MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA RAI 2005
Wednesday, August 10, 2005
HATA NJAA NI HATARI KULIKO
UKIMWI!
Siku chache baada ya hotuba ya Rais wa Jamhuri ya muungano wa` Tanzania, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, kwa wananchi,31Julai 2004, hotuba ambayo ilielezea hatari ya ugonjwa wa Malaria, kwamba ugonjwa huo unaua watu wengi kuliko UKIMWI, nilimsikia Mheshimiwa Makamba, mkuu wa Mkoa wa Dar-es-Salaam, akipiga kelele kwamba ajali za mabarabarani zinaua watu wengi kuliko UKIMWI!! Si lengo la makala haya kupingana na waheshimiwa wanaofikiri kwamba Malaria na ajali za barabarani ni hatari zaidi ya UKIMWI.
Lengo ni kuongezea hapo, kwamba hata na baa la njaa ni hatari na linaweza kuua watu wengi kuliko UKIMWI. Kwa maneno mengine ni kwamba bila mpangilio mzuri wa kuihudumia Jamii, kila kitu kinaweza kuwa hatari. Ni jukumu la serikali inayoongoza kutekeleza sera ( kama zipo) za chama tawala za kuihudumia jamii husika. Serikali yenye utawala bora inaelekeza matumizi ya pato la taifa katika kuidumia jamii. Ethiopia, ilipokumbwa na baa la njaa, watu wengi na hasa watoto walipoteza maisha yao, ukweli huu haukuizuia serikali ya Ethiopia, iliyokuwa madarakani kwa wakati huo kuendelea kulitumia pato la taifa kwa mambo yasiyokuwa ya msingi! Viongozi wa serikali ya Ethiopia, waliendelea na safari zao za Ulaya za mapumziko na matanuzi, waliendelea kujenga majumba ya kifahari, waliendelea kuwasomesha watoto wao nchi za nje kwa kutumia pato la taifa lao. Mbaya zaidi waliendelea kutumia pesa za taifa lao kununulia silaha za kuwalinda waendelee kukaa madarakani wakati wananchi wanaendelea kufa kwa njaa. Tatizo la njaa la Ethiopia, lilishughulikiwa na mataifa ya nje, kuliko lilivyoshughulikiwa na viongozi wa nchi hiyo! Mungu, apishe mbali ikitokea hapa Tanzania, tukakumbwa na baa la njaa, ni kiasi gani cha watu watakufa? Ni wazi wengi kuliko wale wanaokufa kwa ugonjwa wa UKIMWI, lakini je ukweli huo unaweza kuyazuia mashangingi kuendelea kutembea? Misafara ya RAIS na viongozi wengine wa serikali itapungua? Viongozi wa serikali wataacha kutibiwa nje kwa gharama kubwa?
Ajali za barabarani zinatokea kila siku. Ni nani anajali kufuatilia chanzo cha ajali hizo? Magari ya abiria yanapakia kupindukia, ni nani anajali kufutilia? Polisi, wana njaa, wakipewa senti kidogo wanaachia magari yaendelee na safari. Au magari hayo ni mali ya vigogo serikalini ?– ni nani ana uwezo wa kulizuia gari la kigogo hata kama gari hilo ni bovu na halifai kuwapakia abiria? Bila mpangilio mzuri wa huduma za jamii, kila kitu ni hatari.
Rais Mkapa, katika hotuba yake anatuelezea kwamba, Nusu ya vifo vyote barani Afrika husababishwa na magonjwa yanayozuilika na kutibika kama ilivyo malaria. Barani Ulaya ni asilimia 2 tu ya vifo husababishwa na magonjwa hayo.
Ni kwa nini? Viongozi wa Serikali za nchi za Ulaya, wana mpango mzuri wa kushughulikia huduma za jamii. Tofauti na viongozi wa Afrika. Viongozi wa Afrika, wanaangalia matumbo yao, anasa, majigambo na mashindano ya mtu binafsi. Marehemu Mobutu, alikuwa akitumia ndege ya rais na pesa za watu masikini wa Zaire, kwenda Amerika, kukata nywele!! Ninasikia kinyozi huyo alikuwa akilipwa zaidi ya dola 50,000 kwa safari moja! Katika kichaa kama hiki ni lazima magonjwa yanayotibika yawatafune Waafrika maana kiasi kikubwa cha pato la kitaifa kinatumika kumhudumia mtu mmoja. Kiongozi mwingine wa Afrika, alikuwa anatumia ndege ya serikali kuwapeleka watoto wake shuleni Ulaya, asubuhi na kuwarudisha jioni!! Rais, mwingine alitumia pesa nyingi kwa mashindano ya kujenga kanisa kubwa kuliko la mtakatifu Petro la Roma! Juzi tu tumesikia kelele za Waganda, kwamba Rais Museveni, alitumia ndege ya Rais, kumpeleka mtoto wake Ujerumani, kujifungua! Wanasema pesa zilizotumika zingeweza kuwasaidia wanawake zaidi ya 500 kujifungua salama nchini Uganda. Ipo mifano mingi inayoonyesha kwamba watawala wa Afrika, wanafanya vituko vya kusikitisha badala ya kutumia rasmali za nchi zao kushughulikia huduma za jamii.
Kama takwimu alizozitoa Rais Benjamin, ni za kweli, basi hali ni ya hatari na inaonyesha kuna kasoro kubwa katika uongozi wa taifa: “ Malaria huua wastani wa Watanzania 100,000 kila mwaka, yaani sawa na kuua mtu mmoja katika kila dakika 5”
Matamshi kama haya, yangetolewa na kiongozi wa nchi zilizoendelea, kesho yake vyombo vya habari vingejaa habari za kumtaka kiongozi huyo kujiuzulu!! Haiwezekani katika nchi zilizoendelea kiongozi wa nchi ataje kwamba watu 100,000 wanakufa kila mwaka kwa ugonjwa unaotibika, akaendelea kutawala.
Lazima maswali yangekuwa mengi: Kwani serikali haikupanga mipango ya kupambana na malaria? Kwanini serikali haikusambaza vyandarua na madawa? Kwanini serikali haikuwaelimisha wananchi juu ya hatari ya ugonjwa wa malaria. Kila mtu angechunguza bajeti ya serikali na kuangalia ni kitu gani kilipewa kipaumbele na kupuuzia ugonjwa wa hatari. Wangeagalia magari, ndege,posho za viongozi, safari za viongozi na matumizi mengine yasiyokuwa ya lazima sana. Vifo 100,000 kila mwaka ni vingi. Uchunguzi ungefanyika na kuiweka serikali Kitimoto- hasa kushinikiza wanaohusika kuwajibika.
Sisi tunaelezwa kwamba watu 100,000, kila mwaka wanakufa kwa ugonjwa wa malaria, na Rais wetu anaeleza haya bila woga wowote na kwa kujiamini, tunabaki kimya. Tunajua wazi serikali ina mpango wa kununua ndege ya Rais, kwa mamilioni ya pesa. Kwanini pesa hizo hazikutumika katika mpango wa kuitokomeza malaria? Serikali yetu ina vyanzo vingi vya mapato: Watalii, wanaingia nchini mwetu kwa maelfu, hawa wanaleta pesa za kigeni. Tuna migodi mingi, una viwanda vinauza minofu ya samaki nje ya nchi na kuingiza mamilioni ya dola, makampuni ya wawindaji kutoka nje yanaingiza mamilioni ya dola kila mwaka, tunazalisha mazao mengi nk., si kweli kwamba uwezo wa Serikali ni mdogo kama anavyotaka tuamini Mheshimiwa Rais, wetu. Serikali yenye uwezo mdogo haiwezi kuwa na mpango wa kununua ndege ya Rais, na kuwa na uwezo wa kuwatibisha viongozi wa juu Serikalini kule Ulaya, kuwa na uwezo wa kumuda msafara wa magari zaidi ya kumi mumsindikiza Rais,Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na Mawaziri wengine wanaopenda mbwembwe za ukubwa wanapoyatembelea majimbo yao. Ukiangalia bajeti inayotumika kuwatunza viongozi wetu, inakuwa vigumu kuamini kwamba Serikali yetu ina uwezo mdogo.
Ni imani yangu kwamba hakuna Mtanzania asiyejua hatari ya malaria. Hata mtoto mdogo anajua kabisa dalili za malaria. Hata bila vipimo atakwambia ana malaria na ukimpima utakuta ana malaria. Mwaka, 1982, karibia nipoteze maisha kule Ujerumani. Nilisikia dalili za malaria, nilikwenda kwa daktari mjerumani na kumwambia anipatie dawa za malaria. Daktari huyo hakuamini, alisistiza kunipima kwanza. Hakuelewa nijueje nina malaria bila kunipima. Kupima kulichukua muda mrefu, unaju tena ukiwa mwafrika wanataka wapime kila kitu. Huku mimi nilikuwa hoi, malaria iliendelea kupanda. Wakati wanagundua kuwa nilikuwa na malaria, nilikuwa katika hali ya kutisha! Sisi tunaifahamu malaria – hasa watu wa vijijini wanaifahamu vizuri. Hakuna haja ya kuwaelezea wala kuwakumbusha. Tatizo ni wafanye nini:
Zahanati za vijijini hazina madawa, watu wa vijijini hawana uwezo wa kununua vyandarua - wale wenye uwezo wanahitaji kuelimishwa. Ni kazi ya serikali kuwaelimisha watu. Mfano, watu wanapoteza pesa nyingi kwenye pombe. Wanakunywa pombe bila kuzijali afya zao na za familia zao. Pesa wanazozitumia kwenye pombe zinatosha kumnunulia kila mwanafamilia chandarua na kumtibisha.
Elimu ni muhimu sana kule vijijini. Siku moja nilikuwa nikiongoza ibada ya Jumapili, familia moja ilitoa sadaka ya shilingi 1500. Baada ya ibada, familia hiyo iliniomba msaada wa usafiri kumpeleka mtoto hospitali. Nilipotaka kujua ni kwa nini mtoto hakupelekwa hospitali hadi malaria ikapanda hivyo, nilijibiwa kwamba hawakuwa na pesa. Niliamua kuwarudishia pesa zao walizokuwa wametoa sadaka ili wazitumie kumtibisha mtoto. Ni wazi niliiingia matatani baadaye kwa kulaumiwa kuzitumia pesa za sadaka vibaya; heshima, ni kwamba mtoto alipona! Vijijini watu wanaweza kupata shilingi 1500 kutoa sadaka au kuchangia sherehe za kumkaribisha mkuu wa wilaya kijijini wakashindwa kupata pesa za kununua dawa za kumtibu mtoto!
Tunaimba kwamba kilimo ni uti wa mgogo wa uchumi wa taifa letu. Tunajua wazi kwamba kilimo kwa asilimia kubwa kinaendeshwa na watu wa vijijini. Ni watu hawahawa wanaoshambuliwa na malaria, ugonjwa unaotibika na kuna uwezekano wa kujikinga mtu asishambuliwe na mbu. Kwanini basi serikali isiwe na mpango maalumu wa kupambana na malaria? Kwanini serikali isinunue vyandarua na kuvisambaza vijijini, kwa nini serikali isihakikishe zahanati zetu zote zina madawa ya kutibu malaria?
“ Kinachosikitisha zaidi ni kuwa wengi wa wanaougua na kufa kwa malaria ni watoto wetu wadogo wenye umri wa chini ya miaka 5. Kitakwimu, tangu nimeanza kuzungumza nanyi, dakika tano zilizopita, watoto zaidi ya 300 wameambukizwa malaria na wanaweza kufa. Kila mwaka tunapoteza watoto 70,000 wanaokufa kwa malaria. Yaani, kwa kila vifo 10 kutokana na malaria, 7 ni vya waoto hao chini ya umri wa miaka5” (Hotuba ya Rais).
Huwezi kusema ukweli huu katika nchi zilizoendelea ukategemea utaendelea kuwa kiongozi wa nchi. Kwanini ugonjwa unaotibika uendelee kutupokonya taifa la kesho? Hawa wanaokufa si watoto wa viongozi, si watoto wa matajiri, ni watoto wa masikini – ni watoto wa vijijini. Hawa ni watoto wanaoishi kwenye nyumba za kimasikini ambazo hata wakipewa vyandarua hawezi kupata mahali pa kuzifunga! Tunapoongelea malaria, hatuwezi kukwepa jambo la uchumi. Rais, wetu anasema kwamba, Tanzania tunasogoza kwa vifo vya malaria katika nchi zote za SADC. Maana yake ni kwamba Tanzania, tunaongoza kwa umasikini katika nchi za SADC. Pia, tunaongoza kwa mbwembwe za viongozi; misafara ya viongozi wetu inatumia pesa nyingi. Hatutaki kuonyesha maendeleo yetu katika kuboresha huduma za jamii. Tunataka kuonyesha maendeleo yetu katika magari ya bei mbaya, nyumba za kifahari, mavazi ya gharama kutoka kwenye maduka makubwa ya Ulaya na kuwa na ndege ya kisasa ya Rais.
Ninajua ni dhambi kubwa kumwambia Rais, ajiuzulu – kama mawaziri wanashindwa kujiuzulu kwa makosa yaliyowazi, itakuwa Kamada wao! Lakini tukitaka kuwa wawazi na kufuata falsafa ya Uwazi na Ukweli, Rais, kutamka na kukiri kwamba watu 100,000 wanakufa kila mwaka kwa malaria, ugonjwa unaotibika, analazimika kuwajibika kwa kujiuzulu;
Vinginevyo kujitokeze utetezi: Mwaka 1995, wakati ninaingia madarakani idadi ya watu waliokuwa wanakufa kwa malaria kila mwaka ni 300,000 Idadi hii ilipungua na kufika 200,000 mwaka 2000 nilipochukua uongozi kwa kipindi cha pili. Sasa hivi ninapoelekea kumalizia kipindi changu cha pili, idadi ya watu wanaokufa kila mwaka kwa ugonjwa wa malaria imepungua na kufikia 100,000!, Huu unaweza kuwa utetezi! Maana inaonyesha kwamba juhudi fulani imefanyika. Lakini kusema tu kwamba Tanzania, inawapoteza watu 100,000 kila mwaka kwa ugonjwa wa malaria na kwamba Tanzania inaongoza kwa vifo vya malaria katika nchi za SADC, inatosha kukiweka chama cha CCM, kiti moto katika uchaguzi wa mwaka kesho.
Sasa hivi njaa inanyemelea. Kwanini tuwe na uhaba wa chakula wakati tumezungukwa na maziwa makubwa matatu? Bila kuitaja bahari ya Indi? Ni bora kuwa macho, bila mpangilio kila kitu ni hatari kubwa. Tusiangalie malaria na ajali za barabarani tu! Kuna njaa, tishio la ukosefu ajira ujambazi, watoto wa mitaani nk.
Hapa ni lazima kukumbuka ushauri wa bure: Adui wakubwa wa nchi hii, adui wakubwa wa serikali na chama tawala, si wengine bali ni wale wanaouona ukweli wa mambo na kukaa kimya. Ni wale wanaokaa kimya kuyalinda maslahi yao; hawa ni hatari kubwa kuliko UKIMWI!
Na, Padre Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment