Monday, June 14, 2004
Makala hii ilitoka kwenye gazeti la Rai, mwaka 2004.
MTOTO WA AFRIKA, MTOTO WA KIJIJINI!
Wanangu wapendwa watoto wa Tanzania, tarehe 16.6.2004, kama ilivyo kila mwaka ni siku ya mtoto wa Afrika. Mtacheza ngoma ,mtaimba na kucheza michezo mbalimbali.Ni siku ya kumkumbuka mtoto wa Afrika, anayeishi katika mazingira magumu, anayefanyishwa kazi ngumu, anayeshuhudia ukatili wa kila aina, anayepigwa shuleni, anayekufa kwa malaria na magonjwa mengine yanayotibika. Ninajua mna maswali, mtasema si watoto wote wa Afrika wanaishi katika mazingira magumu. Wapo watoto wanaoishi kwenye mazingira mazuri sana hata kuliko watoto wa nchi zilizoendelea. Hawa ni wachache! Mtasema wachache maana yake nini? Wataalamu wa uchumi na takwimu hawataki kusikia neno wachache, baadhi na wengi, wanataka namba na asilimia!! Mfano wanataka kusikia kwamba watoto elfu tano wa Tanzania ambao ni sawa na asilimia mbili wanaishi maisha mazuri na watoto asilimia 98 wanaishi katika maisha magumu! Hiyo ndio lugha ya kitaalamu!
Ndio tunavyoishi. Mwanadamu anapenda sana takwimu ingawa wakati mwingine azimsaidii sana Nilipokwenda Ulaya kwa mara ya kwanza mwaka 1982, nilialikwa kwenye sherehe. Nje ya ukumbi nilikuta magari kama hamsini yameegeshwa. Akilini nilifikiri sherehe hiyo itakuwa na watu zaidi ya mitatu au minane. Lakini kwa mshangao mkubwa niliwakuta watu hamsini tu maana kila mtu alikuwa na gari lake! Kijijini kwetu sherehe yenye magari hamsini itakuwa na watu zaidi ya mianne maana kila gari linabeba zaidi ya watu kumi!!
Takwimu, takwimu!! inategemea unazitumia wapi na kwa faida gani. Namba ya watu waliokufa kwenye meli ya MV, itajulikana baada ya miaka hamsini! Hii ni sawa sawa na namba ya watu waliokufa kwenye ajali ya train. Vurugu za Zanzibar na watu waliokufa hadi leo idadi yao ni kitendawili. Takwimu zinapumbaza na kutoa mwanga kwa kutegemea zinatumika vipi. Mtu aliyefiwa na jamaa wengi kwa ugonjwa wa UKIMWI, akiulizwa na shirika la misaada idadi ya watu aliowapoteza, kama ni watano, atataja kumi na watano, ili auhurumiwe na kupata misaada mingi. Wakati mwingine wengine wanawakusanya watoto wa majirani ili kuongeza idadi ya watoto yatima walioachwa na hao jamaa kumi na watano waliokufa kwa UKIMWI.
Hata kama takwimu zimetengenezwa na watafiti. Zinapindapinda kutegemea ni nani anafanya utafiti, anawafanyia watu gani na kwa manufaa gani. Kama unafanya utafiti wa kuleta msaada katika kijiji, hakuna mwanakijiji atakayekupatia takwimu sahihi za mapato yake. Atakudanganya ili umwingize kwenye orodha ya watu wakusaidiwa. Au mfano mwingine, ukiingia kijijini kufanya utafiti unatembea kwa miguu, huwezi kupata takwimu zinazofanana na mtu atakayeingia kijijini na shangingi au “Landcuiser”. Anayetembea kwa miguu anaweza kuwa na takwimu zinazokaribia na ukweli. Tafiti nyingi zinazofanyika hapa nchini ni zile zinazoendeshwa na mashirika makubwa yenye magari na watu wenye hali nzuri na wakati mwingine Wazungu. Hawa wanatoa picha ya watu wa kutoa misaada. Takwimu wanazozipata kutoka kwa wanavijiji ni zile za kuonyesha hali ngumu na matatizo ili wasaidiwe.
Mwaka jana nilisoma ripoti ya mtafiti Fulani wa hapa Tanzania, akitaja kwamba asilimia 45 ya watoto yatima wa mkoa wa Kagera, wanaishi peke yao. Kwa maana, hawatunzwi na mjomba, shangazi, baba mdogo au ndugu yeyote yule. Wanaishi peke yao kwa kujitegemea. Nimetembelea vijiji 15, vya mkoa wa Kagera, nikifanya utafiti sikufanikiwa hadi sasa kukutana na nyumba hata moja ambayo watoto yatima wanaishi kwa kujitegemea!! Matokeo haya yanafanana na ya wenzangu waliotembelea vijiji vingine 36!
Takwimu zina uongo wake na ukweli wake! Basi kwa makala hii ninawalenga watoto wangu wengi wanaoishi kwenye mazingira magumu. Ingawa neno “ watoto wengi” linabaki likielea hewani hasa ukizingatia lugha ya “ Wataalamu” ,nitasimama kwenye msemo wa Kiswahili usemao “Mwenye macho haambiwi tazama”. Mwaka jana kama mnakumbuka nilimwandikia mwanangu Mwidunda, maneno ya kumfariji. Mwidunda ni mtoto mwenzenu aliyelazimishwa na jamii kuuza mwili wake na kupewa jina la “Changudoa”!
Ninajua jinsi mlivyotapakaa nchi nzima ya Tanzania. Wengine mko kule Mererani na kwenye migodi mingine. Wengine mnavuna chai na katani, wengine mnafanya kazi majumbani, wengine mnabeba mizigo inayowazidi nguvu, wengine ni Machinga, wengine ni wapiga debe, orodha ni ndefu.
Leo ningependa kumtuliza, kama kweli nitapata maneno ya kumtuliza; mtoto anayeishi kijijini. Mtoto anayeshinda uchi, anayechezea matopeni na mchangani, asiyeoga asiyekuwa na lishe, anayeugua na kufa kwa magonjwa yanayotibika, anayesoma chini ya mti, anayeolewa akiwa mtoto! Nimetembelea vijiji kadhaa vya mkoa wa Kagera na kushuhudia jinsi watoto wa vijijini wanavyoishi maisha magumu. Pamoja na ugumu huo watu wa vijijini, wanaendelea kuzaa, hawana habari na uzazi wa mpango, barabarani utakutana na vitoto vingi viko uchi vikicheza matopeni na mchangani, vingine vina utapiamlo na vingine afya iko mashakani; maisha ya mbele ya watoto hawa ni kitendawili! Watoto wa vijijini wa mkoa wa Kagera, hawana tofauti na watoto wa vijijini wa sehemu nyingine za Taifa letu. Kwa kutaka kuwa mwaminifu, ninaandika makala hii nikiwafikiria na kuwakumbuka watoto wa kijiji cha Kibare. Kijiji hiki ni kati ya vijiji vya Wilaya ya Karagwe, vilivyotelekezwa au kwa maneno “Matamu” ya wanasiasa viko mbali! Niliishi katika kijiji hiki majuma mawili nikifanya utafiti mwezi wa nne mwaka huu.
Ninasikitika sana kwamba watoto wangu wa Kibare, hawawezi kusoma haya ninayoyaandika. Gazeti hazifiki! Si gazeti tu, mambo mengi hayafiki Kibare. Sipendi kunukuliwa, lakini ukweli ni kwamba yale yanayofika, kama soda, bia, sukari, mafuta ya taa na petroli bei yake ni ya Kibare, na wala haijulikani kwingineko Tanzania!
Mtoto wa Kibare, anatembea zaidi kilomita 20 kila siku kwenda shuleni na kurudi! Umande, mvua jua na changarawe ni mateso yake ya kila siku; havai viatu, atavaaje viatu wakati baba na mama hawana uwezo wa kununua hata mafuta ya taa? Hawezi kukwepa kuugua minyoo, pepopunda na magonjwa mengine ya kuambukizwa maana njia anazozipitia kwenda shuleni si salama . Bila viatu, mchubuko kidogo unaweza kuyakatisha maisha ya mtoto! Ni mtoto asiyejua kifungua kinywa wala mlo wa mchana, anasomea chini ya mti, anapigwa ovyo na walimu, anafanyishwa kazi za kuchota maji, kuchanja kuni na kupika chakula cha mwalimu.
Nikutulize kwa maneno gani wewe mtoto wa kijiji cha Kibare? Niwatulize kwa maneno gani nyinyi watoto wa Tanzania, mnaoishi katika mazingira magumu? Niseme: Nchi yetu ni changa, tumepata uhuru miaka 40 iliyopita! Ni vigumu kulinganisha maendeleo yetu na nchi kama Amerika zenye miaka zaidi ya 200 ya uhuru ! Nchi yetu ina kazi kubwa ya kuwatunza waheshimiwa viongozi wetu. Viongozi wetu wanahitaji magari mazuri na ya gharama kubwa kama yale wanayoyaita mashangingi, wanahitaji mishahara mikubwa na majumba ya kifahari ili waweze kutoa huduma nzuri katika jamii. Serikali inahitaji pesa nyingi kutunza afya za viongozi wetu. Mnavyojua, hatuna hospitali nzuri ya kuweza kuwatibu viongozi wetu. Msitegemee hospitali nzuri ipatikane siku za hivi karibuni. Sisi bado tunakula nchi, nyinyi pia mtakula nchi, wajukuu zenu watakula nchi , maana huu ni ugonjwa wa kurithiana. Hatujapata muujiza wa kuwapata watu wanaozaliwa bila meno ya kutafuta na kuila nchi! Bado nchi yetu ni changa kuwa na uwezo wa kuwazaa watu wasiokuwa na meno! Viongozi wetu ni lazima watibiwe nchi za nje. Na hii inahitaji pesa nyingi sana.
Nimekumbuka kitu cha kukutuliza wewe mtoto wa Kibare. Subiri shule ya Museveni, ya Nyamihaga, imalizike. Hapa utapata elimu, hapa utasoma vizuri! Usiniulize hii shule itamalizika lini; labda wewe utakuwa umefikia umri wa uzee. Wakati wa mapambano ya kuikomboa Uganda. Rais Yoweri Museveni, alikuwa na kambi yake kwenye maeneo ya Kibare. Baada ya mapambano na mafanikio ya Uganda, Museveni, alitoa zawadi ya dollar 20,000 ili zijenge shule pale Nyamihaga. Pesa ziliyeyuka! Wenye meno walizitafuna na kuzila. Lakini bado Rais Museveni, ana ahadi ya kujenga shule ya kimataifa kwenye maeneo ya Kibare. Kufuatana na yale yaliyotokea kwa zawadi yake ya kwanza, haitashangaza zamu hii akiamua kuwaleta mafundi kutoka Uganda na kusimamia shule hiyo hadi mwisho. Si matusi, akiamua kuleta walimu na uongozi wa kuiendesha shule hiyo kutoka Uganda! Hata hivyo ndio Utandawazi! Waganda watakuja na kufundisha na kuendesha shule na sisi tutabaki kupiga gongo, kufanya magendo na kuuza kahawa yetu kwa Museveni! Kwa mtoto wa Kibare, ninayemwandikia leo hii shule ya Museveni, itawanufaisha watoto wake au wajukuu! Ndo hivyo taifa letu bado ni changa!
Ninajua mnakufa kwa malaria. Hamna chandarua. Na malaria ni ugonjwa unatibika. Ni dhambi ya mauti mtoto kufa kwa malaria. Ila ninawaomba mvumilie. Mungu, atawakinga vumilia kama miaka mingine 40!
Si nia yangu kukukatisha tamaa. Wewe mtoto wangu uliye na umri wa miaka 18, wewe ambaye unaruhusiwa na sheria ya Tanzania, kupiga kura, ni wakati wako kuwa macho. Toka usingizini. Angalia na kutambua ni mtu gani ana nia njema na Taifa letu. Ni mtu gani ana mipango ya baadaye ya Taifa letu. Ni mtu gani ana sera ya kuyaboresha maisha ya vijijini. Sera yake ni ya miaka mingapi? Tumemaliza 40 ya uhuru, vijiji bado vina hali mbaya: hakuna maji, barabara mbaya, magonjwa mengi, uchumi unapendeza mijini tu na vijijini ni hali mbaya. Angaza na kuona ni mtu gani bado ana nguvu za kufanya kazi na muda mrefu wa kuishi. Wengine bado wana muda mfupi, wanapenda waishi kwa starehe na amani siku zao za mwisho. Hawana muda na Tanzania, ya miaka 100 ijayo. Hawa hawana faida kwako na kwa taifa! Kura yako inaweza kuleta tofauti kubwa! Kumbuka kwamba watanzania wengi wanaishi vijijini na wala si mijini!
Msicheke, hii ni kweli! Nimesoma habari ya watafiti wakisema uchumi wa Tanzania unakua! Si uongo! Wana maana ya Dar-es-Salaam, Mwanza na Arusha! Wana maana ya maisha ya mjini. Hapo mwanzo nimewaambia ukweli wa takwimu na uongo wa takwimu. Wakati nyinyi mnatembea kilomita kumi kwenda shuleni watoto wenzenu wa mijini wanabebwa na magari kwenda shule kwa umbali wa kilomita mbili au tano. Wakati ninyi mnajifunza kwa kuandika udongoni, wenzenu wanatumia computer! Wakati mnafundishwa kwa simulizi, wenzenu kila kitu wanakiona kwa macho yao.
Hii inanikumbusha nilipoitembelea shule mojawapo ya Kibare, nikamkuta mwalimu anafundisha juu train. Kwa kuelezea kwamba train, ni mfano wa nyoka na hutembea kama nyoka. Mtoto mwenye akili alikuwa na mashaka kubwa, maana kama train inatembea kama nyoka kwenye njia iliyotengenezwa kwa chuma ni lazima itapata ajali mara nyingi maana ni lazima iteleze!
Mtoto wa Afrika, mtoto wa kijijini, siku yako isipite kwa kuimba na kucheza ngoma tu. Itumie siku hii kwa kutafakari na kwa kutoa mchango wako katika maendeleo ya taifa letu la Tanzania. Mchango wako unaweza kuleta tofauti kubwa!
Na,
Padre Parivatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment