MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2005.
MAASKOFU KUPIGANA NI ISHARA YA NINI?
Tarehe 16 mwezi huu gazeti hili liliandika habari za kusikitisha na kushangaza:
“Maaskofu watatu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) wiki hii walipigana makonde na kurushiana viti wakati Halmashauri ya KKKT ilipoketi kujadili ripoti ya tume iliyoundwa kuchunguza tuhuma dhidi ya aliyekuwa Katibu mkuu wa kanisa hilo, Amani Mwenegoha. Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinasema kwamba katika tukio lililofanyika kwenye ukumbi wa Mbagala Spiritual Centre, Dar es salaam, ugomvi huo ulianzishwa na Askofu wa Dayosisi ya Arusha, Thomas Laizer, aliyenyanyuka na kumrukia Askofu mwenzie, Dk Benson Bagonza wa Dayosisi ya Karagwe”. (Tanzania Daima Jumapili Januari 16, 2005)
Kupigana ni kitendo cha kishenzi. Hata kama Askofu Laiser, alikuwa na sababu za msingi dhidi ya Askofu Bagonza, angezijibu kwa hoja na wala si kipigo. Kumpiga mtu ni kumdhalilisha! Hata katiba yetu ya nchi inapinga kitendo hiki. Haki za Binadamu zinapinga kitendo hiki. Ustaarabu na kuelimika kunapinga matendo ya kishenzi kama kupigana. Katika nchi zilizoendelea, kitendo cha Askofu Laiser, ni sababu tosha ya yeye mwenyewe kuwajibika na kuacha cheo cha Uaskofu!
Askofu ni mtu wa aina gani:
“Mtu akitaka kuwa askofu katika Kanisa, huyo anatamani kazi nzuri. Basi, kiongozi wa kanisa anapaswa awe mtu asiye na lawama; anapaswa awe na mke mmoja tu, awe mwenye kiasi, nidhamu na utaratibu, ni lazima awe mkarimu na anayeweza kufundisha, asiwe mlevi au mtu wa matata, bali awe mpole, apendaye amani……….. Anapaswa awe mwenye sifa njema kati ya watu walio nje ya kanisa, ili asije akalaumiwa na kuanguka katika mtego wa Shetani.” (Timoteo 3:2 – 7 ).
Kitendo cha kumpiga Askofu mwenzake, Askofu Laizer, anaondolewa sifa zote zilizotajwa hapo juu. Watu walio nje ya kanisa wanamlaumu na kumkusanya Askofu Laizer, kwenye kundi la watu washenzi, maana kupigana ni kitendo cha kishenzi. Anayepigana anakuwa ameanguka kwenye mtego wa Shetani!
Kupigana si kitendo cha Ukristu. Tunaambiwa katika maandiko matakatifu:
“Mmesikia kwamba ilisemwa: Jicho kwa jicho, jino kwa jino. Lakini mimi nawaambieni, usimlipize kisasi mtu mbaya. Mtu akikupiga kofi shavu la kulia, mgeuzie pia shavu la Pili. Mtu akikupeleka mahakamani kutaka kukuchukulia shati lako, mwache achukue pia koti lako. Na mtu akikulazimisha kuubeba mzigo wake kilomita moja, ubebe kilomita mbili….” (Matayo 5:38 – 41).
Haya ni miongoni mwa mafundisho magumu ya Bwana Yesu Kristo. Ndio maana si watu wote ni Wakristu na si watu wote ni maaskofu. Hata na wale wanaojiita Wakristu, Yesu mwenyewe akirudi leo hii watajificha au yeye mwenyewe atawakana! Tunashuhudia wale wanaojiita Wakristu wakipelekana mahakamani. Majambazi, walarushwa na wenye tabia ya kunyanyasa ndugu zao, ni miongoni mwa wale wanaojiita Wakristu. Hakuna Mkristu anayepigwa shavu la kushoto akageuza na la kulia! Sote ni binadamu na kila mtu ana udhaifu wake. Kwa Mkristu aliyeikubali imani hii, akishindwa kuitekeleza ni lazima kuwajibika. Zipo njia nyingi za kuwajibika, kwa Wakristu walio wengi tendo la kuungama dhambi ni njia mojawapo ya kuwajibika. Lakini haitoshi kutubu, ni lazima kuwepo na ishara ya wazi. Enzi za zamani na leo hii kwa wale ambao wana mtazamo wa kizamani, ishara ya wazi ni kama kufanya kazi za mikono, kama kulima mashamba ya kanisa, kusomba mawe na matofali ya ujenzi wa majumba ya kanisa au mchango wa pesa au wengine kuitesa miili yao kwa kupigwa na kujipiga wao wenyewe na kuichoma miili yao kwa vitu vikali.
Askofu ni mfano wa kuonyesha njia ya kuishi imani ya Kikristu. Anaposhindwa, kama alivyoshindwa Askofu Laiser, ishara ya wazi ya kutubu si kulima kwenye mashamba ya kanisa, kusomba mawe na matofali ya ujenzi wa nyumba za kanisa, au kutoa pesa, ni kujiuzulu kazi ya uaskofu na kuwaachia nafasi wengine wenye uwezo kuhimili mapigo ya dunia hii ya utandawazi.
Ukiuchunguza ule unaoitwa mgogoro wa KKKT, utagundua kwamba kanisa hili sasa hivi linawahitaji maaskofu wa kuhimili mapigo ya dunia ya leo. Mgogoro huu ni magomvi kati ya maaskofu vijana, wasomi na maaskofu wazee ambao walichaguliwa kushika nafasi zao si kwa usomi bali kwa uzoefu. Maaskofu vijana na wasomi wanatumia hoja za kisomi, wazee wanatumia uzoefu na vitisho vya heshima ya uzee na madaraka, ikishindikana hiyo basi ni kiboko maana kwa Mwafrika, mtoto ni lazima achapwe pale anapoonyesha ukaidi. Hayo ndio yalitokea kwa Askofu Laizer mzee na Askofu Benson Bagonza, ambaye ni kijana.
Maaskofu Vijana, hawakubali kuwekwa mfukoni. Wengi wao wamesoma Amerika na Ulaya. Njia za kutafuta wahisani wanazifahamu, lugha ya kuongea nao wanaifahamu, utaalamu wa kuandika miradi wanaujua. Hivyo wanajua njia za kuingiza pesa katika diosisi zao bila ya kumtegemea Katibu mkuu wa KKKT. Maaskofu vijana wanapingana na ukabila, ukanda na lugha ya huyu ni mwenzetu. Wanaiona KKKT, kama kitu kimoja na mtu apewe madaraka kufuatana na sifa zake, si kwa vile ni mtoto wa fulani au mtu wa kabila fulani. Wanapinga kuanzisha diosisi za kikabila, hasa zenye kabila moja.
Bahati mbaya inayowakumba Maaskofu Wazee wa KKKT, ni kwamba mfumo wa KKKT, ni wa kidemokrasia. Hauna chombo chenye nguvu na madaraka kama ROMA, kwa upande wa Wakatoliki. Vatican, inajua kuwadhibiti Maaskofu vijana na wenye mawazo ya kisasa. ROMA, ina mfumo wa kimafia wa kuwafutilia vijana wakati wanasoma. Kama mtu ana mawazo ya kisasa hawezi kupata uaskofu katika kanisa katoliki. Na mfumo wa Kikatoliki, hauruhusu mtu asiyekuwa Askofu, kuingia kwenye mikutano ya maaskofu. Hivyo wakipigana kwenye mikutano yao, siri zinabaki ndani. Si kwamba mambo yao yanakwenda vizuri kuliko ya KKKT, labda yao ni mbaya zaidi, lakini kwa vile wanakutana peke yao, kuta ndizo mashahidi! Na kuta hazina uwezo wa kuandika na kutoa habari kwenye vyombo vya habari! Habari zao zinaweza kuvuja akijitokeza Askofu mkorofi, lakini pia kuna njia za kumtorosha na kumficha kifungoni kule ROMA!
Kitendo cha Askofu Laizer, ni lazima kiwe changamoto kwake yeye na kwa kanisa nzima. Atawezaje kusimama na kufundisha kuvumiliana, kuchukuliana na kuheshimiana. Atawezaje kutoa ushauri katika serikali yetu ambayo sasa hivi inahitaji majadiliano na si ngumi na kurushiana viti? Atawezaje kukemea maovu katika jamii yetu ya Kitanzania. Atawezaje kuwakemea majambazi yanayovamia watu na kuwapiga? Atawezaje kuwakemea wanaume wanaowapiga ovyo watoto wao na wake zao? Atapata wapi nguvu za kufanya kazi zake za kiuchungaji?
Kanisa lianze kufikiria kwa makini kuwapandisha wanawake katika daraja la Uaskofu. KKKT, ina wachungaji wanawake, lakini bado haijakubali kuwa na maaskofu wanawake. Mawazo kwamba Yesu, alimchagua Petro na mitume kuliongoza kanisa hauna utetezi wowote kwenye Agano Jipya. Chenye utetezi ni hiki:
“Mmejengwa juu ya msingi uliowekwa na mitume na manabii, naye Kristo mwenyewe ndiye jiwe kuu la msingi. Yeye ndiye mwenye kulitegemeza jengo lote na kulikuza hata liwe hekalu takatifu kwa ajili ya Bwana. Katika kuungana naye, ninyi pia mnajengwa pamoja na wote wengine, muwe makao ya Mungu kwa njia ya Roho wake.” (Waefeso 2:20 – 22)
Utetezi huu unaonyesha jinsi mtu yeyote yule anayekubali kuungana na Kristo na kusimama juu ya msingi uliojengwa na mitume na manabii anaweza kuliongoza kanisa. Sharti hili haliangalii jinsia! Mawazo ya jinsia yameingizwa na wahuni, wapenda madaraka walioivuruga historia nzima ya kanisa.
Pamoja na huruka ya wanaume ya kupenda madaraka, unyanyasaji, uhuni, ujambazi, ukatili, kutokuwa na huruma, kulipiza kisasi na kupenda vita, wana tabia ya woga. Kristu, alipokamatwa hadi kufa msalabani alikuwa amezungukwa na wanawake peke yao. Inashangaza jinsi Kristu, angefanya uamuzi wa kuacha kanisa lake mikononi mwa watu wenye woga kama wanaume, wakati alijua magumu yaliyokuwa yakilikabili kanisa lake.
Ushuhuda wa Matayo:
“ Na pale walikuwako wanawake wengi wakitazama kwa mbali. Hao ndio wale waliomfuata Yesu kutoka Galilaya wakimtumikia. Miongoni mwao walikuwa Maria Magdalena. Maria mama yao Yakobo na Yosefu, pamoja na mama wa wana wa Zebedayo” (Matayo 27:55 – 56).
Kufuatana na Matayo, hakuna mwanaume aliyekaribia msalaba wa Yesu. Imani ya Kikristu, inasimama juu ya fumbo la msalaba, kufa na kufufuka. Wanaume waliyakimbia matukio haya, iweje waachiwe jukumu la kuyasimamia na kuyaeneza?
Ushuhuda wa Marko na Luka, unafanana na wa Matayo. Wote wanakubaliana kwamba msalabani walikuwepo wafuasi wanawake. Wanaume walikuwa wanaogopa. Wote walimkana Kristu kama Petro. Ushuhuda wa Yohana, ni tofauti kidogo, lakini ni msaada mkubwa maana unafumbua fumbo ambalo limewasumbua watu siku nyingi. Kama Yesu, alimwacha mama yake mikononi mwa wanawake basi na kanisa aliliacha mikononi mwa wanawake. Hakuna popote katika Agano la kale panapoonyesha kwamba Yesu, alikuwa karibu sana na mtume mwanaume, hakuna! Mtu, anayeonyeshwa kuwa karibu naye ni Maria Magdalena. Huyu ndiye aliyeshuhudia ufufuko! Kama tunasema imani ya Kikristu, imesimama juu ya fumbo la msalaba, kufa na kufufuka, shuhuda mkubwa ni Maria Magdalena. Alimsindikiza Yesu, katika maisha yake yote ya taabu na raha, ni mtu pekee aliyeonyesha kumjali hadi kusafisha miguu yake na kuipangusa kwa nywele zake, alimsindikiza hadi Msalabani na kushuhudia ufufuko wake.
“Karibu na msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mama yake na dada ya mama yake, Maria mke wa Kleopa, na Maria Magdalena. Yesu alipomwona mama yake, na karibu naye amesimama yule mwanafunzi aliyempenda, akamwambia mama yake: “Mama! Tazama, huyo ndiye mwanao” Halafu akamwambia yule mwanafunzi: “Tazama, huyo ndiye mama yako”. Na tangu saa ile huyo mwanafunzi alimchukua akae nyumbani kwake.” Yohana 19:25 – 27)
Haiwezekani huyu mwanafunzi aliyependwa na Yesu, awe mwanaume. Haikuandikwa popote na wala hakuna tukio katika Agano Jipya, la kuuonyesha uhusiano wa karibu kati ya Yesu na mtume mwanaume. Hata hivyo hakuna injili inayoonyesha kwamba wanaume waliukaribia msalaba. Hata hivyo waliokuwa na nyumba na mali na kumtunza Yesu, ni wanawake! Luka, anashuhudia jambo hili:
“Pia wanawake kadhaa waliokuwa wamepagawa na pepo, au wagonjwa ambao Yesu, alikuwa amewaponya, waliandamana naye. Hao ndio akina Maria (aitwaye Magdalena), ambaye alitolewa pepo wabaya saba; Yohana, mke wa Kuza, mfanyakazi mkuu wa Herode; Susana na wengine kadhaa. Hao wanawake walikuwa wakiwatumikia kwa mali yao wenyewe.” (Luka 8:2 – 3)
Hakuna mtu mwingine anayetajwa kumtunza Yesu na watu wake, isipokuwa wanawake. Mitume wanaume walikuwa wavuvi na walalahoi. Hawakuwa na uwezo wa mali kumtuza mama ya Yesu na kulitunza kanisa la mwanzo. Kanisa la mwanzo liliishi na kutunzwa kwenye nyumba za wanawake. Ushuhuda wa Paulo:
“Salamu zangu ziwafikie Priska na Akula, wafanyakazi wenzangu katika utumishi wa Kristo Yesu. Wao walihatarisha maisha yao kwa ajili yangu. Wanastahili shukrani; si tu kutoka kwangu bali pia kutoka kwa makanisa yote ya watu wa mataifa mengine. Salamu zangu pia kwa kanisa linalokutana nyumbani kwao.” (1 Wakorinto 16:19)
“Salamu zetu kwa ndugu zetu wa Laodikea; msalimuni dada Nimfa pamoja na jumuiya yote ya waamini inayokutana nyumbani kwake” (Wakolosai 4:15)
“Mimi Paulo, mfungwa kwa ajili ya Kristo Yesu, na ndugu Timoteo, tunakuandikia wewe Felemoni, mfanyakazi mwenzetu na kanisa linalokutana nyumbani kwako, wewe dada Afia, na askari mwenzetu Arkupo.” (Barua ya Paulo kwa Filemoni 1:1 – 2)
Ipo mifano mingi inayoonyesha jinsi kanisa la kwanza lilivyokuwa mikononi mwa wanawake na jinsi wanawake walivyokuwa viongozi bora na imara. Hata historia ya kanisa ina mifano mingi ingawa kwa vile historia hii imeandikwa na wanaume, mifano ya matendo ya wanawake imepuuzwa na kutupwa pembeni!
Maaskofu kupigana ni ishara tosha kwamba wanaume sasa wanaelekea kushindwa kuliongoza kanisa. Ili imani ya watu isipotee, ni wakati mzuri wa kulikabidhi kanisa mikononi mwa wanawake.
Na
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment