ASKOFU MWOLEKA- KUMBUKUMBU YA MIAKA MIWILI

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA RAI October 10, 2004

MAREHEMU ASKOFU CHRISTOPHER MWOLEKA- KUMBUKUMBU YA MIAKA MIWILI

Wanyakyusa, wana utamaduni mzuri wa kumaliza matanga. Niliushuhudia utamaduni huu mnamo mwaka wa 1986,nilipoishi Mbeya. Baada ya mwaka mmoja wa kifo cha marehemu, na hasa kama mtu huyo alikuwa ni mzee, huandaliwa kikundi cha ngoma kikiandamana na ndugu, jamaa na marafiki, ambacho huzunguka Sehemu zote kijijini ,vijiji vya jirani na mjini alipokuwa akipendelea kutembea marehemu. Kazi inayofanyika kwenye sehemu hizo ni kuimba, kucheza, kunywa na kufurahi kwa lengo la kufuta kabisa kumbukumbu za marehemu. Ni njia ya kujihakikishia kwamba sasa marehemu hayupo kati yao tena.

Kesho kutwa tarehe 16.10.2004, ni kumbukumbu ya miaka miwili ya kifo cha marehemu Askofu Christopher Mwoleka, aliyekuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge(Mkoa wa Kagera). Labda zamu hii, tofauti na mwaka jana, utamaduni wa Kinyakyusa ungetusaidia. Tuandae kikundi cha ngoma: Saida Karoli, Mau,Kakau Band au kikundi cha Taarabu (Marehemu Askofu Mwoleka, alipendenda kusikia nyimbo na kuangalia mikanda ya taarabu, siku za mwisho wa maisha yake) tuzunguke sehemu zote alizopenda kutembelea Askofu Mwoleka, tucheze, tuimbe, tule na kunywa na kufurahi kama njia mojawapo ya kujihakikishia kwamba sasa Mwoleka hayupo kati yetu tena. Safari yetu ni lazima ianzie Nyabihanga, wilayani Ngara, kilichokuwa kijiji cha ujamaa, alichokianzisha na kuishi Askofu Mwoleka, kwenye miaka ya sabini. Safari yetu itupeleke hadi Karagwe-Bushangaro, yaliyokuwa makao makuu ya jumuiya yake ya Mkamilishano,alipapenda sana Bushangaro,alitamani kuzikwa hapo ingawa “Hekima” ya kanisa haikuruhusu! Tukiwa na pesa za kutosha ni lazima safari yetu iendelee hadi Morogoro na Dar-es-Salaam, kwenye jumuiya Integration. Pamoja na kwamba jumuiya ya Integration, ilimtumza kwenye nyumba zake na Dar na Morogoro, Askofu Mwoleka, alikuwa na mapenzi makubwa na mji wa Dar. Aliishi Dar, wakati wa ujana wake. Wito wa kuwa padre aliupata akiwa Dar-es-salaam, kwenye kanisa la Mtakatifu Joseph, akiwa kijana mzima wa miaka 28!Pacha wake Mheshimiwa sana Padre John Joseph Rwechungura, wa jimbo katoliki la Bukoba, anaifahamu vizuri zaidi historia hii. Ili safari yetu iwe ya mafanikio ni lazima itupeleke hadi Roma Italia, kwenye kanisa la Mtakatifu Petro, chini ya miguu ya sanamu ya mtakatifu Petro, alipokuwa akikimbilia Askofu Mwoleka, kusali na kufunga alipokuwa akitingwa na jambo. Na ili kufuta kabisa kumbukumbu za Mwoleka, tungelazimika kukamilisha safari yetu nchini Ujerumani na kuongea na Mama Wallbrecher, mwanzilishi wa jumuiya ya Integration, jumuiya aliyoiona Askofu Mwoleka, mwaka wa 1977,akasema maneno yaleyale ya “Yametimia Bwana, sasa waweza kumchukua mtumishi wako...”.Mama Wallbrecher, ni mama wa kipekee, mwenye imani imara, upendo wa kanisa na ubinadamu, upeo, karama, na theolojia ya kisasa ya kulipatia kanisa sura mpya!

Wasiwasi wangu ni kwamba utamaduni wa Kinyakyusa, ungeshindwa kufuta kabisa kumbukumbu ya Mwoleka, kwenye nyoyo za watu walioishi na kufanya kazi naye kwa karibu. Alikuwa ni mtu mwenye matendo yasiyosahaulika haraka:

Mfano: Mwoleka, alikuwa mtu mwenye ukarimu mkubwa. Hakujua amsaidie mtu hadi kiasi gani wakati mwingine kiasi cha yeye kubaki mifuko mitupu! Hakujua kupima kiwango cha zawadi. Angeweza kumnunulia mtu kilo 25 za nyama, kusalimia msiba au kumpongeza mtu aliyepata mtoto, badala ya kilo mbili au tatu. Angeweza kumzawadia mtu sukari kilo 50, badala ya kilo nne au tano. Kwa rambirambi za msiba, ambazo kijijini tunatoa elfu moja hadi tano, yeye alitoa laki yote! Tulimpachika jina la “Old Man of the Big quantity”.Mtu aliyekuwa mbali naye angeshawishika kusema, Anafuja mali! Hakuambatana na mali wala pesa. Aliambatana na wanadamu na Mungu wao!
Yeye alikuwa hanywi pombe, na si kwamba alikuwa anakunywa na kuamua kuacha baada ya kushukiwa na Roho wa Bwana! Hakunywa kabisa, lakini nyumba yake ilikuwa na pombe za aina mbali mbali kwa kuwakaribisha na kuwafurahisha wageni wake. Yeye alikuwa tofauti na watu wengine ambao huanzia kwenye ulevi, tena ulevi wa kupindukia wa kuvua nguo nakutembea uchi, wakishukiwa na Roho Mtakatifu na kuacha ulevi na kuacha kuonja pombe kabisa, wanakuwa na misimamo mikali ya kuchukia pombe na kuwachukia marafiki zao walevi waliokuwa wakipigana na kubebana enzi zile za ulevi, Wanafiki wakubwa. Askofu Mwoleka, hakuwa mnafiki!

Askofu Mwoleka, asingeweza kula chakula bila kuhakikisha anawahudumia (yeye mwenyewe) wale wote aliokaa nao kwenye meza ya chakula. Wakati mwingine alihitaji msaada wa kumkumbusha alipokula chakula au kuwakaribisha watu hotelini, aliendeleza huduma yake huko! Alikuwa ni mtu wa kuwahudumia wengine. Alikuwa mtumishi, si utumishi wa ishara na maneno, bali matendo. Aliwafulia watu nguo zao, aliosha vyombo baada ya chakula, aliwalimia watu mashamba yao, alishiriki kuvuna mazao, kujenga nyumba nk.

Mbali na ukarimu wake, kitu kingine ambacho hakisahauliki kwa urahisi katika maisha ya Askofu Mwoleka, ni nia yake ya kutaka kuwajengea nyumba bora na za kisasa wananchi masikini wa Karagwe,Biharamulo na Ngara. Hakupenda kuishi kwenye nyumba bora zaidi ya nyumba za wenyeji waliokuwa wakimzunguka. Kama kuna dhambi kubwa aliyoiacha nyuma yake ni kushindwa kujenga nyumba ya kifahari ya Askofu na wala hakuwa na mpango. Kilichomsumbua sana ni kuwajengea watu masikini nyumba bora, imara na za kisasa. Wazo hili lilimchukulia muda wake mwingi. Yeye alikuwa ni mtaalamu wa kutumia mashini ya kuchapa na computer. Hivyo alichora kwa kutumia mashini ya kuchapa na computer michoro ya nyumba hizi alizotaka kuwajengea watu masikini. Kilichomsumbua zaidi ni kujenga nyumba bora na za kisasa kwa gharama nafuu. Sementi ilikuwa inapatikana kwa shida na kwa bei ya juu. Padre Jacob Mwenge(marehemu), alimshauri kwamba kulikuwa na uwezekano wa kujitengenezea sementi, na yeye alimhakikishia kuufahamu mmea fulani unaoashiria kuwepo sementi kwenye ardhi. Baada ya kuutambua mmea huo, ambao na mimi nilionyeshwa, Askofu Mwoleka, alianza kuyazungukia mapori yote ya Biharamulo,Ngara na Karagwe, akitafuta uwezekano wa kupata sementi kwa kuangalia mmea alioonyeshwa na Padre Jacob Mwenge! Huyu Padre, alikuwa mzaliwa wa Bukoba, lakini mwenye asili ya Uganda. Alikuwa mtaalamu wa mambo mbalimbali mnyenyekevu kupindukia, hakuna na tamaa ya mali, alimiliki kanzu lake na kiko! Alikuwa mtu wa kuaminika, hivyo Askofu Mwoleka, alimwamini na kuwa na matumaini ya kupata sementi kwa kuichimba ardhini!

Kwenye barabara ya Karagwe-Ngara,pori la Kimisi, siku hizi maarufu kama pori la majambazi, kuna mti unaojulikana kwa jina la “Mti wa Askofu”. Wakati wa safari zake nyingi za Karagwe-Ngara, Askofu Mwoleka, alizoea kusimama kwenye kivuli cha mti huo na kupumzika kidogo, aliamini mti huo ilikuwa alama ya katikati ya safari ya Karagwe-Ngara. Aliugundua mti huo akiwa kwenye harakati za kuutafuta mmea wa sementi! Watu wengi hawakujua ukweli huu. Zoezi zima la sementi lilishindwa!

Baadaye walijitokeza wataalamu kutoka Kigoma, sisi tuliwapachika jina la “Self made geologist”, wataalamu hawa walidai kwamba miamba ya mlima ulio karibu na Keza, kwenye barabara ya Nyakahura-Rulenge,ingeweza kutengeneza chokaa. Utaalamu wenyewe ilikuwa ni kuipasua miamba na kuyachoma mawe kwa moto mkali sana, yakishachemka sana unayamwagia maji na kuyeyuka, vumbivumbi anayotokana na myeyuko huo inatengeneza chokaa. Mawe alichomwa kwelikweli. Yalipomwagiwa maji hakuna kilichotokea! Yalibaki vilevile! Mradi huu ulichukua pesa nyingi bila ya mafanikio yoyote. “Wapelelezi wa Roma” waliomshitaki Askofu Mwoleka, kwa kosa la ubadhirifu wa pesa, itakuwa waliutaja na mradi huu na mingine mingi ambayo haikufanikiwa. Ingawa mara nyingi Askofu Mwoleka, alikuwa hafanikiwi katika miradi yake, lakini daima alikuwa na lengo la kuwasaidia watu masikini. Hakutumia pesa kwa matumizi binafsi!
Kwa kutaka kukwepa gharama za mabati, alitaka nyumba za watu wa masikini ziezekwe kwa Vigae. Aliamini watu wangeweza kujitengenezea vigae. Hii inanikumbusha mwaka 1983, nilipokutana naye Ujerumani na kunielezea nia yake ya kutaka kujenga nyumba za vigae. Aliwaomba Wajerumani wampatie vigae viwili vya mfano. Alinificha nia yake ya kutaka kubeba vegae hivyo hadi Tanzania. Vigae vyenyewe vilikuwa vizito. Siri yake ilifichuka kwenye uwanja wa ndege wa Munich. Mzigo wake ulizidi uzito. Alipoambiwa kulipia au kupunguza uzito wa mzigo, alifungua mzigo wake na kutoa vigae viwili na kusema: Ninaomba mnisaidie, vigae hivi ni vya kuwafundishia watu wangu masikini, wajue kuvitengeneza na kujenga nyumba bora, imara na za kisasa. Maneno yake yaliulainisha moyo wa binti mdogo aliyekuwa anapima mizigo, alicheka tu na kumruhusu Askofu Mwoleka, kupita na vigae vyake bila kuvilipia. Zoezi la kujenga nyumba za vigae lilifanikiwa kiasi fulani. Hadi leo zipo nyumba ambazo chini zimejengwa kwa udongo, lakini paa ni za vigae. Askofu Mwoleka, alinunua mashini ndogo za kutengeneza vigae na kuzisambaza kwenye vituo mbalimbali. Bahati mbaya wajanja wachache waliiba hizi mashini na kuzitumia kufanya biashara kwa kuezeka nyumba za matajiri. Hivyo nia kamili ya Mwoleka ya kuwajengea maskini nyumba bora ikawa haikufanikiwa kiasi kizima. “Wapelelezi wa Roma” wakapeleka habari kwamba anafuja pesa!

Katika harakati za kutaka kujenga nyumba bora, imara na za kisasa kwa masikini, Askofu Mwoleka alianzisha kikundi cha vijana wajenzi wa nyumba bora “Better housing scheme”. Vijana hawa waliandaliwa na kupata mafunzo ya ujenzi. Kikundi hiki bado kipo na kina mafundi bora, wachapakazi na waaminifu. Kwa upande fulani Askofu Mwoleka, alifanikiwa kwa asilimia kubwa, maana vijana wote kwenye kikundi hiki walijijengea nyumba bora, mara na za kisasa na waliweza kuwajengea masikini wachache nyumba bora. Kikundi hiki bado kipo na kinaendelea kujenga nyumba bora na za kisasa za kanisa, mashirika ,serikali na watu wenye uwezo. Kwa upande mwingine lengo la Askofu Mwoleka, halikufanikiwa kiasi kizima. Kikundi kama kikundi, ili kiendelee, kujitegemea na kujiendesha bila misaada ya kutoka nje, ilibidi kitafute mikataba ya majengo ya serikali, mashirika na watu matajiri. Labda siku za mble kikundi hiki kitakumbuka lengo la Askofu Mwoleka, na kuamua kuwajengea nyumba bora, imara na za kisasa walao masikini watatu kila mwaka.

Askofu Mwoleka, hakuchoka katika jitihada za kutaka kuwajengea masikini nyumba bora, imara na za kisasa. Miaka michache kabla ya kifo chake alianza kufikiria na kuchora aina ya matofali ya kuunganishwa bila kutumia sementi. Michoro ya matofali haya bado ipo, na haionyeshi kama aliigiza au kuibia mawazo ya mtu. Mwaka 2001, nilipotembelea kituo cha Uhandisi cha Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam, nilishaagaa sana nilipowakuta wataalamu wakihangaika kutengeneza matofali ya kuunganishwa bila kutumia sementi. Nilipomweleza Askofu Mwoleka, habari hizo, wakati huo akiwa anaumwa na kuelekea mwisho wa maisha yake, alicheka sana na kusema, Mungu, angekubali kurudisha maisha yangu nyuma nikawa na miaka 35, ningewajengea watu wangu wote nyumba bora, imara na za kisasa. Bahati mbaya mauti yalimkuta, kabla ya kushuhudia nyumba zilizojengwa kwa matofali ya kuunganishwa bila kutumia sementi. Utaalamu huu sasa umeenea sehemu nyingi za Tanzania.

Askofu Mwoleka, alikuwa mjenzi. Alikuwa na upeo, karama na roho ya kutaka kuwajengea watu wake nyumba bora, imara na za kisasa. Aliamini Mungu, anatutaka tuishi vizuri, tule vizuri, tuwe na afya bora na tushirikiane katika kujenga Ufalme wake. Sambamba na hili, Askofu Mwoleka, alitaka kujenga jamii bora, imara na ya kisasa. Theolojia yake ilikuwa Theolojia ya ujenzi. Maoni yake yalikuwa kwamba wamissionari walifyatua matofali na kuacha marundo. Walileta imani, walibatiza na kugawa sakramenti, lakini hawakujenga jumuiya za Kikristo. Watu walisali pamoja kanisani, lakini baada ya hapo kila mmoja alirudi nyumbani kwake na kuendelea kuishi maisha yake peke yake. Kanisa, halikuunganisha jirani na jirani, familia na familia, kitongoji na kitongoji na kijiji na kijiji. Waumini walibaki kama rundo la matofali! Wamissionari Walishughulikia imani ya mtu mmoja mmoja, kwa maneno mengine waliacha rundo la Wakristu, rundo la matofali, bila kujenga nyumba bora, imara na ya kisasa. Kazi ya wanateolojia wazawa, ni kuyatumia matofali hayo, mabaya na mazuri, kujengea nyumba bora, imara na ya kisasa. Kujenga kanisa la kisasa, lenye sura mpya. Maisha yake yote, Askofu Mwoleka, alijishughulisha na ujenzi huu wa nyumba bora, imara na ya kisasa. Ni wazi katika ujenzi kuna makosa ya hapa na pale, kuna kukwama na kuishiwa vifaa! La msingi ni lengo, na nia.

Kwa mtu mwenye akili finyu, asiyekuwa na upeo, anaweza kusema Mwoleka, hakufanya kitu, au kwamba Mwoleka, alifuja pesa. Ujenzi ni kitu kigumu. Wengine wanajenga, nyumba zinakwamia kwenye msingi, wengine kwenye madirisha, wengine wanashindwa kuweka milango na kupiga sakafu. Wengine majengo yanageuka magofu. Tunaambiwa kanisa la mtakatifu Petro, la Roma, lilijengwa kwa muda wa miaka 400! La msingi ni kuendeleza ujenzi, mbaya ni yule anayevunja na kusambaratisha matofali. Mwenye hekima daima anaendeleza ujenzi. Ukristu wenyewe hadi leo hii umejengwa kwa miaka elfu mbili na nyumba yenyewe haijasimama imara, Askofu Mwoleka, angefanya miujiza ipi kwa kipindi cha miaka 27 ya uaskofu wake? Ingawa nyumba yake sasa hivi imevunjwa na kusambaratishwa, lakini msingi wake utadumu daima. Msingi wa nyumba yake umejengwa kwenye nyoyo za watu, labda Mungu, lakini hakuna binadamu mwenye uwezo wa kuuvunja msingi huo. Tutakukumbuka daima Christopher Mwoleka, uliyekuwa Askofu wa jimbo Katoliki la Rulenge.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

1 comments:

Christian Bwaya said...

Karibu sana Padre kwenye uwanja huu mpya.

Bila shaka sasa tutaweza kupata mijadala moto moto bila kulazimika kusubiri vyombokale vya habari ili kusoma makala zako.

Nakupongeza kwa uamuzi wako wa kutumia blogu.

Post a Comment