SANGARA NI ADUI WA WAVUVI WADOGO

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA RAI 2004

SANGARA NI ADUI WA WAVUVI WADOGO!


Kabla ya samaki aina ya Sangara, kulivamia ziwa Victoria, kwenye miaka ya sabini, hakukusikika kitu kama uvuvi haramu (kutumia nyavu zisizoruhusiwa na kuvua kwa kutumia sumu), hakukusikika uharamia na ujambazi wa ziwani. Hakukusikika uharibifu wa mazingira kwa upande wa uvuvi. Hakukuwa na viwanda vya kusindika minofu ya samaki kwenye mikoa ya kanda ya ziwa wala soko la nje. Hakukusikika kashfa yoyote ile iliyozunguka wavuvi na biashara ya samaki. Uvuvi uliendeshwa kwa utulivu na ulifanywa na watu waliojulikana kama “wavuvi”. Mara chache kulitokea ajali za mitumbwi kupinduka na kuyapoteza maisha ya wavuvi, na hii ilisababishwa na mitumbwi isiyokuwa imara na iliyokuwa inapakia mizigo kupindukia.

Leo hii tunaongelea uvuvi haramu, uharibifu wa mazingira, uharamia na ujambazi katika ziwa Victoria, kashfa ya minofu ya samaki, rushwa katika idara ya uvuvi na uvuvi umeshambuliwa na watu wengine tofauti ya “wavuvi”. Haya yote yamesababishwa na uvamizi wa samaki aina ya Sangara katika ziwa Victoria na baadhi ya sheria mbovu za nchi yetu.

Sangara ni samaki mvamizi. Si samaki wa asili katika ziwa Victoria. Samaki huyu ameleta faida kubwa kwa upande wa “pato la kitaifa” na viongozi pamoja na matajiri wa nchi hii. Kwa upande wa wavuvi wadogo Samaki huyu ameleta hasara zaidi ya faida.

Samaki wa asili (Endermic Species) wa ziwa Victoria ni: Sato, Nembe, Gogogo, Ningu, Soga,Dagaa, Furu, Kamongo,Ngege, Mumi, Hongwe,Mbofu, Kuyu nk. Samaki hawa walivuliwa kwa kutumia nyavu za inchi 2½ hadi inchi 3. Katika mazingira ya kawaida samaki hawa hawawezi kunenepa kufikia kiasi cha kuvuliwa na nyavu za inchi 5. Samaki hawa ni watamu na wenye lishe bora na walipendwa sana na wakazi wa mikoa ya kanda ya ziwa. Uvuvi ilikuwa kazi ya kudharauliwa na watu wengi hawakuikimbilia.

Sheria inayoongoza uvuvi ni sheria ya uvuvi namba 6 ya mwaka 1970. Leo hii sheria hii imepitwa na wakati inahitaji mabadiliko makubwa. Ilitungwa wakati uvuvi ukionekana kuwa kitu cha watu wachache na kabla ya Sangara kulivamia ziwa na kusababisha vitu kama uvuvi haramu, wavuvi wakubwa(matajiri wenye pesa), uharibifu wa mazingira, ujambazi, uharamia, viwanda vya kusindika minofu na soko la nje. Sheria hii ilitungwa kabla ya watu kugundua utajiri mkubwa uliojificha kwenye ziwa Victoria.

Sheria ya uvuvi namba 6 ya mwaka 1970 kanuni ya 1994 tangazo la serikali No. 370(tarehe 7.10.1994) inapiga marufuku kuvua samaki kwa kutumia nyavu zilizo chini ya inchi 5. Hiki ndicho kilio kikubwa cha wavuvi wadogo wanaolizunguka ziwa Victoria ambao uchumi wao na lishe bora vinategemea kwa kiasi kikubwa uvuvi wa samaki wa asili ambao kwa kawaida huvuliwa kwa nyavu za inchi 2½ hadi inchi 3. Sheria hii inawabana sana, wakikamatwa wakivua kwa kutumia nyavu hizi, nyavu zao zinachomwa moto, wananyang’anywa samaki na wakati mwingine wanawekwa ndani. Kwa kukwepa usumbufu huu, baadhi ya wavuvi wadogo wameamua kutumia ndoana, lakini ili mtu apate samaki wengi kwa kutumia ndoana analazimika kuwa na chambo, na kwa kawaida chombo wazuri ni samaki wadogo, ili kuwapata samaki wadogo ni lazima kutumia nyavu zisizoruhusiwa! Unakuwa ni mzunguko wa umasikini!

Wakati sheria hii ya kutotumia nyavu zisizoruhusiwa inawabana wavuvi wadogo, inatoa mianya ya rushwa kwa wavuvi wakubwa wenye pesa za kuwahonga wahusika na kuendelea kuvua kwa kutumia nyavu zisizoruhusiwa. Hili nitaliongelea baadaye.

Wakati watu wengine wanashikilia hoja kwamba Sangara, alipandikizwa kwenye ziwa Victoria mnamo miaka ya 1960, baadhi ya wataalamu wanasema samaki huyu alitokea ziwa Tana. Mafuriko ya ziwa Tana, kwenye miaka ya sitini, yalimlazimisha samaki huyu kuingia mto Nile na kusafiri hadi ziwa Kyoga. Kutokea Kyoga, samaki huyu aliingia ziwa Victoria. Hadi leo hii samaki aina ya sangara, anapatikana kwenye ziwa Tana. Lakini ni samaki mdogo sana. Ziwa Tana, ni dogo na halina chakula cha kutosha. Wataalamu wamegundua kwamba sangara ananenepa katika mazingira ya ziwa kubwa na lenye chakula cha kutosha kama ziwa Victoria.

Watafiti wa uvuvi wa Afrika Mashariki, walianza kugundua kuwepo kwa sangara katika ziwa Victoria kule Jinja Uganda kwenye miaka ya sabini na miaka mitano baadaye samaki huyu alionekana Kisumu Kenya. Kila baada ya miaka mitano, samaki huyu alikuwa akijitokeza kwenye maeneo mbali mbali ya ziwa Victoria na katika maumbile mbalimbali kama kuendelea kunenepa sana. Sangara wa kwanza mkubwa mwenye kilo zaidi ya 250 alivuliwa Busisi- Mwanza mwanzoni mwa miaka ya themanini. Ndipo ilipogunduliwa kwamba ziwa Victoria lilikuwa limevamiwa na samaki mgeni mwenye mwendo wa kasi kuliko samaki wote akimfuatia papa.
Iligunduliwa pia kwamba tabia ya sangara ni kuwala samaki wengine kwa kasi ya kutisha na kwamba wanazaliana kwa wingi. Samaki mmoja wa sangara, ana uwezo kutaga mayai zaidi ya milioni mbili na asilimia 90 ya vifaranga wanakua na kufikia hatua ya uvunaji kwenye kipindi kisicho zidi miezi mitatu!

Kati ya miaka ya 1982-1989 ziwa Victoria lilikuwa limekwisha jazana samaki aina ya sangara. Samaki wa asili walikaribia kutoweka, maana wengi waliliwa na sangara na wengine walikimbilia pembezoni mwa ziwa na kuvuliwa kwa urahisi. Samaki aina ya Furu, waliokuwa wakilitawala ziwa Victoria, walipotea kabisa. Watu wanaolizunguka ziwa Victoria, hawakumpenda huyu samaki aina ya sangara, alikuwa na mafuta mengi na ukubwa wake ulitisha! Samaki hawa walikuwa wengi sana, na watu hawakujua wafanye nini na samaki hawa. Wale wenye kumbukumbu nzuri watakumbuka kwamba kwa kipindi hiki cha 1982-1989, sangara walikuwa wanaoza tu!

Baadaye wavuvi wadogo, walipata maarifa ya kuwakausha samaki hawa na kuwasafirisha hadi Dodoma, Dar-es-Salaam, Malawi, Msumbiji, Sumbawanga, Kigoma ,Zaire. Soko la sangara likapatikana. Baada ya soko kupatikana na kuonekana sangara ni chanzo kizuri cha mapato, wavuvi wakubwa, au kwa maneno mengine matajiri wa nchi hii wenye uwezo wa kununua mitumbwi mikubwa ya kuongozwa kwa injini, wenye uwezo wa kununua nyavu za inchi 5 na kuendelea ambazo ni za bei ghali, wenye uwezo wa kukausha samaki wengi kwa wakati mmoja, wenye uwezo wa kukodi magari makubwa walilivamia ziwa Victoria. Wavuvi wadogo walisukumwa kando au kubaki ni watumishi wa wavuvi wakubwa. Kipindi hiki ndicho kilishuhudia uharibifu mkubwa wa mazingira. Miti ilikatwa ovyo ili kukausha sangara.

Wakati Tanzania, inahangaika kukausha sangara, Kenya, ilishapata soko la sangara wabichi kule Ulaya. Mwaka wa 1992 “Samaki industry” ya Kenya, ilianzisha viwanda vya kuuza samaki wabichi na kusindika minofu ya sangara kwa soko la Ulaya. Viwanda hivi vya Kenya, vilianza kununua sangara wabichi kutoka Tanzania. Wanunuzi hawa kutoka Kenya, walidai samaki hao walikuwa ni kwa matumizi ya ndani ya nchi Kenya, kumbe ulikuwa uongo. Waliwanunua sangara kwa bei ya chini hapa Tanzania, na kupata faidia kubwa kwa kuwauza kwenye soko la Ulaya. Katika kipindi hiki samaki aina ya sangara walivuliwa kwa kasi kubwa. Matajiri wa Kenya na Tanzania, walianza kuvua kwa kutumia meli za uvuvi za kisasa. Meli hizi zina uwezo wa kuvua samaki wengi kwa muda mfupi. Kipindi hiki ndicho kilianza kushuhudia magari makubwa yenye majokofu yaliyokuwa yakizunguka Musoma, Mwanza hadi Bukoba kununua samaki. Hiki ndicho kipindi pia kilichoshuhudia kwa mara ya kwanza uharamia wa ziwani. Kwa tamaa ya kupata samaki wengi na pesa, wavuvi wakubwa walianza kunyang’anyana samaki ziwani kwa kutumia silaha.

Serikali ya Tanzania, ilizinduka mwaka 1994. Sheria ya Uvuvi namba 6 ya mwaka 1970 kanuni ya 1994, ilipitishwa na ikapiga marufuku kuvua samaki ziwa Victoria kwa kutumia meli za kisasa, na pia ilipiga marufuku kuvua samaki kwa kutumia nyavu zilizo chini ya inchi 5. Lengo likiwa kumlinda sangara, aliyeonyesha kuwa na manufaa makubwa kiuchumi. Serikali, haikuangalia kwa undani, ilitupilia mbali maslahi ya wavuvi wadogo wanaoishi kwa kutegemea samaki wa asili wanaovuliwa kwa nyavu za inchi 2½ hadi inchi 3.

Serikali pia ilizuia sangara wabichi kuuzwa kwa wafanyabiashara wenye viwanda nchini Kenya. Wakenya wenye asili ya Kiasia kwa kushirikiana na watanzania wenye asili ya Kiasia walianza kujenga viwanda vya kusindika minofu ya sangara Mwanza, kwa kupitia mgongo wa utandawazi na uwekezaji. Viwanda hivi vinawanyanyasa wavuvi wadogo na mawakala. Jambo hili linahitaji makala inayojitegemea. Mungu, akijalia nitaiandika siku za mbeleni!

Mnamo mwaka wa 1996, Sangara, ilipata soko duniani kote. Kwa mara ya kwanza serikali ya Tanzania, ikautambua umuhimu wa idara ya uvuvi. Siku za nyuma idara ya uvuvi, haikuonekana kama ina maana yoyote ile. Kwa vile walipuuziwa na kutelekezwa, maafisa uvuvi, walikuwa wakijifanyia kazi nyingine kama kufanya biashara ndogo ndogo na kilimo. Serikali sasa ilianza kuongelea hifadhi ya mazingira yanayolizunguka ziwa Victoria. Sangara, alianza kulindwa! Maafisa uvuvi wakawa na kazi ya kufanya na kuonekana watu muhimu katika jamii. Lakini pia uvuvi ukawa umeingiliwa na vigogo. Mengine yanajulikana na si lazima kuyataja, mfano kashifa ya minofu ya samaki na ukwepaji ushuru.

Kabla ya mwaka 1995, nyavu zilizotumika kuvulia sangara ni zile za inchi 8-12. Maana kwa kipindi hicho walikuwa wakikamatwa sangara wakubwa. Kwa sababu ya uvunaji mkubwa uliosababishwa na viwanda, wavuvi matajiri na soko la sangara nchi za nje, sangara wakubwa walianza kupungua. Hivyo kati ya 1997-1998, zilitumika nyavu za inchi 6-7. Kwa sababu ya uchu wa kupata samaki wengi, wavuvi wakubwa, walianza kutumia hata nyavu za kuvulia samaki wa asili zenye inchi 2½ hadi inchi 3 kuvulia sangara. Hii ilisababisha uvunaji wa sangara wachanga na kutishia maisha ya sangara katika ziwa Victoria.

Kanuni ya 1994, ya sheria ya uvuvi namba 6 ya mwaka 19970, ilipitishwa ili kuwazuia wavuvi wa kubwa kutumia nyavu za kuvulia samaki wa asili, kuvua sangara wachanga. Lakini kanuni hii ilisahau kutilia maanani maslahi ya wavuvi wadogo na wenyeji wanaozunguka ziwa Victoria ambao hawakuwa na uwezo tena wa kula samaki hawa wa biashara. Walikuwa wakiambulia vichwa vya sangara na mifupa inayotupwa na viwanda baada ya kuondoa minofu yote. Zamani samaki ilikuwa mboga ya bei rahisi, mboga ambayo kila mwananchi angeweza kuinunua. Leo hii, kwa sababu ya sheria mbovu, samaki ni mboga ya watu wenye pesa. Inasikitisha pale hata na watu wanaoishi kandokando ya ziwa kushindwa kumudu kutumia mboga ya samaki.

Uvunaji mkubwa wa sangara, na baada ya samaki wa asili kumzoea sangara na kujua namna ya kumkwepa, samaki hawa wa asili walianza kuzaliana tena na kuongezeka. Kufuatana na sheria inayozuia nyavu za wavuvi wadogo, samaki hawa hawavuliwi. Uchumi na lishe wa wavuvi wadogo na wenyeji wanaoishi kandokando ya ziwa Victoria unaendelea kuwa mbaya siku hadi siku wakati wana hazina kubwa ndani ya ziwa Victoria!

Wakati wa kipindi cha neema ya Sangara, wavuvi wadogo hawakufaidika maana samaki wao wa asili walimezwa na sangara na hawakuwa na uwezo wa kujiingiza katika ushindani wa biashara ya sangara. Sasa hivi wakati samaki wa asili wameanza kuongezeka, wavuvi wadogo wanabanwa na sheria ya kutovua kutumia nyavu zilizo chini ya inchi 5!

Ninaandika makala haya kuelezea kilio cha wavuvi wadogo na wenyeji wanaoishi kandokando mwa ziwa Victoria. Ninatangaza mateso ya watu wasiokuwa na sauti, watu wasiojua wamkimbilie nani! Wabunge wao wamewatelekeza kwa kushuhudia, kupitisha na kuzisindikiza sheria mbovu za unyanyasaji, sheria zinazoangalia maslahi ya wakubwa na wenye pesa nyingi.

Ninaandika makala haya kuonyesha wasiwasi wa wananchi walionao juu ya baadhi ya sheria za Tanzania, zinazopitishwa bila tafakari na umakini wa kutosha. Je Bunge, letu ni makini? Je Bunge letu linawawakilisha watu wa aina zote, masikini na matajiri? Ni Bunge la wananchi?

Nimeshuhudia kwa macho yangu jinsi wavuvi wadogo wanavyotimua mbio ovyo wanapoliona gari la afisa uvuvi, nimeshuhudia nyavu za watu masikini zikichomwa moto, watu masikini wasiokuwa na nyumba bora za kuishi, wasioweza kuwasomesha watoto wao, wasioweza kulipia matibabu yao na familia zao, watu ambao utajiri wao wote wanakuwa wameuwekeza kwenye nyavu za kuvulia samaki! Nyavu hizi zinachomwa bila ya utetezi wowote! Nimeshuhudia wavuvi wadogo, tena masikini wakinyang’anywa samaki waliowavua kwa taabu za ziwani za usiku kucha, nimeshuhudia wavuvi wadogo wakikamatwa na kuwekwa ndani. Nimeshuhudia ukatili wa watu wanaoifuata sheria kama roboti bila kutumia akili yao za kuzaliwa!

Nimeandika makala haya kupendekeza kwamba kanuni ya 1994 ya sheria ya uvuvi namba 6 ya 1970, irekebishwe. Mwenye akili nyingi atauliza, Serikali, itatambuaje kwamba nyavu za inchi 2½ hadi 3 zitatumika kuvulia samaki wa asili tu. Jibu, watu wanaoishi kandokando mwa ziwa Victoria, washirikishwe, waruhusiwe kutunga sheria zao za kulilinda ziwa, wenyewe kwa kushirikiana na serikali wahakikishe hakuna mtu anayetumia nyavu za kuvulia samaki wa asili kuvua sangara. Kufuatana na mateso waliyoyapata kutokana na uvamizi wa sangara, kazi hii ya kulilinda ziwa wanaweza kuifanya vizuri. Wanawafahamu wavuvi wakubwa wanaowaingilia. Wanawafahamu viongozi wa serikali wanaokazania sheria kumbe wao ndio wanaongoza uvuvi haramu – kwa vile hawana sauti, wanakaa kimya. Wakipewa sauti, wakipewa nguvu wanaweza kuchangia katika kuleta mabadiliko ya uvuvi katika ziwa Victoria. Hii inaweza kuwa njia bora kuliko unyanyasaji wanaofanyiwa wavuvi wadogo kwa kuchomewa nyavu zao na kulazimishwa kuishi kwenye mzunguko wa umasikini. Njia nyingine ni kuanzishwa kwa ushirika wa wavuvi wadogo. Wizara ya Ushirika na masoko, inaweza kusaidia sana katika jambo hili. Tusikalie kuimba utandawazi, uwekezaji na ubinafsishaji bila kujenga misingi imara ya kuwasaidia watanzania kuogelea katika ziwa hili la kijiji hiki kimoja.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment