KUJICHUKULIA SHERIA MKONONI

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA RAI -2004

KWANINI WATANZANIA WAMEAMUA KUJICHUKULIA SHERIA MIKONONI?

Zamani, wengine watahoji zamani ya lini? Sina maana zamani ya mwaka 2000, kwa wengine ni zamani!, Sina maana zamani ya miaka ya tisini au thamanini katikati, ninamaanisha zamani ya miaka ya 50,60,70 na 80 mwanzoni, kulikuwepo na wahalifu wa aina mbali mbali: majambazi, wezi, vibaka, wahaini nk. Walikamatwa, walifikishwa polisi, polisi walifanya kazi yao kwa uaminifu na uzalendo na wahalifu walifikishwa mahakamani na sheria ilichukua mkondo wake kwa msingi wa haki. Wahalifu walipatiwa haki yao ya kikatiba ya kusikilizwa na kujitetea. Mwamwindi, alinyongwa baada ya kesi yake kusikilizwa kwa muda wa kutosha na baada ya jitihada za serikali za kuhakikisha kama Mwamwindi, alikuwa na akili timamu wakati wa kitendo cha mauaji aliyoyafanya ya aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Iringa. Baada ya mauaji hayo ya kwanza na ya aina yake hapa Tanzania, ya kiongozi wa ngazi ya juu katika serikali, Mwamwindi, alijisalimisha mwenyewe na kuubeba kwenye gari mwili wa marehemu hadi kwenye kituo cha polisi. Polisi, hawakujichukulia sheria mkononi, kwa kumpiga risasi Mwamwindi, hapohapo. Alikuwa amefanya kosa kubwa la mauaji ya kiongozi wa serikali. Aliwekwa ndani na kesi yake iliendelea na kutangazwa kwenye vyombo vya habari. Hakukuwepo na siri hadi kila mtu aliamini kwamba haki ilitendeka!

Wale waliotaka kuipindua serikali ya Kambarage, na njama zao kugundulika dakika za mwisho, kesi yao iliendelea kwa miaka mingi na kutaganzwa kwenye vyombo vya habari. Karibu wahaini wote waliachiwa huru.

Zamani hizo wahalifu waliopatikana na makosa, walipatiwa adhabu ya vifungo. Baadhi yao kifungo ilikuwa ni nafasi ya ukarabati, elimu na toba. Wengi walijifunza mambo mbali mbali kama ufundi, kilimo, ufugaji na lugha mbali mbali. Baada ya kifungo majambazi, wezi na vibaka waligeuka na kuwa raia wema na kuendelea kutoka mchango wao katika kulijenga taifa letu la Tanzania.

Ipo mifano mingi inayoonyesha kwamba zamani kila raia alikuwa na haki sawa mbele ya sheria kama inavyosema katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania:
Ibara 13(1) “Watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki, bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria.
13(3) “ Haki za raia, wajibu na maslahi ya kila mtu na jumuiya ya watu yatalindwa na kuamriwa na mahakama na vyombo vinginevyo vya mamlaka ya nchi vilivyowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria.”
13(6) “Kwa madhumuni ya kuhakikisha usawa mbele ya sheria, mamlaka ya nchi itaweka taratibu zinazofaa au zinazozingatia misingi kwamba :-
(6) a) “ Wakati haki na wajibu wa mtu yeyote vinahitaji kufanyiwa uamuzi wa mahakama au chombo kinginecho kinachohusika, basi mtu huyo atakuwa na haki ya kupewa fursa ya kusikilizwa kwa ukamilifu, na pia haki ya kukata rufani au kupata nafuu nyingine ya kisheria kutokana na maamuzi ya mahakama au chombo kinginecho kinachohusika;
(6) d) “ Kwa ajili ya kuhifadhi haki ya usawa wa binadamu, heshima ya mtu itatunzwa katika shughuli zote zinazohusu upelelezi na uendeshaji wa mambo ya jinai na katika shughuli nyinginezo ambazo mtu anakuwa chini ya ulinzi bila uhuru, au katika kuhakikisha utekelezaji wa adhabu;
(6) e) “ Ni marufuku kwa mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazomtweza au kumdhalilisha.”

Leo hii majambazi, wezi na vibaka wanahukumiwa kifo bila kufikishwa polisi au mahakamani. Wananchi wenye hasira wanajichukulia sheria mkononi. Mtu asiyekupenda, mwenye chuki binafsi nawe, akikunyoshea kidole na kusema wewe ni mwizi, katikati ya jiji la Dar-es-Salaam, Mwanza au miji mingineyo ya hapa nchini, atakuwa anakutakia kifo; utavikwa tairi shingoni, utamwagiwa petroli na kuchomwa moto! Matukio kama haya ni mengi kiasi cha mtu kuwa na maswali mengi juu ya umuhimu wa kuwa na katiba. Watu, ambao wengi wao ni vijana wa kulijenga taifa hili wanapoteza maisha yao kwa kukwapua saa, mikufu ya dhahabu, pesa, simu nk.

Hakuna mtu anayeunga mkono matendo ya ujambazi, vibaka na wezi. Haya ni matendo yanayovunja amani na utulivu katika jamii. Jambo muhimu la kujiuliza ni je, jambazi, kibaka au mwizi hana haki ya kujieleza mbele ya sheria kama inavyotajwa kwenye katiba ya nchi yetu? Je, jamii yetu haina la kujifunza kutokana na matendo haya? Je, jamii haina la kuwafundisha na kuwakarabati majambazi, vibaka na wezi? Je, jambo la msingi ni kuwaua watu hawa au ni kutafuta chanzo cha matendo yao kiovu na kutafuta mbinu za kuyaponya? Vibaka na majambazi wana mangapi ya kuilaumu na kuishutumu jamii yetu? Wana kero ngapi ndani ya roho zao? Ni mangapi yamewazunguka na kuwalazimisha kutenda yale ambayo wasingependa kuyatenda? Je, wanaiba ili kuwapeleka watoto shule? Wanaiba ili kupata pesa za kulipia matibabu? Wanaiba ili kupata pesa za kununua viwanja na kujenga nyumba za kuishi? wanaiba ili wanunue nguo, chakula na kuishi maisha bora? Je, wanaiba ili watoe sadaka na zaka kwenye dini zao - maana pesa zafanana, ziwe za wizi au zile zilizopatikana kwa njia za halali – viongozi wa dini wanapokea tu bila kuhoji – kwao la msingi ni pesa! Wanaiba kwa vile hawana kazi? Au wanaiba kwa vile karibu watanzania wote ni wezi – kama si majambazi wa kuvamia, basi wanaiba na kupora mali ya taifa! Je, bila ya kuwapatia majambazi, vibaka na wezi nafasi ya kuwasikiliza tunawezaje kugundua chanzo? Mbona kadri majambazi, vibaka na wezi wanavyouawa na wananchi wenye hasira ndivyo ujambazi na matendo mengine ya uovu yanavyoongezeka kwa kasi ya kutisha? Je, si kweli kwamba majambazi, vibaka na wezi wanakuwa na watu wengi nyuma yao? Je, si ukweli kwamba matendo haya ya uovu yanaongozwa na vigogo? Vigogo hawa, si wanaendelea kuishi na kuyafurahia maisha wakati watu wanyonge wanakamatwa na kuchomwa moto?

Je, kama uchumi wa nchi unakuwa mikononi mwa watu wachache, tunawezaje kuthibiti ujambazi? Wananchi wanasema majambazi, vibaka na wezi ni kero kubwa katika jamii ya leo. Tofauti na zamani ambapo vibaka na majambazi walikuwa wanashughulikiwa na sheria, siku hizi wakikamatwa baada ya siku mbili au tatu wanakuwa tena mitaani wakienelea na vitendo vyao viovu. Rushwa na hongo inatumika kuwaachia. Hivyo wananchi wanaona njia pekee ya kumaliza kero hii ni kifo. Serikali yetu inayaona haya yakitendeka, badala ya kuyakemea na kuielimisha jamii juu ya kuifuata katiba, utawala wa kisheria, elimu ya uraia na kuheshimu haki za binadamu, inashikwa na kigugumizi. Viongozi wetu kama vile waheshimiwa wabunge wanaogopa kuwakemea wananchi wanaojichukulia sheria mkononi ili wasinyimwe kura. Wanatanguliza maslahi binafsi, bila kutanguliza maslahi na heshima ya taifa letu.

Jambo tunalolisahau wote ni kwamba Tanzania, kuna kero nyingi. Je, kila kero wananchi wakiamua kujichukulia sheria mkononi mwao, ni nani atakuwa salama? Waheshimiwa Wabunge hawatakuwa salama, viongozi wa serikali hawatakuwa salama, viongozi wa kidini hawatakuwa salama, matajiri hawatakuwa salama na sisi sote hatutakuwa salama! Mifano ni mingi. Rwanda, Maaskofu walichinjwa, mapadre, masista, viongozi wa dini mbalimbali, viongozi wa serikali, matajiri na kila mnyarwanda hawakupona. Ni hatari wananchi wakiamua kujichukulia sheria mkononi. Ni bora kuthibiti mapema hali hii inapojitokeza katika jamii.

Msemo wa Waswahili wa: “ Usipoziba ufa utajenga ukuta” utufikirishe. Ilianza kero ya vibaka. Wananchi walichoka na kuamua kujichulia sheria mkononi. Sasa hivi imekuwa ni desturi ambayo ni kazi ngumu kuizuia! Akikamatwa kibaka anavikwa tairi shingoni, anamwagiwa petroli na kuchomwa moto! Ikafuata kero ya majambazi. Wananchi walichoka na kuamua kujichukulia sheria mkononi. Ukisikiliza taarifa ya habari, utasikia jinsi wananchi wanavyowazingira majambazi na kuwaua. Baada ya hapo utasikia pongezi za polisi! Leo hii ni kero ya wavuvi wanaovua kwa kutumia sumu. Mikoa ya Kagera, Mara na Mwanza, inashuhudia mauaji ya kimyakimya ya wavuvi wanaovua kwa kutumia sumu. Iwe ni kusingiziwa au ni kweli unavua kwa sumu, hukumu ni kifo! Inatisha!

Ni tendo baya, la kiovu na la hatari kuvua kwa kutumia sumu. Ni hatari kwa viumbe vya majini, ni hatari kwa maisha ya watu wanaokula samaki na kuyatumia maji ya ziwa Victoria na pia ni hatari kwa soko la nje la samaki. Hakuna ubishi juu ya haya. Swali la kujiuliza ni je mauaji haya yamekomesha kabisa uvuvi haramu wa kuvua kwa kutumia sumu? Mbona kuna habari kwamba sato karibu wote wanaosambazwa nchi nzima ni sumu tupu? Je, watu hawa wanapouawa bila yakufikishwa mbele ya sheria ukweli kwamba miradi hii ya uvuvi wa kutumia sumu inaendeshwa na vigogo ambao wengine ni viongozi wa ngazi ya juu serikalini utajulikana vipi? Ukweli huu wanao hawa vibarua na wanyonge wanaouawa kinyama na kimyakimya. Mauaji haya yanatisha na kutoa picha kwamba sasa hivi Tanzania, haifuati utawala wa kisheria na kuziheshimu haki za binadamu. Ingawa mauaji haya yanatokea kwenye mikoa yote inayolizunguka ziwa Victoria, inashangaza zaidi na kusikitisha mauaji haya yakitokea kwenye jimbo la uchaguzi la Waziri wa Ulinzi, Mheshimiwa Mzee Dr.Sarungi. Nchi zilizoendelea, hili lisingekuwa jambo la kujadiliwa. Waziri, angejiuzulu haraka. Mauaji ya kinyama, ya kimyakimya, yasiyofuata sheria na kuheshimu haki za binadamu, kutokea kwenye jimbo la uchaguzi la Waziri wa Ulinzi ni aibu na kashifa kubwa. Hii ni sababu tosha ya kulifanya jambo hili kuagaliwa kwa makini.

Katika kijiji cha Kyomwami, kata ya Komuge, tarafa ya Suba, wilaya ya Tarime, mauaji ya wavuvi wanaovua kwa kutumia sumu yanaendelea kimyakimya. Hakuna anayeguswa na mauaji haya, isipokuwa jamaa wa karibu sana na marehemu. Miezi kama miwili iliyopita Bwana Paul Tunduye George, wa kijiji cha Kyomwami, aliuawa kwa kushutumiwa kuvua kwa kutumia sumu. Hakuna aliyekamatwa kufuatana na kifo cha Bwana Paul, hadi pale kaka yake Bwana Damiana George, alipowasili kutoka Holland, anakoishi na kufanya kazi mwanzoni mwa mwezi huu. Bahati nzuri alipata ushirikiano mzuri wa polisi makao makuu Dar-es-Salaam na Mara. Baadhi ya watu walikamatwa na kuhojiwa katika kijiji cha Kyomwami. Juhudi za Damian George, za kutaka waliofanya mauaji ya mdogo wake wakamatwe na kufikishwa mbele ya sheria hazikupokelewa vizuri na wanakijiji wa Kyomwami na vijiji vya jirani kama Kinesi,Komuge na tarafa yote ya Suba hadi makao makuu ya wilaya ya Tarime.

Nilipotembelea kijiji cha Kyomwami, tarehe 8.11.2004, nilikuta malalamiko kijijini kwamba Damian George, alikuwa analeta usumbufu kijijini. Hata jamaa zake wa karibu hawakutaka aendelee kufuatilia swala la kifo cha mdogo wake. Mipango ilikuwa ikifanyika ili Damian George, akamatwe na kuwekwa ndani kwa usumbufu aliousababisha wa kuwaleta mapolisi kijijini na kuwasumbua watu. Wakati Damian George, aliamini ni haki yake kikatiba kutetea haki ya watu waonyonge wanaopoteza maisha yao kimyakimya, wananchi walimnyoshea kidole na kumtuhumu kuwa yeye ni adui wa umma!

Wananchi hawataki mtu anayevua kwa kutumia sumu kufikishwa mbele ya sheria. Wanasema mbele ya sheria hakuna haki! Kwamba mbele ya sheria mwenye pesa ndio anapatiwa haki yake. Inaaminika wavuvi wana pesa! Ukiwapeleka mbele ya sheria huwezi kuwashinda! Dawa ni kuwaua kimyakimya. Siku nilipokitembelea kijiji cha Kyomwami, mvuvi mwingine alikuwa ameuawa na hakuna aliyekuwa anajishughulisha kujua chanzo cha kifo chake. Maiti ilikuwa haijazikwa baada ya siku mbili, walikuwa wakisubiri polisi kutoka Tarime! Hakuna aliyeonyesha kusikitika maana walijua kwamba ni hao hao wavuvi wanaovua kwa kutumia sumu na hukumu yao ni kifo tu!

Hakuna ubishi kwamba uvuvi wa sumu ni wa hatari na ni kero kubwa. Swali ni je, kila kero wananchi wakiamua kujichukulia sheria mikononi mwao tutafika wapi? Je, hawa wavuvi wakipewa nafasi ya kujitetea mbele ya sheria si wanaweza kufichua madhambi makubwa yanayozunguka biashara ya uvuvi wa samaki: uonevu wa matajiri, wizi wa mitumbwi, wizi wa nyavu, matambiko(ya binadamu),dhuluma ya viwanda vya samaki, ukwepaji ushuru, wamiliki waviwanda wanaodai ni watanzania kumbe ni hewa tupu hadi kufikia mzunguko unaomgusa kila mtu katika jamii awe ni kiongozi wa serikali, kiongozi wa jadi, kiongozi wa dini nk.! Mwisho wa mwisho kila mtu anaweza kujikuta anahusika!

Na je, kero nyingine ambazo hazijulikani vizuri kwa wananchi, siku zikijulikana itakuwaje? Mfano mmoja. Kata ya Komuge, ina soko kubwa la Nyamaguku. Ni soko linalofanyika kila siku ya Jumanne. Nilikwenda kwenye soko hilo kununua mbuzi, nikakutana na mambo ya kustaajabisha. Mtu anayeuza mbuzi analipa ushuru wa soko na mtu anayenunua mbuzi analipa ushuru wa soko! Ni hivyo hivyo kwa Ng’ombe, kuku na wanyama wengine. Soko lenyewe halina choo, vibanda vilivyojengewa na huduma nyingine za kuhalalisha malipo ya ushuru wa soko. Nilipotaka kujua ushuru huo ulikuwa ni wa kitu gani. Niliambiwa ushuru huo ni kati ya vyanzo vya mapato ya halmashauri ya wilaya ya Tarime! Tunatangaziwa kwamba ushuru mdogo uliokuwa kero kwa wananchi umeondolewa, Wilaya ya Tarime Mbuzi, Ng’ombe, Kuku na wanyama wengine wanatozwa ushuru mara mbili – kwa maana ya anayeuza na anayenunua! Je, siku wananchi wa Komuge, wakifunuliwa juu ya kero hii wajichukulie sheria mkononi na kufanya kama yale wanayowafanyia wavuvi wanaovua kwa kutumia sumu?

Ni imani yangu na imani ya watu waliostaarabika kwamba hakuna mtu anayetamani kuwa jambazi, kibaka au kutenda maovu katika jamii kama vile kuvua kwa kutumia sumu na kuwatoza watu ushuru usioruhusiwa. Kuna mambo mengi yanayochangia hali hii: Siasa mbovu, uchumi mbovu, maadili mabaya, dini za kitapeli, uchoyo wa viongozi wa serikali, dini na jadi, ufa mkubwa kati ya walionacho na wasiokuwanacho.

Ni bora kukaa chini tukatafuta chanzo cha matatizo katika jamii yetu na kutafuta njia za kuyaondoa kuliko kuwaachia wananchi kujichukulia sheria mkononi. Tunaendelea kuwapoteza vijana wenye nguvu ambao kama wangekarabatiwa, kurekebishwa, kuelimishwa, kuelekezwa na kuwezeshwa wangebadilika na kuwa raia wema wa kulijenga taifa letu. Tujifunze kuifuata na kuiheshimu katiba ya nchi yetu. Anayekiuka katiba awajibishwe. Hivyo ndivyo wanavyoishi watu waliostaarabika na kuishi kwa kuziheshimu haki za binadamu.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment