake, mchawi humtambua mchawi mwenzake, mlevi humtambua haraka mlevi mwenzake, mzinzi humtambua haraka mzinzi mwenzake..... Lakini mwizi hakubali kuitwa mwizi , mchawi hakubali kuitwa mchawi, mzinzi hakubali kuiitwa mzinzi na mlevi hakubali kuitwa mlevi. Ukitaka magomvi umwambie mlevi kwamba amelewa. Atakwambia: “Pombe umeninunulia wewe?”. Watu wanaotumia kondomu, wanakuwa mstari wa mbele kupinga matumizi ya kondomu! Wale wanauona ubaya wa tangazo la Usione Soo, Sema Naye, ni wale wale!
Wale wanaopinga tangazo hili wanasema msichana na mvulana wanaonekana wakielekea gizani. Walitaka waelekee wapi? Kwenye mwanga? Huko kutakuwa ni kuigiza! Giza ndio ukweli wa mambo. Utamaduni wetu ni wa kufanya mambo haya gizani. Wengine wanasema kwenye wimbo ule wa Ishi kuna binti anayekata kiuno isivyo kawaida. Wanasisitiza kwamba si heshima kuonyesha msichana akikata kiuno kwenye luninga. Unafiki mkubwa! Miziki yote ya Kitanzania ni ya kukata viuno. Ukifungua luninga, ni hiyo tu. Kama tu wa kweli, basi na miziki hiyo ipigwe marufuku!
Msema kweli mpenzi wa Mungu. Kinachopigwa vita kwenye tangazo hili la Usione Soo, Sema Naye! Ni KONDOM. Hili lilikuwa tangazo la aina yake lililoelekeza matumizi ya kondomu waziwazi. Lakini pia ni tangazo lililokuwa limetengenezwa kwa heshima zote maana halionyeshi tendo wala sehemu za siri. Kosa kubwa ni kuhimiza matumizi ya kondomu! Ukiangalia matangazo ya kuhamasisha elimu juu ya UKIMWI, katika nchi nyingine – mambo mengi yanawekwa wazi na kutumia maneno yasiyokuwa na mafumbo yoyote. Mfano mzuri ni wa Uganda. Kwa wale wanaosikiliza redio za Uganda, watakubaliana na mimi – katika lugha ya Kinyankole, kondomu, imepatiwa jina la kitendo cha ngono na inatamkwa hivyo hivyo bila aibu au kificho.
Mzee Swallo, analiweka wazi jambo hili katika barua ya wasomaji:
“ Tunaomba elimu iendelee kutolewa juu ya maana ya UKIMWI, ukubwa wa tatizo, athari za tatizo hili mpaka sasa, tiba au kinga ya tatizo hili. Wataalamu wetu wasianze na sehemu hii ya mwisho, yaani tiba au kinga kwa kutafuta njia ya mkato ya kondomu. Kondomu haina ufumbuzi wa UKIMWI kama mtu hawezi kubadilisha tabia yake, wengi hupenda kuitumia badala ya kuwa waaminifu” (RAI 580).
Wapo watu wengi wenye mawazo kama ya mzee Swallo. Tatizo linalojitokeza ni je, elimu juu ya ukimwi itolewe vipi? Kama njia bora zinazotumika hivi sasa zinapigwa vita zitatumika zipi? Na wale wanaozipiga vita mbinu zinazotumika hawapendekezi njia mpya na wala hawatoi maelekezo kwa vijana. Kazi yao ni kupiga marufuku basi – kutafuata nini, hawana habari. Mbaya zaidi viongozi wetu wako kwenye kundi lenye mashambulizi makali. Baadhi yao wana nyumba ndogo vibustani na watoto. Inaaminika kwamba ugonjwa wa ukimwi, unaenezwa na watu wenye pesa...viongozi wetu wana pesa!
Labda mtu angemhoji huyu mzee Swallo, ana maana gani anaposema uaminifu. Ni nani amefanikiwa kuonyesha uaminifu katika tendo la ngono? Ni ndoa ngapi zimetunza uaminifu? Si kulaumiana uaminifu, na hasa katika tendo hili la kujamiiana, ni kitu kigumu – kama ukweli ndio huo, basi tutumie kinga! Mwenye maoni tofauti na haya, ana uhuru kujitokeza na kutetea uaminifu katika ndoa. Litakuwa jambo zuri la kuondoa mawazo potovu kwamba ni vigumu kukuta familia yenye uaminifu katika ndoa.
John Kerry, ameshindwa urais wa Amerika, baada ya kuonyesha msimamo wake wa kuunga mkono ndoa za mashoga na utoaji mimba. Hakutaka kuwa mnafiki, alisimamia yale anayo yaamini. Viongozi wa dini na hasa kanisa katoliki linapinga sana ndoa za mashoga, utoaji mimba na matumizi ya kondomu. Rais Bush, anapinga ndoa za mashoga, utoaji mimba na matumizi ya kondomu. Hii ilimsaidia kujipatia kura za ziada zilizomsaidia kushinda kwenye majimbo muhimu kama Florida, Iowa na Ohio.
Hapa Tanzania, dini bado zina nguvu. Viongozi wa dini wakishikamana na kuamua kumpiga mtu kisogo ni vigumu mtu huyo kupata mafanikio ya kisiasa kama kushinda kura katika uchaguzi mkuu. Tujuavyo viongozi wa dini wanapinga vikali matumizi ya kondomu. Kuruhusu kondomu ni kuunga mkono uzazi wa mpango, jambo ambalo kanisa katoliki limepiga vita siku zote. Viongozi wa serikali ya Tanzania, wamejifunza kutoka Amerika. Hawataki kukipoteza kiti cha urais kama alivyokipoteza John Kerry, kwa kwenda kinyume na matakwa ya viongozi wa dini. Kupiga marufuku tangazo la Usione Soo, Sema Naye! Ni mbinu za wazi za kisiasa za serikali ya CCM kutafuta kuungwa mkono na viongozi wa dini. Tangazo hili limepigwa vita baada ya uchaguzi wa Amerika! Inawezekana viongozi wa dini walishinikiza siku nyingi lipigwe marufuku, lakini serikali ilikuwa haijafumbuka macho hadi Kerry, alipoanguka!
Viongozi kama waziri mkuu Frederick Sumaye, waliokuwa wameonyesha ujasiri wa kuunga mkono matumizi ya kondomu, sasa hivi wanafanya jitihada zote na kwa gharama kubwa kurudisha uhusiano mwema na viongozi wa dini. Siku za hivi karibu tumemshuhudia Waziri Mkuu Sumaye, akihudhuria sherehe zote za kidini hata na zile ambazo si za muhimu sana. Kupiga marufuku tangazo la Usione Soo, ni msaada mkubwa kwa watu kama waziri mkuu. Hii imemjenga na kurudisha imani yake kwa viongozi wa dini. Hali ilivyokuwa kule nyuma ilikuwa inaelekea Sumaye, kupata kadi nyekundu kutoka kwa viongozi wa dini kufuatana na msimamo wake wa kuunga mkono matumizi ya kondomu. Ni bahati mbaya kwamba hatujapa watu wakusimamia yale wanayoyaamini kama Kerry. Bado, tuna watu wanaofuata upepo ilimradi waingie madarakani! Watu wa namna hii ni wa hatari maana wanaweza kuyumbishwa wakati wowote na kulitelekeza taifa letu.
Kama waheshimiwa wabunge na mheshimiwa rais Benjamin William Mkapa, wameamua kupiga marufuku tangazo la Usione Soo, Sema Naye, kwa vigezo vya kisiasa na kutafuta kuungwa mkono na viongozi wa dini, watakuwa wamebeba dhambi kubwa isiyokuwa na msamaha. Kuzuia mafundisho juu ya ugonjwa huu wa hatari ni dhambi kubwa. Kila mtu ana haki ya kupata elimu juu ya UKIMWI. Ni vigumu kuongelea UKIMWI, bila kugusia matumizi ya kondomu, Ni wazi kuna mabishano makali juu ya matumizi ya kondomu. Wengine wanasema kondomu, si salama asilimia mia moja. Ila inaaminika kwamba ni salama karibu asilimia tisini na tano! Hivyo ni bora kuliko kutotumia – maana asalimia tisini na tano ni nyingi. Wengine wanasema kondomu, ni mradi wa wajanja wa kutengeneza pesa. Wengine wanasema kondomu, zinabeba virusi! Jambo ambalo halina ubishi ni kwamba kwa kiasi kikubwa virusi vya UKIMWI vinasambazwa kwa tendo la ngono. Na kwa vile (tukitupilia mbali unafiki na udanganyifu) hakuna mtu aliyeonyesha ubingwa au ushujaa wa kujizuia kutenda tendo la ngono. Kondomu, inabaki njia pekee na ya salama zaidi katika kuzuia maambukizo. Jambo la msingi kuliko yote katika kupambana na janga la UKIMWI, ni kuizia maambukizo. Tangazo la Usione Soo, Sema Naye, lilikuwa likilenga huko. Bila kuzuia maambukizo kizazi chote kitateketea!
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment