MAKALA HII ILITOKA KATIKA GAZETI LA RAI 2005.
K.K.K.T WANAVUNJA AMANI
Katika makala zangu nyingi kwenye ukurasa huu, nimekuwa napigia kelele huku nikijenga hoja juu ya kujenga jamii yenye maadili. Na wito wangu daima umekuwa ni kujenga maadili ya kitaifa ambamo utu, uadilifu na heshima vinapewa kipa umbele. Msingi wa maadili kitaifa katika taifa changa kama letu, ni kuwepo kwa dhamira na makusudi kwa viongozi wa ngazi zote kujiheshimu na kutanguliza maslahi ya taifa na ya watawaliwa. Yawezekana sana hii ni falsafa isiyovutia masikioni mwa wengi na kwa kweli katika hali tuliyo nayo hivi sasa, wengi wanaposikia hizi kelele zangu wanaweza kukimbilia kusema kuwa ni ndoto zisizowezekana. Uvivu wa kufikiri utaendelea kuwa sumu katika mustakabali wa taifa changa kama letu.
Daima nimekuwa nikisema kwamba ili kujenga taifa lenye maadili, lenye amani na mshikamano tunahitaji mfumo au chombo cha kutufikisha huko. Nimekuwa nikionyesha mashaka juu ya mifumo tuliyonayo kwa sana. Mawazo yangu ni kuunda mifumo mipya au kuboresha ile tuliyonayo. Mifumo ya dini tulizonazo kwa sasa hivi inaweza kuwa mizuri pale tu tutakapofanya jitihada ya kuiboresha. Mfano makanisa, yakiboreshwa yanaweza kutoa mchango mzuri.
Makanisa ni taasisi nyeti sana katika nchi yetu. Watu wengi wanayaheshimu sana kutumainia mema tu kutoka huko. Watawala wa dola wanatazamia makanisa yawe mfano wa uadilifu, uvumilivu na ukomavu wa fikra. Mambo ya makanisa daima hubakia huko huko makanisani, na waumini wakati wote hutoa utii usio na mipaka katika kuwaheshimu viongozi wa makanisa. Kwa maana nyingine, viongozi wa makanisa ni nguzo muhimu katika kuandaa kile ninachokipigania daima yaani, “maadili ya kitaifa”. Watu wamejenga imani ya kupindukia katika makanisa. Makanisa yakienda tenga, jamii nzima inakwenda tenge. Hivyo ni jukumu la viongozi wa makanisa kuwa waangalifu kwa kila jambo wanalotenda kufanyia uamuzi. Ni jambo la lazima viongozi wa makanisa kufanya maamuzi bila kutanguliza maslahi binafsi, bali kuliangalia kanisa zima na taifa letu la Tanzania.
Wiki iliyopita na hii tuliyomo, vichwa vya habari vya magazeti vimeripoti kila siku juu ya mgogoro wa KKKT. Niliwahi kuandika katika ukurasa huu juu ya mgogoro ule na wakati nilihoji juu ya nani ananufaika na mgogoro huu wa kanisa kubwa la KKKT? Sasa ni wazi hakuna anayenufaika na lakini pia ni wazi, ni nani anaumizwa na mgogoro huu. Watu wengi tunajiuliza hivi Mwenegoha ni nani hata maaskofu watwangane makonde mkutanoni? Mwenegoha ni nani hata maaskofu waanikwe aibu yao hadharani? Mwenegoha ni nani hadi mamilioni ya shilingi yateketee kwa vikao visivyoisha na watu waendeshe magari nchi nzima kufanya kampenini ya kumpinga mkuu wa kanisa hilo? Kinachonijia mawazoni kama mmoja wa wanaokerwa na mgogoro huu, ni kuwa tatizo sasa si la Mwenegoha ni la maaskofu wasiokuwa na msimamo; maaskofu wanaotanguliza maslahi yao na ya Mwenegoha; na maaskofu wasiopenda ukweli unaowahusu ujulikane. Matokeo ya kukosa msimamo kwa maaskofu, kumeleta ufa mkubwa katika imani ya watu dhidi ya viongozi wa dini. Hali hii inavunja AMANI na isiachwe kuendelea.
Kitendo cha Askofu kumshambulia mwenzake kwa ngumi kinavunja amani ya jamii. Askofu akipigana, waumini watafanya nini? Yeye ni kiongozi na ni mfano wa kuangalia! Hali hii haitakiwi kufanywa hata miongoni mwa wanasiasa au hata majambazi walio katika kundi la kukamilisha kazi zao. Kwa Askofu kuamua kutumia ngumi badala ya hoja au sala, ni kiwango kwa mwisho kabisa cha ustaarabu wa Askofu huyo. Nimewahi kuona Askofu mmoja katika nchi moja ya Ulaya aliyevuliwa uaskofu kwa kitendo cha kumsalimia mwana mama kisha akamfinya vidole vyake. Kitendo hicho ambacho kwa wengi hapa kingeonekana cha kawaida, kwa wenzetu wanaojali maadili na nafasi ya mtu, kilimwondolea hadhi na heshima ya kuendelea kuwa Askofu. Huyu Askofu aliyeamua kutumia ngumi badala ya hoja na sala, anaweza kujiona ni Askofu lakini ajue anaongoza miili ya waumini na siyo roho zao.
Ninajenga hoja ya KKKT kuvunja amani kwa sababu viongozi wa dini na hasa maaskofu, kwa wengi bado wanaonekana kama watemi na wafalme wenye himaya kasoro bendera. Kwa hiyo Askofu (Mkuu wa himaya) kumshambulia mwingine, ni kutangaza vita kati ya himaya mbili. Himaya ya yule aliyeshambuliwa ingekuwa na kila sababu kutamka kuwa “sababu, nia na uwezo” wanavyo kuhakikisha wanalinda utu na heshima ya himaya yao. Pengine ndiyo maana mtunza hazina wa Askofu wa aliyeshambuliwa aliamua kupoteza maisha yake na kudundwa magumi na Askofu mshambuliaji ili amlinde Askofu wake. Hali hii ya kulindana kwa magumi na kulazimisha maamuzi kwa magumi ni utamaduni mpya si tu ndani ya kanisa bali hata ndani ya jamii. Mwenegoha atakumbukwa kwa kuasisi na kuendeleza utamaduni huu wa magumi mikutanoni, japo unavunja amani.
Wasomaji na waumini tumefika mahali pa kujiuliza kuna nini kati ya Mwenegoha na maaskofu wa Kaskazini pamoja na yule wa Iringa? Kwanini inaonekana wale wanaopinga uamuzi wa Halmashauri kuu ni wa upande mmoja? Wanataka kujenga ukanda ambao ni adui mkubwa wa nchi yetu. Wanataka hata na wanasiasa waanze kuiga mfano huu wa kujigawa kufuatana na ukanda? Hii ni mbegu mbaya ambayo ni lazima ipingwe vita na kila mtaziania mwenye kulitakia mema taifa letu. Mgogoro huu usiangaliwe kwa upande mmoja wa kanisa (KKKT), uangaliwe kwa upana maana watanzania ni wale wale, walio makanisani ndiyo walio kwenye siasa na kwenye nyanja mbali mbali katika taifa letu.
Mwanzoni tulijiuliza kuna nini kati ya Mwenegoha na maaskofu saba? Matamko ya maaskofu saba tuliyasoma magazetini na sasa Mkuu wa kanisa kwa tamko lake wiki hii ametuthibitishia kuwa tuhuma za maaskofu saba dhidi ya Mwenegoha zimethibitishwa na tume iliyozichunguza. Halmashauri Kuu ikaamua kumfukuza kazi Mwenegoha. Kwa hiyo sasa tunajua kisa cha maaskofu saba na Mwenegoha. Bado tunajiuliza kuna nini kati ya Mwenegoha na Maaskofu wanaomuunga mkono? Haiwezekani maaskofu hawa kuamua kuasi maamuzi ya vikao halali na hata kutishia kuunda kanisa lao wenyewe na Mwenegoha bila sababu nzito! Hawa ni watu wazima sawa na wale saba ambao sasa tunaambiwa tuhuma zao zimethibitishwa. Siri ya mshikamano wa hawa maaskofu wa kaskazini na Mwenegoha inavunja amani ya nchi na ni vema ikajulikana kwa sababu mshikamano wao ni maumivu ya waumini na taifa letu.
Maaskofu hawa wanaovunja amani (kwa kuanzisha ngumi mkutanoni na sasa kuchochea kukaidi maamuzi waliyoyapitisha wao wenyewe), ni mfano wa halisi wa mgogoro wa kukosekana kwa maadili ya kijamii. Hata kama Mwenegoha ndiye kiini cha wao kuungana kukaidi maamuzi halali ya kanisa, lakini si Mwenegoha anayeupa uhalali ule mshikamano. Nikiwa mwanakanisa (si Mlutheri), kwangu mimi nauona ule mshikamano kama umejengwa juu ya kulinda uovu wa aina fulani. Ndani ya mshikamano wa namna hii atakuwemo mtu mmoja au wawili aliyeshikilia siri nyingi za kundi hilo ili lisisambaratike. Siku siri hizo zikiwa wazi, kundi litakombolewa na kuwa huru. Tutaanza kuwasikia wakizungumza mikutanoni bila kutumia ngumi na hatutasikia wakitumia magari kuzunguka nchi nzima baada ya vikao ili kufanya kampeni za kubadili maamuzi.
Niliwahi kusema pia makanisa yana miundo mbali mbali iliyo wazi na isiyo wazi. Mfano kanisa Katoliki, mambo mengi mazuri na mabaya yanabaki ndani. Kuna maaskofu wanatunza chuki zaidi ya miaka kumi, wengine wanavunja maadili, wengine wana ukabila, wengine ni walevi kupindukia nk., yanatunzwa kwa mfumo wao umeundwa kisiri na si wazi kama mfumo wa KKKT. Haya yanayovunja amani kutokea katika KKKT yanafanyika pia katika makanisa mengine ila tofauti yake ni kuwa huko hayatangazwi na haya ya KKKT yanatangazwa. Ndani ya makanisa mengine wapo watu kwa sababu ya umri, nafasi, na uzoefu wao ndani ya kanisa wanapata nafasi ya kujua madhaifu ya walio chini au juu yao. Wakati wa mgogoro kama huu, hupenda kutumia nafasi hiyo kuwanyima mateka wao nafasi ya kuwa na uhuru wa kufikiri na kuamua wapendavyo. Kwa nafasi ya uaskofu hii ni tabia ya maaskofu wastaafu wakiitumia vizuri kuwanyima uhuru maaskofu walio kazini. Ikiwa hii ndiyo dhana inayoendelea ndani ya KKKT nashauri maaskofu walio kazini waamue kuasi utumwa huu kwa maslahi ya kanisa na amani katika jamii.
Huko Zambia, kuna Askofu mmoja ambaye kabla hajawa Askofu mlevi na mvuta sigara kupindukia. Ulevi ule ukamfanya ambake mtoto wake wa kike na kufanya mapenzi naye! Aliyekuwa Askofu wakati huo akalitunza jambo hilo likaishia ndani ya nyumba ile na huyu mume (Askofu sasa) akaacha ulevi na sigara, lakini pia mke wake akaacha kujuana na mmewe. Yule Askofu mzee alipostaafu akahakikisha huyu mrithi hawi na uhuru wa kuamua kwa sababu ya dhambi ile. Licha ya kuwa dhambi ile sasa inajulikana, lakini Askofu wa sasa ameshindwa kabisa kujikomboa na hawezi kuamua lolote mpaka Askofu mzee atakapokufa. Askofu mzee anakiuka maadili ya kutubisha dhambi pale anapowaweka utumwani wale waliotubu kwake. Hili kama linatokea katika mgogoro wa KKKT ni kosa la maaskofu vijana na si la wazee au Mwenegoha anayejua madhambi ya hawa maaskofu. Wote tunajua kuwa maaskofu wanazo dhambi na washarika wako tayari kuwasamehe iwapo maaskofu wazee au watendaji kama Mwenegoha watazitaja hadharani. Kufunika dhambi kusivunje amani ya nchi na kudhalilishana kama ilivyotokea Mbagala.
Gazeti moja wiki iliyopita liripoti kuwa tume iligundua ubadhilifu wa fedha nyingi katika KKKT na jingine likaripoti kuwa Mkuu wa Kanisa alilazimika kuvunja ofisi ya Mwenegoha pale Mwenegoha alipokataa kufika katika makabidhiano. Mambo haya pia yanavunja amani. Watu wengi wanaamini kanisani ni mahali patakatifu, hakuna wizi, hakuna ubadhilifu, hakuna ufuska, hakuna kughushi na ukaidi. Itakuwa vema KKKT ili kurejesha imani ya waumini ichapishe ile ripoti ya uchunguzi ili kila mtaziania ajionee maana kanisa ni taasisi ya watu na inakusanya fedha (sadaka) kutoka watu. Aidha kitendo cha kuvunja ofisi ya kanisa kwa kutumia polisi kinaashiria kabisa kuwa Bw. Mwenegoha anazo sababu nyingine zaidi ya zile anazodai ni haki zake. Katika ofisi nyingi hata mtu akisimamishwa kazi kwa wiki moja anakabidhi ofisi. Mwenegoha amefukuzwa kazi na hakuenda mahakamani hadi ofisi zinavunjwa. Ukaidi wa namna hii katika ofisi ya umma ni kuvunja amani.
Mwisho KKKT inavunja amani pale ambapo inafumbia macho vitendo viovu viendelee ndani ya kanisa kwa muda mrefu bila kuvishughulikia. Ni wazi matendo maovu kama hayo yanayotajwa na vyombo vya habari kama ni ya kweli, yanaiweka hata serikali mahali pagumu maana serikali inayaheshimu mno makanisa. Lakini kwa sasa kwa kuwa ni wazi KKKT inavunja amani ni vema serikali ikalichukulia hili kwa uzito wake. Hufika wakati hata wale tuliowadhania wana hekima wakabainika wamefilisika. Nani alijua dayosisi za Kaskazini ambazo ndizo kitovu cha Ulutheri leo ziwe msitari wa mbele kutetea kinachoonekana wazi ni kinyume kabisa na sura ya kanisa? Sasa si tatizo tena la Mwenegoha, ni tatizo la maaskofu wanaomkumbatia Mwenegoha. Kwa manufaa ya taifa letu, ni vyema maaskofu hawa wakamaliza tatizo hili vinginevyo watapunguza nguvu za kanisa katika kulinda na kutetea amani katika taifa letu.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment