2004 KUELEKEA 2005

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA RAI 2004.

2004 KUELEKEA 2005.

Tunaelekea kuumaliza mwaka wa 2004, na kuuanza mwaka wa 2005. Wale wote watakaofanikiwa kuingia mwaka wa 2005 wanawajibika kumshukuru Mwenyezi Mungu. Si kwa ubora wao wameendelea kuishi, si kwa wema wao wameendelea kuishi na wala si kwa umuhimu wao wameendelea kuishi. Tulikuwa na watu bora wenye wema wa kupindukia na muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa letu, lakini hatunao tena! Hawakubarikiwa kuiona 2005! Kuendelea kuwepo, kuendelea kuishi ni neema na huruma ya Mwenyezi Mungu. Hivyo kwa wale waliobahatiwa kuendelea kuishi ni lazima kumshukuru Mwenyezi Mungu. Uhai ni zawadi. Tunazawadiwa bila ya kustahili! Zawadi hii inaweza kuondoka saa yoyote bila taarifa na bila ya majadiliano. Anayeitoa ndiye anayeitwaa. Kwanini anatwaa ya huyu na kuacha ya yule, hiyo ni kazi yake! Anayebahatiwa kuendelea kuishi, kazi yake kubwa ni kumshukuru Mwenyezi Mungu.

Baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, wale wote waliopata bahati ya kuendelea kuishi wana changamoto mbele yao. Je, ni kwa nini Mungu, amewaruhusu kuendelea kuishi? Wanaishi ili wafanye nini? Wanaishi ili wale na kunywa? Wanaishi ili wayashughulikie maisha yao tu au wayashughulikie maisha ya watu wengine? Wanaishi ili wacheze ngoma, muziki na kuimba nyimbo? Wanaishi ili walete amani na utulivu au walete vurugu na kuuweka uhai hatarini? Kwanini waendelee kuwepo? Je, Mungu, anataka nini kutoka kwao? Uhai tunazawadiwa, hakuna anayeuomba ! Lakini baada ya kuzawadiwa kila mwenye uhai ana wajibu wa kuulinda . Uhai ukishapotea haurudi tena! Hivyo ni wajibu wa kila mwenye uhai, kila aliyebahatika kuumaliza mwaka 2004 na kuingia mwaka wa 2005 kuulinda uhai wake, uhai wa wengine na uhai viumbe vingine vyote vinavyomzunguka. Ni wajibu wa kila mwenye uhai kuulinda uhai wa mazingira yetu ili na mazingira yetu yachangie kuulinda uhai wetu!

Kwa bahati mbaya Tanzania, bado ina mambo mengi yanayotishia uhai wa wananchi. Nchi nyingine na hasa nchi za mataifa yaliyoendelea, zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuyapunguza mambo yanayotishia uhai. Na hii imefanikiwa kwa sababu nchi hizi zimekazania utawala bora, demokrasia na kuziheshimu haki za binadamu. Hapa Tanzania, akinamama wajawazito bado wanapoteza uhai wakati wa kujifungua. Hili ni jambo la kusikitisha maana uhai huu wa akinamama unapotea pasipokuwa na sababu yoyote ile. Katika ulimwengu wa leo, ulimwengu wa utandawazi, wakati mwanadamu ameendelea kiasi cha kwenda mwezini na kutalii kwenye anga za mbali, mjamzito kupoteza maisha ni dhambi ya Ulimwengu mzima. Pamoja na maendeleo yaliyofikiwa na dunia ya kwanza, kuendelea kutuacha nyuma kiasi hicho ni dosari kubwa na ni dhambi mbele ya Mwenyezi Mungu, maana yote waliyonayo wanapewa bure na Mwenyezi Mungu, bila yao kuwa bora kuliko wanadamu wengine na bila ya kustahili! Hata hivyo hii haiondoi lawama kwa serikali isiyowajibika na kuuthamini uhai wa watu wake. Serikali ikiboresha huduma za afya, ikaboresha huduma kwenye hospitali za serikali na zahanati za vijijini, ikaboresha barabara za vijijini na kuhakikisha zahanati zina usafiri wa kuaminika vifo hivi vya wajawazito vitakoma! Hivyo katika jitihada za kila Mtanzania kuulinda uhai ni pamoja na umakini wa kuiweka madarakani serikali yenye uwezo wa mikakati, uzalendo wa kulinda uhai wa watanzania wote likiwemo hili la kuboresha huduma ya Afya.

Magonjwa kama Malaria na UKIMWI yanatishia uhai wa watanzania. Wale waliopata bahati ya kuuanza mwaka wa 2005, wana mashaka makubwa ya kuuona mwaka wa 2006, maana Malaria na UKIMWI, ni tishio kubwa. Pamoja na jitihada za serikali inayowajibika, magonjwa haya yanamtaka kila mtu kuwajibika. Ni lazima watu kujenga tabia ya kutumia chandarua na kuwapeleka haraka watoto hospitali wanapoonyesha dalili za malaria. Watoto wengi wa Tanzania wamepoteza uhai kutokana na uzembe wa wazazi wao. Ni wazi kuna familia ambazo haziwezi kumudu kununua chandarua na kulipia matibabu ya watoto. Kwa vile kuulinda uhai ni mradi wa pamoja, basi viongozi wa serikali za mitaa na viongozi wa dini wasaidie kuwatambua watu hawa ili wasaidiwe. Kama kauli mbiu ya kampeni dhidi ya malaria inavyosema kwenye vyombo vya habari: Malaria haikubaliki! Iwe mwiko kwa Mtanzania yeyote kupoteza uhai wake kwa ugonjwa huu wa malaria!

UKIMWI ni hatari zaidi. Hadi leo hii ni ugonjwa usiokuwa na tiba. Mbaya zaidi ni ugonjwa ambao ni vigumu kwa kutazama tu kujua ni wangapi wameambukizwa. Maisha yanaendelea kama kawaida! Ni nani anaweza kusema ana mke mmoja? Ni nani anaweza kusema hatembei nje ya ndoa yake? Ni nani anaweza kusema ana mpenzi mmoja? Hili linabaki kwa mtu binafsi, hii ni siri inayobebwa kwenye moyo wa kila mwanadamu. Mwanadamu si kisiwa, daima anaishi miongoni mwa watu, na kila kukicha ni lazima kujitokeze mahusiano mapya – swali ni je ni upi mpaka wa mahusiano? Ni rahisi kujibu na daima tunajibu haraka bila ya kuwa wa kweli. Mtu asipokamatwa anajifanya kuishi kana kwamba ukweli wa siri iliyo moyoni mwake haupo! Tunajidanganya hivyo hadi pale tunapoumbuliwa na ugonjwa. Aliye salama leo ni mashaka makubwa kama kesho atakuwa salama! Watu walio wengi hawajakubaliana na ushauri wa kupima. Kwa vile kulinda uhai ni mradi wa pamoja, hatuna budi kushirikiana kwa pamoja kupambana na ugonjwa huu wa hatari. Kwa vile wale ambao bado tunaishi tunalindwa na Mwenyezi Mungu, pasipokustahili, hakuna haja ya kushutumiana wala kulaumiana. Hakuna haja ya kunyosheana kidole cha uzinzi. Maana neno hili ni pana kidogo na hakuna shujaa. Mtu aliye timamu, lolote linaweza kutokea kama mwizi wa usiku!:
“ Mmesikia ya kuwa watu waliambiwa: ‘Usizini!’ Lakini mimi nawaambieni, atakayemtazama mwanamke kwa kumtamani, amekwisha zini naye moyoni mwake.” (Matayo 5:27-28).

Kwa mantiki hii ni nani wa kuukwepa Uzinzi! Labda yule anayeishi juu mbinguni. Lakini anayeishi kwenye dunia hii, jambo hili ni gumu sana. Wanafiki wanaweza kujigamba mbele ya binadamu lakini si mbele ya Mwenyezi Mungu. Mungu, anaona yote na kupenyeza kwenye unafiki wetu! Jambo la msingi ni kushirikiana kupambana na adui. Kwa pamoja tuhimizane kupima afya zetu, tuhimizane kuwa waaminifu na tuhimizane kujikinga. Tuzingatie ukweli kwamba sote ni wadhaifu mbele ya uhusiano kati ya mtu na mtu; iwe ni chuki, kusengenya, kupendelea, mapenzi, kulaumiana, kusingizia, kuvutia upande mmoja nk., hakuna mwenye kipimo cha kujivuna na kujigamba. Sote tunalindwa na huruma ya Mwenyezi Mungu. Mungu yule yule anayeturuhusu kuendelea kuishi ndiye anayetupatia akili za kutengeneza kinga. Ni wajibu wetu kushirikiana na muumba wetu.

UKIMWI, unatishia uhai wa familia zetu. Ndoa nyingi zimesambaratika, watoto yatima wamezagaa kila sehemu kuanzia mitaani hadi machimboni. Wakati tunatafuta tufanye nini ni bora kuwasikiliza waathirika wa ugonjwa huu. Tuwasikilize pia na watu wanaoyaishi maisha ya ndoa, wanaoguswa na tatizo zima la ukosefu wa uaminifu, tatizo la kumpoteza mwenza wa maisha, tatizo la kutengwa na jamii. Mtu hata akisoma kufika mwezini, kama hana uzoefu wa kitu ni vigumu kukisemea. Mtu asiyecheza mchezo ni vigumu kutunga sheria za mchezo! Mtu anaweza kusoma juu ya ndoa na maisha ya ndoa, akawa mtaalam wa kuzishauri ndoa, bila yeye kuishi maisha ya ndoa ushauri wake utakuwa na walakini. Ndio maana wataalam wa aina hii wanauona UKIMWI, kama kilema na kwamba wale wenye ugonjwa huu waachane na ngono!

UKIMWI ni tishio la uhai kiasi kwamba tusipokubali kushirikiana na kuacha unafiki, huruma ya mwenyezi Mungu, itatutupa mkono na kufikia 2110, uhai wa watanzania wengi utakuwa mashakani. Kizazi kitafutika! Utakuwa ni uzembe wa kizazi chetu hiki na historia itatuhukumu!

Njaa nayo ni tishio la uhai. Mvua isiponyesha ya kutosha. Baadhi ya maeneo ya Tanzania, yanakumbwa na uhaba wa chakula na miaka mingine inakuwa mbaya kiasi cha watu kufa. Ni aibu jambo hili kutokea kwenye nchi yenye maziwa na mito na ardhi ya kutosha. Wakati mwingine ni uzembe na kutowajibika. Kuna mikoa inakuwa na chakula kingi wakati mikoa mingine watu wanakufa kwa njaa. Tatizo kubwa likiwa usafiri wa kusafirisha chakula hicho kutoka mkoa hadi mwingine. Barabara zilikuwa mbaya! Sasa hivi barabara zinatengenezwa. Kazi kubwa iliyo mbele ya kila Mtanzania ni kuiweka madarakani serikali itakayoendeleza ujenzi wa barabara na kubuni miradi ya kilimo cha umwagiliaji ili kupambana na baa la njaa.

Umaskini na ujinga vinatishia pia uhai wa watanzania walio wengi. Pamoja na jitihada za serikali inayowajibika, kuondoa umaskini na ujinga ni mradi wa pamoja pia! Ni lazima kila Mtanzania kushiriki katika jitihada za kuutokomeza umaskini na ujinga. Hatuwezi kuutokomeza umaskini bila kufanya kazi kwa bidii. Watanzania tuna utamaduni wa uzembe. Kazi iliyofanyika wakati wa Mjerumani, aliyewalazimisha Watanganyika kufanya kazi kwa viboko, haikufanyika wakati wa utawala wa Mwingereza, wakati wa uhuru hadi leo hii. Mjerumani aliondoka na viboko vyake na juhudi ya kazi ikayoyoma. Kiboko cha Mjerumani kitarudi kwa namna nyingine katika ushirikiano wa nchi za Afrika Mashariki, tutakapomezwa na kunyimwa ajira kwa sababu ya uzembe wetu ndipo tutakapozindukana na kuanza kufanya kazi kwa bidii zote!

Je, Mungu, ametuacha hai ili tushuhudie awamu ya nne ya uongozi wa taifa letu? Tuushuhudie uchaguzi mkuu wa 2005? Tushiriki kuiandika historia hai ya taifa letu na kushuhudia demokrasia ikikua na kukomaa?

Ye yote atakayevuruga uchaguzi wa 2005 na kuuweka uhai wa watanzania hatarini ni bora asingeiona 2005 ni heri mtu huyu singezaliwa kabisa! Kwa kutumia maneno ya biblia:
“ Ye yote atakayemkwaza mmoja wa hawa wadogo wanaoniamini, ingekuwa afadhali afungwe shingoni jiwe kubwa la kusagia na kuzamishwa kwenye kilindi cha bahari. Ole wa ulimwengu kwa sababu ya vikwazo vinavyowaangusha wengine. Vikwazo hivyo ni lazima vitokee lakini ole wake mtu yule atakayevisababisha.” ( Matayo 18: 6-7).

Maneno haya yalitamkwa zaidi ya miaka 2000 iliyopita. Lakini bado yana maana leo hii maana mwanadamu ni yule yule, mwenye tamaa, uchu wa madaraka, kujipenda, chuki, kulipiza kisasi nk. Na ukweli mwingine ni kwamba pamoja na ukorofi wa mwanadamu, Mungu, hachoki kumvumilia. Huruma ya Mungu, ndiyo inatufanya tuendee kuishi. Kwa vile bado Mungu bado ametusimamia, tushirikiane naye kuulinda uhai wetu na uhai wa taifa letu. Heri ya mwaka mpya!

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment